HERI, WALE MUNGU ASIOWAHESABIA MAKOSA YAO.

by Admin | 31 January 2019 08:46 pm01

Shalom! Mtu wa Mungu karibu tujifunze maandiko, kwa pamoja. Maandiko yanatuambia katika kitabu cha Zaburi 32:1-2 kwamba…

Zaburi 32:1 “Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake.

Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila.”

Mstari huu pasipo ufunuo wa Roho ni mgumu kidogo kueleweka, unaweza ukajiuliza inakuwaje Mungu aliye mkamilifu na asiyechangamana na dhambi kuwa na kikundi cha watu Fulani ambao hata watendeje dhambi yeye hawahesabii makosa, na wakati huo huo pia anacho kikundi cha watu ambao kila dhambi wanayoitenda ina hesabiwa mbele zake. Ni mstari kidogo wenye utata na mgumu kuelewa.

Lakini ashukuriwe Mungu kwa kumpa Mtume Paulo ufunuo wa Neno hilo kwa uweza wa Roho, ambaye alielezea kwa undani kabisa maana ya mstari huu Mfalme Daudi aliouandika katika Zaburi 32. Alisema…

Warumi 4: 6 “Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na HAKI PASIPO MATENDO,

7 Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao.

8 HERI MTU YULE AMBAYE BWANA HAMHESABII DHAMBI.”

Unaona hapo! Paulo anaelezea vizuri kuwa uheri ni kwa wale ambao Mungu ANAWAHESABIA HAKI PASIPO MATENDO, yaani wale waliompokea Bwana Yesu Kristo na kuvua utu wa kale na kuvaa upya, hao ndio kundi la watu ambao Mungu hawahesabii makosa yao haleluya!.

Sasa swali lingine linakuja..Je! watu waliompokea Bwana Yesu na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu na kuzaliwa mara ya pili wanakuwa na makosa? Na wakati huo huo maandiko yanasema katika 1 Yohana 3: 9 “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu”.

Maadamu tunaishi katika huu mwili hatuwezi kuwa wakamilifu asilimia 100, tunayo madhaifu mengi na kuna makosa tunayoyafanya mengi pasipo kujua hata kama hatutayaona, hayo ndio makosa ambayo kwa mtu aliyezaliwa mara ya pili, Mungu hayahesabu, Na pia mtu aliyezaliwa mara ya pili hawezi kutenda dhambi kwa makusudi, hawezi kwenda kuzini, au kuiba, au kutukana, au kula rushwa..hizo ni dhambi za dhahiri kabisa na sio za madhaifu, yapo makosa ya udhaifu, kama hasira zinazomjia mtu pasipo kujijua, na ufahamu ukimrudi anajua kosa lake na haraka anakwenda kutubu na kujirekebisha, lakini sio hasira mpaka za kwenda kupiga mtu au kusababisha madhara yoyote. Na madhaifu mengine yote ambayo pengine ulimkosea Mungu au Mtu mwingine pasipo kujijua, mpaka siku alipokuja kukwambia kwamba pale ulinikosea, ndipo unapojua kosa lako. Hayo yote mbele za Mungu hayahesabu kwa wale waliompokea yeye.

Ili kuelewa vizuri maana ya mambo haya hebu tafakari mfano huu.

Mzazi (ambaye hamjui Mungu) ana mtoto wake anayempenda na hapo hapo ana mfanyakazi aliyemwajiri.

Na wote wawili wakafanya makosa kila mtu kwa sehemu yake, unadhani ni atakayepata adhabu kubwa zaidi kuliko mwingine, yupi atafukuzwa ndani ya nyumba na yupi ataachwa…ni wazi kuwa Yule mfanyakazi atafukuzwa kutoka ndani ya ile nyumba na mtoto kuachwa…. Kwahiyo hapo tunaweza kujifunza kuwa kwa namna Fulani makosa ya watoto yanafunikwa na wazazi kuliko makosa ya watu wasio watoto wao, huwezi kukuta mahali popote mzazi ambaye hamjui Mungu anamsema vibaya mwanae mbele ya watu..zaidi ya yote hapendi kusikia mwanawe anasemwa vibaya hata kama ni mwovu kiasi gani.

Na kwa Mungu wetu wa mbinguni ndio ivyo hivyo, watoto wake (yani wale waliomwamini mwanawe mpendwa Yesu Kristo), hawahesabii makosa, hata kama watakuwa na madhaifu mengi kiasi gani, yeye bado atabaki kuwa baba yao tu! Ndio maana biblia inasema WANA HERI HAO HAWAHESABIWI DHAMBI ZAO. Haleluya!.

