TIA MIZIZI CHINI, ILI UZAE MATUNDA JUU.

by Admin | 25 August 2024 08:46 pm08

Nakusalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo, Karibu tujifunze habari njema za uzima wa roho zetu.

  Neno la Mungu linatuambia..

2 Wafalme 19:30

[30]Na mabaki yaliyookoka ya nyumba ya Yuda yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu. 

Unaelewa maana ya mstari huu? Anazungumzia kustawi kwa nyumba ya Yuda (ambao ndio sisi kanisa)..

Lakini kustawi kwake hakuji hivi hivi, matunda yake kutokea kule juu, anasema kanuni yake ni lazima pia mizizi yake ikite chini.

Haiwezekani mti ukazaa kama hauna mzizi, jiulize je wewe una mizizi imara ya rohoni, ya kukufanya uweze kuzaa matunda yampendezayo Bwana?

Kumbuka kuthamini kwako wokovu, ndivyo hueleza urefu wa mizizi yako yenye nguvu, itakayokuwezesha kustawisha matunda juu.

Jani haliihitaji mizizi yoyote ya maana, kwasababu halina matunda ya kutoa. 

Ukiona huwezi kuzama ndani katika wokovu, hauwi siriazi na maisha yako ya rohoni ujue pia hautakuwa na matunda yoyote kwa Mungu wako.

Katika ule mfano wa mpanzi Bwana Yesu alieleza kitu kilichofanya ile mbegu ya nne kustawi mpaka kuzaa matunda..anasema ilizaa kwa kuvumilia.(Luka 8:15)

kuvumilia nini?

Kuvumilia hatua zote 3 za mwanzo. yaani alihakikisha adui haibi mbegu iliyopandwa ndani yake, ni mtu ambaye aliweza kuvumilia dhiki, na majaribu yaliyozuka kinyume na lile neno lililopandwa moyoni mwake, alijiepusha na anasa, na kutoruhusu masumbufu ya ulimwengu huu kumsonga akashindwa kuivisha chochote. Hayo ndio mambo aliyovumilia.

Huyu ni mtu ambaye yupo makini na wokovu alioupokea.

Swali la kujiuliza je tunayo matunda hayo? kumbuka Hayaji kwa kutamani au kusubiri yanakuja kwa urefu wa mizizi yetu yenye uwezo wa kufikia vyanzo vya chini kabisa vyenye virutubisho vyote vya kustawisha matunda.

Ndio maana biblia inasema

Zaburi 1:1-3

[1]Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.

[2]Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.

[3]Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa. 

Anza sasa kushughulika na mizizi yako, mpaka ifikie kwa hakika mito hiyo ya maji.

Usipoe kimaombi, kimifungo, kiibada, kiuinjilisti, na kiusomaji Neno.

2 Wafalme 19:30

[30]Na mabaki yaliyookoka ya nyumba ya Yuda yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu. 

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

KWA KUVUMILIA AKAIPATA ILE AHADI.

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/08/25/tia-mizizi-chini-ili-uzae-matunda-juu/