Daudi aliyekuwa mfalme wa Israeli, mwenye sifa ya kuupendeza moyo wa Mungu na ushujaa mwingi, lakini chanzo cha kunyanyuka kwake kilikuwa cha kipekee sana, habari hii tunaisoma katika 1 Samweli 17, Tunaona pale ambapo Daudi alitoka kama mtu asiyejua wala kuwa na uzoefu wowote wa vita na kumuua mtu ambaye alikuwa jemedari wa vita wa jeshi la wafilisti(Goliathi).
Kumbuka Daudi alikuwa ni kijana mdogo tu na mchungaji aliyekuwa anakaa maporini akichunga kondoo wa baba yake, hii ni shughuli isiyokuwa na mahusiano yoyote na vita, tunasoma na ilipofika wakati vita kutokea wafilisti kupigana na waisraeli ndipo wafilisti wakamnyanyua Goliathi aliyekuwa hodari wa vita, kwa ukubwa wake na uzoefu wake wa vita, hakuna shujaa yoyote wa Israeli aliyeweza kumkaribia kupigana naye kwa hofu.
Tunasoma kijana mmoja mdogo Daudi asiyekuwa miongoni mwa wale mashujaa wa Israeli waliokuwa na ujuzi wa vita kwa miaka mingi, aliweza kunyanyuka na kumwangusha yule simba wa wafilisti.
Lakini siri ya Daudi kushinda na kuwa jemedari ni ipi?
Tukisoma …
1 Samweli 17:31 “Na maneno hayo aliyosema Daudi yaliposikiwa, watu wakamweleza Sauli; naye akatuma mtu kwenda kumwita.
32 Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu.
33 Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake.
34 Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi,
35 mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua.
36 Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.
37 Daudi akasema, BWANA ALIYENIOKOA NA MAKUCHA YA SIMBA,NA MAKUCHA YA DUBU, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe. “
Hapa katika habari hii tunaona Daudi akitoa ushuhuda wa matendo makuu ya Bwana aliyomtendea, katika nafasi yake ya udogo aliyokuwa nayo, jinsi alivyoweza kuwaua dubu na simba alipokuwa akichunga kondoo wa baba yake, AKAHESABU kuwa kama Mungu aliweza kumshindania katika makucha ya maadui wa mifugo yake, hatashindwa pia kumwokoa kutoka katika makucha ya maadui wa ndugu zake na Taifa lake Israeli.
Pengine Sauli alitegemea kusikia kutoka kwa Daudi ushuhuda wa madaraja mangapi ya uluteni amepitia, au mafunzo mangapi ya kijeshi amepitia, alitegemea kusikia aidha kama alishawahi kupitia mafunzo ya ukomandoo, lakini badala yake aliishia kusikia shuhuda za mbuzi na kondoo zaidi ya yote alionekana ni kijana laini hata mkuki hawezi kubeba vizuri, hivyo kwakuwa hawakuona jemedari mwingine kwa kujitokeza kupambana wakaona wamwache aende tu kama vile kwa shingo upande.
Lakini hawakujua kuwa Daudi anao UFUNUO wa Mungu ni nani kwake, ALIMUHESABIA MUNGU kuwa ni muweza wa yote. Hivyo hakutumia njia zao walizozizoea kumkabili adui yake, hakwenda na chepeo na dirii bali alikwenda na JINA LA BWANA WA MAJESHI (YESU KRISTO)
1 Samweli 17:45 Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.
46 Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya aWafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.
47 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu. “
Amina.
Kumbuka katika safari ya kuwa askari wa Mungu kwenye shamba lake, jua tu utakumbana na changamoto nyingi ikiwemo kukatishwa tamaa, na kibaya zaidi watakao kukatisha tamaa sio watu wengine bali ni hao askari wenzako waliokutangulia katika hilo shamba, kama vile tu Daudi alivyokatishwa tamaa na wale ndugu zake, walimwambia ana kiburi, na wakataka kumfukuza arudi kuchunga mbuzi za baba yake, lakini Daudi alipuuzia.
