NDOA NA HARUSI TAKATIFU.

NDOA NA HARUSI TAKATIFU.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, Mkuu wa Uzima libarikiwe. Karibu tujifunze Neno la Mungu, ikiwa ni mwendelezo wa mafunzo ya ndoa ambapo leo tutajifunza juu ya ndoa takatifu jinsi inavyofungwa ..kwa kufuata misingi ya kimaandiko.

Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa kuna ndoa za aina mbili, kuna ndoa zetu sisi wanadamu, zinazohusu mwanaume na mwanamke, na Pia kuna ndoa ya kimbinguni inayomuhusu Yesu Kristo na Kanisa lake. Na ndoa ni kitu cha kimaandiko kabisa na ni mpango wa Mungu kamili. Na shetani siku zote hapendi ndoa takatifu inayofungishwa na Mungu mwenyewe, kwasababu anajua itamzuilia mambo yake mengi maovu ambayo angeweza kuyafanya kwa mtu husika au jamii kama ndoa isingekuwepo. Na ndio maana biblia inasema katika siku za mwisho “yatatokea mafundisho ya uongo ya kuwazuia watu wasioe” Tutaelewa jambo hili kwa undani zaidi kwa jinsi tunavyoendelea kujifunza.

Tukianza kwa kuzizungumzia kwa ufupi ndoa zetu za kibinadamu; Kwanza ni lazima ziwe na utaratibu, kwasababu Mungu ni wa utaratibu, ndoa ya kwanza ilifungishwa Edeni na Mungu mwenyewe, lakini unaona Mungu alikuwa na utaratibu katika kuifungisha ile ndoa..Tunaona alimwumba kwanza Adamu ambaye ni mwanaume kabla ya Hawa kufunua kuwa mwanamume ndiye kiongozi wa ile ndoa, na kabla hajamwumba Hawa, alimpa Adamu Majukumu ya kuilima na kuitunza Bustani, ili mkewe ajapo akute kila kitu kipo tayari, awe kama ni msaidizi tu, na sio aanze kuteseka nayeye kufanya hivi na vile. Kwahiyo unaona huo ni utaratibu mzuri, kwamba mwanamume akitaka kwenda kuoa ni sharti aandae mazingira ya atakapomweka mke wake na tayari awe ameshajiweka tayari kiakili kwa majukumu yaliyopo mbele yake.

Hivyo baada ya ndoa ya kwanza kufungishwa na Mungu mwenyewe utaratibu ulibadilika haikuwezekana tena ndoa nyingine zinazofuata wanawake watoke kwenye ubavu wa mwanamume, au Mungu atoe maagizo moja kwa moja tena kutoka mbinguni kama hapo kama kwanza, hapana bali ni lazima watu wazaliwe..kwahiyo mwanadamu akapewa jukumu na uwezo wa kutengeneza mwanadamu mwingine kutoka katika tumbo lake na viuno vyake. Hii ikiwa na maana pia azisimamie kwa utaratibu ndoa zote zitakazofuata mbele yake, kwamba zizaliwe kupitia kwenye mikono ya ya watu wa Mungu, kwamba lazima ndoa ihalalishwe mbele za Mungu kwa kupitia watu.

Hivyo huo utaratibu ukaendelea hivyo vizazi na vizazi, mwanamume anapotaka kumwoa mwanamke ni lazima ataratibu ufuatwe, kwanza wazazi washirikishwe, na sheria za Mungu zihusike ndipo hiyo ndo iwe halali. Sio sawa na sio jambo la kimaandiko kabisa watu wawili kuchukuana pasipo utaratibu wowote na kuishi pamoja na kusema wameonganishwa na Mungu, hapo hawajaunganishwa na Mungu bali shetani. Kwasababu Mungu ni Mungu wa utaratibu. Adamu hakumwona Mzazi kwasababu alikuwa hana wazazi, na kadhalika Hawa…Lakini baadaye unaona Mungu anasema “mwanamume atamwacha babaye na mamaye na kuungana na mkewe nao watakuwa mwili mmoja”. Kumwacha pale mzazi sio kumwacha kwa shari bali kwa heri..