Lakini kinyume chake ni OLE WAKE YULE AMBAYE BWANA ANAMHESABIA MAKOSA YAKE.

Sasa Mtu anahesabiwaje makosa yake?.

Kwa kutomwamini Yesu Kristo, na kutokuzaliwa mara ya pili, ni sawa na kuwa nje ya familia ya Mungu, hivyo mtu kama huyo akifanya uovu tu wowote ule uwe wa bahati mbaya uwe wa makusudi, kwasababu hana mtetezi juu yake,anakuwa kama yatima, basi huo uovu wake utahesabiwa

Hiyo ndiyo hasara aliyonayo mtu ambaye hajampokea Yesu Kristo katika ulimwengu huu tuliopo wa dhambi, anakuwa anaishi katika dunia ambayo hana kibali chochote mbele za Mungu, anakuwa anaishi katika dunia ambayo maombi yake yanakuwa hayasikilizwi na yanakuwa hayana thamani yoyote, anakuwa anatoa sadaka ambazo hazina thawabu kubwa mbele za Mungu, anakuwa anatenda wema ambao hauhesabiki au kama unahesabika unakuwa na thamani na heshima ndogo sana mbele za Mungu. Kamwe anakuwa hawezi kumpendeza Mungu. Siku zote anakuwa hana amani na maisha yake.

Ndio maana utasikia wengi leo hii wanakwambia “mimi kumfuata Yesu siwezi” lakini natenda mema halafu anaulizwa kwani nitahukumiwa??..Ndugu yangu wema wako nje ya familia ya MUNGU ni kupoteza Muda..Fanya hima uwe kwanza MWANA WA MUNGU ili wema wako uweze kuhesabiwa!. Hata wauzaji wa madawa ya kulevya wapo wakarimu, kuliko wewe, lakini Mungu hawatambui kwasababu sio wake,…Ni sawa na mfanyakazi anayejitahidi kumpendezesha bosi wake kwa kufanya kazi kwa bidii, na kuwa mwaminifu ili mwisho wa siku awe mrithi, hata atende wema mwingi kiasi gani URITHI atapewa Mtoto wa Yule Bosi hata kama Yule mtoto ni mpumbavu kiasi gani.

Na ndicho tunachopaswa kufanya sisi, sio kutafuta kutenda mema kwanza, hapana bali kutafuta kuwa WANA WA MUNGU. Kutafuta kuzaliwa mara ya pili kutoka katika kuwa WATUMWA WA DHAMBI(Wafanya kazi) na KUWA WANA WA MUNGU, Ndipo tutapata kibali mbele za Mungu katika hii dunia tunayoishi na katika ulimwengu ujao.

Kama hujampa Bwana maisha yako, huu ndio wakati, usisubiri kesho kwasababu biblia inasema “usijisifu kwa ajili ya kesho kwasababu hujua yatakayozaliwa katika siku moja”..Kesho huijui, mkabidhi Bwana leo maisha yako, unachotakiwa kufanya ni kutubu kabisa dhambi zako kwa kudhamiria kuziacha kuzifanya kuanzia leo na kuendelea, kisha baada ya hapo haraka sana nenda katafuta mahali wanapobatiza ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kama hujabatizwa bado,(Zipo batizo nyingi, lakini unapaswa uujue ubatizo sahihi wa kimaandiko ni upi kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako).

kisha baada ya kubatizwa Bwana Mwenyewe atafanya yaliyosalia,atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu atakayekuwezesha kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya Biblia. Na hapo utakuwa umeshazaliwa mara ya pili kulingana viwango vya Baba wa Mbinguni anavyovitaka yeye, lakini ukiendelea kudumu katika UTAKATIFU, basi utakuwa nawe ni mmoja wa wana wa Mungu, wasiohesabiwa makosa yao, na wanaopewa thawabu haraka hata kwa yale madogo wanayoyafanya, utakuwa miongoni mwa waliobarikiwa wazao wateule, ukuhani wa kifalme, watu wa Milki ya Mungu, warithi wa Utajiri wote wa Mungu.

Bwana akubariki sana, Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

UZAO WAKO UTAMILIKI MALANGO YA KUZIMU;

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/31/heri-wale-mungu-asiowahesabia-makosa-yao/