MANA ILIYOSHUSHWA KUTOKA MBINGUNI.

MANA ILIYOSHUSHWA KUTOKA MBINGUNI.

Katika agano la kale, wakati wana wa Israeli wakiwa safarini kuelekea nchi ya ahadi, walioahidiwa na Mungu mwenyezi, tunaona Bwana Mungu, alijua shida iliyokuwa mbele yao kwamba watapita katika nchi ya jangwa isiyokuwa na kitu, isiyokuwa na kupanda wala kuvuna, nchi kame, hivyo alikuwa ameshawaandalia namna ya kuwalisha kabla hata hawajatoa miguu yao Misri, na ndio tunaona, aliwashushia MANA itokayo juu mbinguni, lakini Bwana alikuwa na sababu kubwa sana ya kufanya vile, kutowapitisha njia yenye chakula tele, au yenye masoko ambayo wangeweza kununua chakula.

Sasa moja ya muujiza mkubwa wa ile mana, ni kwamba haikuwa mikate kama mikate, hapana bali zilikuwa ni chembe ndogo kama za mtama, ambazo walipoamka kila asubuhi walizikuta juu ya ardhi, na walipozikusanya walienda kuzisaga, na kuwa unga kisha kuzitengeneza kuwa mkate.

Wale waliokusanya mana nyingi, waliwapunguzia wale waliokusanya vichache hivyo hakuna aliyemzidi mwenzake…

Kutoka 16:14-18” Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi.

15 Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao Bwana amewapa ninyi, mle.

16 Neno hili ndilo aliloagiza Bwana, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi,kama hesabu ya watu wenu ilivyo ;ndivyo mtakavyotwaa,kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake.

17 Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua.

18 Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa”

Sasa jambo tunaloweza kujifunza hapo, ni kwamba Bwana alitaka kuwafundisha watu wake kwamba waishi kama ndugu, wahudumiane kila mtu na nduguye, mmoja anapokusanya kingi na mwingine anapokusanya vichache, yule mwenye nyingi ampunguzie yule mwenye vichache, kwasababu wamepewa bure.

Jambo hilo hilo linaendelea sasa katika Roho, kama vile wana wa Israeli walipewa mana ya mwilini kuwafanya waishi kule nyikani, leo hii Bwana Mungu ametoa MANA YA ROHONI kutufanya sisi tuishi katika Jangwa hili la Roho, na kama vile mana ile ilishuka tu kwa wana wa Israeli na sio watu wote wa ulimwengu mzima, vivyo hivyo na mana hii ya sasa ya Rohoni, itawafaa wale tu, waliokuwa tayari kuchukua gharama za kutoka Misri(ya rohoni) na kuelekea kaanani.

SASA HII MANA NI IPI?

Hii mana mpya si mwingine Zaidi ya BWANA WA UTUKUFU, YESU KRISTO. Biblia inasema katika…

Yohana 6: 28 “Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu?

29 Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.

30 Wakamwambia, Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani?

31 Baba zetu waliila mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale.

32 Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni.

33 Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.

34 Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki.

35 Yesu akawaambia, MIMI NDIMI CHAKULA CHA UZIMA; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe”.

Unaona hapo? Bwana Yesu ndio chakula cha uzima, mfano wa mana, sasa aliposema chakula hakumaanisha vyakula vya kupikwa na wanadamu, hapana! Ukisoma katika tafsiri nyingine za kiingereza tafsiri hapo ya chakula ni “bread” yaani “mkate”John 6: 35”Then Jesus declared, “I am the bread of life. Whoever comes to me will never go hungry”

Hivyo kama vile, MANA ilivyokuwa inaliwa na wana wa Israeli siku kwa siku, vivyo hivyo Mana hii mpya ya rohoni tuliyopewa na Baba, tunaila siku baada ya siku, ikiwa na maana kuwa, tunajifunza maneno ya YESU KRISTO siku kwa siku, hatuachi mpaka siku tutakayoingia kaanani yetu(mbingu mpya na nchi mpya).

