by Admin | 26 November 2024 08:46 am11
Luka 19:37 “Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona,
38 wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu.
39 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako.
40 Akajibu, akasema, NAWAAMBIA NINYI, WAKINYAMAZA HAWA, MAWE YATAPIGA KELELE”
Maana rahisi kabisa ya mstari huo ni kwamba “WANADAMU WAKINYAMAZA KUMSIFU MUNGU, BASI MAWE YATANYANYUKA YAMSIFU MUNGU”
Hii inatupa kuelewa kuwa Mungu haishi kwa sifa zetu, wala sifa zetu si maalumu sana kwake kiasi kwamba asipozipata basi hataendelea kuwa MUNGU, au hataendelea kusifiwa…. la! Ataendelea kuwa MUNGU na kusifiwa na kuabudiwa pasipo hata sifa yangu na yako.
Mimi na wewe tukikataa kumwabudu MUNGU bado yeye atabaki wa kuabudiwa, kwani analo jeshi kubwa la MALAIKA ambao idadi yao ni kubwa kuliko ya wanadamu, hao usiku na mchana wanaanguka mbele zake wakimsifu na kumtukuza, tena katika utakatifu Zaidi ya tulio nao sisi wanadamu..sasa jiulize mimi na wewe tunampunguzia nini Mungu ikiwa hatutataka kumwabudu??.
Isaya 6:1 “Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu.
2 Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka.
3 Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake”.
Hapo anasema “Dunia yote imejaa utukufu wake”… Sasa kama dunia nzima imejaa utukufu wake, ni kitu gani kinachotufanya tujione maalumu sana, kiasi kwamba tusipomtukuza kuna kitu anapungukiwa??
Vile vile tusipotaka kumtumikia yeye hata sasa anatumikiwa na mamilioni ya malaika mbinguni..
Danieli 7:9 “Nikatazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao.
10 Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; MAELFU ELFU WAKAMTUMIKIA, NA ELFU KUMI MARA ELFU KUMI wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa”.
Jiulize mimi na wewe tukigoma kumtumikia, tunampunguzia nini?..Soma pia Yuda 1:14
Vile vile usipomwamini na kumpokea maishani mwako bado yeye atabaki tu wa kuaminiwa..
2Timotheo 2:13 “Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe”.
Hivyo Imani yangu au yako kwake si kwa faida yake yeye MUNGU, kana kwamba amepungukiwa na watu au viumbe vinavyomwamini,…. La! yeye hata sasa anaaminiwa na mabilioni ya malaika mbinguni, na hata shetani na mapepo yake wapo miongoni mwa wanamwamini soma Yakobo 2:19.
Lakini anapotufundisha au kutuhubiria habari za kumwamini yeye, tu kumtumikia, au kumtukuza… hiyo ni kwa faida yetu sisi Zaidi ya yakwake yeye. Anapotufundisha tumwamini mwanae mpendwa ni ili tusiangamie, na pia tupate faida hapa duniani, kwani maandiko yanasema hata haki tuifanyayo au haki tuifanyayo si kwa faida wala hasara ya MUNGU bali yetu sisi na wanadamu wenzetu.
Ayubu 35:5 “Ziangalie mbingu ukaone; Na mawingu yaangalie, yaliyo juu kuliko wewe.
6 Ikiwa umefanya dhambi, umefanya nini juu yake? Yakiwa makosa yako yameongezeka, wamfanyia nini yeye?
7 Ikiwa u mwenye haki, wampa kitu gani? Au yeye hupokea nini mkononi mwako?
8 Uovu wako waweza kumwumiza mtu kama wewe; Na haki yako yaweza kumfaa mwanadamu”
Ayubu 22:2 “Je! Yumkini mtu awaye yote kumfaa Mungu? Hakika yeye aliye na hekima hujifaa mwenyewe.
3 Je! Mwenyezi hupata furaha katika wewe kuwa mwenye haki? Au je, ni faida kwake, kwamba wafanya njia zako kuwa timilifu?
4 Je! Ni kwa wewe kumcha yeye anakukemea? Na kuingia hukumuni nawe?”
Tukiyajua haya basi hatuna budi Kumtumikia MUNGU kwa MOYO, na si kwa kulazimishwa…. tukifahamu kuwa jambo hilo ni WAJIBU WETU, kwasababu tumeumbwa na yeye, vile vile tutamwamini kwa mioyo yetu, tukifahamu kuwa ni kwa faida yetu si yake yeye, vile vile tutamsifu na kumwabudu kwa mioyo yetu yote, tukitambua kuwa pia hiyo ni kwa faida yetu, na wala si kwamba kapungukiwa na sifa.. na ndivyo Mungu atakavyopendezwa na sisi kwasababu TUMEJITAMBUA!!!..
Kama ni mhubiri nenda kahubiri injili kwa bidii zote na pia usidhani usipoenda kuhubiri basi ndio injili haitahubiriwa,.. injili itaendelea kuhubiriwa tu, pasipo mimi wala wewe, Bwana analo jeshi lisiloisha!, na tena la marika yote..
Vile vile usiposimama kumsifu MUNGU kwa sauti yako au kipawa chako, usidhani kwamba ndio umemrudisha nyuma, kinyume chake wewe ndio umejirudisha nyuma kwasababu yeye ataendelewa kusifiwa na kuabudiwa, usiku na mchana..
Vile vile kama ni kumtolea MUNGU mtolee sana, na wala tusidhani kwamba tusipomtolea basi ndio injili yake itasimama, haitasimama bali itaendelea mbele, wala hakuna hasara kwa MUNGU, bali hasara ni kwetu sisi.
Na mambo mengine yote hatuna budi kuyafanya kwa bidii kwa MUNGU kwani ni kwa faida yetu.
Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
SI KWA FAIDA YA MWENYEZI, BALI KWA FAIDA YETU.
TENDA HAKI KWA FAIDA YAKO MWENYEWE.
REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.
Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.
USITAFUTE FAIDA YAKO MWENYEWE BALI YA WENGINE.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/11/26/yeye-atabaki-wa-kusifiwa-na-kuaminiwa/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.