by Nuru ya Upendo | 9 September 2025 08:46 am09
SWALI: Ayubu alipopata yale majaribu, alimwambia mkewe;
Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Swali ni je! Mambo mabaya yanatoka pia kwa Mungu?
JIBU:
Ayubu 2:10
[10]Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.
Ukweli ni kwamba Mungu hatoi mabaya, bali sikuzote hutoa mema…mabaya huwa yanatoka kwa adui..
Isipokuwa katika kuyapokea mema ya Mungu, yapo mapito ambayo (mbele ya macho yetu), tunayaona kuwa ni mabaya lakini kiuhalisia ni njia tu ya kufikia Mema yetu Mungu aliyotuandalia..wala hakuna lolote linaloharibika..
Angalia mwisho wa Ayubu…kumbe Mungu alitaka kumpatia mara dufu, ya vile alivyokuwa navyo hapo mwanzo, na ndio maana ilinpasa vile vya mwanzo viondoke…
Tengeneza picha miaka mingi baadaye labda tuseme miaka 30 baada ya lile pito, akiwa na watoto wake wapya ambao ni mashuhuri wenye hadhi na nguvu za Mungu..Tena Akiwa Mwenye utajiri mwingi na heshima kuliko mwanzoni..bila shaka huwenda alipokumbuka zile nyakati ambazo alikuwa analia na kusema “ilaaniwe siku ile niliyozaliwa” alikuwa anacheka na kusema Mungu Nisamehe nilikuwa sijui nitendalo!
Yakobo 5:11
[11]Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.
Mungu hutujenga katika nyakati zote nyakati za furaha lakini pia nyakati za mateso.Ukishalitambua hili kama mwana wa Mungu hutasumbuliwa na tufani..Bali utamtukuza Mungu katika mazingira yote,, ukijua kuwa kusudi la Mungu linatimia katika mazingira yote…Wala hakuna lolote linalo haribika..
Nyakati tuzionazo mbaya huleta baraka..majeshi ya washami yalipowazunguka Israeli, mwisho wake ulikuwa ni kuziachilia nafaka na mali kwao, Samsoni alipokutana na Simba, kumbe ni asali aliletewa..mwanamke apatapo na utungu hawezi kusema ni mabaya anapitia, kwasababu anajua kuwa hiyo ni njia tu ya kupata kiumbe kipya duniani.
Vitu kama Saburi, unyenyekevu, upole Mungu anavijenga ndani ya watoto wake katika nyakati kama hizi (ambazo sisi tunaziita ni mbaya)…
Hivyo jifunze kuliona kusudi la Mungu katika nyakati zako zote.
Kwa hitimishi ni kuwa Ayubu aliposema ‘Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya?’
Alimaanisha nyakati za huzuni..ambazo zinatimiza kusudi la Mungu….lakini sio mabaya mfano wa mabalaa na vifo, ambayo mwisho wake ni uharibifu. Mungu kamwe haleti uharibifu kwa mtoto wake, hawezi kutupatia samaki na wakati huo huo kutupatia nyoka.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/09/09/je-tupate-mema-mkononi-mwa-mungu-nasi-tusipate-na-mabaya/
Copyright ©2026 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.