SWALI: Je ni halali kiongozi wa imani (Wachungaji), kugombea nafasi za kiserikali kama vile udiwani au kuwa wanasiasa au wafanya-biashara?
JIBU: Kabla ya kuangalia kiongozi wa imani. Embu tuangalie kwanza kwa mtu aliyeamini.
Je mtu aliyeamini kugombea nafasi za kiutawala ni dhambi?
Kugombea nafasi ya kiutawala, biblia haijaeleza moja kwa moja kuwa ni kosa au si kosa, Yategemea lengo/ nia ya huyo mtu, Ikiwa ataenda kule ili kutetea haki, huku akitembea katika misingi ya imani ni wazi kuwa hakuna kosa lolote yeye kufanya hivyo. Kwenye maandiko tunarekodi ya watu wa Mungu waliokuwa na vyeo katika nafasi ya kiserikali, lakini waliweza kuhifadhi misingi ya imani yao, mfano wa hao ni Yusufu na Danieli, ijapokuwa walikuwa katika falme za kipagani lakini waliweza kutembea na Mungu hatimaye wakapendwa sana.
Mfano mwingine katika historia kuna mkristo mmoja maarufu aliyeitwa William Wilberforce, yeye alizaliwa mwaka 1759, alipokuwa mtu mzima aligombea nafasi ya ubunge uko ulaya akaipata, lengo lake likuwa ni kuomba sheria ya biashara ya watumwa ifutwe ulaya, ijapokuwa shitaka lake lilipingwa na kupuuziwa kwa miaka mingi sana, lakini aliendelea kulipigania bila kuchoka mpaka mwisho wake lilikuja kupitishwa, hivyo kwa ajili yake yeye, biashara ya utumwa ilifutwa kule ulaya karne ya 18. Hivyo ikiwa mkristo atajiunga kwa madhumuni kama haya, si dhambi.
Lakini tukirudi katika eneo la “kiongozi wa kiroho”. Mpaka aitwe kiongozi maana yake wapo watu chini anaowachunga, ambao Bwana amempa awaangalie, na siku ya mwisho atatolea hesabu kwa ajili yao.
Sasa ikiwa ni hivyo. Mtu kama huyu kujihusisha na nafasi ya serikalini, au siasa, au kuwa mfanya-biashara ni makosa.
Ikumbukwe kuwa Bwana Yesu alitoa mipaka juu ya utumishi wake. Akasema mtu hawezi tumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Aidha atampenda huyu na kumchukia huyo
Mathayo 6:24 Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpendahuyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.
Pengine utaliuza vipi kuhusu Paulo? maana alikuwa fundi wa kushona mahema?.
Ndio kiongozi au mchungaji anaweza akawa na shughuli yake ndogo ya pembeni kumsaidia kupata kipato, ili tu aweze kujitimizia mahitaji yake ya msingi,(ikiwa ni lazima) mfano alivyofanya mtume Paulo, alipokwenda kushona mahema (Matendo 18:3). Lakini sio kwa lengo la kuwa mfanya-biashara na wakati huo huo askofu. Paulo alifanya vile ili kumudu tu mahitaji yake ya msingi. Tofauti na inavyochukuliwa na watu leo kuwa “Alishikilia mambo yote” maana kama ni hivyo Paulo asingemwambia Timotheo maneno haya;
Timotheo 2:4 Hakuna apigaye vita ajitiaye katika shughuli za dunia, ili ampendeze yeye aliyemwandika awe askari.
Umeona? Mlango wa kujihusisha na mambo mengine, haupo.
Ndio maana kipindi kile baada ya Bwana Yesu kufufuka Petro alijaribu kurudia kazi yake ya uvuvi, alipohangaika usiku kucha na kukosa, asubuhi yake alipokutana na Yesu, swali la kwanza aliloulizwa Je! Petro unanipenda? Swali hilo aliulizwa mara tatu. Akajibu ndio…Yesu akamwambia basi lisha kondoo zangu.
Yaani toa akili zako huko kwenye uvuvi kafanye kazi ya utume uliyoitiwa. Baada ya hapo hatuona mahali popote Petro, akivua huku anafanya utume. (Yohana 21). Na hata kama ilitokea basi haikuwa kwa lengo la kuwa mfanya-biashara, bali kupata riziki ya siku.
Ukishakuwa kiongozi wa kiroho, tambua wewe hujatengenezwa kwa utumishi wa mambo mengine, bali kumtumikia Mungu tu, kazi uliyonayo ni kubwa zaidi ya zote ulimwenguni, na bado inawatenda kazi wachache, Bwana Yesu alisema. Hivyo hii ni kazi inayoweza kukufanya uwe bize wakati wote. Hupaswi kuwa mkuu wa mkoa wakati huo huo, ni mchungaji, kuwa mbunge au waziri, wakati huo huo ni askofu, utakwama tu mahali pamoja.
Na ni muhimu kufahamu kuwa huduma ya Kristo haipaswi kuhusishwa na utafutaji fedha ndani yake, bali ni kazi ya wito ambayo malipo yake hasa yapo mbinguni. Hivyo Bwana akikubariki, au asipokubariki, hilo halikufanya uache huduma na kuwekeza akili yako kwingineko, lakini fahamu kuwa aliahidi hatakuacha wala kukupungukia kabisa.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Je! Kushiriki au kujihusisha kwenye michezo ni dhambi?..
MAMBO NANE (8), AMBAYO WEWE KAMA KIONGOZI UTAIGWA.
IMANI “MAMA” NI IPI?
Rudi Nyumbani
Print this post