Nini maana ya Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, (Wimbo 2:7)

by Devis | 26 July 2025 08:46 pm07

SWALI: Sulemani ana maana gani kusema..Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha,  Hata yatakapoona vema yenyewe.? 

Wimbo Ulio Bora 2:7

[7]Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, 

Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha,  Hata yatakapoona vema yenyewe.


 

JIBU: Mwandishi anaeleza hekima ya kweli juu ya mapenzi halisi yanavyoundwa.. na hivyo anawaasa wale wote wanayoyatafuta…wajue kanuni hizo ili wasiingie katika hasara kama sio majuto.

Andiko hilo linalenga nyanja zote mbili;

  1. Mahusiano ya mwilini (mwanaume na mwanamke)
  2. Mahusiano ya rohoni.(Kristo na Kanisa lake)

Anaposema nawasihi enyi binti za Yerusalemu..

Anawakilisha kanisa, au watu wote wanaotaka kuingia katika mahusiano ya kindoa..

Anasema;

 Kwa paa na kwa Ayala wa porini… Anaapa Kwa wanyama hawa, lakini tunajua mara nyingi kwenye agano la kale watu walikuwa wanaapa kwa jina la Mungu…lakini hapa anatumia wanyama hawa ambapo ni Paa na Ayala.

Ni aina ya swala, ambao kwa eneo la Mashariki ya kati ilikuwa ni kawaida sana kuwaona kwenye mapori tulivu..

Wanyama hawa wana sifa ya:

  1. Upole na umakini
  2. Wanaaibu na kutishika kwa haraka, 
  3. Wana wepesi kwenye kukimbia.
  4. Na wakipotelea porini, si rahisi kuwapata tena.

Hivyo mwandishi anawasihi watu wanapotaka kuingia katika mapenzi wayaone Kama ni kuwawinda Ayala na Paa… Ambao hawahitaji pupa…

Ndio maana anasema; 

“Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe.”

Akiwa na maana kuwa unapochochea mapenzi kwa haraka utayapoteza…mfano tu unapomvamia Ayala kwa pupa, hutampata atapotelea mbali…

Bali unapokuwa mtulivu na kumsogelea kidogo kidogo, ni rahisi kumnasa…

Hivyo Katika mahusiano ya mwilini anatuasa kuwa mahusiano ya kweli, yanajengwa katika muda…sio kwa kuyapaparikia…vijana wengi, wanang’ang’ania kuingia katika mahusiano kabla ya umri sahihi, au nyakati sahihi au wengine wakikutana hata wiki haijakwisha, ndani ya muda mfupi sana, utaona wameshaahidiana kuoana, na hatimaye kujikuta, wapo kwenye mahusiano hayo, kipindi kinapopita na kugundua uhalisia wao, na kasoro nyingi wanaanza kujuta kulitokea nini? Ni kwasababu walikurupukia mapenzi wala hawakuruhusu yaamke yenyewe katika wakati wake.

Lakini katika Roho, Bwana anaeleza mahusiano kati ya yeye na mtakatifu wake..Upendo kwa Kristo thabiti, hujengwa kwa jinsi tunavyokaa na kudumu ndani yake, na kujua sifa zake, tabia zake, na uweza wake, Na hiyo inakuja kwa kusoma Neno, maombi, na ibada…watu wanaotembea katika mambo hayo kwa kipindi kirefu ndio wanaozama katika mapenzi ya kweli na Kristo.

 

Lakini mtu anayempenda Yesu kwasababu kaponywa ugonjwa, au kwasababu kasaidiwa Biashara yake kustawi, au Bwana amemwonekani mahali fulani kipekee, mwingine anamtumikia Mungu kwasababu ya shinikizo fulani la watu…Hapo ni sawa na kumrukia Ayala kwa pupa…hatimaye utamkosa..

 

Watu hawa wanakuwa ni upendo wa kitambo tu, mambo yakishabadilika waanza kusema mioyoni mwao, kama Yesu mwenyewe ndio huyu ni heri nirudie tu maisha yangu ya nyuma…

 

Hiyo yote ni kwasababu alikurupuka…bila kujua sifa na tabia za ampendaye.

 

Usikubali upendo wako kwa Kristo ujengwe kwa matukio ya ghafla…ujenge upendo katika mahusiano ya muda.. ndipo yatakapokuwa thabiti.

 

Wimbo Ulio Bora 2:7

[7]Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu,  Kwa paa na kwa ayala wa porini, 

Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha,  Hata yatakapoona vema yenyewe. 

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> 

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

 

JAWA NA UPENDO UNAOTAFUTA.

USIKAWIE- KAWIE KUUFUNGUA MOYO WAKO

Maombi Maalumu ya Kuombea Ndoa.

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/07/26/nini-maana-ya-msiyachochee-mapenzi-wala-kuyaamsha-wimbo-27/