UTIMILIFU WA TORATI.

UTIMILIFU WA TORATI.

Tukisoma Agano la Kale, biblia inaelezea maisha ya watumishi wake, jinsi walivyokuwa na jinsi walivyoishi. Tunajua kabisa wengi maisha yao hayakukamilika, kwasababu torati waliyopewa isingeweza kuwakamilisha na kuwa wakamilifu, Kwasababu torati yenyewe haikutimilika..

Ndio maana utamwona Mtu kama Daudi aliyependwa sana na Mungu, alioa wake wengi, na mwanawe Sulemani alikuwa na wake wengi vile vile. Utamwona Daudi mtu aliyeupendeza Moyo wa Mungu alikuwa anaua, na aliua watu wengi na bado BWANA hakumuhesabia makosa.

Utamwona Daudi hakubatizwa lakini bado alikuwa ni mtu anayeupendeza moyo wa Mungu. Alikuwa anashindana na kuwatakia shari maadui zake, na kuwachukia lakini bado alikuwa ni mteule wa Bwana.

Sasa kwa jicho la haraka haraka unaweza ukasema, kama Daudi alikuwa ana wake wengi, alikuwa anawashambulia na kushindana na maadui zake, alikuwa anaua na bado ni mtumishi wa Mungu, na mimi sio vibaya nikifanya hayo hayo na bado kwani Mungu atakuwa na mimi. Ni rahisi kusema hivyo.

Lakini ningependa ufahamu kitu kimoja, agano la kale(au agano la kwanza) lilikuwa sio utimilifu wa mambo yote…lilikuwa ni muhtasari tu wa Agano halisi la Mungu. Na ndio maana Bwana Yesu alisema katika..

Mathayo 5:17 “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.”

Unaona hapo? Bwana alikuja KUITIMILIZA, yaani kuifanya ieleweke vizuri…yaani ikiwa na maana kuwa, Torati iliposema USIUE, Haikumaanisha tu kumkamata mtu na kuutoa uhai wake bali iliimanisha kwanza USIMCHUKIE KABISA NDUGU YAKO, Vivyo hivyo Torati iliposema USIZINI, Haikumaanisha tu kwenda kufanya zinaa ya nje, hapana bali ilimaanisha pia MTU HATAKIWI KUTAMANI KABISA NDANI YA MOYO WAKO. Kwahiyo unaweza ukaona hapo kutoka “kuzini” mpaka “kutokutamani” huko ni kukitimiliza kile kipengele kilichosalia..kwasababu Torati asili yake ni Rohoni.

Hivyo Daudi na watakatifu wa agano la kale walipokuwa wanaua hawakuwa wanafanya jambo lililosahihi, ingawa kwa wakati ule Bwana aliruhusu wafanye vile kwasababu wakati wa Utimilifu wa Torati, ulikuwa bado haujafika.

Kadhalika Daudi, na Sulemani mwanae, na watakatifu wote wa Agano la kale walipooa wake wengi, walikuwa hawafanyi jambo lililo sahihi machoni pa Bwana, ilikuwa sio mpango kamili wa Mungu wawe na wake na wengi, Lakini Bwana aliliruhusu waendelee kuoa wake wengi na kutoa talaka,hivyo hivyo mpaka UTIMILIFU utakapofika.

Watakatifu wa agano la kale, walikuwa wanaapa, lakini hayakuwa ni mapenzi ya Mungu mwanadamu yeyote aape, lakini Bwana aliwaruhusu waendelee kufanya hivyo mpaka wakati wa Utimilifu utakapofika. Na mara nyingine aliruhusu ifanyike hivyo kwasababu tu ya ugumu wa mioyo yao.

Ndipo wakati wa UTIMILIFU ulipofika, Mungu alimtuma mwanawe mpendwa Yesu Kristo ili kuhubiri UTIMILIFU wote WA TORATI.

Na ndio hapo Bwana Yesu alisema..

Mathayo 5:21 “Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.

22 Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto”.

Mathayo 5:27“Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; 28 lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake”.

