1 Petro 4:1 “Basi kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni silaha ya nia ile ile; KWA MAANA YEYE ALIYETESWA KATIKA MWILI AMEACHANA NA DHAMBI”.
Kumbe KUTESWA KATIKA MWILI ndio kanuni ya KUACHANA NA DHAMBI!
Sasa ni nani aliyewahi kuteswa katika mwili na akaachana na dhambi,ili tuuige mfano wake?..
Huyo si mwingine zaidi ya Bwana wetu YESU KRISTO, yeye aliteswa katika mwili na kuachana na dhambi…
Sasa hakuteswa kwaajili ya dhambi zake kwasababu yeye hakuwahi kufanya dhambi, bali Baba alimtwika dhambi zetu na hivyo akahesabika mwenye dhambi kuliko watu wote…..na akateswa kwaajili ya dhambi hizo (za ulimwengu),
Na baada ya kuteswa alikufa,na baadaye akafufuka bila zile dhambi (huo ni muujiza mkubwa sana), kwani aliziacha zile dhambi zote kaburini.
Warumi 6:10 “Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu”.
Na sisi ili tuachane na dhambi ni lazima tufuate kanuni hiyo hiyo, ya KUTESWA, KUFA na KUFUFUKA.
Lakini kwa kuwa hakuna mwanadamu yoyote anayeweza kutembea katika ile njia ya BWANA YESU asilimia mia moja, yeye Bwana katurahisishia zoezi zima hilo la KUTESWA, KUFA na KUFUFUKA.
Kwamba tunapomwamini na kubeba misalaba yetu, na kuukataa ulimwengu (Hapo ni sawa na KUTESWA)..
Vile vile tunapozama katika yale maji mengi wakati wa ubatizo (Hapo ni sawa tumekufa pamoja naye)
Na tunapoibuka kutoka katika yale maji wakati wa ubatizo (Hapo ni sawa tumefufuka pamoja naye).
Wakolosai 2:12 “Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu”.
Na kama hatua hizo tatu (kujikana nafsi na ubatizo) zinalinganishwa kisahihi kabisa na Kuteswa, kufa na kufufuka..basi lile andiko la kwamba “YEYE ALIYETESWA KATIKA MWILI AMEACHANA NA DHAMBI (1Petro 4:1)”. Linafanya kazi hapa hapa..
Wagalatia 5:24 “Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake”.
Sasa ukiona bado dhambi inakutawala kiasi kwamba uasherati una nguvu juu yako, ulevi una nguvu juu yako, uuaji una nguvu juu yako, uchawi, udui, wivu, husuda na mambo mengine yote yaliyotajwa katika Matendo 5:19-20, ni ishara kuwa bado haujausulibisha mwili wako kwa KRISTO, na hiyo ndio sababu dhambi inakutawala.
Suluhisho ni Kujikana nafsi na kubeba msalaba, kisha kutafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la BWANA YESU (Matendo 2:38) na ubatizo wa Roho Mtakatifu.
Ukiyapata mambo hayo matatu dhambi haina nguvu tena juu yako!, kwasababu unakuwa umeifia dhambi..
Warumi 6:2 “Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?”
Ni sawa na mgonjwa aliyekuwa anasumbuliwa na homa, baada ya kupata dawa, ile homa yote inaondoka…Naam ni hivyo hivyo mtu anayejikana nafsi kweli kweli na kumfuata YESU, anakuwa amemeza kidonge cha kwanza cha matibabu ya dhambi inayomtesa, kidonge cha pili na cha tatu ni ubatizo wa maji mengi na ubatizo wa Roho Mtakatifu.
Warumi 6:10 “Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu
11 Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu
12 Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake”.
Bwana akubariki.