RABONI!

RABONI!

Shalom mpendwa, karibu tujifunze Maneno ya Uzima.

Kama tukifakari kwa ukaribu matukio yaliyokuwa yanatokea baada ya Bwana wetu Yesu kufufuka, tutaona siri nyingi sana zimejificha ndani yake, kwamfano embu leo tuitazame siku ile ya kwanza kabisa ya Juma (Jumapili alfajiri), ambayo Mariamu Magdalene aliamka mapema sana kuliko hata watu wengine wote na kwenda kaburini kwa Yesu kutazama, Kwanza mpaka hapo hii inatuonyesha ni kwa jinsi gani huyu mama alikuwa anaupendo wa kipekee kwa Bwana zaidi hata ya watu wengine wote , lakini tunasoma alipofika tu makaburini kwa bahati nzuri au mbaya, alikuta tayari Kristo ameshamtangulia kufufuka, alichokiona ni jiwe tu la kabuni likiwa limeviringishwa pembeni na hakuna mtu ndani yake, wala chochote maeneo hayo, hivyo kwa hofu kubwa na kwa kuogopa akarudi haraka kwenda kuwaita mitume waje kulithibitisha hilo, ndipo tunaona Petro na mwanafunzi mmoja wakaondoka kwa kasi nyumbani pale, kuelekea makaburini,na walipofika kule ni kweli hawakuona mtu wala kitu chochote isipokuwa vitambaa vya sanda tu vimezongwa zongwa pembeni, hiyo iliwasikitisha sana lakini wakawa hawana namna isipokuwa kurudi tu nyumbani kuendelea kuomboleza…

Yohana 20:6 “Basi akaja na Simoni Petro, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala,

7 na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwa-zongwa mbali mahali pa peke yake.

8 Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini.

9 Kwa maana HAWAJALIFAHAMU BADO ANDIKO, YA KWAMBA IMEMPASA KUFUFUKA.”

Japo mitume ndio waliokwenda kuitwa lakini hawakuweza kudumu kwa muda mrefu pale makaburini kuangalia mwisho wake utakuwa vipi, badala yake wao moja kwa moja walirudi nyumbani, Lakini Mariamu aliendelea kubaki pale makaburini akijiuliza kwa uchungu moyoni mwake ni nini kinachoendelea mahali hapa na ni nani aliyeyafanya haya yote! Kwanini haya yote yampate Bwana?..Lakini wakati alivyokuwa anazidi kulia pale pembezoni mwa kaburi la Bwana, alirusha macho yake kwa mbali na ndani ya kaburi aliona malaika wawili wameketi mmoja kichwani na mwingine miguuni pa Yesu alipokuwa amelazwa, mahali pale pale wakina Petro walipokuwa wanapaangalia kwa makini wakizipapasa zile Leso,..Kumbe hakawajua mahali pale pale walikuwa wameketi malaika wa Bwana wakiwatazama tayari wakisubiria tu muda wa kusema nao, Lakini kwa kukosa kwao kuwa na subira waliondoka kwa huzuni, na ndio sasa tunamwona Mariamu akiwaona, na kuwauliza…

Yohana 20:12 “Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu.

13 Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka”.

Hiyo habari hapo inatufundisha nini?..Tusiwe wepesi kuondoka uweponi mwa Bwana, Pale ambapo tunaona hakuna tegemeo kwa Mungu, tumaini lote la mwisho limepotea, kumbe hapo hapo ndipo Mungu kaketi ili kutuhudumia..Tusiwe wepesi kuondoka uweponi mwa Bwana.

Lakini tukirudi kwa Mariamu hilo peke yake halikutosha kumpa yeye majibu ya maswali yake, japo aliwaona malaika wa Bwana yeye alizidi kuendelea kulia tu, na muda kidogo mahali alipokuwa amekaa akasikia kama mtu anatembea maeneo ya karibu na pale alipokuwepo wala Mariamu hakuwa na muda wa kumtazama wala kumsemesha kwani alidhani atakuwa ni MTUNZA BUSTANI tu, hivyo Yule mtu akamfuata na kumwambia maneno haya:

Yohana 20:15 “Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa.

16 Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, RABONI! (Yaani, MWALIMU WANGU).

