UFANYE BIDII KATIKA KUSOMA.

by Nuru ya Upendo | 28 January 2026 08:46 am01

1Timotheo 4:13 “Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika KUSOMA, Kuonya na Kufundisha”.

Wakristo wengi hawapendi “KUSOMA” wanapenda “kusomewa”.. hawapendi “Kujifunza” wanapenda “Kufundishwa” hawapendi “Kujiaminisha” wanapendwa “kuaminishwa”… Kwaufupi wanapenda kutafuniwa na kusaidiwa kila kitu na wanadamu.

Ni kweli MUNGU anatumia watu, lakini “hategemei watu”.. Ukitegemea kusaidiwa kila kitu katika mambo ya rohoni, imani yako itakuwa imesimama juu ya watu, kiasi kwamba Yule mtu unayemtegemea akisomee maandiko, au akufundishe akirudi nyuma wewe nawe ni lazima utarudi nyuma tu.

Akibadilika wewe nawe utabadilika tu, akifa kiroho wewe nawe huna siku nyingi za kuwa hai kiroho.. iko hivyo, kwasababu imani  yako ipo kwake hata kama hukiri hilo.

Lakini Biblia inatufundisha kila mtu “KUSOMA” tena kwa bidii.. sio kusoma Geografia, au hisabati au siasa.. bali KUSOMA NENO LA MUNGU.

ZIFUATAZO NI FAIDA CHACHE ZA KUSOMA NENO LA MUNGU, badala ya kusubiri kufundishwa.

   1. UNAMPA ROHO MTAKATIFU NAFASI YA KUSEMA NAWE.

Unaposoma Biblia binafsi, katika utulivu… kunakuwa kuna “tafakari” za kiMungu zinapita ndani ya kichwa chako, hizo tafakari nyingi zinakuwa ni sauti ya Roho Mtakatifu, kukufundisha kwa kile unachokisoma.

Sasa unaposikiliza mhubiri akihubiri, yeye anazunguza kile Roho alichokiweka ndani yake, na anaposema hawezi kurudia mara mbili, alichokisema kinakuwa kimepita, hivyo huna nafasi ya kutosha wewe kukichakata kile ulichokipokea, labda upate nafasi ya kurudia kusikiliza tena mafundisho yake katika utulivu..

Lakini unapokuwa msomaji wa Biblia, unayo nafasi ya kwenda kituo baada ya kituo huna haraka hivyo inakuwa unampa nafasi nzuri Roho Mtakatifu kusema nawe.

   2. UNAPATA UHAKIKA WA MAMBO.

Ukiwa msomaji wa Biblia binafsi, unakuwa unapata uhakika wa mambo uliyowahi kuyasikia au kufundiswa, kama ni ya kweli au si  ya kweli, lakini usipokuwa msomaji ni ngumu kuhakiki mambo.

   3. UWEZO WA KUUNGANISHA MAANDIKO UNAONGEZEKA.

Unapokuwa msomaji mzuri wa Neno ule uwezo wa kuyaunganisha maandiko, kwamba andiko hili linaladnana na andiko lingine, unapanda!.. hiyo itakusaidia sana kumwelewa MUNGU.

   4. HAMASA YA KUMJUA MUNGU ZAIDI INAONGEZEKA.

Unaposoma mwenyewe Biblia zaidi ya kufundishwa, ile hamasa ya kutaka kumjua MUNGU zaidi inaongezeka, kila mstari unaoumaliza unakupa hamasa ya kuendelea mbele kusoma mwingine, na hiyo ni faida kubwa kwani utajikuta inaipenda Biblia na inakuwa ni kitabu chako.

    5. UNAONGEZA UZOEFU WA KUIJUA BIBLIA.

Unapokuwa msomaji wa Neno uzoefu wako wa kulisoma Neno unaongezeka, ninaposema uzoefu, simaanishi kulizoelea Neno, La!.. bali ile namna ya kujua mpangilio mzuri wa Maandiko na mistari unapanda, hiyo inakuongezea urahisi wa kujifunza Neno la kulielewa.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

WhatsApp
DOWNLOAD PDF

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/01/28/ufanye-bidii-katika-kusoma/