by Nuru ya Upendo | 9 September 2025 08:46 am09
Swali: Kwanini Nabii Yeremia ailaani siku aliyozaliwa?, na je ni sahihi kulaani siku tulizozaliwa?
Jibu: Turejee maandiko hayo kuanzia ule mstari wa 14 hadi wa 17..
Yeremia 20:14 “Na ilaaniwe siku niliyozaliwa, isibarikiwe siku ile aliyonizaa mama yangu.
15 Na alaaniwe mtu yule aliyemletea baba yangu habari, akisema, Umezaliwa mtoto mwanamume; akimfurahisha.
16 Mtu huyo na awe kama miji ile, ambayo Bwana aliiangamiza, asijute; na asikie kilio asubuhi, na kelele za fujo adhuhuri;
17 kwa sababu hakuniua nilipotoka tumboni, na hivyo mama yangu angekuwa kaburi langu, na mimba yake sikuzote nzito”.
Utaona sababu kuu ya Nabii Yeremia kuzungumza maneno yale ni “mateso aliyokuwa anayapitia katika huduma yake”.. kwani alipitia mapigo na vifungo vingi na aliwindwa kila mahali kwasababu ya maneno ya Mungu (Soma Yeremia 20:1-2, Yeremia 37:15-16, Yeremia 38:6, Yeremia 15:5)…kama mstari wa 18 unavyoelezea.
“..18 Nalitoka tumboni kwa sababu gani, kuona taabu na huzuni, hata siku zangu ziharibike katika aibu?”
Na si tu Nabii Yeremia aliyeilaani siku yake aliyozaliwa, bali tunaona pia Ayubu naye alisema hayo hayo..
Ayubu 3:1 “Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake.
2 Ayubu akajibu, na kusema;
3 Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba.
4 Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie.
5 Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe.
6 Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu; Usihesabiwe katika siku za mwaka; Wala kutiwa katika hesabu ya miezi”.
Sasa swali ni je! Walifanya sahihi kuzilaani siku zao?, na sisi je tunapopitia dhiki zilizozidi ni sahihi kuzilaani siku tulizozaliwa na watu waliotuzaa, na matumbo yaliyotuzaa?.
Jibu ni La! Si sahihi kabisa kuzilaani siku tulizozaliwa, wala kulaani matumbo yaliyotuzaa, hata tupitie dhiki kiasi gani?..
Nabii Yeremia na Ayubu walisema maneno yale kwakuwa yalionekana kama ni mambo mapya kwao, kwamba inawezekanaje uwe Nabii uliyetumwa na Mungu, unayesema maneno ya kweli, au inakuwaje uwe mtu wa Mungu, mwelekevu na mkamilifu halafu unakubwa na mambo mazito kama yale?.
Kwahiyo yale yaliyowapata yalikuwa ni mambo mapya kwao, hawakuwa na mifano ya waliowatangulia waliopitia kama hayo katika kiwango hiko, hivyo walisema yale kwa udhaifu wa kibinadamu, lakini hawakuwa sahihi, ndio maana baadaye utaona Ayubu anakuja kutubu, kwa kusema “amesema maneno yazidiyo”
Ayubu 42:3 “Ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa? Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, Mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua.
4 Sikiliza, nakusihi, nami nitanena; Nitakuuliza neno, nawe niambie.
5 Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu linakuona.
6 Kwasababu hiyo NAJICHUKIA NAFSI YANGU, NA KUTUBU Katika mavumbi na majivu”.
Umeona? Hapa Ayubu anakuja kutubia maneno yake, baada ya kumjua Mungu zaidi, na ni hivyo ivyo Yeremia alikuja kuona makosa yake, soma Yeremia 15:18-19.
Na hatuoni tena Ayubu baada ya kuponywa msiba wake wala Yeremia baada ya kustahereshwa wakirudia kusema hayo maneno, hivyo wao walipitishwa katika mapito hayo ili iwe darasa kwetu sisi, kwamba ukiwa mtumishi wa Mungu, au mtu mkamilifu mbele za MUNGU, sio tiketi ya kutopitia majaribu!, LA! Majaribu yanawapata watu wote (wakamilifu na wasio wakamilifu), hivyo hatupaswi kulalamika wala kulaani yanapokuja bali kuomba na kumngoja BWANA.
Na hiyo ndio sababu ya Bwana wetu YESU kuwatahadharisha wanafunzi wake, na hivyo anatutahadharisha hata sasa kwamba tutakapopitia dhiki kwaajili ya Imani tunapaswa tuwe wapole kama hua na wenye busara kama nyoka.
Mathayo 10:16 “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.
17 Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga;
18 nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa”.
Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba si sahihi kuzilaani siku za kuzaliwa au siku nyingine yoyote, wakati wote tunapaswa tuwe watu wenye busara, na watulivu..hakuna faida yoyote katika kunung’unika wala kulalamika.
Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Laana ya torati maana yake ni nini?
JE NI LAANA KULELEWA NA BABA AU MAMA WA KAMBO?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/09/09/kwanini-yeremia-ailaani-siku-yake-ya-kuzaliwa-yeremia-2014/
Copyright ©2025 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.