JIFANYIE RAFIKI KWA MALI YA UDHALIMU.

JIFANYIE RAFIKI KWA MALI YA UDHALIMU.

Shalom! Mwana wa Mungu, Karibu tujifunze Neno la Mungu, ambapo leo tutajifunza somo lenye kichwa kinachosema “Tujifanyie rafiki kwa Mali ya udhalimu”. Somo hili linatoka katika kitabu cha Luka 16:1-10, Ni Mfano ambao Bwana aliutoa kwa wanafunzi wake wakati fulani, akifananisha hekima ya wana wa Ulimwengu huu wasiomjua Mungu (walio wadhalimu), wanavyotumia Busara katika kuamua Mambo yao ya kidunia..Na sisi jinsi tunavyopaswa kutumia hekima na Busara katika kuamu hatima yetu ya maisha ya umilele zaidi yao.

Biblia inasema:

Luka16 : 1 “Tena, aliwaambia wanafunzi wake, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake.

2 Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena.

3 Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya.

4 Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao.

5 Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu?

6 Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini.

7 Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani? Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini.

8 Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.

9 Nami nawaambia, Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele.

10 Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia.

11 Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli?

12 Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?”.

Ili kuufanya mfano huu ueleweke vizuri tunaweza kuufupisha hivi,

“Kulikuwa na mtu mmoja Tajiri, aliyekuwa na meneja wake, wa kusimamia mzunguko wa fedha za biashara yake pamoja na shughuli zake zote alizokuwa nazo, lakini ulifika wakati yule meneja hakuwa mwaminifu, akawa anaanza kutapanya fedha za Yule Tajiri wake (mwajiri wake),anachukua faida iliyopatikana na kutumia kwa anasa zake mwenyewe, Na hivyo ikapalekea kuleta hasara kubwa kutokana na matumizi mabaya ya zile fedha, Lakini siku moja ikafika waajiriwa wengine wakagundua anachokifanya wakampelekea taarifa Yule boss wao mkubwa kwamba Meneja wako ana matumizi mabaya ya fedha., Hivyo Yule tajiri alipochunguza akagundua ni kweli yule mtu alikuwa na matumizi mabaya, akamwita Yule Meneja na kumwoji, ikawa wazi kuwa alikuwa ni mtu ambaye sio mwaminifu hivyo kilichobaki ni kufukuzwa kazi tu, hakuna lingine.

Lakini kwakuwa Yule Meneja alikuwa na Busara hata katika hali yake ya utapanyaji wa fedha, alijua tayari hata iweje kibarua hana tena,na Bosi wake kashamchukia hivyo ikambidi atafute namna ya kujipatanisha na wale Wadaiwa wa Bosi wake,wale matajiri ili siku atakapoishiwa kabisa, wale wadeni wa Bosi wake wasimtupe,wamfadhili, angalau wawe wanamkaribisha majumbani mwao, na hata kama kutatoke fursa yoyote wamkumbuke ili asiwe omba omba huko mtaani, mtu asiyekuwa na msaada, wa kudharauliwa na kila mtu.

Kwahiyo alichokifanya Yule Meneja ni kwenda kuchukua baadhi ya zile mali chache alizobakiwa nazo na alizojilumbukizia na kuwatafuta wale watu wote waliokuwa wanadaiwa na Yule Tajiri wake…Kama kuna aliyekuwa anadaiwa lita 1000 za mafuta , alimlipia lita 500, na kumwachia zile nyingine 500 zilizosalia ajilipie mwenyewe, na Mwingine kama alikuwa anadaiwa magunia 100 ya ngano alimlipia magunia 20 na kuacha yale 80 yaliyosalia ajilipie mwenyewe ”..Hivyo wale watu wote waliopunguziwa mzigo wa Madeni yao walimpenda sana Yule Meneja kwa vile alivyowapunguzia mizigo yao, hata ingekuwa ni wewe unapewa misamaha ya madeni yako usingeacha kumfurahia huyo anayekupa ofa hiyo. kwahiyo alijua hata kama akiondolewa katika Umeneja wake, siku atakapoishiwa kabisa yupo mtaani hawatamtupa kwasababu aliwasaidia katika shida zao.

