Wabadili fedha ni watu gani kwenye biblia? (Mathayo 21:21)

by Admin | 29 November 2024 08:46 am11

Mathayo 21:12 Yesu akaingia ndani ya hekalu, akawafukuza wote waliokuwa wakiuza na kununua hekaluni,akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao waliokuwa wakiuza njiwa;

13 akawaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.

Bwana aliwaagiza wana wa Israeli, kwamba waendapo mbele zake mahali patakatifu alipopachagua wakusanyike kwa ajili ya upatanisho. Kila mtu mwenye umri wa miaka ishirini na zaidi atatoa nusu shekeli kama kodi, ambapo fedha hiyo ilitumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za hekaluni .  Hivyo watu wote walipokwenda hekaluni kwa ajili ya ibada, walihakikisha wanabeba sadaka hiyo kwa ajili ya gharama za hekalu.

Utalisoma hilo katika vifungu hivi;

Kutoka  30:11 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

12 Utakapowahesabu wana wa Israeli, kama itakavyotokea hesabu yao, ndipo watakapompa Bwana kila mtu ukombozi kwa ajili ya roho yake, hapo utakapowahesabu; ili kwamba yasiwe maradhi kati yao, hapo utakapowahesabu.

13 Nacho watakachotoa ni hiki, kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa atatoa nusu shekeli kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu; (shekeli ni gera ishirini;) nusu shekeli kwa sadaka ya Bwana.

14 Kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa tangu huyo ambaye umri wake ni miaka ishirini, au zaidi, atatoa hiyo sadaka ya Bwana.

15 Matajiri hawataleta zaidi, wala maskini hawataleta kilichopungua, katika hiyo nusu shekeli, watakapotoa hiyo sadaka ya Bwana, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu.

16 Nawe utapokea hizo fedha za upatanisho mikononi mwa hao wana wa Israeli, na kuziweka kwa ajili ya utumishi wa hema ya kukutania; ili kwamba ziwe ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli mbele ya Bwana, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu.

Lakini sasa kwa sababu fedha hiyo ilipaswa itolewe kwa fedha ya kiyahudi, na si za kigeni, ikizingatiwa kuwa watu walikuwa wanatoka mataifa mbalimbali ulimwenguni kote kuja kumwabudu Mungu pale Yerusalemu, Sasa hawa wanaoitwa wabadili fedha ndio wakapatia hapo fursa ya kuanzisha biashara hiyo pale hekaluni.

Lakini badala ya kufanya kama huduma, kuwasaidia watu kazi hiyo bila riba, wao  wakageuza pale kuwa ni mahali pao pa kujipatia faida, pakawa  kama kiini cha soko la fedha ukanda ule wote. Watu walipokuja na fedha zao, waliwageuzia kwa riba ya juu.

Hiyo ndio sababu Yesu kuchukizwa na wale watu, na kwenda kuzipindua meza zao, pamoja na wale wauza njiwa

Hata sasa, desturi hii ya adui inatenda kazi katika nyumba nyingi za Mungu duniani.

Watu hutumia mambo ya kiibada kama njia ya kujipatia faida. Si ajabu hata Mtume Paulo aliliona hilo akasema,

wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida. (1Timotheo 6:5).

Utakuta mtu anafanya biashara ya biblia, kando kando ya kanisa. Atakuwa radhi kuzitoza bei zaidi ya kiwango stahiki ili ajinufaishe, kwasababu anajua watu wenye uhitaji wa vitabu hivyo kwa watu huo ni wengi. Mwingine atakuwa anauza maji au mafuta (wayaitayo ya upako), lengo sio kuwasaidia hao watu wapokee huduma, bali ni kujipatia faida.

Injili ya Kristo imekuwa biashara, kumwona mtumishi uombewe, ni lazima uandikiwe kuponi ya fedha, vinginevyo huwezi  kumwona.

Sas watu kama hawa Yesu hawezi waonea huruma atazipindua  meza zao, kama tu vile alivyozipundua za wale hekaluni. Maana yeye ni yeye Yule jana, na leo na hata milele.

2Timotheo 3:9 Lakini hawataendelea sana; maana upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile na upumbavu wa hao ulivyokuwa dhahiri.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je! Habari iliyo katika 1Nyakati 21:25, na 2Samweli 24:24, ya Daudi kununua kiwanja  inajichanganya?

UFALME WA MUNGU HAUPATIKANI KIRAHISI.

ALIFANYIKA SADAKA KWA AJILI YETU!

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/11/29/wabadili-fedha-ni-watu-gani-kwenye-biblia-mathayo-2121/