by Nuru ya Upendo | 27 February 2026 08:46 pm02
Yeremia 2:13
[13]Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka maji.
Ndugu Ipo tofauti kati ya chemchemi na birika, chemchemi ni chanzo cha asili ambacho hutoa maji yake yenyewe, haihitaji kuchimbwa, wala kukarabatiwa lakini birika ni hivi visima ambavyo mtu hutumia jasho lake kuchimba na hutegemea mvua ili kuwa na maji, lakini bado huvujisha maji yake chini ya ardhi ndio maana baadaye hukauka…maji ya visima kikawaida hayawagi masafi sana kwasababu hayatembei, ni rahisi kuona vyura, ngala, ruba, tofauti na ya chemchemi.
Sasa Bwana anasema watu wake wamefanya makosa MAWILI. Kwanza wamemuacha yeye aliye chemchemi ya maji ya uzima, Maana yake wana kiu, lakini hawataki maji yaondoayo kiu…hicho huitwa kiburi, au dharau na matokeo ya kiburi ni maangamizi. Ni sawa na mtu anajijua kabisa ni mgonjwa halafu analetewa tiba anasema sinywi dawa zako.
Lakini kama hilo halitoshi, wanaenda kufanya kazi ya kuunda chemchemi zao bandia, kwa kuchimba wenyewe ili wajihifadhie maji yao ambayo ni ya muda…hii ndio huitwa ibada ya sanamu..watu wanapoona fedha inaweza kusimama badala ya Mungu, hiyo ni sawa na kujichimbia birika ..wanapoona elimu, ushirikina, anasa, ulevi, ujuzi..vinatosha kuwa mbadala wa Mungu ni kujichimbia birika lako mwenyewe..
Ndio maana wanataabika, kutafuta ukweli wote ndani yake hawapati, wanapata raha za kitambo baada ya hapo ni majuto kurudi.
Ndugu tulia kwa Kristo ambaye alishamaliza kuunda chemchemi yake, kwake yeye huhitaji kutendea kazi, nenda tu unywe maji, kiu ya dhambi na mambo mengine maovu ya kidunia ife, uishi maisha ya amani na kustawi. Maji hayo ukinywa hata ukifa utakuwa unaishi, na kumpokea Yesu ndio kuyapokea maji. Ukimwamini Yesu na kumfanya Bwana na mwokozi wa maisha yako, na kumtii baada ya hapo ujue ndani ya roho ya maji yameshawasili.
Yohana 4:13-14
[13]Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena;
[14]walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.
Achana na mabiriki.
Mungu atusaidie.
Shalom
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/02/27/shughuli-mbovu-za-uchimbaji-mabirika/
Copyright ©2026 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.