DANIELI: Mlango wa 2

DANIELI: Mlango wa 2

Kulikuwa na sababu kwanini Mungu aliinyanyua Babeli kuwa taifa lenye nguvu kuliko yote duniani na kutawala falme zote za dunia kwa wakati ule, hata kudhubutu kulichukua taifa teule la Mungu Israeli kulipeleka utumwani, pamoja na kuteketeza mji na Hekalu la Mungu..Aliruhusu kwasababu alitaka kuonyesha kuwa ijapokuwa ni mji uliokuwa umetukuka sana, lakini siku moja kwa wakati ulioamriwa mji huo utaanguka na kuwa makao ya mbuni, na hayawani wote wa mwituni usioweza kukalika na watu . Hivyo ndivyo itakavyokuwa pia kwa BABELI YA ROHONI iliyopo leo ijapokuwa imetukuka sana, biblia inasema kwenye ufunuo 18 itaanguka na kuwa ukiwa na watu wote watauomboleza kwa kuanguka kwake.

Tunasoma miaka kadhaa kabla ya kuanguka kwake Mungu alishaanza kutoa maonyo kwa watawala wa Taifa hilo, na ndio maana tunaona ndoto zote na maono waliyoyaona yaliwafadhaisha sana, kwasababu walikuwa wanafahamu kwa namna moja au nyingine zinawahusu wao na utawala wao. Na kibaya zaidi ni kuona jinsi yale maono yalivyokuwa yanaishia.

Kama tunavyosoma katika sura hii ya pili Mfalme Nebukadneza aliota ndoto, ambayo ilimhuzunisha sana mpaka kufikia kwenda kuwaita waganga, na wachawi pamoja na watu wote wenye hekima waliokuwa Babeli wampe tafsiri ya ndoto ile, lakini hakuonekana hata mmoja ambaye angeweza kutoa tafsiri, waganga wote na wachawi walikiri kuwa hakuna awezaye kuingia katika vyumba vya ndani vya moyo wa mwanadamu isipokuwa Mungu peke yake. Na ni kweli ndivyo ilivyo shetani hana uwezo wa kuingia ndani ya mtu na kuyafahamu mawazo yake, ndio anaweza kutuma mawazo mabaya lakini hawezi kutambua fikra za mtu zikoje, mwenye uwezo huo ni Mungu tu,

Waebrania 4:12-13″ Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu. “

Kwahiyo Mfalme alipoona hakuna mtu wa kumtafsiria ndoto yake, akakusudia kuwaangamiza waganga na wenye hekima wote wa Babeli lakini Mungu akamjalia Danieli na wenzake neema ya kufahamu tafsiri ya ile ndoto, na kuipeleka kwa mfalme. Tunasoma..

Danieli 2:26″ Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, aliyekuwa akiitwa Belteshaza, Je! Waweza kunijulisha ile ndoto niliyoiona, na tafsiri yake.

27 Danieli akajibu mbele ya mfalme, akasema, Ile siri aliyoiuliza mfalme, wenye hekima hawawezi kumfunulia mfalme; wala wachawi, wala waganga, wala wanajimu;

28 lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho. Ndoto yako, na njozi za kichwa chako ulizoziona kitandani pako, ni hizi;

29 Wewe, Ee mfalme, mawazo yako yaliingia moyoni mwako kitandani pako ya mambo yatakayokuwa halafu; na yeye afunuaye siri amekujulisha mambo yatakayokuwa.

30 Lakini mimi, sikufunuliwa siri hii kwa sababu ya hekima iwayo yote niliyo nayo zaidi ya watu wengine walio hai, bali kusudi mfalme afunuliwe ile tafsiri, nawe upate kujua mawazo ya moyo wako.

31 Wewe, Ee Mfalme, uliona, na tazama, sanamu kubwa sana. Sanamu hii, iliyokuwa kubwa sana, na mwangaza wake mwingi sana, ilisimama mbele yako; na umbo lake lilikuwa lenye kutisha.

32 Na sanamu hii kichwa chake kilikuwa ni cha dhahabu safi; kifua chake na mikono yake ni ya fedha; tumbo lake na viuno vyake ni vya shaba;

33 miguu yake ni ya chuma; na nyayo za miguu yake nusu ya chuma na nusu ya udongo.

34 Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande.

35 Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote.