Mathayo 5.33 “Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako;

34 lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;

35 wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu.

36 Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.

37 Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu”

Mathayo 5:38“Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino;

39 Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili.”

Kaka/dada unayesoma haya, UMESIKIA kwamba imenenwa unaweza ukaokolewa tu, maadamu unatenda mema, na kuzishika amri 10 za Mungu, lakini Kristo anasema.. Mtu hawezi kuuona ufalme wa mbingu, asipozaliwa mara ya pili.

Na tena umesikia mahali wanasema ubatizo sio wa lazima, mbona hata Daudi hakubatizwa lakini Mungu alimkubali, Ndugu usiamini huo uongo leo KRISTO ANAKUAMBIA… “AAMINIYE NA KUBATIZWA ATAOKOKA ASIYEAMINI ATAHUKUMIWA” (Marko 16:15-16).

Umeona hapo? Anasema asiyeamini atahukumiwa, Ndugu yangu usipoamini na kubatizwa utahukumiwa, hayo ni maneno ya Mkuu wa Uzima mwenyewe YESU KRISTO, Na yeye hawezi kusema uongo.

Inawezekana mahali Fulani umesikia mtu Fulani akikuambia kwamba unatakiwa umfuate Yesu tu, kwa wepesi usijiweke rehani saana..Lakini yeye anakwambia leo

Luka 9:23-25 “..Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?.”

tena umesikia mahali pengine wakisema kuwa ni ruksa kuwa na wake wengi au waume wengi..lakini kristo mtimilifu wa torati anakuagiza leo maneno haya

Luka 19: 9 “nami nawaambia ninyi, kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini…..

7 wakamwambia, jinsi gani basi musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?

8 akawaambia, musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi”.

Tena umesikia dhehebu Fulani likisema, mtu akifa leo hupitia kwanza TOHARANI kutakaswa dhambi zake kisha atakwenda mbinguni, na wengine wanasema mtu akifa amekufa wala hakuna kiyama ya wafu. Lakini Bwana Yesu anasema “27 Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;(Waebrania 9:27)”. Unaona? Usidanganyike ndugu kufanya ibada za wafu, au kuwaombea wafu, wala usidanganyike kuwa ukifa leo ni unapotea tu kama wale masadukayo walivyokuwa wanaamini. Fahamu kuwa ukishakufa wewe utakuwa ni wakusubiria hukumu aidha peponi au jehanum, Hivyo usikubali kusikiliza hadithi za kutungwa, zitakazokufanya ustarehe katika dhambi zako ukidhani kuwa kuna nafasi ya pili uko uendako, au kuna kupotea tu hakuna hukumu.

Ndugu, mtii YESU KRISTO leo, usiseme kwasababu Daudi alikuwa na wake wengi, basi na wewe ndio uwe na wake wengi, usiseme kwasababu Daudi hakubatizwa na wewe usiutafute ubatizo leo, usiseme kwasababu Daudi alikuwa anashindana na maadui zake na kuwaua na wewe leo ukatafute kuwaangamiza wale wanaokuchukia.. usifanye hivyo mtimilifu wetu yesu kristo ndiye anayetuagiza tusifanye hivyo. tusishindane na watu waovu, wala tusijilipize kisasi. sio kila njia ya watakatifu wa agano la kale ilikuwa ni kamilifu, mtazame YESU Kristo yeye ndiye njia na kweli na uzima. na ndiye aliyepakwa mafuta kutufundisha maneno ya uzima. huyu yesu kristo ndiye aliyefanyika bora kuliko wanadamu wote na malaika wote..na ndio maana ile sauti ilitoka mbinguni na kusema… “huyu ndiye mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”.

Waebrania 2: 1 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi,

2 mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika mwana [yesu kristo], aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.

3 yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa ukuu huko juu;

4 amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao.”

Mwamini YESU uokolewe hizi ni saa za majeruhi.

ubarikiwe

tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na mungu atakubariki.


Mada Nyinginezo:

UBATIZO SAHIHI

MVUTO WA TATU!

ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO

NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments