YAKUMBUKE YA NYUMA.

by Admin | 15 August 2019 08:46 pm08

Nguvu ya kuendelea mbele tunaipata kwa kutazama tulipotokea…Usipokuwa na jicho la kutazama ulipotokea, usipokuwa na jicho la kukumbuka ni wapi ulipitia, utaishia kuwa mtu wa kunung’unika na kulalamika …

Ili tuweze kuishi Maisha ya ushindi siku zote katika haya Maisha ya hapa duniani, ni lazima tuishi Maisha ya kutafakari ni mambo gani ya nyuma Mungu aliyotutendea….unatazama kama Mungu wakati fulani alikupigania kwa kile, wakati huu atanipigania pia kwa hichi, Imani ndio inapokuja hapo..Ukishindwa kukumbuka ya nyuma kamwe hutaweza kuyashinda yanayokuja.

Ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana, wakati mwingine kuandika chini, mambo yote makubwa na madogo Mungu anayokutendea ili usisahau, hiyo itakusaidia pindi utakapokutana na tatizo kama hilo basi utakumbuka kirahisi uweza wa Mungu aliokupigania huko nyuma na utapata nguvu mpya.

Uweza wa Mungu unadhihirika mahali palipo na Imani, na Imani haiwezi kuja kama utayasahau matendo makuu ya Mungu aliyokutendea nyuma…Ndicho kilichowatokea wana wa Israeli wakati wanatoka Misri, ilikuwa kila mara wanasahau mambo makuu Mungu aliyowatendea nyuma na hivyo kuishia kumdharau Mungu kwa mambo madogo yanayotokea mbele yao, Walipotuma wapelelezi kuipeleleza nchi ya Kaanani na kukuta wenyeji wa kule ni majitu makubwa, badala wakumbuke kuwa Mungu alishawapigania huko nyuma kumwangusha Farao ambaye alikuwa na nguvu kuliko hayo majitu, wao wakasahau na kuanza kujiona nafsi zao kama mapanzi, hivyo ikawa dhambi kubwa mbele za Mungu,

Hayo yamewapata ili kutuonya sisi watu wa zamani hizi, tunapaswa tukumbuke uweza wa Mungu..aliotutendea huko nyuma pindi tunapokutana na jaribu fulani mbele yetu..Hata mwanafunzi ili aweze kulipata swali kisahihi, ni lazima awe na uwezo wa kukumbuka ni wapi alishafanya swali kama hilo, na wapi mtego wa swali hilo upo..asipokuwa na uwezo huo kila kitu kwake kitakuwa ni kipya.

Na ndio maana katika agano la kale Wanyama ambao walikuwa hawacheui walijulikana kama najisi, Mnyama anayecheua ni ambaye anao uwezo wa kula chakula na kukihifadhi tumboni baadaye anakirudisha na kikitafuna tena na kukimeza kama vile ng’ombe,..Inafunua kuwa sisi kama wanyama wa Kristo tusio najisi, tunapaswa tuwe na uwezo wa kukumbuka mambo yote makuu Mungu aliyotutendea nyuma, huko ndio kutafuna tena kile tulichokula, lakini tukiwa wasahauji, ndio yatatukuta kama yale ya wana wa Israeli.

1 Wakorintho 10:9 “Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka.

10 Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu.

11 Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.

12 Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke

Unapopitia kupungukiwa kidogo, kumbuka kuna kipindi ulipitia hali ngumu kuliko hiyo na Mungu alikufungulia mlango, hivyo tumia huo ushuhuda kukabili tatizo lililopo sasa, useme kama Mungu alinipigania kipindi kile cha taabu atanipigania na sasahivi, kwasababu Mungu ni yule yule habadiliki!…Kama unapitia ugonjwa fulani sasa, kumbuka kipindi fulani nyuma ulipitia ugonjwa wa hatari na Bwana akafungua mlango wa wewe kupona…tumia huo ushuhuda kukataa mawazo ya kukata tamaa sasa..

Kama umezungukwa na hatari, au unakabiliana na hatari, au tatizo mbele yako, sio wakati wa kupaniki, ni wakati wa kurudisha kumbukumbu zako nyuma na kukumbuka Bwana alivyokuokoa kwenye mikono ya waovu, na alivyokuepusha na hatari kimiujiza miujiza.n.k n.k, na kusema kama alifanyia vile, atanifanyia na hata sasa vile vile kama aliwafanyia wale, atakufanyia na wewe,…Mungu aliwaambia wana wa Israeli maneno haya wakati wanakwenda kukabiliana na maadui zao katika nchi ya Kaanani..

Kumbukumbu 7:17 “Nawe kama ukisema moyoni mwako, Mataifa haya ni mengi kunipita mimi; nitawatoaje katika milki yao?

18 Usiwaogope; KUMBUKA SANA Bwana, Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote;

19 uyakumbuke hayo majaribu makuu yaliyoyaona macho yako, na hizo ishara, na maajabu, na mkono wa nguvu, na mkono ulionyoka, aliokutolea nje Bwana, Mungu wako; ndivyo atakavyowafanya Bwana, Mungu wako, mataifa yote unaowaogopa.

20 Tena Bwana, Mungu wako, atampeleka mavu kati yao, hata hao watakaosalia, hao wajifichao, waangamie mbele zako.

21 Usiingiwe na kicho kwa sababu yao; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu katikati yako, Mungu mkuu, mwenye utisho.”

Bwana akubariki!, kama utapenda kujifunza Zaidi na kwa urefu juu ya “kukumbuka wema wa Mungu, aliokufanyia nyuma” unaweza kufungua ujumbe huu >>> MAISHA ULIYOPITIA NYUMA NI USHUHUDA TOSHA WA WEWE KUMTUMIKIA MUNGU

Maran atha! . jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/08/15/yakumbuke-ya-nyuma/