by Admin | 23 November 2024 08:46 pm11
Somo la nyuma tuliona msingi wa Ukristo ni nini.. kwamba Yesu Kristo Bwana wetu ndiye msingi wenyewe..Yeye huitwa jiwe kuu la pembeni, na mwamba ambao juu yake sisi sote tumewekwa, pasipo Yesu hakuna ukristo. Yeye ndio msingi wa imani yetu.
Lakini pia kikawaida msingi ukishakaa chini, huwa nguzo zinafuata juu yake, kazi ya nguzo ni kulifanya jengo liweze kushikamana na kusimama vema toka juu kwenye paa mpaka chini kwenye msingi wenyewe.
Hivyo wewe kama mkristo ukishaweka msingi chini wa nyumba yako ya kiroho, fahamu pia moja kwa moja utanyanyua na nguzo zake, ili kuliunda jengo. Je nguzo zenye ni zipi?
Hizi ndizo nguzo kuu saba (7), za ukristo .
Ni wajibu wa kila mwamini aliyekombolewa na Kristo, pindi tu alipookoka aanze kukua ki-upendo. Hii ndio nguzo mama, kwasababu Mungu mwenyewe ni upendo (1Yohana 4:8). Zaidi sana anapaswa afahamu kuwa, upendo wa ki-Mungu sio kama ule wa kibinadamu
wa kupenda wanaokupenda, hapana ..huu ni upendo unaozidi usio na sharti wa kujitoa, ambao unapenda mpaka maadui, zaidi na kuwaombea wanaokuudhi.
Mtu asiyejijenga katika huu, haijalishi atajitaabisha vipi kwa Kristo, kazi yake itakuwa ni ya hasara siku ile ya mwisho.
1 Wakorintho 13 : 1-13
1 Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.
2 Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi
cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.
3 Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama
sina upendo, hainifaidii kitu.
4 Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;
5 haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;
6 haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;
7 huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.
8 Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha,
zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.
Ili maisha ya mkristo yasimame vema, maombi ni nguzo nyingine inayomkamilisha. Biblia inasema maombi yanapaswa yawe ni jambo la daima.
Wakolosai 4:2 Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani;
Maombi ni sawa na maji mwilini, au mafuta kwenye gari, vikikosekana hivi vitu hakuna utendaji kazi wowote utakaoendelea, vivyo hivyo ukristo wako usipokuwa wa maombi, hautaendelea sana. Utakufa tu siku moja
Ili tujengeke vizuri kiwango cha chini Bwana alichotaka tuombe kwa siku ni saa moja (Mathayo 26:40). Bwana Yesu alikuwa mwombaji, mitume walikuwa waombaji, sisi yatupasaje?
Ukishaokoka, jambo linalofuata ni kuwa karibu na biblia yako. Katika hiyo utapata kuelewa mpango kamili wa Mungu katika maisha yako. Huku ukisaidiwa na waalimu na wakufunzi wako kwenye usomaji wako wa biblia, kama Bwana wetu Yesu alivyokuwa mdogo akifanya bidii kuwasikiliza waalimu wake.
Kujifunza na kusoma kunapaswa kuwe ni tendo la kila siku. Neno ni kama chakula na maombi ni maji. Hivi viwili ndivyo vinakukuza kiroho na kukujenga nafsi. Hupaswi kuacha kusoma.. Mkristo asiyeifungua biblia yake ni rahisi sana kuchukuliwa na upepo wa ibilisi kwa mafundisho potofu. Kwasababu hamjui Mungu.
Hekima, maarifa, imani, ufahamu,na mamkala vinatoka katika kulijua Neno na mafundisho. Hivyo soma hiyo kila siku, pia sikiliza mafundisho kutoka kwa waalimu wako sahihi wa kweli, kwasababu ni muhimu sana kuvipata.
Matendo 2:41 Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.
42 Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.
1Timotheo 4:13 Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha
Ushirika ni kukutana pamoja na wenzako kujengana. Ushirika ni umoja wa Roho katikati yetu.
Waebrania 10:25 wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.
Kama mtakatifu, hupaswi kujiaminisha utakuwa na utimilifu wote wa ki-Mungu ndani yako kivyako. Utahitaji kukamilishwa na wengine kwa sehemu baadhi, Ndio hapo suala la ushirika linakuja.
Ndio sababu Mungu ameweka karama tofauti tofauti ili tujengane. Katika ushirika mtaombeana, kushiriki meza ya Bwana pamoja, mtafarijiana, mtasaidiana n.k.
Na pia biblia inasema wawili walalapo watapata joto.
Mhubiri 4:9 Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao.
10 Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake
aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua!
11 Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona
moto?
12 Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatuhaikatiki upesi.
Muwapo pamoja kuna ulinzi wa kipekee unaongezeka juu yenu. Hivyo kamwe usijaribu ule ukristo wa kivyako-vyako. Ni lazima tuwe washirika wa kanisa. Kama kanisa la kwanza lilivyoweza kusimama kwa kanuni hiyo.
Utakatifu ni utambulisho wa ukristo. Huwezi kuwa mkristo, halafu ukawa mwovu, huwezi kupokea Roho Mtakatifu halafu sifa za utakatifu usizionyeshe ndani yako. Kwasababu maandiko yanasema Mungu tunayemtumikia ni Mtakatifu hivyo na sisi pia hatuna budi kuenenda katika utakatifu. Bwana Yesu pamoja na watakatifu wa kwanza walizingatia viwango vyote vya usafi na ukamilifu. Vivyo hivyo na sisi
1Petro 1:16 kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.
Ushuhudiaji unaanza pindi tu unapookoka. Kila mkristo ameitwa kuitenda kazi ya Bwana. Na ni lazima afanye hivyo kama sehemu ya maisha yake, ili safari yake ya wokovu hapa duniani iwe imara ni lazima azae matunda. Uwakili ni kazi yetu ya daima. Ukristo bila uinjilisti hauwezi kuwa imara. Kanisa la kwanza lilikuwa la kiinjilisti. Kila mmoja alitambua wajibu wake wa kuisambaza injili kila mahali walipokuwa wakilizingatia lile agizo la Bwana.
Matendo 8:4 Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno.
.
Sifa ya Mungu ni utoaji, ndio maana mpaka leo tunanufanika na mengi katika ulimwengu wake. Hata tulipopotea katika dhambi alijitoa kwa ajili yetu kwa kumtoa mwanawe awe fidia.
Na sisi kujitoa kihali na kifedha kwa ajili ya injili na kanisa la Kristo, ni nguzo muhimu sana. Unawajibu wa kuisapoti huduma inayokukuza kiroho, kwa zaka na changizo zako, pamoja na kuwasaidia ndugu (maskini). Kwasababu, Bwana Yesu na kanisa la kwanza lilikuwa na desturi hiyo.
1 Wakorintho
16:1 Kwa habari ya ile changizo kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo
Hivyo sisi sote tukizitendea kazi nguzo hizo muhimu, basi tuwe na uhakika jengo letu la Imani litakuwa imara sana, linaloweza kustahili tufani na majaribu yote, lililoundwa vyema, kwa utukufu wa Mungu, hata siku ile ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Rudi Nyumbani
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/11/23/nguzo-kuu-za-ukristo-ni-zipi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.