Na Yule Tajiri alipopata taarifa za busara za Yule Meneja wake dhalimu alimsifu ijapokuwa alimwibia fedha nyingi lakini zile fedha alikwenda kuzitumia kuwapunguzia madeni wale aliokuwa anawadai..Kwahiyo hata kama alikuwa hataki kumsamehe kwa kitendo kile pengine siku hasira yake ikipoa anaweza kumrudisha tena kwenye kazi yake ya Umeneja” Haleluya.

Mfano huo Bwana alioutoa unatufundisha nini? Kwamba Na sisi tuwe na Hekima kuliko hata watu wa ulimwengu huu, ya kufahamu kuwa, tutakachokifanya leo kinachompendeza Yeye tutapata malipo yake baadaye.

Tutakachomfanyia Bwana Yesu leo hii katika dunia hii, kiwe kizuri au kibaya kitakuja kuwa na malipo yake katika ulimwengu ujao,.

Leo hii umepata chochote aidha ni mali, chakula, mavazi, makazi, uzima, uwezo au chochote kile na umepata kwa njia yoyote ile..hiyo ni kama “mali ya udhalimu mbele za Mungu”..Nenda kawatafute wale watu ambao hawanakabisa hivyo vitu (Hususani walio Wakristo) wapatie, wale watumishi wa Mungu unaojua ni waaminifu, sio lazima uwapatie vyote, hapana bali sehemu tu, angalau asilimia 20 au zaidi, Hiyo ni sawa umewalipia madeni wale wanaodaiwa na Mungu..

Kwasababu siku zinatakuja katika Mbingu Mpya na Nchi Mpya, hao waliokuwa na uhitaji leo (wanaomcha yeye), watairithi nchi, watakapopewa ufalme, na mamlaka..Watakukaribisha katika makao ya Milele hata kama haukuwa mkamilifu kwa viwango vile vinavyotakiwa, watakutaja mbele za Bwana na kukukaribisha katika makao ya Milele, kwasababu walipokuwa wapo uchi, uliwavisha nguo,walipokuwa na kiu uliwanywesha maji, walipokuwa na njaa uliwapa chakula, walipokuwa wagonjwa ulikwenda kuwatembele, walipokuwa na uhitaji uliwasaidia..Na kwasababu uliwasaidia hao basi ni sawa na ulimsaidia Kristo Mwenyewe.

Mathayo 25: 31 “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake;

32 na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;

33 atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.

34 Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu;

35 kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha;

36 nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.

37 Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuonauna njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha?

38 Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika?

39 Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia?

40 Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi”

Je! Na wewe umemtendea Kristo nini?..Kwasasa yupo Mbinguni, hahitaji fedha wala mavazi wala haumwi, wala hayupo kifungoni…Lakini yupo ndani ya watu wengi walio kifungoni, wanaohitaji mavazi, wanaohitaji chakula n.k n.K..Nani atakayekuwa mtetezi wako siku ile??..Kitakapokosekana kila kitu cha kukuvukisha ng’ambo kule?? Ni nini kitakachokutetea basi? Kama leo hii hujifanyii urafiki kwa mali ya udhalimu? Siku ile Utaangukia kwenye hili kundi..

Mathayo 25: 41 “Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;

42 kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe;

43 nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama.

44 Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe u

na njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie?

45 Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi.

46 Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele”

Mtetezi wako atakuwa ni nani siku ile?

