KARAMA TUZIPATAZO KWA MSAADA WA WATU WENGI.

by Nuru ya Upendo | 3 January 2026 08:46 pm01

Karama kibiblia humaanisha uwezo utokao kwa Mungu wa kufanya/ kutenda mambo yaliyo juu ya uwezo wa kibinadamu katika kutimiza kusudi la ki-Mungu. Karama kwa jina lingine huitwa neema za Mungu.

Kwamfano mmoja huwepa uwezo wa kuponya magonjwa, mwingine unabii, mwingine lugha, mwingine kufundisha, mwingine kukirimu, mwingine uinjilisti N.k.

Sasa neema/karama hizi, zipo za aina kuu tatu.

1) Karama zitokazo moja kwa moja kwa Mungu mwenyewe.

Hii ni aina ya karama(neema) ambayo mtu hupewa sio kwa kuomba, au kupanga au kuchagua…hapana bali Mungu humwita mtu mwenyewe na kuweka wito ndani yake, kwamfano kwenye biblia watu kama Yeremia, Isaya, Mitume na Paulo, walichaguliwa na kupewa neema hizi kwa kusudi maalumu na uwezo maalimu ndani yako, wa kufanya kazi.

2) Karama tuzipatazo ndani ya Kristo.

Hizi hupewa kila mwamini, pindi tu anapoamini na kupokea Roho Mtakatifu. Neema hizi, Roho Mtakatifu Humgawia kila mtu kwa jinsi apendavyo yeye. Ndio hizo tuzisomazo katika (1Kor 12:8-10).

3) Karama tuzipatazo kwa msaada wa watu wengi.

Hii ni aina nyingine ya neema ambayo mtu haipokei kwa jinsi ya kivyake, bali huipokea kwa jinsi anavyohudumiwa na watu wengi ndani ya kanisa la Kristo.

 Ndio hii tunaisoma katika; 

2 Wakorintho 1:11

[11]ninyi nanyi mkisaidiana nasi kwa ajili yetu katika kuomba, ili, kwa sababu ya ile karama tupewayo sisi kwa msaada wa watu wengi, watu wengi watoe shukrani kwa ajili yetu. 

Karama hii huja kwa maombi ya watu wengi.

Na hapa ndipo wengi hupapuuzia kwa viongozi wao. Kwasababu maendeleo ya kanisa, huduma, au madhabahu hutegemea sana uimara wa wale wabeba maono/viongozi…ikiwa wabeba maono hawaombewi kuna viwango hawatavuka hata kama watakuwa na juhudi kiasi gani, watakuwa waombaji kiasi gani, watakuwa waaminifu kiasi gani..kama hawataombewa, watabakia kwenye ngazi fulani sikuzote, lakini viwango vya juu hawatafika.

Kufanikiwa kwa Paulo, hakukutegemea tu wito wake, au utendaji kazi wa Roho Mtakatifu Peke yake, bali pamoja na watu wengi waliokuwa wanamwombea.

Kwamfano huduma hii (nuru ya upendo), inategemea maombi mengi ili iinuke. Ikiwa utaguswa kuchukua muda wako kuiombea maana yake ni kuwa unaitia nguvu viongozi na hatimaye injili inahubiriwa kwa uvumilivu na ujasiri zaidi, na watu wanamwamini Mungu na kumshukuru, matokeo yake yanakuwa kupokea thawabu kwa Mungu kwa zile shukrani.

2 Wakorintho 1:11

[11]ninyi nanyi mkisaidiana nasi kwa ajili yetu katika kuomba, ili, kwa sababu ya ile karama tupewayo sisi kwa msaada wa watu wengi, watu wengi watoe shukrani kwa ajili yetu. 

Sisi (wana nuru ya upendo), na watumishi wengine wa Mungu tunahitaji maombi yenu sana, ili tuihubiri injili kwa ujasiri, kama alivyoomba Paulo.

Waefeso 6:18-19

[18]kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; 

[19]pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili; 

Mungu awabariki

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu.

PALE MAOMBI YANAPOGEUKA KUWA MAPAMBANO.

ENYI WAJINGA, ACHENI UJINGA, MKAISHI

WhatsApp
DOWNLOAD PDF

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/01/03/karama-tuzipatazo-kwa-msaada-wa-watu-wengi/