17 Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.

18 Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo”.

Unaona hapo dakika za mwisho kabisa Mariamu anakuja kumwona na kumtambua Bwana Yesu, Lakini swali la kujiuliza hapo, ambalo hasaa ndio kiini cha somo letu la leo ni kwanini Bwana alimwambia “USINISHIKE; KWA MAANA SIJAPAA KWENDA KWA BABA”?

Sasa kama ukichunguza hapo, utaona Mariamu alipomwona Bwana, huyu mwandishi wa kitabu hichi cha Yohana Mtakatifu, hakunukuu maneno yale Mariamu aliyozungumza kwa kumuita Yesu Bwana au mwana wa Mungu au jina lingine lolote, wala hakutumia neno la moja kwa moja la mwalimu, badala yake aliandika kwa lugha ya kiebrania RABONI, ikiwa na maana MWALIMU WANGU..Sasa Uandishi huo haukuandikwa ili kutufundisha sisi maneno ya kiebrania, hapana kuna sababu kubwa kwanini hakuwenda moja kwa moja kuandika “mwalimu wangu” bali alianza na neno RABONI!, Hiyo ilikuwa ni kuweka msisitizo wa uzito wa kauli hiyo aliyoitoa Mariamu kwa BWANA…

Na ndio maana baada ya Maneno hayo kutoka kinywani mwa Mariamu tunaona Bwana akamwambia sasa USINISHIKE; KWA MAANA SIJAPAA KWENDA KWA BABA”?…Sasa hilo ni Neno usinishike, haimaanishi kuwa usinishike mwili wangu hapana bali Bwana alimaanisha kuwa.

“kwa kauli yako hiyo, ya kunifahamu mimi kama Raboni/mwalimu wako, usinijue mimi hivyo kwasasa, mpaka nitakapopaa kwenda kwa Baba…”

Na sio kwamba alimaanisha usinishike mwili wangu, kama wengi wanavyodhani,..Ikumbukwe kuwa kulikuwa na wakati mwingine walikuja kukutana naye yeye pamoja na Mariamu yule wa pili, na wote wakamshika miguu na kumsujudia (Mathayo 28:9). Sasa kama ingekuwa ni kumshika mwili asingeruhusu kitendo hicho kifanyike tena mahali hapo.

Hivyo Bwana alikuwa anamaana gani kusema vile?. Kumbe Japo walimwona YESU kama ni MWALIMU wao, lakini kiukweli walikuwa bado hawajamwelewa, na ndivyo Yesu alivyowaona….Lakini watakuja kumwelewa vizuri atakapopaa kwenda kwa Baba yake…Kwasababu kama wangekuwa wamemwelewa tangu zamani wasingekuwa wanapoteza muda kwenda kulia makaburini, badala yake saa ile ile wangepaswa wafurahie ushindi ambao wameupata kwa kufufuka kwake, kama alivyotabiriwa lakini wao kinyume chake walikuwa wanawaza habari za kuibiwa kwa mwili wake..Ni wazi kuwa walikuwa bado hawajamwelewa kama Mwalimu wao.

LAKINI NI KWANINI BWANA APAE KWANZA?

Jibu lipo wazi ndio hili kama tunavyosoma katika..

 Yohana 16:7 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo MSAIDIZI hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.

8 Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.

9 Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi;”

Umeona hapo? Kupaa kwa Bwana ni kwa ajili yetu sisi tupate msaidizi, ambaye kama tungemkosa huyo basi tungebaki katika mafumbo mengi ya kutomwelewa Kristo kama RABONI wetu, hata kama tungejifanya kumwita mwalimu kiasi gani,kama hatuna Roho mtakatifu haiwezekana kumwelewa Kristo. hata kama Kristo atatembea na sisi na kulala na kula na kunywa na sisi kila siku kama alivyofanya kwa mitume, kama tutakosa Roho Mtakatifu hatutakaa kamwe tumwelewe yeye..Huo ndio ukweli!

Na ndio maana Bwana Yesu aliweka wazi kabisa katika..

Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.”