Ndio maana tunashiriki meza ya Bwana,(divai na mkate) kipindi baada ya kipindi, kuashiria kuwa katika roho zetu tunakula maneno ya Yesu Kristo siku kwa siku.

Na kama vile ile mana si wote waliokota kwa kipimo kimoja, wengine waliokota kingi wengine pungufu, lakini aliyeokota vingi alimpunguzia yule aliyeokota vichache, vivyo hivyo na katika MANA hii ya rohoni, tumepewa agizo la kukusanyika pamoja ili Bwana atuhudumie Neno lake kila mtu kwa kipimo cha karama alichomkirimia, na ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana wa kukusanyika pamoja.

Tunakuwa tunaula mwili wa Yesu kristo ambaye ndiye chakula kitokacho mbinguni siku baada ya siku. Na ndio maana Bwana aliendelea na kusema ..

Yohana 6: 48 “Mimi ndimi chakula cha uzima.

49 Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa.

50 HIKI NI CHAKULA KISHUKACHO KUTOKA MBINGUNI, KWAMBA MTU AKILA WALA ASIFE.

51 Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.

52 Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, AWEZAJE MTU KUTUPA SISI MWILI WAKE ILI TUULE?

53 Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, MSIPOULA MWILI WAKE MWANA WA ADAMU NA KUINYWA DAMU YAKE, HANA UZIMA NDANI YENU. 

54 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.

55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.

56 AULAYE MWILI WANGU NA KUINYWA DAMU YANGU HUKAA NDANI YANGU”.

Umeona Umuhimu wa Yesu Kristo kwa wakati huu? Wana wa Israeli wasingeweza KUFIKA KAANANI pasipo kupitia njia ya jangwa Mungu aliyoikusudia wala pasipo kuila MANA chakula Mungu alichokichagua, Kadhalika na wakati huu wa sasa Hutuwezi kufika mbinguni pasipo kupitia njia ya jangwa wala pasipo kuila ile mana ya rohoni Mungu aliyoikusudia (yaani Yesu Kristo).

Njia zipo nyingi ndugu, lakini njia pekee ya kumfikia Mungu ni Yesu Kristo ndiye, na yeye alisema mwenyewe,..

Mathayo 16: 24 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.

25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. 

26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? “

Chukua gharama ya kutoka katika utumwa wa dhambi (Misri) na ingia gharama za kumfuata Bwana YESU katika njia ya jangwa kama unataka kufika mbinguni. Huko katika kaanani ya watakatifu, hawataingia waasherati, hawataingia walevi, hawataingia wasengenyaji, hawataingia wauaji, hawataingia wavaaji wa vimini wala wapakaji wanja wala watoaji mimba, hawataingia mashoga,wala watazamaji pornography, wala wasiosamehe, hawa wote sehemu yao itakuwa ni katika lile ziwa la moto biblia inasema hivyo. Wanaokuambia utaingia mbinguni kwa kufanya vitu hivyo wanakudanganya hawana haja na roho yako, wanataka vya kwako.

Hivyo geuka leo, ukatwae mkate wa uzima (Yesu Kristo). Mkate unaoshiriki kule kanisani, halafu bado ni muasherati, utapata hatia juu ya mwili wa Yesu Kristo na damu yake, kwasababu unashiriki isivyopasa.

1 Wakorintho 11: 23 “Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate,

24 naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.

25 Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.

26 Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.

27 Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana ISIVYOSTAHILI, ATAKUWA AMEJIPATIA HATI YA MWILI NA DAMU YA BWANA. 

28 Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe.

29 Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili.

30 Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala.

31 Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa”.

Hivyo kula mana sasa, na hii hatuipati pengine mbali na pale wana wa Mungu wakusanyikapo.

Ubarikiwe.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

CHAKULA CHA ROHONI.

TABIA ZA ROHONI.

NI HALALI KUBATIZA WATOTO WADOGO?

KUNA HUKUMU ZA AINA NGAPI?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments