MRUDI MWANAO NAYE ATAKUSTAREHESHA

by Admin | 27 November 2024 08:46 am11

Mithali 29:17 “Mrudi mwanao naye atakustarehesha”.

Kumrudi mtoto sio “kumwadhibu tu”. Bali pia kumrekebisha (Kauli zake na njia zake).

Ni kweli maandiko yanaruhusu kumwadhibu mtoto kwa kiboko pale anapokosea, lakini hiyo iwe hatua ya mwisho baada ya kuona harekebishiki kwa maneno..

Katika hatua hiyo maandiko yameruhusu kutumia mapigo kwa huyo mtoto, ili kuiokoa roho yake na kuzimu.

Mithali 23:13 “Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. 

14 Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu”.

Soma pia Mithali 22:15.

Wengi wanaogopa kuwaadhibu watoto wao kwa mapigo wakiamini kuwa watapata madhara ya kisaikolojia na hata kiafya.. pasipo kujua kuwa hapo biblia imesema ukimpiga “hatakufa”..maana yake Mungu atazuia madhara yote ya kiafya, ikiwa lengo lako si lingine zaidi ya kumjenga.

Lakini kabla ya kufikia hatua hiyo ya matumizi ya fimbo, ni muhimu kuanza na maonyo, na makemeo.

Maana yake kama mtoto amekosea kusema ni lazima arekebishwe kusema kwake mapema, kwasababu watoto wanasikia mambo mengi na kuyachukua tu pasipo kupambanua.

Tuliwahi kufanya maombi sehemu fulani, tukakuta mtoto wa miaka 5 anatukana matusi makubwa na anarudia tusi hilo hilo moja, mara ya kwanza tulidhani ni mtoto ana mapepo, lakini baadae tuligundua kuwa hana mapepo na hata matusi aliyokuwa anayatamka alikuwa hajui maana yake, alitamka tu akidhani kuwa ni maneno ya kawaida, pasipo kujua kuwa alikuwa anatukana.

Sasa mtoto ni kwamba alisikia hayo matusi pengine kwa watoto wenzake anaocheza nao, wasio na maadili na yeye akidhani ni neno la kawaida akalichukua na kulitumia popote alipoona mazingira hayampendezi.

Sasa mzazi hakuchukua jukumu sahihi la kumrekebisha, badala yake tu alianza kumpiga kila alipotaja hilo neno akidhani kuwa anafanya makusudi, na hata sisi tulipofika alitukana na mamaye alimfinya, lakini alipolia bado aliendelea kutukana.

Mama alidhani mtoto anakiburi na mkorofi, kumbe mtoto alilia akijitetea kwa kudhani kuwa lile neno ni sahihi kutamka mahali pale.

Sasa laiti kama mzazi angepata wasaa wa kumketisha na kumwonya na kumwambia anachokisema si sahihi na hakifai, kabla ya mapigo… mtoto angeelewa na kubadilika.

Kwahiyo ni muhimu kuwasikiliza watoto wanasema nini na kuzirekebisha kauli zao mapema,

Ni vizuri kuangalia watoto wako wanachokiangalia na kukikosoa mbele yao kama hakifai…

Pia ni muhimu kufuatilia michezo yao wanayoicheza na kuikemea mapema mbele yao,…..kwani wao ni kuiga tu siku zote…ni vichache wanabuni wenyewe..

Vingi wanaiga kutoka kwa watu pasipo kupambanua, na wanajifunza kutoka kwa watu wanaowazunguka, ikiwemo wanafunzi wenzao mashuleni na pia kupitia Tv.

Kwahiyo kagua maisha ya watoto wako, na “warudi mapema”..wala hawatakuchukia, au kuwashusha kisaikolojia bali utawajenga kwa maisha yao ya baadae..

usipowarudi mapema na wakikua katika misingi hiyo itakuwa ni ngumu kubadilika ukubwani, kwani ile dhambi wameanza kuifanya tangu utotoni na hivyo hawawezi kushawishika kuona madhara yake ukubwani, na ili hali hawakuona madhara yake utotoni.

Mtoto akiwa na kiburi au mtukutu basi mkanye kila wakati, na panapobidi basi tumia kiboko ila usimwache akakua na hiyo tabia.

Na pia akiwa hasikii, tafuta kila namna awe anasikia, usiache na kusema huyu karithi hiyo tabia kwa watu fulani waliotangulia..

Na pia mfundishe kauli za kibiblia, na kuomba, mfundishe

salamu za kibiblia, na misemo ya kibiblia…akue katika hiyo hata kama bado hajaweza kuipambanua lakini mfanye akariri hivyo hivyo kwani itakuja kumsaidia mbeleni kwasababu itakuwa moyoni mwake.

Kwa kumlea hivyo biblia inasema baadaye atakustarehesha..

Mithali 29:17 “Mrudi mwanao naye atakustarehesha”.

Kustarehesha maana yake “hatakuja kukusumbua huko mbeleni”…

Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/11/27/mrudi-mwanao-naye-atakustarehesha/