by Nuru ya Upendo | 30 June 2026 08:46 pm06
Ni kawaida Mtu mwenye malengo yake au mpangilio wa ratiba zake, mfano kukatokea mvurugano fulani mambo mengine yakaingilia ratiba zake huwa anakereka sana, na kujiona ameshindwa, kusimamia maono yake.
Lakini kama mwana wa Mungu, si kila wakati mwingiliano wa vitu, ni kutoka kwa adui. Wakati mwingine ni kwa Mungu, hivyo kuliko kulaumu, kuvunjika moyo au kuchukia embu tulia kisha litazame kama mwito wa ki-Mungu, kutimiza kusudi fulani.
Kwamfano kuna wakati Petro alialikwa kwenye nyumba ya Kornelio, katikati ya somo lake, pengine hata watu hawajaelewa vizuri, Roho Mtakatifu akawashukia watu waliokuwa pale wakaanza kunena kwa lugha kabla hata ya kubatizwa, au kuhubiriwa toba, na kuwekewa mikono.
Kama mhubiri angeweza kusema, “Naomba kuwe na utulivu” tusikilize Neno, …lakini Petro alibakia tu kushangaa jambo lile, liliwezekanikaje kwa haraka vile kwa mataifa wasiomjua Mungu kujazwa Roho.,Akaendelea kumwacha Mungu afanye kazi zake.
Bwana Yesu hakuwa mtu wa kulaumu au kukatiza kila mvurugano uliokuja mbele yake, bali alijifunza kutulia na kumsikia Mungu, wenda yupo nyuma ya mwingiliano huo.
Kwa mfano Wakati fulani alikuwa anaelekea Tiro na Sidoni kuwatafuta kondoo waliopotea wa Israelitu, lakini mwanamke mmoja ambaye si mwisraeli aliingilia ziara yake, na kutaka kuhudumiwa…Mwanzoni Yesu hakumsemesha kitu, watu wakasema..achana naye anatupigia kilele, lakini Yeye akatulia kwa muda na kuanza kuhojiana naye..mwishowe akamtendea muujiza ambao mpaka leo tunausoma kama fundisho la imani. Kama angesema achana na mimi, ni marufuku kukusikiliza akaendelea na safari yake…kusudi la Mungu la siku hiyo lisingetimia.
Mathayo 15:22-28
[22]Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.
[23]Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.
[24]Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.
[25]Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie.
[26]Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.
[27]Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.
[28]Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.
Miujiza mingi ya Yesu ilifanyika nje ya ratiba alipokuwa njiani kuelekea katika ziara zake, mafundisho mengine aliyafundisha kulingana na matukio aliyopishana nayo, si yale aliyokusudia kuwaambia watu.
Hii ni kuonyesha kuwa na sisi, sehemu kubwa ya mwito wa Mungu unaweza kuwa katika mambo yanayotuingilia kila siku..
Unaweza kupangilia fedha yako, kwa wiki nzima au mwaka mzima ufanyie hivi au vile…lakini ikatokea tu mtoto wa mjomba ni mgonjwa inahitaji fedha ya matibabu, na ukalazimika kuitoa karibu yote, sasa ni rahisi kulalamika mbona nikiweka malengo sifikii…mbona nikipata tu kinatoka…mbona nikipata kitu kinang’ang’aniwa na wengine, mimi sivitumii.
Kabla hujahuzunika Jifunze kuusikia mwito wa Mungu nyuma ya mivurugano hiyo, kwasababu sehemu kubwa ya maisha yetu ni mivurugano, Na huko huko Mungu hutimiza makusudi yake.
Bwana akubariki.
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/06/30/miingiliano-mingine-ipokee-kama-mwito-wa-ki-mungu/
Copyright ©2026 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.