Na ndivyo tunavyokuja kuona kwenye maandiko mara baada ya Kristo kuondoka Roho alipoachiliwa kwa wale wote waliotaka kumpokea siku ya Pentekoste, kuanzia huo wakati na kuendelea, tunaona jinsi mitume walivyomwelewa Kristo kwa namna ya kipekee hata zaidi ya ule wakati walipokuwa naye duniani..Tunaona jinsi gani walivyokuja kumwelewa sana KRISTO kama RABONI!, MWALIMU WAO MKUU, kwa Yule Roho tu Mtakatifu aliyeachiwa ndani yao……Unaona umuhimu wa kuwa na ROHO MTAKATIFU ndugu?

Vivyo hivyo na hata leo, haijalishi unampenda Bwana Yesu kiasi gani, haijalishi wewe ni mfuasi wa Yesu kiasi gani, haijalishi utajiita ni mwanafunzi wa Yesu kiasi gani, haijalishi utaona maono kiasi gani, haijalishi Yesu atakutokea mara ngapi, na kula na wewe na kutembea na wewe..KAMA hauna ROHO MTAKATIFU, basi fahamu kuwa bado upo mbali sana na KRISTO, kama vile Mashariki ilivyo mbali na Magharibi.

Kumbuka pia Roho Mtakatifu sio kunena kwa Lugha, ni zaidi ya hivyo vitu..Unaweza ukanena kwa Lugha na bado Roho wa Mungu akawa mbali na wewe vile vile…Uthibitisho wa kuwa na Roho Mtakatifu ni Matunda ya Roho katika tunavyoyasoma katika biblia Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”..yaani kwa ufupi “UTAKATIFU”….Kunena kwa lugha, maono, miujiza,uponyaji hivyo vyote ni vipawa vya Roho na sio matunda ya Roho…Na vipawa hivi havifanani kwa watu wote, kila mtu kapewa cha kwake, kwa jinsi roho alivyomjalia…Kwahiyo mtu anaweza akajazwa Roho na asinene kwa lugha bali akaonyesha karama nyingine labda uponyaji, imani au unabii, Neno la Maarifa n.k…

Kwahiyo uthibitisho pekee wa kujitambua kama unaye Roho Mtakatifu au la! ni UTAKATIFU ulionao..ambao ni upole, uvumilivu, huruma, fadhili,furaha, mwenye kiasi, mwaminifu n.k…Na sio kunena kwa lugha…Vipawa vya Roho ni uthibitisho namba mbili…lakini uthibitisho namba moja ni Utakatifu.

Biblia inasema..

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.

Hivyo na wewe ndugu, hata sasa Roho wa Mungu anataka kuja juu yako maana ahadi hii ni ya kwako pia, na anataka akufanye uwe mwanafunzi wa YESU KRISTO kweli kweli ili afanyike kuwa RABONI! Kwako Katika maarifa yote..Unachopaswa kufanya ni kutubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kabisa kuziacha hapo ulipo, Unakusudia kuacha ulevi kama ulikuwa mlevi, unakusudia kuacha uasherati kama ulikuwa mwasherati, unakusudia kuacha usengenyaji kama ulikuwa msengenyaji, unakusudia kuacha utazamaji wa picha chafu mitandaoni kama ulikuwa unafanya hivyo n.k kisha hatua inayofuata ni kwenda kutafuta mahali wabatizwapo ubatizo sahihi wa kimaandiko, yaani ule wa kuzamishwa katika maji mengi na uwe ni kwa JINA LA YESU KRISTO na si vinginevyo, Kumbuka hayo ni maagizo Bwana aliyoyatoa kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu, na ikiwa hayo yote umemaanisha kuyafanya kwa kumaanisha kabisa kuanza kuishi maisha mapya matakatifu ya kumwishia Mungu, basi fahamu kuwa kuanzia huo wakati na kuendelea Roho wa Mungu atakuja juu yako kukufanya kuwa mwanafunzi wa KRISTO. Na kukupa uwezo wa kumwelewa mwana wa Mungu kwa mapana yake yote na marefu yake,..

Mafundisho hayo sio wote wanapewa isipokuwa wale tu waliopokea Roho wa Mungu.

Hivyo ni maombi yangu kuwa utachukua uamuzi huo leo. Na Bwana akubariki sana. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

BADO KITAMBO KIDOGO HAMNIONI

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOKUJA JUU YA MTU.

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments