by Nuru ya Upendo | 12 July 2026 08:46 pm07
Jina la Mwokozi YESU libarikiwe, karibu tujifunze Biblia, Neno la MUNGU wetu lililo taa na Mwanga wa njia yetu (Zab. 119:105).
Sayansi ya mwili inatuonesha kuwa “moyo” wa mtu upo upande wake wa “kushoto”..jambo ambalo ni kweli kabisa, ukiweka mkono wako kufuani utaona moyo ni kama umelalia upande wa kushoto.
Lakini katika roho ni kinyume chake, Kwani Biblia inatufundisha kuwa Moyo wa mwenye hekima upo upande wake wa kulia(kuume), na kinyume chake moyo wa mpumbavu upo upande wake wa kushoto.
Mhubiri 10:2 “MOYO WAKE MWENYE HEKIMA UPO UPANDE WA KUUME; Bali moyo wake mpumbavu upo mkono wa kushoto”.
Sasa kwanini inasema moyo wa mwenye hekima upo upande wake wa kuume na wa mpumbavu upo upande wake kushoto?..
Je kuna ubaya gani moyo kuwepo upande wa kushoto kiroho?.
Jibu ni la! Lakini Kibiblia mkono wa Kuume unawakilisha “WINGI WA SIKU” na mkono wa kushoto unawakilisha “UTAJIRI NA HESHIMA”.
Mithali 3:16 “Ana wingi WA SIKU KATIKA MKONO WAKE WA KUUME, Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto”.
Wingi wa siku unaozungumziwa hapo ni “Uzima wa milele”….kwahiyo mtu mwenye hekima moyo wake utaegemea zaidi kufikiri habari za “Wingi wa siku” yaani uzima wa milele siku zote.
Yaani akose kila kitu lakini si uzima Uzima wa milele/Wingi wa siku..
Lakini kinyume chake mtu mpumbavu moyo wake utakuwa unaegemea zaidi habari za “Utajiri na heshima”..na wala hawazi sana juu ya “Wingi wa siku/Uzima wa milele).
Hawazi baada ya miaka yake kuisha hapa duniani atakuwa wapi huko anakokwenda…
Je moyo wako upo upande gani? Wa “Uzima wa milele” au mali na fahari za dunia?…Upo upande wa kuume au wa kushoto?.
Sasa si vibaya kuwa tajiri na kupata heshima duniani, ni vizuri lakini iwe ni sehemu ya kushoto ya maisha yetu, na si upande wetu wa kuume.
Kwasababu Bwana YESU alisema..
Marko 8:36 “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?
37 Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?”
Kuna faida gani kupata utajiri wote na hauna uzima wa milele?..
Geuka leo hii na ufanye moyo wako ukae kuumeni mwako?..Fikiri zaidi kuhusu uzima wa milele, (wingi wa siku).
Kumbuka YESU anarudi, na uzima huu wa milele upo tu kwake na si kwa mwingine..
1 Yohana 5:11” Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe.
12 Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima”.
Zaburi 110:5 “Bwana yu mkono wako wa kuume; Ataseta wafalme, Siku ya ghadhabu yake”.
Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/07/12/weka-moyo-wako-upande-wako-wa-kuume/
Copyright ©2026 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.