Kuna usemi unaosema kuwa Agano la kale hakukuwa na utaratibu wa kuoa..na hivyo watu walikuwa wanajitwalia wake tu! manabii walikuwa wanajitwalia wake, usidanganyike ndugu, utaratibu ulikuwepo. Na leo tutaenda kujifunza huo utaratibu.

Katika desturi za kiyahudi (yaani waisraeli) utaratibu wa ndoa ulikuwa kama ifuatavyo. Kulikuwa na hatua mbili kuu za ndoa, ilikuwa baada ya mwanamume kumpenda mwanamke na kutaka kumwoa, anakwenda kutoa taarifa kwa wazazi wake, na kisha wazazi wake wanakwenda nyumbani kwa mwanamke na kuzungumza na wazazi wa mwanamke, na endapo wazazi wakiridhia hatua nyingine zinafuata.

Hatua ya kwanza ni KUPOSA: Hatua hii inahusisha mwanaume Pamoja na washenga, kutoka kwao na kwenda nyumbani kwa mwanamke, ambapo watatoa mahari, kufanya karamu ndogo, na kikubwa zaidi WATABADILISHANA VIAPO na kuwekeana mkataba kwamba watakuwa waaminifu wote wawili mpaka siku Harusi itakapofungwa. Hivyo baada ya kukamilisha hiyo hatua, mwamume na mwanamke wanakuwa wamefungwa na hicho kiapo, mpaka siku ya Harusi yenyewe itakapofika.

Hapo mwanamume anakuwa huru kurudi kwao, na kuendelea kutengeneza maisha yake, ataendelea kuandaa nyumba ya kumweka mkewe, kama alikuwa hana, na mambo mengine ya muhimu ya kifamilia, na hapaswi kuwa na mahusiano na mwanamke mwingine yeyote, na mwanamke naye ni hivyo hivyo, hapaswi kujihusisha na mahusiano yoyote na mwanamume mwingine, na katika kipindi hichi pia wapendwa hawa wawili hawapaswi kukutana kimwili kabisa (yaani kufanya tendo la ndoa)..Mpaka siku ya harusi itakapofika, ingawa wana ruhusa ya kuitwa mume na mke, Na kipindi hichi cha matengano kinaweza kikadumu kwa miezi kadhaa au hata zaidi ya mwaka, inategemea na hali ya kimaisha ya mwanamume.

Kipindi hichi ndicho kipindi ambacho Mariamu alionekana ana mimba, ya Bwana Yesu Kristo, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, baada ya kuposwa na Yusufu.

Na hatua ya PILI inayofuata baada ya KUPOSWA Ni Harusi yenyewe. Katika siku hiyo ya arusi, Mwanamume atatoka kwao pamoja na kundi la wanaume wenzake, na ndugu zake wakiume atakwenda kwa matarumbeta na shangwe nyumbani kwa mwanamke, na kisha atamchukua mwanamke na kwenda naye nyumbani kwa mwanamume (kwa Baba wa mwanamume) na kule watakwenda tena kurudia vile VIAPO walivyotoa wakati wa kuposa. Na watakuwepo Marabi ambao watasoma maandiko machache ndani ya TORATI, yanayohusiana na ndoa Na baada ya kufanya hivyo hiyo ndoa inakuwa ni halali na Takatafu na inabarikiwa. Na mfano wa mazungumzo hayo ni huu:

Mwanzo 24: 57 “Wakasema, Na tumwite huyo msichana, tumwulize mwenyewe.

58 Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda.

59 Ndipo wakampeleka Rebeka ndugu yao, na yaya wake, na mtumishi wa Ibrahimu, na watu wake.

60 Wakambarikia Rebeka, wakamwambia, Ndugu yetu, uwe wewe mama wa kumi elfu, mara elfu nyingi, na wazao wako waurithi mlango wa hao wawachukiao.