Wakati Fulani vita vilipotokea katika Israeli, na Israeli walipokuwa wanakawia kawia kwenda kupigana na Maadui zao wafilisti,Yonathani aliyekuwa mwana wa Mfalme Sauli, Mungu alimtia Moyo wa Ushujaa na kwenda kuvamia kambi ya wafilisti na kuishinda ile vita, Hivyo Yonathani akawa ameleta wokovu na ushindi katika ile vita siku ile, lakini Baba yake (ambaye ni Mfalme Sauli). Alitoa amri kwa kiapo mbele za Mungu kwamba mtu yoyote asile chochote mpaka jua litakapozama, na yeyote atakayefanya hivyo amri ilitolewa auawe. Na kiapo hicho Mungu akakisikia na akakithibitisha, hivyo Israeli wote hawakula siku hiyo chochote ingawa walikuwa na njaa kali ya kuishiwa nguvu kabisa, lakini wakati anatoa hiyo amri Yonathani mwanawe ambaye ndiye aliyekuwa sababu ya ushindi wa vita hakuwepo muda huo, hivyo hakuisikia hiyo amri, na wakati anapita porini alikutana na sega la asali, akala!. Na baba yake hakujua, na ilipopita muda kidogo Baba yake akaenda kumwuliza Mungu habari za kwenda kuteka nyara za wafilisti Mungu hakumjibu. Ndipo alipogundua kuwa kuna kosa limefanyika mbele zake, ndio maana Mungu hajibu chochote, na wakatumia Urimu kumuuliza Mungu ndipo ikajulikana kuwa na kugundua kuwa ni mwanae Yonathani ndiye aliyevanja kiapo kile kwa kula asali wakati wa vita.

Hivyo Yonathani akawa katika hatari ya Kufa, kwasababu ndiye Mungu aliyemteua afe kutokana na kile kiapo cha Baba yake. Kumbuka Yonathani aliyekuwa sababu ya kushinda vita sasa ndiye anayepaswa kufa, Lakini tunasoma nini??, Kwa wema wake alioutenda hata kuwapa furaha na wokovu Jeshi la Israeli, shauri lake la kufa likabatilishwa, Ile hati ya mashtaka mbele za Mungu ilibadilishwa. Watu wakamwokoa Yonathani mbele ya ghadhabu ya Mungu na ya baba yake.

1 Samweli 14: 42 “Basi Sauli akasema, Sasa piga kati ya mimi na mwanangu Yonathani, [naye awaye yote ambaye Bwana atamtwaa, atakufa. Nao watu wakamwambia Sauli, La! Sivyo hivyo; lakini Sauli akawaweza watu. Nao wakapiga kati ya yeye na mwanawe Yonathani,]

43 Ndipo Sauli akamwambia Yonathani, Niambie ulilolifanya. Basi Yonathani akamwambia, akasema, Nikweli, mimi nalionja asali kidogo kwa ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwangu; na tazama, imenipasa kufa.

44 Naye Sauli akasema, Mungu anifanyie hivi, na kuzidi; kwa kuwa hakika utakufa, Yonathani.

45 Walakini watu wakamwambia SAULI, JE! ATAKUFA YONATHANI, AMBAYE NDIYE ALIYEUFANYA HUO WOKOVU MKUU KATIKA ISRAELI? HASHA! AISHIVYO BWANA, HAUTAANGUKA CHINI HATA UNYWELE MMOJA WA KICHWA CHAKE;

kwa maana ametenda kazipamoja na Mungu leo. HIVYO HAO WATU WAKAMPONYA YONATHANI, ASIFE”

Na ndivyo itakavyokuwa siku ile kwa mema wale wachache watakayowatendea watu wa Mungu, ndio yatakayowaepusha na adhabu ya Milele, watakatifu watakuwa watetezi wao siku ile, lakini kwa wema wao waliowatendea watu wa Mungu (wataokolewa siku ile). Yonathani alijifanyia urafiki kwa mali ya udhalimu ili ilipokosekana hata kama alistahili kufa watu walimponya. Ni matumaini yangu Bwana atazidi kutujalia kuyaona hayo siku zote za maisha yetu.

Mungu akubariki

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

 

 

 


Mada zinazoendana


MWINUE YESU KRISTO KATIKA MAISHA YAKO.

JIANGALIENI BASI JINSI MSIKIAVYO.

TUKAZE MWENDO KWA TULIYOANDALIWA.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments