MAISHA YA IMANI NI KAMA SIFA YA MTI.

by Nuru ya Upendo | 2 July 2026 08:46 pm07

Mti una sifa moja, hautembei kutoka sehemu moja Kwenda nyingine, Utaupanda eneo fulani, utaridhika kubakia hapo hapo, haijalishi ni pabaya kiasi gani, utaenda utarudi miaka na miaka utaukuta pale pale, tofauti na viumbe hai vingine, ambavyo vyenyewe, vikiona hali si nzuri ya mahali, huama na Kwenda kutafuta makazi pengine. Lakini Mti hauna sifa hiyo, na bado utaendelea kustawi na kuwepo kwa miaka mingi zaidi ya viumbe hai vingine,  haijalishi ni kipindi gani kitapita.

Siri ya mti ipo wapi?

Jibu ni kwenye mizizi yake. Ijapokuwa hautembei kwa juu, lakini chini unatembea. Kwa juu utauna upo pale pale, lakini kwa chini mizizi yake ina mwendo, kila siku inaendelea katika safari ya huku na huko kutafutia virutubisho na maji.

Ni nini Bwana anatufundisha katika maisha ya mti.

Yeye hutupanda apendako.

Leo hii ni rahisi kulalamika, kwanini nimezaliwa hili taifa, kwanini hili kabila, kwanini hii familia, kwanini hii jinsia, kama ningezaliwa kwenye nchi ile, kabila lile, familia ile yenye Uchumi mkubwa ningekuwa mbali sana, ningestawi vizuri sana, ningeimarika kiroho kwa kasi kubwa mno… Kama umekuwa na Mawazo hayo, basi kuna tatizo la kiufahamu.

Mafanikio ya mwanadamu hayapo katika mazingira yake sasa. Mafanikio yake yapo katika mizizi yake rohoni. Mti ukikosa mizizi, hata uwe kwenye udongo mzuri kiasi gani hauwezi kukua popote.

Kama mwamini fahamu mzizi uliyopewa inauwezo wa kukustawisha popote, isipokuwa sifa yake ni ile ile yaani huwa haionekani kwa juu, hukaa matopeni, na huzidi Kwenda chini kila siku sio kurudi juu. Vivyo hivyo na sisi tujue nguvu yetu ipo rohoni, (pasipoonekana), Na katika unyenyekevu kwa Mungu wetu kila siku, ndivyo tutakavyoleta ustawi mema wa maisha yetu.

Kunyenyekea kiroho ni mjumuiko wa mambo : kumkubali Kristo, kutii maagizo yake (ikiwemo maombi, ushirika), kuliishi Neno, na kumtumikia yeye.

Huko ndiko kurefusha mizizi.

2 Wafalme 19:30

[30]Na mabaki yaliyookoka ya nyumba ya Yuda yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu. 

Kristo alipaswa aishi Yerusalemu, mji  wenye sifa za kiroho na kisomi, lakini alipelekwa Nazareti , mji mnyonge, lakini huko huko alimzalia Mungu matunda, kwasababu mizizi yake ilienea sana.

Yusufu aliuuzwa utumwani, akawa msikwao, asiye na makazi kule Misri, lakini aliendea kuiimarisha mizizi yake, ijapokuwa kwa nje, hakukuonekana dalili ya badiliko lolote, lakini hatimaye, Mungu akamwinua akawa, mkuu kule kule Misri, Ndivyo ilivyokuwa kwa Danieli, Ayubu na watumishi wa Mungu.

Kabla ya kulalamikia mazingira, jiuliza kwanza je! Mizizi yangu, ipo sawa? Kwasababu haiwezekani mizizi ikawa sawa, mti ukafa. Haiwezekani ukawa mtakatifu halafu ukamezwa na mazingira.

Imarisha kiroho chako.

Shalom.

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

WhatsApp
DOWNLOAD PDF

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/07/02/maisha-ya-imani-ni-kama-sifa-ya-mti/