MAONO YA NABII AMOSI.

by Admin | 28 January 2020 08:46 am01

Shalom mwana wa Mungu, karibu tujifunze tena maneno ya uzima.

Amosi 3:7 “Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake”.

Maneno haya aliyaandika nabii Amosi..Alisukumwa kuandika hivyo, mara baada ya Mungu kumwonyesha mambo ambayo yalikuwa yanakwenda kuipata nchi ya Israeli katika wakati wake aliokuwa anaishi, pamoja na yale ambayo yalikuwa yanakwenda kuipata dunia nzima katika siku za mwisho. Hivyo akamshukuru Mungu, kwasababu aliona laiti kama yangemkuta kwa ghafla bila kujua angekuwa katika hali gani.

Hivyo, mambo mengine aliyoonyeshwa nabii Amosi, ni juu ya adhabu zitakazowapata matafa yaliyokuwa kando kando ya Israeli, na nchi ya Israeli kuchukuliwa utumwani. Alionyeshwa pia TETEMEKO KUBWA la ardhi ambalo lilikuwa linakwenda kuikumba nchi ya Israeli siku za usoni..Na ndio maana utaona mwanzoni kabisa mwa kitabu cha nabii Amosi aliandika na kusema maono yale alionyeshwa miaka miwili kabla ya tetemeko la Ardhi kutokea..

Amosi 1:1 “Maneno ya Amosi, aliyekuwa mmoja wa wachungaji wa Tekoa; maono aliyoyaona katika habari za Israeli, siku za Uzia, mfalme wa Yuda, na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli, miaka miwili kabla ya tetemeko la nchi”.

Unaona? Kama ukisoma utaona nabii Amosi, alionyesha mambo mabaya waliyokuwa wanayafanya Israeli, jinsi dhuluma za watu matajiri zilivyozidi, watu kula rushwa, watu kutokuwa waaminifu katika kazi zao, watu wasiotenda haki, na ziadi ya yote watu waliomsahau Mungu kwa ujumla, Hivyo akaonywa awaambie watubu wamrudie Mungu wao pengine Mungu atawasamehe na kughairi kuwaletea mapigo hayo,.. kwamba wamtafute yeye anayeweza kuleta uharibifu wa ghafla (Amosi 5:6-9) lakini hawakusikia hadi jambo hilo lilipowapata..

Amosi 8:8 “Kwa ajili ya hayo, je! Haitatetemeka nchi, na kuomboleza kila mtu akaaye ndani yake? Naam, itainuka yote pia kama huo Mto; nayo itataabika na kupwa tena kama Mto wa Misri”.

Tetemeko hilo lilikuja kutokea na lilikuwa kubwa ambalo halikuwahi kutokea katika nchi ya Israeli tangu lianze kuwa taifa, Nabii Isaya alionyeshwa pia athari za tetemeko hilo kwa jinsi lilivyokuwa kubwa katika siku hizo za mfalme Uzia..

Isaya 5:25 “Kwa sababu hiyo hasira ya Bwana imewaka juu ya watu wake, naye amenyosha mkono wake juu yao; akawapiga, navyo vilima vilitetemeka, na mizoga yao ilikuwa kama takataka katika njia kuu. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa”.

Watu walikufa wengi sana, nyumba nyingi zilibomoka, watu walikuwa wanakimbia ovyo ovyo kama vile vichaa mabarabarani,(Amosi 2:13-16) na ndio maana ukisoma tena kile kitabu cha Zekaria utaona habari hiyo inagusiwa tena ikifananishwa na tetemeko kubwa ambalo litakuja kutokea huko mbeleni Kristo atakaposhuka hapa duniani..

Zekaria 14:4 “Na siku hiyo miguu yake [yaani YESU KRISTO] itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake, upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka kwenda upande wa kusini.

5 Nanyi mtakimbia kwa njia ya bonde la milima yangu; kwa maana bonde lile la milima litaenea hata Aseli; naam, mtakimbia, KAMA VILE MLIVYOKIMBIA MBELE YA TETEMEKO LA NCHI, SIKU ZA UZIA, mfalme wa Yuda; na Bwana, Mungu wangu, atakuja, na watakatifu wote pamoja naye”.

Unaona, Hapo Zakaria anawakumbushia tukio ambalo lilikuwa limeshatendeka miaka mingi sana huko nyuma, lakini bado machungu yake yalikuwa yanakumbukwa hadi huo wakati wa Nabii Zekaria.

Sasa, turudi pale kwa nabii Amosi, ambaye alionyeshwa mambo hayo kabla hata tetemeko halijatokea. Pamoja na kuonyeshwa tetemeko hilo..Lakini pia alionyeshwa na matukio mengine ambayo yatakuja kutokea katika siku za mwisho..Na ndio maana akaandika na kusema..

Amosi 5:18 “Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya Bwana; kwani kuitamani siku ya Bwana? Ni giza, wala si nuru.

