by Nuru ya Upendo | 19 January 2026 08:46 pm01
Je Mkristo, anapaswa KULEWA?..
Jibu ni NDIO! Anapaswa alewe lakini si kwa MVINYO (yaani kwa pombe)… bali kwa ROHO MTAKATIFU.
Waefeso 5:18 “Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; BALI MJAZWE ROHO”
Roho Mtakatifu ni Kilevi cha Mkristo, ni lazima sote tujae Roho Mtakatifu katika kiwango cha KULEWA KABISA!!.
Ndio maana ile siku ya Pentekoste watu walipopokea ujazo Roho Mtakatifu na kuanza kunena kwa lugha mpya walisomeka kama “Walevi wa mvinyo mpya” mbele ya waliowasikia.
Matendo 2:12 “Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?
13 Wengine walidhihaki, wakisema, WAMELEWA KWA MVINYO MPYA.
14 Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu.
15 Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana;
16 lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli,
17 Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote ROHO YANGU, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto.
18 Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake ROHO YANGU, NAO WATATABIRI”.
Umeona?…Mitume walipopokea ujazo wa Roho Mtakatifu walionekana ni walevi.
Ni kweli kabisa walilewa lakini si kwa mvinyo bali Roho Mtakatifu.
Na maandiko yanazidi kutuonyesha kuwa Roho Mtakatifu, TUNAMNYWA!!.. Ni kinywaji tunachokinywa, na kila kilevi lakini si cha kidunia bali cha kimbinguni.
1 Wakorintho 12:13 “Kwa maana katika ROHO MMOJA sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote TULINYWESHWA ROHO MMOJA”.
Sasa sifa za Mlevi ni zipi?
1. UJASIRI.
Mlevi anapolewa huwa kiwango chake cha ujasiri kinapanda..utaona mtu akishakunywa basi atakuwa anaongea neno lolote linakuja kinywani mwake bila haya, hiyo ni sifa mojawapo ya mlevi.
Na halikadhalika mtu aliyejazwa Roho Mtakatifu, huwa anakuwa ana ujasiri mkuu kuzungumza lolote kuhusu ufalme wa MUNGU aoni aibu, ndivyo tunavyosoma pia katika maandiko..
Matendo 4:31 “Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri”
Hivyo kama umelewa na Roho Mtakatifu basi utaona ujasiri wa kuzungumza habari za Ufalme wa MUNGU pia unaongezeka, ujasiri wa kukemea dhambi unaongezeka, ujasiri wa kusifia mema pia unaongezeka.
2. GANZI
Mtu mlevi, akishalewa anaweza kulala popote hata mtaroni, wala hasikii baridi na wala wadudu kama mbu hawamsogelei, kwanini?..ni kwasababu mwili wake umepata ganzi.
Hali kadhalika mtu aliyejawa na Roho Mtakatifu huwa anapata ganzi katika utumishi, maana yake mazingira yoyote anaweza kwenda katika utumishi wake bali kuona shida mfano wa mtumishi wa Mhngu Mtume Paulo.
2 Wakorintho 11:23 “Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi.
24 Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja.
25 Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini;
26 katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang’anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo;
27 katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi”.
Nasi ni lazima tufe ganzi katika mwili wakati wa kuhubiri injili.
2 Timotheo 4:2 “lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho”.
3.KUNYWA KILA SIKU.
Mlevi halisi haiwezi kupita wiki bila kulewa, atahisi kuumwa!…ni lazima ajaze tanki lake karibia kila siku ili ajisikie vizuri..
Vile vile Mlevi wa Roho Mtakatifu ni lazima ajazwe Roho Mtakatifu karibu kila siku na Roho Mtakatifu anajaa ndani ya watu kwa njia ya maombi na kumsifu MUNGU.
Luka 11:13 “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”
Hivyo maisha ya maombi kwa mtu aliyejaa Roho mtakatifu, yanapaswa yawe sehemu yake daima.
Swali ni je na wewe umeleweshwa na kiti gani??..Ni dhambi? Au Roho Mtakatifu??….Fahamu kuwa ulevi wa pombe matokeo yake ni ufisadi sawasawa na Waefeso 5:18 na hivyo ni upotevu.
Mpokee leo YESU kama bado haujampokea na Ujazwe Roho mtakatifu.
Bwana YESU akubariki sanWashirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/01/19/ni-kipi-kinakulewesha/
Copyright ©2026 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.