MGAWANYIKO WA ISHARA ZA UJIO WA BWANA YESU KRISTO.

MGAWANYIKO WA ISHARA ZA UJIO WA BWANA YESU KRISTO.

Ujio wa BWANA YESU duniani umegawanyika katika sehemu kuu Tatu (3).

Sehemu ya Kwanza: Ni kuzaliwa kwake kupitia bikira Mariamu.

Luka 1:30 “Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu.

31  Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.

32  Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake”

Sehemu ya Pili: Unyakuo wa kanisa.

Luka 17:34  “Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.

35  Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.

36  Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.

Unyakuo wa kanisa utakapotokea si kila mtu atajua, na si kila mtu atamwona BWANA YESU, isipokuwa wale tu watakaonyakuliwa na wafu waliokufa katika Bwana… wengine wataendelea na shughuli zao, na biashara zao, na usingizi na wengine waliokufa nje ya Kristo wataendelea katika mauti zao. Na Hatua hii ndiyo tunayoingojea sasa, na hata mmoja wetu hapaswi kuikosa!.

Sehemu ya Tatu: Ujio wa utawala wa miaka elfu moja ambapo kila jicho litamwona.

Ufunuo 1:7 “Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina”

Hiki ni kipindi ambacho, wale wote waliosalia kwasababu ya kuukosa unyakuo, na wakabaki kuipokea ile chapa ya mnyama, baadhi yao watakufa katika ile hukumu ya mataifa, na wachache watakaosalia basi watamwona BWANA  YESU mawinguni akija kwa nguvu nyingi, na utukufu mwingi, kama umeme wa radi, na wataangamia kwa mwako wake. Na Lengo la KRISTO kuja ni kwaajili ya ule utawala wa miaka elfu unaotajwa katika Ufunuo 20.

> Sasa ZIPO ISHARA ZILIZOTANGULIA KUJA KWA KWANZA KWA KRISTO (yaani kipindi Bwana YESU anazaliwa).

> Na pia ZIPO ISHARA ZINAZOTANGULIA KUJA KWA PILI  KWA KRISTO (yaani kipindi cha unyakuo wa kanisa).

> Na pia ZIPO ISHARA ZINAZOTANGULIA KUJA KWA TATU WA KRISTO (yaani kipindi cha utawala wa miaka Elfu, ambapo kila jicho la watakaokuwepo duniani litamwona.)

Kwa ufupi sana tuzitazame ishara hizo au dalili hizo.

1. Ishara za kuja kwa kwanza: Kuzaliwa kwa Bwana.

Ishara kuu ya kuja kwa kwanza, au kukaribia kutokea kwa Bwana duniani ni UJIO WA ELIYA, kwani maandiko yalitabiri kwamba kabla ya kuzaliwa kwa Masihi basi Bwana Mungu atamtuma kwanza mjumbe atakayetangulia kumtengenezea njia, ambaye huyo atakuwa na roho ya Eliya ndani yake, na huyo hakuwa mwingine Zaidi ya Yohana Mbatizaji.

Luka 1:13  “Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.

14  Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake.

15  Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye.

16  Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao.

17  NAYE ATATANGULIA MBELE ZAKE KATIKA ROHO YA ELIYA, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa”

Soma pia Mathayo 11:10 na Mathayo 17:10-13, utaona ishara ya ujio wa Yohana mbatizaji kama Eliya.

Hivyo Yohana Mbatizaji alikuwa ni ishara ya kuja kwa Bwana dunia kwa mara ya kwanza kupitia kuzaliwa katika tumbo la bikira.

Na wote walioweza kumwelewa Yohana kiufunuo, walijua kuwa Masihi amekaribia kutokea au hata tayari kashatokea yupo duniani.

  2. Ishara ya kuja kwa Pili: Yaani Unyakuo wa kanisa.

Kabla ya kanisa kunyakuliwa yapo mambo yatakayotangulia kutokea yatakayotambulisha kuwa ule wakati umekaribia au umeshafika, na mambo hayo ni baadhi ya yale yaliyotajwa katika Mathayo 24, na Luka 21 na Marko 13, ambayo ni Tetesi za vita, upendo wa wengi kupoa, maasi kuongezeka na kuzuka kwa manabii wa uongo, ambao watadanganya hata yamkini walio wateule.

Mathayo 24:4  “Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye.

5  Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi.

6  Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado.

7  Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali.

8  Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu”.

Ishara hizi hata sasa zimeshatokea, hivyo tumeukaribia sana unyakuo.

Hivyo kwa walio na macho ya rohoni, wakiziona hizo wanatambua kuwa wapo katika siku za kurudi kwa YESU kwa pili na wakati wowote unyakuo unatokea.

 3. Ishara ya kutokea kwa tatu kwa Bwana: Kila jicho litamwona.

Huu ni wakati ambao kanisa limeshanyakuliwa, na dhiki kuu imepita, na KRISTO anarejea kwaajili ya utawala wa miaka elfu (na atarejea pamoja na watakatifu walionyakuliwa) sawasawa na ufunuo wa Yuda 1:14.

Na atakaporudi basi wale waliomchoma mkuki ubavuni (wakiwakilisha wale wote waliomkataa, waliopo duniani) wataomboleza na kulia, na wataharibiwa kwa mwako wa ujio wake.

Sasa zipo ishara zitakazotangulia kabla ya yeye kutokea mawinguni, na hizi kanisa hawataziona kwani tayari walishanyakuliwa, bali watakaoziona ni wale watakaokuwa wamesalia dunia na  kuipokea chapa ya mnyama.

Luka 21:25 “ Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake;

26  watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika.

27  Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi”.

Na moja ya ishara hizo, zitakazotangulia ambazo zitawafanya watu wa mataifa wavunjike mioyo na kuwaza ni nini kitaukumba dunia, ni jua kuzima (kuwa jeusi) pamoja na mwezi kuwa damu na nyota kuanguka.

Mathayo 24:29 “Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika;

30  ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.

31  Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu”.

Soma pia Isaya 13:9-12 na Ufunuo 6:12-17 utaona unabii wa ishara hiyo na hofu ya mataifa.

Kumbuka tena: Kanisa litakalokwenda kwenye unyakuo halitaona ishara hii ya jua kutiwa giza, na mwezi kuwa damu na nyota kuanguka, kwani ishara hizi zitatokea baada ya dhiki kuu, ambapo kanisa litakuwa halipo, limeenda kwenye unyakuo.

Ndio zaweza kuonekana ishara chache chache mfano wa hizo kama ile iliyotokea katika sehemu za Ulaya mwaka  1780, ambapo giza lilionekana katika sehemu za uingereza, lakini kwa habari ya jua lote kuwa giza, na nyota kuanguka, ni jambo ambao kanisa halitalishuhudia.

Je umempokea YESU na unao uhakika kwamba akirudi leo utaenda naye kwenye unyakuo?.. Kama huna uhakika huo, basi utafute kwa bidii sana.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Kati ya Unyakuo,dhiki kuu, utawala wa miaka 1000 kipi kinaanza

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

SAUTI NYUMA YA ISHARA.

MCHE MWORORO.

HUTATAMBUA LOLOTE, SIKU YA UNYAKUO IKIFIKA.

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments