AKAUKAZA USO WAKE KWENDA YERUSALEMU.

by Admin | 20 November 2024 08:46 am11

Nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu Kristo, karibu tuyatafakari maneno ya uzima. Leo napenda tujifunze tabia nyingine ya Bwana Yesu. Kwasababu yeye mwenyewe alituambia ‘tujifunze kwake’. Hivyo naamini tuna mengi ya kuyajua kuhusu yeye.

Habari hiyo tunaisoma katika vifungu hivi;

Luka 9:51  Ikawa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu;

52  akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali.

53  Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu.

54  Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?

55  Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]

56  Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine.

Kama wewe ni msomaji mzuri wa biblia utakumbuka kuwa kuna wakati ulifika, ilikuwa wazi kwa watu wote, kuwa Yesu anatafutwa ili auawe, (hususani kule Yerusalemu). Na hilo lilimfanya mara kadha wa kadha asitembee kwa uwazi wote mbele ya makutano (Yohana 7:10), kwasababu, saa yake ya kuuawa ilikuwa bado haijafika.

Yohana 11:54  Kwa hiyo Yesu hakutembea tena kwa wazi katikati ya Wayahudi; bali alitoka huko, akaenda mahali karibu na jangwa, mpaka mji uitwao Efraimu; akakaa huko pamoja na wanafunzi wake.

Lakini mambo yalikuja kubadilika baadaye,  hilo halikuendelea kwa wakati wote. Alipoona sasa kazi aliyopewa na Mungu ameimaliza, alionyesha tabia nyingine ambayo haikuwa ya kawaida. Biblia inatuambia, “aliukaza uso wake kuelekea Yerusalemu”, kule kule alipokuwa anatafutwa auawe.

Jambo ambalo lilileta mshtuko hata kwa mitume wake;

Yohana 11:7  Kisha, baada ya hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena.

8  Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena?

9  Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu.

Walishangaa, ujasiri huo ni wa namna gani? Ni sawa na wanajeshi waliokwenda vitani, halafu maadui wakawaua wanajeshi wote, akabakia mmoja tu, halafu huyo mmoja anasema nitakwenda kupambana na jeshi lote hilo peke yangu sitajificha. Ukweli ni kwamba inahitaji nguvu nyingine ya ziada ndani ya huyo mtu.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana Yesu, aliukaza uso wake, kwenda kututetea sisi. Embu Fikiria kama angeulegeza, na kuendelea kuzunguka mahali pengine na sio kule uyahudi(Yerusalemu), wokovu wetu tungeupatia wapi?

Ilibidi, alazamishe mambo, japo mwili wake ulikuwa hautaki, ndio maana akiwa pale bustanini, anaomwomba Baba, akisema ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke, ni kuonyesha kuwa hata mwili wake ulikuwa unagoma kuwepo kule Yerusalemu,  na si mwili tu, bado mazingira pia hayakutaka,  alipokuwa anakatiza kwa Wasamaria wenyeje wa pale hawakutaka kumruhusu akae kwao, kwasababu waliona kama anawaletea matatizo, ikumbukwe kuwa watu hao  hao ndio waliokuwa wanataka kumfanya mfalme hapo mwanzo. Kuonyesha kuwa mazingira yalimgomea. Si mazingira peke yake, hata mitume wake nao, walifanya kama kumsindikiza tu, lakini mioyo yao walishajiandaa kuchukua hatua yoyote lolote litakapotokea, ndio maana pale bustanini, wale watu walipokuja kila mmoja akakimbia na njia yake.

Kwa ufupi kila kitu kilikataa, isipokuwa roho yake tu. Ndio sababu ya kwanini maandiko yanatuambia ‘aliukaza uso wake’ kwasababu haikuwa rahisi, si jambo tena la kuomba, au kubembeleza, au kushawishi, au kusubiri msimu mzuri. Bali ni kujitoa tu wote wote, katika hayo. Watu wengi tunadhani Yesu aliuchukua msalaba wake siku ile alipobebeshwa ule mti, hapana, aliuchukua msalaba wake Kwa kitendo hichi cha kuamua kuukaza uso wake, kuelekea kifoni. Hata aliposema tujitwike misalaba yetu, alilenga, eneo hilo.

Ni nini na sisi tunapaswa tukipokee kwa Bwana Yesu?

Kwa kuwa Roho wake naye yupo ndani yetu, hatuna budi kufahamu kuwa yapo majira katika safari yetu ya wokovu, hatutahitaji mazingira yawe mazuri, ndio tulitimize kusudi la Mungu, au  ndugu kutukubalia, au marafiki kuafikiana na sisi, au miili kutuambia sasa ndio wakati, hapana..bali ni kujitwika misalaba yetu, “kwa kukaza nyuso zetu” na kumfuata Yesu.

Tukingoja vikwazo viondoke, au viondoshwe, tutajidanganya, na tutangoja sana, kwani vita vitaendelea kuwepo mpaka mwisho, mapambano hayaishi, tutashinda tu kwa kukaza tu nyuso zetu. Na Bwana atakuwa pamoja na sisi, ijapokuwa itaonekana ni kujipoteza lakini mwisho wake utakuwa ni uzima kama ulivyokuwa kwa Bwana Yesu.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

RABI, UNAKAA WAPI?

MFALME ANAKUJA.

BADO UPO YERUSALEMU TU..GALILAYA HUTAKI KWENDA?

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/11/20/akaukaza-uso-wake-kwenda-yerusalemu/