ZIDI KUTAFUTA UJAZO WA ROHO MTAKATIFU.

by Nuru ya Upendo | 4 July 2026 08:46 pm07

Luka 11:13 “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni HATAZIDI SANA KUWAPA ROHO MTAKATIFU HAO WAMWOMBAO?”.

Kufuatana na maandiko haya, ni wazi kuwa Biblia inatufundisha  ujazo wa Roho Mtakatifu ni jambo endelevu siku zote za maisha ya mtu.

Ikiwa na maana kuwa ni lazima kila siku tujazwe Roho Mtakatifu kila siku kwa kipimo kipya, kwani maandiko yasema yeye hamtoi Roho kwa kipimo (Yohana 3:34) na tena yanasema Tujazwe Roho..

Waefeso 5:18 “Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; BALI MJAZWE ROHO”.

Sasa tunajazwaje Roho Mtakatifu?.

 Si kwa njia nyingine bali kwa kuomba.

Vifuatavyo ni vipengele muhimu katika maombi ya ujazo wa Roho Mtakatifu.

1.      OMBA KUFUNDISHWA NA ROHO MTAKATIFU.

Yohana 14:26 “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, ATAWAFUNDISHA YOTE…”

Unaposoma BIBLIA, Roho Mtakatifu akawe mwalimu wako katika kulielewa vizuri Neno, tenga muda wa kutosha kumwomba MUNGU akakujaze Roho wake wa ualimu.

Watu waliojaa Roho Mtakatifu kweli kweli, wanajifunza Biblia na kuielewa vizuri kwasababu ndani yao Roho Mtakatifu anawafundisha.

Pia wanakuwa ni watu wenye maisha yaliyostaarabika kwasababu ndani yao wanaye mwalimu anayewafundisha kanuni za maisha.

2.      OMBA KUKUMBUSHWA NA ROHO.

Yohana 14:26 “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na KUWAKUMBUSHA YOTE niliyowaambia”.

Kuna mambo uliyowahi pengine kufunuliwa na MUNGU zamani, kwa njia ya Neno au ndoto, na umesahau, unapojaa Roho Mtakatifu, basi atakukumbusha yote aliyekuambia au kukuonesha.

Na sio tu kukumbusha  maneno ya Mungu au maagizo yake bali hata mambo yako mengine ya kimaisha yaliyo ya muhimu, Roho Mtakatifu atakukumbusha na kukutahadharisha.

Hata katika elimu za Dunia, Wanafunzi waliojaa Roho Mtakatifu, ni ngumu kusahau kabisa waliyojifunza, kwani yupo msaidizi ndani yao anayewakumbusha waliyojifunza.

Hali kadhali watu wenye Roho Mtakatifu kweli kweli huwa hawasahau maelekezo au maneno ya Mungu kwani yupo Msaidizi, Roho Mtakatifu anayewakumbusha kila siku.

Kwahiyo tenga muda wa kutosha kuomba unazo wa Roho Mtakatifu ndani yako.

3.      KUONGOZWA NA ROHO.

Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, ATAWAONGOZA awatie kwenye kweli yote….”.

Pia Roho Mtakatifu kazi yake nyingine ni kumwongoza Mtu, nini cha kusema, nini cha kufanya, au ni wakati gani wa kusema na wakati gani wa kunyamaza, ni wakati gani wa kutenda na wakati gani wa kutulia.

Zaidi sana Roho Mtakatifu pia anamwongoza mtu nini cha kusikiliza na nini ambacho hakifai kusikiliza au kufanya..

Na katika maombi pia, Roho Mtakatifu anamwongoza mtu nini cha kuomba na jinsi ya kuomba.

Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo…..”.

Kwahiyo tenga muda wa kutosha kuomba Ujazo wa Roho Mtakatifu, ili uweze kunufaika na tunda hili la kuongozwa na Roho.

4.      OMBA KUFUNULIWA NA ROHO MAMBO YAJAYO.

Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, NA MAMBO YAJAYO ATAWAPASHA HABARI YAKE”.

  Ni muhimu sana kuyajua mambo yajayo yahusuyo maisha yako, kanisa, familia…kwani uishivyo sasa ni kutokana na kile unachokiona mbele yako, na Roho Mtakatifu pekee ndiye awezaye kufunua mambo yajayo ya mtu au watu kwa usahihi.

Kwa mambo haya manne, tutaimarisha  ile safari yetu ya kuenenda kwa Roho.

Wagalatia 5:16 “Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili”.

Bwana atusaidie.

 

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

WhatsApp
DOWNLOAD PDF

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/07/04/zidi-kutafuta-ujazo-wa-roho-mtakatifu/