Vivyo hivyo inawezekana umesikia wito wa kumtumikia Mungu, watu wa kwanza utakaokutana nao na kukuvunja moyo hawatakuwa watu wasiomjua Mungu bali ujue tu watakuwa ni hao waliokutangulia katika kazi ya Bwana, sio kana kwamba ni watumishi wa shetani la! lakini ndivyo ilivyo, pale utakaposema tu nataka kumtumikia Mungu utasikia “ni chuo gani cha biblia umepitia wewe? “…utaulizwa “umepitia kwanza chini ya huduma ya nani mpaka wewe utake kumtumikia Mungu”..
Utasikia wenye ujuzi wameshindwa wewe ni kama nani, hata biblia huijui vizuri, kwanza ndio umeokoka juzi tu, mchanga wa kiroho, walau hata ungekuwa umepitia kwanza mafunzo fulani ndio uanze..na vitu vinavyofanana na hivyo vya kukatishwa tamaa vingi vitakuja, lakini fahamu kuwa huyo ni shetani akitaka kukatisha tamaa usisonge mbele, kama vile Daudi hakutumia uzoefu unaofanana na wao kumuua Goliathi bali alitumia uzoefu Mungu aliomshindania katika maisha yake aliyokuwa anapitia katika ufugaji wake..na kwa kufanya vile aliweza hata kuwa shujaa, kushinda hata wale askari waliokuwa wanajiona wenye uzoefu mwingi na kupitia mafunzo mengi ya vita kabla yake.
Inawezekana una wito fulani wa kumtumikia Mungu, lakini kulingana na mazingira ya watu waliokutangulia katika huduma yanakufanya ujione kama haustahili, kwasababu haujapitia chuo cha biblia, au hujaenda shule, au hujakaa chini ya mtumishi yeyote unajiona hauwezi, fahamu jambo moja kuwa “UNAWEZA katika yeye akutiye nguvu“..Kwamba unasikia wito wa Mungu ndani yako, kaza mwendo, uendee na Mungu atakuwa na wewe
Kumbuka kama Daudi alivyotumia ujuzi wa mambo yaliyopita ya maisha yake na kumhesabia Mungu kuwa anaweza kumpigania hata sasa na wewe vivyo hivyo kumbuka mambo yote ambayo uliona kabisa Mungu alikupigania kama sio yeye ungekwama, au kama sio yeye usingukuwepo leo, tumia huo huo uzoefu Mungu aliokuonekania katika maisha yako uulete katika kazi ya Mungu. Mungu yule yule aliyekupigania kule ndio huyo huyo atakayekupigania kwenye kazi yake.
Watakao mwangusha Goliathi(shetani) kwenye kanisa hili la mwisho hawatakuwa wanaodhaniwa kuwa wamekuwa katika huduma kwa muda mrefu, bali watakuwa ni vijana(wa kiroho) kama wakina Daudi wenye ufunuo, ambao watamwamini Mungu katika utimilifu wake wote. Hao wengine wataua wafilisti tu lakini Goliathi ni kwa Daudi.Kwa maana Bwana Yesu alisema,
Mathayo 11:25-26 ” Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako.
Na pia alisema..Mathayo 20:16 “Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho. “
Hivyo ndugu ni wajibu wetu kusonga mbele pasipo kukwazwa na jambo lolote, usitazame mpaka upate kitu fulani ndio ufanye kitu kwa ajili ya Mungu. 2Wakorintho 6:2 (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa)
Ni maombi yangu Bwana atupe neema hiyo ya kuwa mashujaa wake kama Daudi.
Mungu akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa maombezi/Ushauri/Ubatizo/ Whatsapp. Tupigie namba hizi: +255693036618
Mada Nyinginezo:
WAKATI WA JIONI KUTAKUWAKO NA NURU
About the author