by Nuru ya Upendo | 22 June 2026 08:46 pm06
Zawadi kubwa na ya kipee alipewa mwanadamu na Mungu, iliyomtofautisha na viumbe vingine vyote, (vya mbinguni na duniani) basi ni Uso wa Mungu.
Ni mwanadamu pekee ndiye aliyeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu (Mwanzo 1:27-28).
Biblia inaposema sura, inafananisha na mfano wa kioo, pale mtu anapojitazama kwenye kioo, anaiona taswira yake vilevile kama yeye alivyo, ikiwa ni mwenye chunusi, basi ataiona chunusi yake kwenye kile kioo, ikiwa ni mweupe vivyo hivyo ndivyo atakavyojiona.
Kwahiyo sisi ni taswira ya Mungu kabisa, lakini ifahamike kuwa taswira hiyo sio hii ya nje, yaani pua, mdogo, masikio, hapana bali ile ya ndani, yaani tabia na sifa alizonazo Mungu, sisi pia tunazo.
Sasa kazi kubwa ya shetani, aliyokuwa nayo kwa Mwanadamu ni kumbadilisha SURA yake. Ili ifanane na kitu kingine tofauti na Mungu.
Na alijua njia pekee na kubwa ambayo hubadili taswira ya mtu, ni IBADA.
Yaani kile ambacho mwanadamu anakiabudu basi moja kwa moja hufanana nacho, wala si kile anachokitazama, au anachokishika, au anachokiangalia Hapana bali kile akifanyiacho ibada, moja kwa moja kinambadilisha taswira yake.
Ndio maana amri ya kwanza na ya pili ambayo Mungu aliwapa watu wake (Kutoka 20), ni kuhakikisha hawajifanyii sanamu ya kuchonga ya aina yoyote na kuiabudu, wala hawawi na miungu mingine, ila yeye.
Kwanini? Kwasababu wamwabudupo yeye, hudumisha tabia zake, na mwonekano wake ndani yao.Lakini wanadamu walipoanza kuabudu miungu, mfano wa Baali, Arishtoreth, n.k. hawakujua kwamba moja kwa moja wanafanana nazo.
Zaburi 115: 4-8
4 Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu.
5 Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni,
6 Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu,
7 Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake.
8 WAZIFANYAO WATAFANANA NAZO, Kila mmoja anayezitumainia
Maandiko yanasema hapo, wazifanyao, hufanana nazo, maana yake Walikuwa vipofu rohoni, viziwi rohoni, wamepooza, kabisa, hawana uhai, ndio maana hata walipokuwa wakihubiriwa Habari za hukumu na manabii hawakuelewa wala kuona ni kitu, hata Kristo alipokuja duniani bado hawakutambua wakati wa kujiliwa kwao, sio kwamba walikuwa wanafanya makusudi, lakini ni kwasababu waliabudu miungu isiyo hai, waliabudu mashetani yasiyojua kesho yao itakuwaje, mizimu isiyojua amani ya kweli ina Ladha gani, mapepo yasiyoweza kuganga mioyo ya watu, mwishowe wakafanana nao, wakawa wakatili, wauaji, wenye wivu .
Lakini tunaposoma biblia tunadhani sanamu ziliabudiwa zamani tu, Hapana, hata sasa sanamu zipo, ambapo zinawakilishwa na vitu vyote vinavyochukua nafasi ya Mungu katika mioyo ya wanadamu.
Fedha, ni sanamu, ukiiabudu ujue utafanana nayo, simu/TV yaweza kuwa sanamu, inapochukua muda wako mwingi, kutazama maudhui zake, na kuacha kabisa kumtafuta Mungu, umeshakuwa mfu hata kama unatembea, mtu anaweza kuwa sanamu, unapomtegemea yeye zaidi ya Mungu, hapo hesabu umelaaniwa.
Lakini unapomwabudu Mungu, yaani unapomtegemea, unapomtii, unapomtumikia, unapomsujudia, ufahamu kuwa ndivyo unavyofanana na yeye, na hatimaye utakuwa hai kama yeye alivyo hai, sikuzote. Mungu anaishi milele, na wewe vivyo hivyo, Mungu ni mweza, na wewe utakuwa vivyo hivyo, Mungu ni mwenye upendo na wewe utakuwa kama yeye.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
KUSUDI LA MUNGU NYUMA YA SAFARI.
AINA ZA FARAJA BWANA AZIACHILIAZO KWA WATUMISHI WAKE.
MTU WA NNE, ANADHIHIRISHWA KWA MOTO
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/06/22/jinsi-mwanadamu-anavyouharibu-uso-wake/
Copyright ©2026 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.