NI NANI TUNAPASWA TUMWONE ZAIDI KILA TUSOMAPO BIBLIA?

by Admin | 1 February 2025 08:46 am02

Je ni nani unayemwona zaidi usomapo biblia?..Je ni Musa?, au Eliya? au Elisha au nabii gani mwingine?..


Je ni habari za nani unapenda kuzihubiri zaidi katika biblia?…

Kama ni taswira za wanadamu ndizo zinazokujia zaidi basi kuna uwezekano macho yako bado hayajafunguka vizuri..

Leo nataka tuangalie ni nani tunayepaswa kumwona zaidi na kumhubiri zaidi kila tusomapo biblia…

Tuyarejee maneno yafuatayo ya Bwana YESU..

Luka 24:25 “Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii!

26 Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?

27 AKAANZA KUTOKA MUSA NA MANABII WOTE, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe”.

Hapa Bwana YESU hakuanza kuwafunulia maandiko kwa kuanza kumtukuza Musa au Eliya na uhodari wao…La! Bali alianza kuelezea habari zinazomhusu yeye mwenyewe..

Wala kumsifu Samson na ushujaa wake, bali kupitia habari za Samson alijionyesha nafasi yake..

Vile vile hakuanza kumsifia na kumtukuza Sulemani na wake zake na mke wake, bali kupitia maisha ya Sulemani alielezea habari zake zaidi..na hivyo hivyo kwa manabii wengine wote, kupitia maisha yao na nyaraka zao alijielezea yeye mwenyewe…

Tuangalie maandiko machache ya manabii yaliyomhusu yeye

》  Nabii Musa aliandika habari za Bwana YESU!!..

Kumbukumbu 18:15 “BWANA, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye”.

》 Nabii Samweli naye aliandika naye habari za Bwana YESU!!..

1Samweli 2:1 “Nami nitajiinulia kuhani mwaminifu, atakayefanya sawasawa na mambo yote niliyo nayo katika moyo wangu, na katika nia yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele ya masihi wangu milele”.

》 Na Nabii Isaya naye aliandika habari za mkuu wa uzima YESU, 

Isaya 9:6 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani”

Soma pia Isaya 7:14.

》 Pia Nabii Mika aliandika habari za YESU..

Mika 5:2 “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele”

》 Bila kumsahau na Daudi naye aliandika habari za YESU.

Zaburi 22:18 “Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura”.

Linganisha na Mathayo 27:35..

》 Nabii Hosea naye hakuacha kumtaja YESU..

Hosea 11:1 “Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri”.

Linganisha na Mathayo 2:14-15.

》 Na Yeremia naye alimzungumzia YESU KRISTO.

Yeremia 31:15 “BWANA asema hivi, Sauti imesikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake; asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako”

Linganisha na Mathayo 2:18.

》Na nabii Zekaria ni hivyo hivyo..

Zekaria 9:9 “Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda”.

Linganisha na Mathayo 21:5.

》 Bila kumsahau Danieli naye alimwona YESU

Danieli 7:13 “Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye.

14 Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa”.

》 Na malaki alimwona pia..

Malaki 3:1 “Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema BWANA wa majeshi”

》 Nabii Yona naye ni hivyo hivyo aliandika habari za YESU..Soma Mathayo 12:40.

》 Nabii Ezekieli alieleza habari zake YESU…Soma Ezekieli 36:26-27 linganisha na Yohana 15:26.

》  Nabii Amos aliandika mahubiri ya yake YESU…Soma  Amosi 8:9 linganisha na Mathayo 24:29.

》 Nabii Yoeli naye alizigusia kazi zake..

Soma Yoeli 2:28-32

》 Ayubu naye alimwona Soma Ayubu 19:25.

Na manabii wengine wote walimwona YESU kabla ya wakati na kuandika habari zake.

Hiyo ni kuonyesha jinsi YESU KRISTO alivyo kiini cha Imani, na kiini cha mafundisho..

Tukiweza kufikia kiwango cha kumwona Bwana YESU zaidi katika biblia zaidi ya mtu mwingine yeyote sisi ni watu wengine na wenye akili, na hapo ndipo tunapoweza kusema kuwa tunaijua biblia..

Luka 24:44 “Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi.

45 Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko”.

Bwana atufune akili zetu tumjue sana Mwana wa Mungu.

Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo”.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/02/01/ni-nani-tunapaswa-tumwone-zaidi-kila-tusomapo-biblia/