36 Hii ndiyo ile ndoto, nasi tutaihubiri tafsiri yake mbele ya mfalme.

37 Wewe, Ee mfalme, u mfalme wa wafalme, na Mungu wa mbinguni amekupa ufalme, na uwezo, na nguvu, na utukufu;

38 na kila mahali wakaapo wanadamu, wanyama wa kondeni na ndege wa angani amewatia mkononi mwako, naye amekumilikisha juu ya hao wote; wewe u kichwa kile cha dhahabu.

39 Na baada ya zamani zako utainuka ufalme mwingine mdogo kuliko wewe; na ufalme mwingine wa tatu wa shaba, utakaoitawala dunia yote.

40 Na ufalme wa nne utakuwa na nguvu mfano wa chuma; kwa maana chuma huvunja vitu vyote na kuvishinda; na kama chuma kisetavyo vitu hivi vyote, ndivyo utakavyovunja-vunja na kuseta.

41 Na kama vile ulivyoziona hizo nyayo za miguu na vidole vyake, kuwa nusu udongo wa mfinyanzi, na nusu chuma, ufalme ule utakuwa ufalme uliogawanyika; lakini ndani yake zitakuwako nguvu za chuma, kama vile ulivyoona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope.

42 Na kama vidole vya zile nyayo vilikuwa nusu chuma na nusu udongo, kadhalika ufalme ule utakuwa nusu yake una nguvu, na nusu yake umevunjika.

43 Na kama vile ulivyokiona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope, watajichanganya nafsi zao kwa mbegu za wanadamu; lakini hawatashikamana, kama vile chuma kisivyoshikamana na udongo.

44 Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.

45 Na kama vile ulivyoona ya kuwa jiwe lilichongwa mlimani bila kazi ya mikono, na ya kuwa lilivunja-vunja kile chuma, na ile shaba na ule udongo, na ile fedha, na ile dhahabu; basi Mungu aliye mkuu amemjulisha mfalme mambo yatakayokuwa baadaye; na ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti.

46 Ndipo Nebukadreza, mfalme, akaanguka kifudifudi, akamsujudia Danielii, akatoa amri wamtolee Danielii sadaka na uvumba.

47 Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, Hakika Mungu wenu ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme, awezaye kufumbua siri, kwa kuwa wewe uliweza kuifumbua siri hii.

48 Basi mfalme akamtukuza Danieli, akampa zawadi kubwa nyingi sana, akamfanya kuwa mkubwa juu ya uliwali wote wa Babeli, na kuwa liwali mkuu juu ya wote wenye hekima wa Babeli.

49 Tena, Danieli akamwomba mfalme, naye akawaweka Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wawe juu ya mambo yote ya uliwali wa Babeli; lakini huyo Danielii alikuwa akiketi katika lango la mfalme.

Na kama vile ulivyoziona hizo nyayo za miguu na vidole vyake, kuwa nusu udongo wa mfinyanzi, na nusu chuma, ufalme ule utakuwa ufalme uliogawanyika; lakini ndani yake zitakuwako nguvu za chuma, kama vile ulivyoona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope.

Katika ndoto hii tunaona Danieli akifunuliwa na Mungu Falme 4 zitakazokuja kutawala mpaka mwisho wa dunia, Kumbuka hakutakuwa na falme nyingine zaidi ya hizo, na ule wa tano ambao ndio uleule wa nne isipokuwa umechanganyikana na udongo ndio utakuwa wa mwisho kabla ya lile jiwe lilolochongwa mlimani pasipo kazi ya mikono kuupiga na kuuharibu kabisa.

Kama Danieli alivyomtafsiria mfalme kwamba kile kichwa cha dhahabu kinamwakilisha yeye(yaani ufalme wake wa Babeli),ambao kulingana na Historia ulidumu kuanzia mwaka 605BC hadi mwaka 539BC, Hichi ni kipindi cha miaka 66 , na baada ya hapo ukaanguka kama kitabu cha Danieli sura ya tano kinavyoelezea pale Mfalme Belshaza alipokuwa anafanyia anasa vyombo vya hekalu la Mungu kukatokea kiganja na kutoa hukumu juu ya kuanguka kwa ufalme wake, tunasoma katika usiku huo huo ufalme wake ulianguka.