61 Rebeka akaondoka na vijakazi wake, nao wakapanda juu ya ngamia, wakamfuata yule mtu. Naye huyo mtumishi akamchukua Rebeka akaenda zake”.

Baada ya ndoa hiyo kufungwa, bibiarusi anajitenga na mumewe kwa siri kwa siku saba, ambapo kuanzia hapo wanaruhusiwa kukutana kimwili na kuendelea na mambo mengine.

Huo ndio ulikuwa utaratibu wa ndoa kwa Wayahudi wa agano la Kale, na hakuna mahali popote watu walijitwalia wake kienyeji na kuishi nao, labda tu watu hao wawe si wayahudi.

Sasa Ndoa ya rohoni nayo pia ina utaratibu huo huo.

Bwana Yesu aliacha enzi na Mamlaka mbinguni kwa Baba yake, akalipenda kanisa lake (ambaye ndio mke wake), ubavu wake, akaja duniani ambapo ndio makao ya mke wake yalipo, Na akaliposa kanisa kwa kulitolea mahari, na mahari hiyo ilikuwa ni DAMU yake iliyomwagika pale Kalvari. Na baada ya kulinunua kanisa(ambaye ndio mke wake)..Ilimpasa aondoke arudi nyumbani kwa Baba yake ili kumwandalia mkewe makao, ili baadaye aje kumchukua tena…

Kama ilivyo desturi za wayahudi kwamba ni lazima mwanamume baada ya kuposa aondoke kwa kipindi fulani kwenda kumwandalia mke wake makazi na kisha baadaye aje kumchukua tena kwa shangwe na tarumbeta na nderemo aende kwake, ndivyo Kristo alivyofanya na atakavyofanya, siku atakaporudi mara ya pili kulichukua kanisa lake, naye atarudi kwa parapanda ya Mungu pamoja na kundi la malaika, na kumchukua mkewe kwenda kwenye makao ya Baba yake,(mbinguni) ambapo huko mbinguni kutakuwa na karamu kubwa ambayo haijawahi kutokea..na bibi arusi atakaa na Bwana arusi mbinguni kwa kipindi cha miaka saba, wakati huo duniani kutakuwa na dhiki kuu, na baada ya hiyo miaka saba ya karamu kuisha Bwana Yesu atashuka na kanisa lake, duniani kuja kuitawala dunia na dunia hii itageuka na kuwa mbingu mpya na nchi mpya, wataishi kwa furaha isiyo na kifani milele na milele.

 

Na kama inavyopaswa mwanamke aliyeposwa awe mwaminifu siku zote, wakati mume wake anakwenda kumwandalia makao, ndivyo inavyotupasa na sisi wakristo tunaoishi sasa, wakati tunamngojea Bwana twende mbinguni kwenye karamu tunapaswa kuwa watakatifu na wasafi katika roho zetu, kwa kujiepusha na uzinzi wa kiroho, kama ibada za sanamu, uasherati, ulevi, anasa na mambo mengine yote machafu. Ili ajapo atukute bado ni waaminifu katika lile agano aliloingia nasi pale Kalvari.

Kwahiyo kwa muhtasari huo mfupi unaweza ukaona ndoa iliyo katika utaratibu ni mpango wa Mungu kabisa..kwasababu ndani yake imebeba siri ya Kristo na kanisa lake.

Hivyo katika Ukristo pia, ni lazima hatua za kufunga ndoa zifuatwe, Baada ya mwanamume kumpenda mwanamke, anapaswa awashirikishe wazazi wa pande zote mbili, ili awaache wazazi wake kwa amani, kisha Mahari itolewe kulingana na makubaliano ya pande zote mbili, kama familia ya mwanamke haitaki mahari basi ni sawa, lakini ni lazima wamtoe Binti yao kwa moyo mweupe, Na baada ya mahari mipango ya ndoa inaanza, hapo ni kipindi cha matengenezo inaweza ikawa baada ya wiki,mwezi au hata mwaka inategemea na maamuzi ya upande wa mwanamume, kisha hatua ya mwisho ni kanisani…

