Je umewahi kutafakari kwanini mapigo yote tisa (9) aliyopigwa Farao bado moyo wake ulikuwa mgumu? Na kwanini lile pigo moja la mwisho la kufa wazaliwa wa kwanza ndipo akawaruhusu wana wa Israeli?.
Sasa hakuna mahali popote maandiko yanasema kuwa “Mungu aliufanya moyo wa Farao kuwa mlaini”
Maana yake Farao aliendelea kuwa na moyo mgumu mpaka alipoingia kwenye ile bahari ya Shamu, na hapo ndio ikawa mwisho wake.
Sasa ni nini kilitokea mpaka Farao akawaachia wana wa Israeli?… Si kingine bali ni ule msiba alioupata,
Na huku bado moyo wake ukiendelea kuwa mgumu, alivunja sheria ya moyo wake na kuwafukuza wana wa Israeli kwa muda. (Lakini moyo wake bado ulikuwa mgumu tu).
Kutoka 11:1 “BWANA akamwambia Musa, Liko pigo moja bado, nitakaloleta juu ya Farao na juu ya Misri; baadaye atawapa ninyi ruhusa mtoke huku; naye hapo atakapowapa ruhusa, atawafukuza mtoke huku kabisa kabisa”
Sasa ni siri gani iliyokuwepo ndani ya wazaliwa wa kwanza wa Misri hata kumfanya Farao awafukuze wana wa Israeli?…Kwani ni wazi kuwa hata Farao angepigwa kwa mapigo gani ya asili asingewaachia wana wa Israeli.
Ila ni nini kilikuwa kwa wazaliwa wa kwanza wa kiMisri?
Kilichokuwa ndani ya wazaliwa wa kwanza wa Misri, ikiwemo mwana wa Farao si kingine zaidi ya “miungu ya kimisri”..
Hivyo kifo cha wazaliwa wa kwanza ilikuwa ni hukumu kubwa kwa miungu yao pamoja kudhalilika kwa miungu yao ambao waliamini ina nguvu nyingi.
Ndio maana MUNGU aliposhuka kuwaharibu wazaliwa wa kwanza pia alisema ataiharibu na miungu yao (ambayo kiuhalisia ilikuwa inaishi ndani ya hao wazaliwa wa kwanza).
Kutoka 12:12 “Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA.”
Zamani katika nchi ya Misri na hata katika mataifa mengine ya dunia, wazaliwa wa kwanza wa kiume waliaminika kama miungu ya familia na ya nchi.
Na wanyama wa kwanza kuzaliwa, ndio waliotumika kwa kafara za miungu yao.
Hivyo watoto wote wa kwanza wa kiume walikuwa wanabeba ukuhani wa miungu, na roho zote za miungu zilikuwa zinakaa ndani yao.
Kwahiyo kilichomwumiza zaidi Farao si msiba wa mtoto, bali ni kuhukumiwa kwa miungu yao iliyokuwepo ndani ya wale watoto!!..
Kwaufupi Farao alichanganyikiwa kidogo, hakuelewa ni nini kimetokea katika eneo lake la imani.
Na hata waMisri wote walichanganyikiwa vivyo hivyo, hakuna ambaye hakulia..wote walilia na kuhofu na kutoelewa ni nini cha kufanya, waliyeyuka mpaka kufikia hatua ya wana wa Israeli kuwateka nyara.
Kutoka 12:33 “Wamisri nao wakawahimiza watu, kuwatoa katika nchi kwa haraka, maana walisema, Tumekwisha kufa sote. 34 Watu wakauchukua unga wa mikate yao kabla haijatiwa chachu, na vyombo vyao vya kukandia wakavitia ndani ya nguo zao mabegani. 35 Wana wa Israeli wakafanya kama neno lile la Musa; wakataka kwa Wamisri vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu, na mavazi. 36 BWANA akawajalia kupendelewa na Wamisri hata wakawapa kila walichokitaka. Nao wakawateka Wamisri nyara”
Kutoka 12:33 “Wamisri nao wakawahimiza watu, kuwatoa katika nchi kwa haraka, maana walisema, Tumekwisha kufa sote.
34 Watu wakauchukua unga wa mikate yao kabla haijatiwa chachu, na vyombo vyao vya kukandia wakavitia ndani ya nguo zao mabegani.
35 Wana wa Israeli wakafanya kama neno lile la Musa; wakataka kwa Wamisri vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu, na mavazi.
36 BWANA akawajalia kupendelewa na Wamisri hata wakawapa kila walichokitaka. Nao wakawateka Wamisri nyara”
Ni ujumbe gani tunapata hapo?..au ni kitu gani kilichokuwa kimewafunga wana wa Israeli?
Si utajiri wala hazina zilizoko Misri kwamaana Bwana aliuharibu utajiri wake wote kwa zile mvua za mawe na nzige, vile vile si uzuri wa Misri, kwasababu Bwana aliharibu uzuri wake kwa zile mvua za mawe lakini bado wana wa Israeli walikuwa kifungoni.
Wala si ushujaa wa waMisri kwasababu Bwana aliwapiga kwa chawa, na majipu na aliwanyima maji ya kunywa kwa siku saba, hivyo walikuwa dhaifu..lakini bado wana wa Israeli walikuwa kifungoni.
Ni nini kilichokuwa kimewashikilia wana wa Israeli???…..jibu ni “miungu ya kimisri” iliyokuwa inaabudiwa ndani ya watu.