Kisha ukanyanyuka utawala mwingine baada yake, tukisoma katika biblia ulikuwa ni utawala wa (Umedi na Uajemi) ambao ndio unawakilishwa na kile kifua na mikono ya fedha, Huu ulianza kutawala pindi tu Babeli ilipoanguka kuanzia mwaka 539BC hadi 331 BC. Nao ulienda kwa kipindi cha miaka 208, Pia kumbuka mwanzoni mwa utawala huu ndio Taifa la Israeli lilipokea Uhuru wake ili kutimiza unabii wa miaka 70 ya kukaa kwake utamwani kama Yeremia alivyotabiri, na kurejea tena katika nchi yake, ili kuijenga nyumba ya Bwana aliyokuwa imeharibiwa na Nebukadreza mfalme wa Babeli.

Agizo hilo la kurejea na kuijenga tena nyumba ya Mungu, liliasisiwa na mfalme Koreshi wa Uajemi. Tunasoma..

Ezra 1:1 Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema,

2 Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi;

3 Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Bwana, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akaijenge nyumba ya Bwana, Mungu wa Israeli, (yeye ndiye Mungu), iliyoko Yerusalemu.

4 Na mtu awaye yote aliyesalia mahali po pote akaapo hali ya ugeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. “

Lakini baadaye mwishoni historia inaonyesha ulikuja ukaanguka.

kisha baada ya huo ulikuja Utawala mwingine wa tatu chini ya Mfalme “Alexander the great” aliyekuwa mfalme mwenye nguvu, tunasoma katika historia na katika biblia ulikuwa ni utawala wa Uyunani ambao unawakilishwa na kile kiuno na shaba, Huu ulianza kutawala kuanzia mwaka 331 BC hadi 168 BC, Ni kipindi cha miaka 163,

Na baada ya huu ufalme wa Uyunani kuanguka ulinyanyuka utawala mwingine uliokuwa na nguvu kama za chuma, uliowakilishwa na ile miguu ya chuma, na huu haukuwa mwingine zaidi ya utawala wa RUMI ya kipagani.Utawala huu ulidumu tangu kipindi cha 168 BC hadi kipindi cha 476 AD, ni zaidi ya miaka 644 na huu ndio utawala uliomsulibisha Bwana Yesu, uliwaua watu wengi kikatili kwa kuwasulibisha misalabani, wengine kwa kuchomwa moto n.k. na ndio maana biblia inasema ulikuwa ni mgumu kama CHUMA.

Tukiendelea tunasoma utawala mwingine wa tano na wa mwisho ulifuatia ambao ni chuma kilichochanganyikana na udongo, huu ni utawala ule ule wa nne isipokuwa hapa unaonekana kama umechanganyikana na udongo, Hivyo ni ule ule wa Rumi lakini umechanganyikana ndio unaowakilishwa na zile nyayo na vidole vya miguu ..

JE! huu udongo uliochanganyikana na chuma ni nini?. 

Mstari wa 43 unasema..

43 Na kama vile ulivyokiona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope, watajichanganya nafsi zao kwa mbegu za wanadamu; lakini hawatashikamana, kama vile chuma kisivyoshikamana na udongo.

Kumbuka hapo kabla, Taifa la Rumi lilikuwa haliingiliani na Taifa la Mungu kiimani kwa kipindi chote lilipokuwa linatawala dunia kama chuma, wakati huo lilikuwa lipo kisiasa na kiuchumi zaidi, lakini lilikuja kubadilika baadaye na kubadili tasira yake kwa kupitia DINI ili kujiingiza katikati ya taifa la Mungu (wakristo na wayahudi) 

1Petro 2:9 Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, TAIFA TAKATIFU, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;

10 ninyi mliokuwa kwanza si taifa, BALI SASA NI TAIFA LA MUNGU; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.

Kumbuka hii ilikuwa ni agenda ya shetani alipoona mambo yamehamia Rohoni na yeye akahamia rohoni.

Kwahiyo ule UDONGO unawakilisha WATU WA MUNGU au TAIFA LA MUNGU, na ndio zile mbegu za wanadamu.

Hivyo taswira hii ya kujigeuza ilianza kujidhihisha wakati wa utawala wa Costantine, pale upagani wa kirumi ulipoingizwa rasmi katika Ukristo, hapo ndipo mafundisho ya kweli ya NENO la Mungu yalipoanza kuchanganywa na mafundisho ya kipagani ya kirumi ili tu kuwafanya watu wabebe taswira ya ufalme wa Rumi na wakati huo huo bado wabebe taswira ya Ufalme wa Mungu (Ukristo), Na ndio maana leo mtu akiulizwa wewe ni nani? atakuambia mimi ni MROMA, badala ya kuwa na utambulisho wa taifa lake la mbinguni (yaani kuitwa mkristo), atakuambia ndio mimi ni mkristo na pia ni Mroma, unaona hapo tayari ameshachanganyikana na ule ufalme wa chuma (ambao ndio Babeli ya rohoni ya sasa), na ndio wenye watu wengi duniani leo.

