TENGENEZA NJIA YAKO.

by Nuru ya Upendo | 20 October 2025 08:46 am10

Je unajua sababu nyingine ya MUNGU kuigharikisha dunia ya wakati wa Nuhu?

Mwanzo 6:12 “Mungu akaiona dunia, na tazama, imeharibika; MAANA KILA MWENYE MWILI AMEJIHARIBIA NJIA YAKE DUNIANI

13 Mungu akamwambia Nuhu, MWISHO WA KILA MWENYE MWILI UMEKUJA MBELE ZANGU; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia”.

Umeona? Kumbe sababu nyingine ya Mungu kuigharikisha dunia ni “WATU KUHARIBU NJIA ZAO DUNIANI”.

Njia yako ina maana sana kwako na kwa MUNGU, ukiiharibu au mwingine akakuharibia basi na uwepo wako duniani utakuwa hauna maana..

Sasa Kila mtu anayo njia ya MAISHA YAKE duniani, na NJIA kila mmoja haifanani na ya Mwingine..lakini haijalishi njia ya mtu ipoje mwisho wake inapaswa imfikishe mtu katika Amani, Furaha, Utulivu, Ushindi, uchaji wa Mungu na mwisho Uzima wa Milele.

Lakini mtu aliyepoteza uelekeo wa njia yake, basi anakuwa anaishi katika tamaa za ulimwengu, dhambi, maasi na mwisho wake ni hukumu ya Mungu.

Lakini habari njema ni kwamba, haijalishi MTU kapoteza uelekeo  kiasi gani, au njia yake imeharibika kiasi gani, maadamu anaishi bado anao uwezo wa kuitengeneza na mapito yake yakawa yamenyooka kabla ya kifo, au hukumu ya Mungu kufika..

Mfano wa mtu katika Biblia aliyetengeneza njia zake kabla ya kufa kwake ni Mfalme Yothamu..

2Nyakati 27:6 “BASI YOTHAMU AKAWA NA NGUVU, KWA KUWA ALIZITENGENEZA NJIA ZAKE MBELE ZA BWANA, MUNGU WAKE.

7 Na mambo yote ya Yothamu yaliyosalia, na vita vyake vyote, na njia zake, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.

8 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita huko Yerusalemu.

9 Yothamu akalala na babaze, wakamzika katika mji wa Daudi; na Ahazi mwanawe akatawala mahali pake”.

SASA TUNATENGENEZAJE NJIA ZETU?

     1. Kwa kulitii Neno la Mungu

Zaburi 119:9 “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? KWA KUTII, akilifuata neno lako”.

Neno la Mungu (kwa ufupi Biblia) ndio taa na mwanga wa njia yetu (soma Zab. 119:105), maana yake tukitaka uelekeo wa maisha tunaupata ndani ya Biblia.

Biblia ni kitabu ambacho kimeelezea kwa ufasaha wote wa rohoni na mwilini namna ya kutembea Duniani, na mtu anayesoma Biblia kwa ufunuo kamwe hawezi kupoteza uelekeo wa Maisha, kwani ndani ya Biblia kuna kanuni za namna ya kupata amani, furaha, utulivu, uvumilivu, ushindi, mafanikio na zaidi sana UZIMA WA MILELE.

Mtu anayeikwepa Biblia na maonyo yake tayari kashajiweka katika hatari ya kuharibu njia yake Duniani, na mabaya yatamfikia tu kwasababu njia yake imeharibika..

Yeremia 26:13 “Basi sasa, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, mkaisikilize sauti ya Bwana, Mungu wenu; naye Bwana atayaghairi mabaya aliyoyanena juu yenu”.

Ukitaka kufikia Amani ya maisha yako, lisome na kulitii Neno la Mungu, Biblia inaposema usifanye jambo fulani basi usifanye, vile vile inaposema fanya jambo fulani basi tii na kufanya..njia yako ya Amani utakuwa umeinyoosha, vile vile njia yako ya furaha utakuwa umeinyoosha, vile vile njia yako ya mafanikio yako ya rohoni na pia UZIMA WA MILELE, zipo ndani ya Biblia.

Yeremia 7:3 “Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa”.

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

WhatsApp
DOWNLOAD PDF

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/10/20/tengeneza-njia-yako/