by Nuru ya Upendo | 7 April 2026 08:46 am04
Je ni mafuta gani umepakwa?.
1 Yohana 2:26 “Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza.
27 Nanyi, MAFUTA YALE MLIYOYAPATA KWAKE YANAKAA NDANI YENU, wala HAMNA HAJA YA MTU KUWAFUNDISHA; lakini kama mafuta yake YANAVYOWAFUNDISHA HABARI ZA MAMBO YOTE, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake”
Awali ya yote hebu tuangalie haya mafuta ya kweli ni ya namna gani kabla ya kujihoji kama yamo ndani yetu au la!.
Kama tunavyosoma hapo juu sifa za mafuta hayo Matakatifu ni “kutufundisha”..Na sio tu kutufundisha, bali “kutufundisha mambo yote”..
Hiyo ndio sifa ya kwanza, lakini sifa nyingine ya pili “YANAKAA NDANI YETU” (yaani moyoni).. Na si nje yetu (kwenye ngozi).. Mpaka kufikia hapo tumeshajua kuwa sio mafuta ya chupa au ya upako yanayozungumziwa hapo..bali ni mafuta mengine tofauti kabisa..
Hebu tusogee mbele zaidi kuangalia kimaadiko haya mafuta ni kitu gani na ni kwa namna gani “yanatufundisha habari za mambo yote”..
Kupitia maandiko yafuatayo tutapata majibu…
Yohana 14:26 “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, ATAWAFUNDISHA YOTE, na kuwakumbusha yote niliyowaambia”.
Kumbe kitu peke pekee chenye uwezo wa kutufundisha mambo yote ni Roho Mtakatifu?.
Bila shaka Yale mafuta yanayotajwa na Mtume Yohana katika 1Yohana 2:27 si mengine zaidi ya “Roho Mtakatifu”.
Na tunazidi kulithibitishaje hilo?.
Kwa kuvichunguza vitabu hivi viwili (1Yohana 2:27 na Yohana 14:26). Tunaona vyote vimeandikwa na mtu mmoja ambaye ni Mtume Yohana kwa uongozo wa Roho Mtakatifu.
Sasa isingewezekana kwa Yohana kumaanisha vitu viwili tofauti katika maandiko hayo mawili…bali alimaanisha kitu kile kile kimoja ambacho ni Roho Mtakatifu.
Na Roho Mtakatifu pekee ndiye anayekaa ndani yetu mandiko yanasema hivyo..
1 Wakorintho 3:16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?”.
Soma pia..
2 Timotheo 1:14 “Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu”.
Na ni kwa namna gani “Ajapo Roho Mtakatifu, hamna haja ya mtu kutufundisha”?..
Turejee Waebrania 8:10-12.
Waebrania 8:10 “Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli Baada ya siku zile, asema Bwana; Nitawapa sheria zangu katika nia zao, Na katika mioyo yao nitaziandika; Nami nitakuwa Mungu kwao, Nao watakuwa watu wangu.
11 Nao hawatafundishana kila mtu na jirani yake, Na kila mtu na ndugu yake, akisema, Mjue Bwana; Kwa maana wote watanijua, Tangu mdogo wao hata mkubwa wao.
12 Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na dhambi zao sitazikumbuka tena”.
Roho Mtakatifu ambaye ndiye “Mafuta ya Mungu ndani yetu” anapoingia ndanj ya mtu, yule mtu anakuwa na shauku ndani ya noyo wake wa kumtafuta Mungu mwenyewe, hahitaji kusukumwa na mtu,
Vile vile yule Roho Mtakatifu anakuwa anamfundisha kwa mafunuo ambayo hawezi kuyapata kutoka kwa watu..
Je umepakwa mafuta na Bwana? Ambaye ni Roho Mtakatifu wake?..Kumbuka wote wasio na Roho Mtakatifu hao sio wake kulingana na Biblia (Warumi 8:9).
Na pia huwezi kujua yote pasipo Roho Mtakatifu..
1 Yohana 2:20 “Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote”
Kanuni ya kupokea Roho Mtakatifu, kwa mujibu wa Biblia ni ile iliyotajwa katika Matendo 2:38.
Matendo 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”.
Epuka elimu za uongo za kutumia mafuta ya kupikia au ya mizeituni kuvuta au kuimarisha ukaribu wako na MUNGU, ni hatari kubwa sana.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Mafuta mabichi ni mafuta ya aina gani? (Zaburi 92:10)
Zaburi ya Pili ni nini? (Matendo 13:33).
Je tunajazwaje maarifa ya mapenzi yake? (Wakolosai 1:9)
Biblia inamaana gani inaposema “Mungu wa neema yote” (1Petro 5:10)
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/04/07/je-ni-mafuta-gani-umepakwa/
Copyright ©2026 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.