Kumbuka huu utawala ndio wa mwisho na hakutakuwa na mwingine baada ya huo (BABELI YA ROHONI) inayozungumziwa katika Ufunuo 17 & 18, Hivyo hii Rumi iliyochanganyikana na udongo ni UKATOLIKI. DINI hii imechukua desturi za Roma za kipagani ikazileta katikati ya watu wa Mungu, kwamfano ibada za sanamu ambazo Mungu alizikemea akilionya taifa lake lisifanye mambo kama hayo ni machukizo (Kutoka 20) lakini hili limeyaleta katikakati ya watu wa Mungu, ibada kama kusali rozari na kuomba kwa wafu, mafundisho ya kwenda toharani, kukataa uongozi wa Roho Mtakatifu kwa kuua karama za Roho na kuweka vyeo vya uongozi wa kibinadamu badala yake, n.k. Haya yote yalipenyezwa katika NENO la Mungu na kuleta mchanganyiko mkubwa sana katika Kanisa la Kristo.

Lakini mwisho wa lile ONO lilionekana JIWE likiwa limechongwa Mlimani na kushuka, tukisoma..

34 Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande.

35 Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote.

Na jiwe hili si mwingine zaidi ya BWANA wetu YESU KRISTO, yeye ndiye atakayebatilisha hizi falme zote mbovu kwa kuupiga ule ufalme wa mwisho kuleta utawala mpya Duniani ambao huo utadumu milele. Kwasababu yeye ni BWANA WA MABWANA, na MFALME WA WAFALME. Haleluya!!..Na jiwe lile lilionekana likiwa milima mikubwa ikishiria kuwa Kristo atatawala duniani kote pamoja na wafalme wengi(wateule wake) milele na milele.

Mstari wa 44 unasema..

” Danieli 2:44 Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.”

Hivyo ndugu kama tunavyosoma hakitasalia chochote katika ile sanamu?, na wewe je! upo kwenye ile sanamu kumbuka utawala wa shetani uliopo leo ndio ule wa tano uliojichanganyika yaani chuma na udongo(shetani ni mdanganyifu, haji kwako moja kwa moja,)..Udongo ni wewe unayejiita mkristo, na chuma ni ROMA, chini ya mwamvuli wa dini ya katoliki, je na wewe umejichanganya humo? kumbuka lile jiwe lilisaga saga chuma na udongo vyote kwa pamoja, hivyo kama na wewe umejichanganya naye utasagwasagwa kama yeye hakitasalia kitu.

Kumbuka yule mnyama anayezungumziwa kwenye Ufunuo 13 & 17 ni dola ya Rumi inayounda ile chapa ya mnyama, na yule mwanamke aliyeketi juu ya yule mnyama ni Kanisa Katoliki, na anafahamika kama mama wa makahaba, ikiwa na maana kuwa anao mabinti wenye tabia kama za kwake za kikahaba, na hawa mabinti si wengine zaidi ya madhehebu mengine yote yaliyoacha uongozi wa Roho wa mtakatifu na kufuata desturi zisizoendana na NENO LA MUNGU.

Na ndio maana NENO LA MUNGU linasema Ufunuo 18:4″ Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake. “

Kanisa tulilopo ni la mwisho linaloitwa LAODIKIA, na Bwana alilikemea kuwa ni kanisa vuguvugu (lililochanganyikana), na Bwana amesema atalitapika kama lisipotubu,

Ufunuo 3:14-20″14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.

18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. “

Huu ni wakati wa kuwa bibi-arusi safi wa Bwana asiwe na mawaa, kwa kujitenga na mafundisho ya uongo pamoja na kuishi maisha matakatifu( waebrania 12:14″ Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;” ) ili BWANA atakapokuja tuwe tayari kwenda naye katika unyakuo.

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Zilper
Zilper
1 year ago

MUNGU aliye hai aendelee kuitunza huduma hii

M
M
1 year ago

Ubarikiwe mtumishi wa Mungu