by Nuru ya Upendo | 13 October 2025 08:46 pm10
Mathayo 20:6
[6]Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?
Bwana Yesu alizungumza mfano ambao unagusia kabisa uhalisia wa kiroho uliopo sasa katika kazi ya Mungu (Ushuhudiaji).
Mfano huo unahusu mtu mmoja aliyetoka asubuhi sana kuajiri wafanyakazi ili kwenda kulilima shamba lake ambalo lilihitaji watu wengi kulihudumia.
Hivyo akatoka alfajiri sana, kuwatafuta na kwa bahati nzuri akawakuta, akawapeleka shambani mwake, akatoka tena saa tatu, akawakuta wengine wamekaa bila kazi, akawatuma shambani, akaenda tena saa sita na saa tisa vivyo hivyo akafanya…Mpaka ilipofika saa kumi na moja akatoka na kuwakuta watu wengine wamesimama tu toka asubuhi mpaka jioni…hawafanyi chochote wapo “Idle”
akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?
Mathayo 20:1-7
[1]Kwa maana ufalme wa mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu.
[2]Naye alipokwisha kupatana na wakulima kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu.
[3]Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi;
[4]na hao nao akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda.
[5]Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile.
[6]Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?
[7]Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu.
Embu jiulize swali moja.. Je! Unadhani watu hawa wa saa kumi na moja hawapo leo?
Kukaa bila kufanya kazi ya Mungu, wakati Kazi ipo kubwa kwa kisingizio kuwa hakuna wa kukuajiri ni ulegevu kiroho… yule Bwana hakuwa na muda wa kusikiliza sababu zao, kwamba waendelee kukaa na kumalizia tu siku kwasababu muda umeenda, bali aliwatuma haraka sana shambani.
1) Hofu ya kutumika
Kusema mimi siwezi, Mimi bado mchanga kiroho, sijui biblia vizuri, Mimi bado mdogo kiumri, mimi siwezi Kuongea nina aibu, nina kigugumizi..sina fedha, sina elimu n.k…haya ndio mambo yanayowakawiisha watu wengi wasimtumikie Mungu..
Ndugu fahamu kuwa Mungu hategemei ukamilifu wetu, kutimiza kusudi lake kamilifu, bali hututumia katika hali zetu hizi hizi, hivyo usingojee siku fulani utakuwa mzoefu ndio umtumikie Mungu..haitafika, anzia na hali yako hiyo hiyo.(1Wakoritho1:26-29)
2) Kungojea muda fulani sahihi.
Kudhani Kuwa upo muda fulani maalimu utaitwa na Bwana rasmi umtumikie, hilo pia limewafanya wengi, kungoja muda mrefu na hatimaye kutoona mafanikio.. saa ya kutumika ni sasa..tayari Wote tulishaitwa tumtumikie yeye tangu siku tulipookoka..ukishaokoka umepewa na vibali vyote na mamlaka ya kumtumikia Bwana..usiongoje utokewe na Yesu kama Paulo Dameski, Usiongoje usikie sauti fulani ikikwambia nenda kawafundishe watu. Anza sasa na Bwana ataungana na wewe mbele ya safari.
3) Masumbufu ya maisha
Mizigo mingi ya kimaisha, utakula nini, utavaa nini, utaishije, linawapunguza watu kasi ya kufikiria kwamba wanahitaji kwanza kuyaandaa maisha yao yawe safi ndipo waamke kwenda kumuhubiri Kristo.
Ndicho walichokifanya wayahudi walipokuwa wanajenga hekalu la pili, ilifika wakati wakaacha ujenzi kila mmoja akaenda kwenye mambo yake, Kwasababu tu, ya kujiangalia hali zao.
Hagai 1:2-4
[2]BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Huu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujenga nyumba ya BWANA.
[3]Ndipo neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema,
[4]Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika?
Usingoje ufanikiwe, uoe, uwe na maisha ndio sasa uanze kuifanya kazi ya Mungu, ukijitazama Sana, hutamtumikia Mungu ndugu.. fahamu kuwa wengi wa wanaokuletea wewe habari njema sio wenye mafanikio, lakini Bwana hawaachi.
4) Ulegevu.
Kupendelea mambo ya kirahisi rahisi, zaidi ya kujitoa..wakati mwingine kukataa kutaabika kwa ajili ya injili..kutaka ijiendeshe Yenyewe, bila kuwa mfuatiliaji na mwombaji, pia hukawiisha utendaji kazi wa injili.
Hivyo, ndugu muda ni mfupi sana, tupo katika saa la kumi na moja yetu, usihudhurie tu kanisani, kuwa sehemu ya utumishi kanisani, usisikilize / kusoma tu mahubiri, hubiri na kwa wengine unachojifunza, Shamba la Bwana linatuhitaji wote.
Ni wakati wa kuamka usingizini, bado hatujachelewa, ikiwa tutatimiza kusudi la Mungu vema, basi tutalipwa sawasawa tu na wale waliowahi..Hivyo amka sasa.. anza kushuhudia.
Shiriki injili kwa kushea na wengine habari hizi
Bwana akubariki
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/10/13/mbona-mmesimama-hapa-mchana-kutwa-bila-kazi/
Copyright ©2025 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.