Hiyo ilipopigwa pamoja na makuhani wake (ambao ndio wazaliwa wa kwanza)..vifungo vikalegea, wana wa Israeli wakaachiwa.
Laiti Bwana Mungu angelileta hilo pigo mwanzoni kabla ya yote, Farao angeshaawaachia Israeli kitambo sana pamoja na moyo wake kuwa mgumu, lakini Mungu aliliruhusu liwe mwisho wa kusudi lake maalumu.
Na ukiendelea kusoma mbele utaona Bwana anawapa amri wana wa Israeli wawatakase wazaliwa wa kwanza na kwamba kila mzaliwa wa kwanza atakuwa ni wa Bwana, maana yake atakuwa kuhani wa Bwana kwa lazima (kwasababu kulikuwa na kitu katika wazaliwa wa kwanza).
Maana yake kila mzaliwa wa kwanza wa wana wa Israeli alipaswa kutolewa kwa Bwana kama Hana alivyomtoa Samweli kwa Bwana (hiyo ilikuwa ni amri).
Lakini sheria hiyo ilikuja kubadilika, na ukuhani wa wazaliwa wa kwanza likapewa kabila la Lawi.
Hesabu 3:12 “Mimi, tazama, nimewatwaa Walawi na kuwatoa kati ya wana wa Israeli badala ya wazaliwa wa kwanza wote wafunguao tumbo katika wana wa Israeli; na hao Walawi watakuwa wangu; 13 kwa kuwa hao wazaliwa wa kwanza wote ni wangu; katika siku ile niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri nikajiwekea wakfu wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, wa wanadamu na wa wanyama; watakuwa wangu; mimi ndimi BWANA”.
Hesabu 3:12 “Mimi, tazama, nimewatwaa Walawi na kuwatoa kati ya wana wa Israeli badala ya wazaliwa wa kwanza wote wafunguao tumbo katika wana wa Israeli; na hao Walawi watakuwa wangu;
13 kwa kuwa hao wazaliwa wa kwanza wote ni wangu; katika siku ile niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri nikajiwekea wakfu wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, wa wanadamu na wa wanyama; watakuwa wangu; mimi ndimi BWANA”.
Hivyo wazaliwa wa kwanza wa wana wa Israeli wanaozaliwa ilikuwa ni sharti wakombolewe kwa sadaka ili watokane na kiapo hiko cha Bwana cha kuwa makuhani.
Na maana ya kukombolewa si kutolewa katika vifungo vya laana, kama mafundisho ya siku hizi za mwisho yanavyofundisha.
Bali ukombozi ilikiwa ni ile hali ya mtoto kutolewa katika nafasi ya kikuhani ambayo angepaswa kuitumikia maisha yake yote.
Hivyo anapokombolewa anakuwa huru kama watu wengine wasio na utumishi wa kikuhani (kwa ufupi anafunguliwa kutoka katika vifungo vya ukuhani)
Na mtoto wa kwanza asipokombolewa anabaki katika kifungo cha dhambi ya nafasi ya kikuhani.
Sasa swali je hata sasa katika agano jipya tunasheria hizo za kukomboa mzaliwa wa kwanza?.
Jibu ni la!..katika agano jipya hatuna sheria za kumkomboa mzaliwa wa kwanza au wa mwisho, kwasababu sote tuliomwamini Bwana YESU na kutakaswa kwa damu yake tunafanyika kuwa makuhani wa Bwana.
Ufunuo wa Yohana 1:6 “na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina”.
Hivyo sote tunayo huduma ya kikuhani na mbele za Mungu, na ukishakuwa tu kuhani tayari ni mzaliwa wa kwanza pasipo kujali rika…Hivyo kanisa la Kristo ni wazaliwa wa kwanza.
Waebrania 12:23 “mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika”.
Kwahiyo hakuna sadaka yoyote ya ukombozi kwa wazaliwa wa kwanza kwa jinsi ya mwili.
Mafundisho na maombi ya kukombolewa kwa wazaliwa wa kwanza si ya kiMungu, bali ni ya ibilisi.
Ndio tunaweza kuwaombea wazaliwa wetu wa kwanza na kuwaweka wakfu kwa Bwana, dhidi ya roho zinazofuatilia, lakini si kuwakomboa….uwakomboe na nini?…je uwakomboe uwatoe katika ukuhani?…maana ndio lengo la ukombozi hilo kibiblia lililokuwepo juu ya wana wa Israeli juu ya wazaliwa wa kwanza.
Zaidi sana watoto wetu wa kwanza wanapaswa wawe wazaliwa wa kwanza kiroho kwa kumwamini YESU na kutakaswa ndipo wanapofanyika makuhani kama wengine wote waliomwamini YESU.
Mwisho, fahamu kuwa kilichowafuga wana wa Israeli ni miungu ya misri, iliyokuwa inaabimudiwa ndani ya kila kiumbe kilichokuwa cha kwanza.
Hali kadhalika vile vitu vinavyojiinua katika maisha yetu vilivyo vya kwanza ndivyo ni lazima tuwe navyo makini kwani hivyo ibilisi anaweza kuvitumia kama mlango wa kutufunga.
Je cha kwanza kwako ni nini?…je ni kazi uliyonayo?…au ni cheo ulicho nacho?..au ni uzuri au ni Bwana YESU?..
Ni heri BWANA YESU akawa wa kwanza kwako, kwani yeye ndiye njia, kweli na Uzima.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Rudi Nyumbani
Print this post