Kwaajili ya kubadilishana viapo, sasa viapo vinavyobadilishwa hapa sio viapo vya upumbavu ambavyo biblia imevikataza, kwamba tusiape kabisa, bali viapo vinavyozungumziwa hapa ni viapo vya ahadi, mtu anaahidi kusema ukweli wa moyo wake wote..ambavyo ni lazima mtu aahidi, kuishi na mume wake/mke wake mpaka kifo kitakapowatenganisha, anaahidi kumpenda na kumjali siku zote za maisha yake…viapo hivi ni NADHIRI, na hivyo havina kugeuka nyuma, mtu atakayoyasema kutoka kwenye kinywa chake yanakuwa yanarekodiwa mbinguni, akiyavunja hayo basi atahukumiwa. Baada ya hapo ndipo ndoa hiyo inajulikana mbinguni na kupigwa muhuri.

Lakini ndoa nyingine inayofungwa nje ya utaratibu huo, sio halali mbele za Mungu, wengi hawapendi kuambiwa hivi kwasababu wameshafanya makosa na hawataki kuyarekebisha makosa yao, hivyo wanatetea uovu wao kwa kutumia maneno ambayo hayapo kwenye biblia.

Wewe kama umeishi na mwanamke/mwanamume ambaye mlichukuana tu! pasipo kufuata utaratibu, na ulifanya hivyo kwa kutokujua, ni rahisi tu kujirekebisha, tubu kwa Mungu wako kwa maana yeye anakuhurumia na kukupenda, kisha anza hizo hatua haraka sana, nendeni kwa wazazi wa pande zote, kama huyo mwanamke hana wazazi basi ndugu zake wa karibu,na mwisho kanisani..Mungu atawabariki, lakini kama umesikia na hutaki kutubu kwa kisingizio kuwa ni wapi manabii walifungishwa ndoa..Umekwisha kuusoma hapa utaratibu wa ndoa ulivyokuwa katika agano la kale..kwahiyo siku ile hutasema hukusikia.

Ni maombi yangu kuwa Bwana atakusaidia katika hilo, na pia kama hujampa Bwana maisha yako, nakushauri ufanye hivyo leo, ukubali kujiunganisha na Bwana, Ndoa ya Muhimu na ya msingi ambayo mtu hapaswi kuikosa ni hii ya rohoni (yaani muunganiko wa Kristo na kanisa lake).Kosa hiyo ya mwilini lakini usikose hii ya rohoni, Mpokee leo Kristo na IKUBALI MAHARI YA DAMU YAKE aliyoitoa pale Kalvari, Hakuna mahari kubwa kama hiyo ambayo ilishawahi kutolewa, ni UPENDO WA AJABU SANA, aliouonyesha Bwana, na baada ya hapo ishi katika uaminifu katika hichi kipindi kifupi tunachomngoja arudi, ili atakapokuja tuingie naye karamuni tusifananishwe na wale wanawali wapumbavu ambao Bwana wao alipokuja hawakuwa na mafuta ya ziada na hivyo wakatupwa nje..Hebu kwa kumalizia chukua muda kutafakari mfano huu wa wanawali na ujifunze kitu.

Mathayo 25 : 1-13

“1 Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi.

2 Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara.

3 Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao;

4 bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao.

5 Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi.

6 Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.

7 Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.

8 Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.

9 Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.

10 Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.

11 Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.

12 Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.

13 Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.”

Bwana akubariki.

Tafadhali “share” ujumbe huu na wengine na Bwana akubariki

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

KARAMU YA MWANA-KONDOO.

ALIPO NA ATAKAPOKUWEPO BIBI-ARUSI WA YESU KRISTO.

UNYAKUO.

ULE MFANO WA WANAWALI 10 (MATHAYO 25), YALE MAFUTA YA ZIADA KATIKA CHUPA ZAO YANAWAKILISHA NINI?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Matana levy
Matana levy
2 years ago

Ahsante sana

Luther m majengo.
Luther m majengo.
3 years ago

Thank you