by Nuru ya Upendo | 4 December 2025 08:46 pm12
Yohana 11:44
[44]Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.
Nakusalimu Katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Nataka tujifunze jambo moja Kwa Lazaro aliyefufuliwa…
Kama tunavyojua mtu huyu alikufa, akazikwa na akaoza pia..lakini Bwana Yesu alipofika kaburini Alifanya muujiza mkubwa wa kumfufua.
Na kweli Lazaro alitoka kaburini akiwa mzima kabisa bila shida yoyote…Lakini wengi wetu tunaishia hapo, na kusema Bwana Ametenda muujiza…Lakini Yesu alipomwangalia aliona bado akatoa agizo akisema mfungueni mkamwache aende zake.. Maana yake ni kuwa ufufuo, ulimpa uzima kweli lakini sio uhuru..
Ilihitaji afunguliwe, maana kaburi lilimfunga mikono yake, miguu yake pamoja na uso wake…hata alipofufuka bado liliacha mizizi yake kwa mtu.
Ufufuo unafananishwa na wokovu, Mtu anapomwamini Yesu anakuwa tayari amefufuka kutoka katika wafu…lakini hilo peke yake halitoshi, bado Anakuwa na kamba za makaburini (maisha ya kale), hivyo anapaswa afunguliwe…
Ukiokoka haimaanishi, tabia za kale zote zitaondoka siku hiyo hiyo, unahitaji kukubali kufunguliwa, ili uwe huru kwelikweli..
Sanda, zilizomzinga Lazaro, uso wake, miguu, mikono, kama wavu wa bui-bui, hutembei, Hushiki wala huoni…ndio maisha Ya wakristo wengi baada ya kuokoka yalivyo..
Zile tabia za kale wanaendelea nazo, uchungu, wivu, hasira, uadui, maumivu, vinyongo, hofu, wasiwasi, wanashindwa kuendelea mbele kwasababu hawatoi nafasi ya kufunguliwa…
Angalia hapo Bwana Yesu anasema..”Mfungueni, mkamwache aende zake…”
Hasemi jifungue…bali mfungueni…yapo mambo huna budi kukubali kusaidiwa ili upone..
Ndio hapo Mungu akaweka…Kanisa.
Ambapo..
Utakutana na wachungaji.. kukusimamia na kukulisha mpaka utakapokomaa Na kukua vizuri kiroho…kuishi bila kanisa yaani mwenyewe mwenyewe tu, ni sawa na kutembea na sanda lako,
Kumbuka Bwana anatarajia umzalie matunda mara baada ya wokovu wako…yapo majukumu ya kufanya baada ya kuokoka..lakini ikiwa miguu na mikono na uso umefungwa unatarajia nini hapo?
Kubali kufundishika, Kubali kuchungwa, kubali mashauri na kuonywa, kubali kuombewa, kubali kuishi na ndugu (katika Bwana), kubali kusoma Neno, kuomba na wenzako utafunguliwa sana.. zaidi ya kuridhika tu na wokovu ulioupokea ukidhani utazalisha chochote katika hali hiyo hiyo ya kiroho ambayo upo peke yako peke yako.
Mara nyingine hata maono yako huwezi kuyafikia kwasababu umefungwa miguu yako. usisonge mbele.. Ogopa sanda, kama vile unavyoogopa mauti.
Ukijiona una tabia ambazo haziendani Na hali mpya ya wokovu ulioupokea basi ndio wakati wa kushughulika na sanda lako, kwa kutii na kufuata hayo maagizo. Jiwajibishe, tendea kazi wokovu Wako, kwasababu kila mtu anawajibu wa kufanya hivyo.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Hofu ya Bwana ni nini? (2Wakorintho 5:11)
Sheria ya uhuru ni ipi? (Yakobo 2:12)
Kutawa ni nini? Sawasa na Luka 1:24
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/12/04/unajisikiaje-kutembea-na-sanda/
Copyright ©2025 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.