Je Bwana YESU alikuwa na amri ya kumwingiza mtu katika ufalme wa MUNGU au hakuwa nayo?

by Admin | 22 February 2025 08:46 am02

Swali: Kwenye Mathayo 20:20-25 Mke wa Zebedayo anamwendea YESU na wanawe akimuomba wakae pande zote za YESU na awape mamlaka alizonazo ila YESU akamwambia hana amri juu ya jambo hilo lakini huku kwenye Luka 23:39 anamwambia mmoja wa wale wanyang’anyi leo hii utakuwa na mimi peponi, naomba ufafanuzi wa mwingiliano huo wa maandiko….Je biblia inajichanganya kwa maneno hayo???…

Jibu: Turejee mistari hiyo..

Mathayo 20:20 “Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno.

21  Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako.

22  Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza.

23  Akawaambia, Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.

24  Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili”.

Hapa tunaona Bwana anatamka kuwa “Hana amri ya kuwaketisha vijana hao upande wa kuume na kushoto katika ufalme wake”

Tusome tena Luka 23:39

Luka 23:39 “Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.

40  Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo?

41  Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.

42  Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.

43  YESU AKAMWAMBIA, AMIN, NAKUAMBIA, LEO HIVI UTAKUWA PAMOJA NAMI PEPONI.”

Sasa swali ni kwanini KRISTO awe na amri juu ya huyu mhalifu na asiwe amri juu ya wale Vijana wa Zebedayo?.

Jibu ni kwamba “walichokiomba wana wa Zebedayo ni tofauti na alichokiomba huyu mhalifu”.. Wana wa Zebedayo wenyewe waliomba nafasi za ukubwa ndani ya ufalme wa mbinguni (kwamba watakapofika mbinguni wakawazidi wengine wote ikiwemo akina Petro na mitume wengine na hata sisi watu wa kizazi hiki)…

Lakini huyu Mhalifu yeye hakuomba ukubwa wowote ndani ya ufalme wa mbinguni kwamba akawe nani huko anakokwenda bali aliomba tu nafasi ya kuuingia ule ufalme wa mbinguni, (habari za kwenda kuwa nani huko aendako hilo hakujali, alichokitamani na kuuingia tu ule ufalme).

Na KRISTO alimpa hiyo nafasi kwani hiyo AMRI anayo kwa watu wote watakaokiri makosa yao Ikiwa na kumwamini Bwana YESU kama alivyofanya huyu Mhalifu. (Na KRISTO alimwambia vile kwasababu alijua hatakengeuka tena, kwani maisha yake ndio yalikuwa yanaenda kuisha, alikuwa amebakisha masaa machache tu ya kuishi).

Lakini wana wa Zebedayo, tayari walikuwa wameshajiwekea hakika wa kuuingia ufalme wa mbinguni, kwasababu walishamwamini Bwana YESU na kutubu kitambo kirefu….na hivyo wakaenda mbali zaidi si kuomba kuuingia ufalme wa mbinguni, bali kuomba nafasi za juu katika huo ufalme wa mbinguni watakaouingia… Jambo ambalo KRISTO asingeweza kuwaahidia.

Ni sawasawa na mwanafunzi anayemwomba mwalimu ampe zawadi ya nafasi ya kwanza darasani na ilihali bado hajafanya mtihani.. Ni wazi kuwa mwalimu hawezi kumpa hiyo zawadi, kwani bado hajafanya/kumaliza mtihani…Matokeo yatakapotoka ndio yatakayoeleza kama anastahili hiyo zawadi ya nafasi ya kwanza au la!.

Na KRISTO hakuwa na amri ya kuwapa hizo nafasi walizokuwa wanazitaka kwani vita vya imani bado walikuwa hawajavimaliza, na ule mwisho bado haujafika, ambapo kazi ya kila mtu itakapopimwa na kupewa thawabu,

Siku ile kama watakuwa wamefanya bora kuliko wengine wote watapata hiyo nafasi waliyoiomba (ya kuketi mkono wa kuume na kushoto), lakini kama watatokea wengine watakaofanya vema kuliko wao, basi wataikosa na nafasi hizo watapewa wengine.

Je umeokoka?

Je unajua kuwa YESU KRISTO anarudi!… na dalili za kurudi kwake karibia zote zimeshatimia?..Je unafahamu kuwa kuishi maisha ya uvuguvugu ni laana? Soma Ufunuo 3:14, leo unaenda kanisani kesho unaenda bar, asubuhi unaimba kwaya, jioni miziki ya kidunia, kwenye kabati una nguo za heshima, na nguo za kikahaba.. Huo wote ni uvuguvugu ambao Bwana YESU alisema matokeo yake ni kutapikwa.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/02/22/je-bwana-yesu-alikuwa-na-amri-ya-kumwingiza-mtu-katika-ufalme-wa-mungu-au-hakuwa-nayo/