19 Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma.

20 Je! Siku ya Bwana haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga”.

Nabii Amosi alionyeshwa hii siku inayoitwa siku ya Bwana..hakuona kingine zaidi ya giza tu, yaani mauti, akalia na kusema sio siku ya kuitamani hata kidogo..

Amosi 8:9 “Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana MUNGU, nitalifanya jua litue wakati wa adhuhuri, nami nitaitia nchi giza wakati wa nuru ya mchana”.

Ndugu yangu, mimi na wewe tusitamani tuwepo huo wakati, Mungu wetu ni wa rehema lakini pia biblia inatuambia ni mwingi wa ghadhabu, embu jaribu kufirikia wakati kama huu mchana saa 7, unaona jua linaondoka, dunia nzima inakuwa ni giza NENE, utakuwa katika hali gani?..na ahishii tu hapo, kumbuka kabla ya hilo jua kuondolewa kutakuwa kumeshatungulia mapigo ya vile vitasa 6 vya mwanzo tunavyovisoma katika Ufunuo sura 16 (Kama hujapata uchambuzi wa mapigo ya vitasa 7 tutumie ujumbe inbox tukutumie maelezo yake)…

Na pigo la mwisho kabisa litaishi na hili la nchi kutiwa giza na tetemeko kubwa la Ardhi ambalo halijawahi kutokea tangu dunia iumbwe hadi sasa,,,tetemeko hilo litakuwa na nguvu sana hadi visiwa vitahama, pengine hichi kisiwa cha Zanzibar utaenda kukikuta nchi ya Peru kule kama kitakuwa hakijatoweka kabisa..(Soma kwa muda wako Mathayo 24:29-31 na Ufunuo 16:17-21)

Kumbuka Tetemeko hilo litatokea ndani ya giza nene. litamaliza wanadamu wale ambao hawakwenda kwenye unyakuo wakati huo, kiasi kwamba kumpata mwanadamu mmoja duniani ni sawa na vile unavyotafuta kipande cha dhahabu kimoja ardhini kwa jinsi wanadamu watakavyoadimika..

Isaya alionyeshwa hivyo..

Isaya 13:9 “Tazama, siku ya Bwana inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.

10 Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze.

11 Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali;

12 nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri.

13 Kwa hiyo nitazitetemesha mbingu, na dunia itatikiswa itoke katika mahali pake, kwa sababu ya ghadhabu ya Bwana wa majeshi, na kwa sababu ya siku ya hasira yake kali”.

Mambo hayo sio hadithi yatakuja kutokea, kama walivyoonyeshwa manabii hawa wa Bwana, hakuna asiyejua kuwa hizi ni nyakati za mwisho, na mambo hayo yatatimia katika majira yetu haya..

Lakini kabla hayajatokea Bwana ameshatupasha habari na anatuonya na sisi..Tumgeukie yeye, tuache dhambi, tutubu dhambi zetu. Ili unyakuo ukipita tusibakie hapa duniani..na kuiingia katika ghadhabu ya Mungu…Wengi wanadokezwa katika ndoto na maono jinsi siku hiyo itakavyokuwa..ni siku ya kutisha sana.

Kama hujatubu basi katika nyakati hizi za kumalizia ni vema ukafanya hivyo kwasababu muda ubakio ni mchache sana. Pia kaa mbali na mafundisho ya manabii wa uongo, ambao hawajali roho yako kwa kuacha kukueleza habari ya mambo ya yajayo, ya ulimwengu ujao, na hukumu ya Mungu, bali mafundisho ya kufanikiwa mwilini tu…Bwana Yesu alisema “Itakufaidia nini kuupata ulimwengu mzima na kisha kupata hasara ya nafsi yako?”

Hivyo tusisikilize mahubiri ya kujirudia rudia pokea hichi pokea kile wakati hata hatujui baada ya kifo ni nini kitaendelea, hujui endapo ukifa katika hali uliyopo ya kuishi na mke/mume ambaye hamjaona ni nini kitatokea!..tusiwafuate hao manabii wasioumia kusikia mtu kafa katika dhambi!.…Sisi tuwafuate manabii hawa waliothibitishwa na Mungu mwenyewe wanaotuonya kuhusu siku za Mwisho, na madhara ya dhambi.. kama nabii Amosi, Isaya, Danieli, Yeremia, Zekaria n.k. Ndio tutakwenda salama katika safari yetu hapa duniani.

Ubarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia masomo kwa njia ya whatsapp ya kila siku basi, bofya hapa uweze kujiunga >>> WHATSAPP Au tuandikie kwa namba hizi +255789001312

Mada Nyinginezo:

VIFUNGO VYA GIZA VYA MILELE.

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

UFUNUO: Mlango wa 16.

SAA YA KIAMA.

SIKU ILE NA SAA ILE.

UNYAKUO WA KANISA UMEPITA LEO!!

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/28/maono-ya-nabii-amosi/