by Nuru ya Upendo | 23 July 2026 08:46 am07
Jina la Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe sana, karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu wetu lililo taa na mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).
Yeremia 18: 1 “Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,
2 Ondoka, ukashuke mpaka NYUMBA YA MFINYANZI, na huko nitakusikizisha maneno yangu.
3 Basi nikashuka mpaka nyumba ya mfinyanzi, na tazama, alikuwa akifanya kazi yake kwa magurudumu. 4 NA CHOMBO KILE, ALICHOKUWA AKIKIFINYANGA, KILIPOHARIBIKA MKONONI MWAKE YULE MFINYANZI, ALIKIFANYIZA TENA KUWA CHOMBO KINGINE, kama alivyoona vema yule mfinyanzi kukifanya”.
Katika mstari wa 4 tunasoma kuwa Mfinyazi alikifinyanga chombo kilichoharibika na kuwa chombo kingine, zingatia hilo neno “chombo kingine” maana yake sio tena chombo kile cha kwanza kilichoharibika.
Tuchukue mfano labda mfinyazi huyu alifinyanga kikombe cha maji hapo kwanza, na baadae akaone kimeharibika au kina kasoro, ndipo anapokivunja vunja kile kikombe cha udongo na kuutia tena maji na kuufinyanga tena kuwa sahani..
Sasa udongo ni ule ule umeweza kutoa chombo kingine kipya tofauti na kile cha kwanza, na MUNGU alimwambia hivo hivyo YEREMIA, lakini Yeremia hayupo sasa, ila sisi tupo, hivyo anatuambia sisi kuwa tujifunze kwa Mfinyanzi kwakuwe yeye (MUNGU) ndiye mfinyanzi mkuu wa maisha yetu.
Yeremia 18: 5 “Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema,
6 Ee nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi huyu alivyotenda? Asema Bwana. Angalieni, KAMA UDONGO ULIVYO KATIKA MKONO WA MFINYANZI, NDIVYO MLIVYO NINYI KATIKA MKONO WANGU, EE NYUMBA YA ISRAELI”.
Je wewe ni chombo cha aina gani?..
Kama maisha yako yametawaliwa na dhambi basi fahamu kuwa ni dhahiri kuwa wewe ni chombo kilichoharibika, kama maisha yako yametawaliwa na ugomvi, uasherati, wizi, masengenyo, kiburi na mambo mengine yote ambayo ni kinyume cha Neno la MUNGU (yaliyotajwa kwenye Wagalatia 5:19-20), huu ni wakati wa wewe kumkimbilia mfinyazi Mkuu YESU KRISTO, akufinyange kuwa chombo kingine cha heshima..
Warumi 9:21 “Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?”
Bwana YESU anaweza kukufanya kuwa mwingine kabisa, mtu wa maana kabisa, ambapo ile hali yako ya ulevi wa pombe au ulevi wa anasa inayokusumbua, kinachotakiwa tu ni kukiri kuwa wewe ni mkosaji mbele zake na unahitaji msaada wake, na baada ya hapo kutubu dhambi zako mbele yake huku ukidhamiria kabisa kuacha mambo yote mabaya, na kumwambia naomba unifinyange tena, kupitia Roho wake mtakatifu atakayeingia ndani yako atakugeuza na kuwa mtu mwingine.
Kumbuka toba isiyo ya kumaanisha haileti matokeo yoyote kwa mtu anayetaka mabadiliko, hakikisha unapotubu dhamiria kujitakasa, kwa kujitenga na vichocheo vyote vya dhambi, kama ulikuwa ni mlevi acha kwenda Bar, kama ulikuwa unajiuza jizuie kwa bidii kwenda vituo vya ulivyokuwa unafanya biashara hiyo, ili uumpe nafasi Roho Mtakatifu ndani yako kukufinganya upya kuwa chombo kingine.
2Timotheo 2:21 “Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema”.
Bwana YESU akubariki sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/07/23/nifinyange-bwana/
Copyright ©2026 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.