Category Archive Uncategorized

MWANANGU, NIPE MOYO WAKO;

Mithali 23:26 “Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu.  27 Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba.  28 Naam, huotea kama mnyang’anyi; Huwaongeza wenye hila katika wanadamu”.

Nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu Kristo. Kwa neema zake karibu tujifunze maneno ya uzima.

Hapo anaanza kwa kusema ‘mwanangu nipe moyo wako’..Halafu baada ya moyo anasema na “macho yako pia yapendezwe na njia zangu”…..Ni kwanini aseme hivyo? Ni kwasababu hapo ndipo kiini cha tatizo sugu la uzinzi kilipo.

Nataka tuone kwa jicho la ndani kwamba kahaba au Malaya anayezungumziwa hapa sio Yule unayekutana naye barabarani,akijiuza, bali ni Yule ambaye amesimama katika macho yako. .. Bwana Yesu alimjua kahaba huyu ndio maana akasema 

Mathayo 5:28  “lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake”

Umeona, huyu anapitia machoni, kisha akishafunguliwa mlango anaingia moyoni mwako kuzini na wewe. Haonekani kwa macho ya kibinadamu, huyu hana gharama yoyote, hatoboi siri, wala hakuzungushi zungushi, wakati wowote ukimuhitaji yupo hapo mlangoni kwenye macho yako anataka kuingia.

Sasa akishapewa  nafasi ya kutosha ndio hapo anapochukua umbile la mtu ili kujidhihirisha kwa nje tu. Ataonekana aidha kwa kumfuata wewe, au yeye kukufuata wewe..sio makahaba wote watakufuata.

Daudi hakufuatwa na mke wa Uria, bali ni yeye ndiye aliyemfuata, mwisho wa siku akatumbukia katika shimbo refu, akajitia unajisi mwenyewe(akajiongezea hila). Ni kwasababu gani? Ni kwasababu alimpa nafasi Yule aliyesimama mbele ya macho yake, alipomwona mwanamke anaoga, badala ayafiche macho yake akimbie mbali, aikatae hiyo hali isiingie moyoni mwake akairuhusu, ndipo kahaba huyo aliyechukua umbile la mke wa mtu akajidhihirisha kwa nje, akamfuata na kwenda kuzini naye.

Samsoni, hakufuatwa na Delila, isipokuwa alivutiwa katika macho yake, alipoona wanawake wa kifilisti ni warembo zaidi ya wakiyahudi,wana maumbile mazuri, wanavaa vizuri, akayatii macho yake..Na ndio hayo hayo yalikuja kupofuliwa baadaye, akatumbukia katika rima jembamba, akafa bado ni kijana.

Sulemani, hakujazuia macho yake, wala moyo wake, Ndio maana akajikusanyia wanawake wengi kwa jinsi alivyopenda, yeye mwenyewe kama alivyoandika katika kitabu cha mhubiri;

Mhubiri 2:10 “Wala sikuyanyima macho yangu cho chote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yo yote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote.

Matokeo yake ikawa ni wao kumgeuza moyo. Na kumkosea Mungu, akaabudu miungu mingine, akawa ni miongoni mwa wenye hila(dosari), katika wanadamu.

Lakini Yusufu, hakuruhusu moyo wake na macho yake yashawishwe na huyu kahaba sugu, hata alipojaribiwa kwa nguvu alikimbia kabisa. Akajiepusha na anguko hilo.

Hii ni kutufundisha nini?

Bwana Yesu alipokitazama kizazi kile, alikiona kama ni kizazi cha Uzinzi (Marko 8:38), sio kwasababu kila mtu alikuwa anazini tu ovyo ovyo huko barabarani, hapana, lakini aliwaona hawa makahaba wa siri wakizini nao mioyoni mwao, 

Tusemeje sasahivi.?

Picha na video za ngono ambazo zimewaharibu watoto na vijana, vipindi vya tv, na tamthimilia na muvi ambazo zinabeba maudhui ya kizinzi ndani yake, vinaongoza matendo haya rohoni.

Kujichua, na mazungumzo mabaya maofisini, mashuleni, na vijiweni  yanaongeza kwa kasi uasherati rohoni. Ni lazima tufahamu Ile kukutana na mvulana/msichana ni matokeo tu ya nje, ambayo hupaswi kujutiwa sana zaidi ya chanzo husika ambacho kinaanzia kwenye macho kisha baadaye moyoni.

Tutawezaje kupona?

Awali ya yote ni kwa kudhamiria kabisa kutubu dhambi zetu na kuuacha ulimwengu, kwa kumkaribisha Yesu mioyoni mwetu. Pili ni kwa kufanya agano na macho yetu, kama alivyofanya mtumishi wa Mungu Ayubu.

Ayubu 31:1 “Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana”?

Usifungue macho yako kushawishwa na kimelea chochote ambacho kinaweza kukusababishia tamaa moyoni  mwako, pambana sana hapo, Ikiwa upo katika ndoa fungua tu kwa mkeo/mumeo..Ikiwa upo nje, usiruhusu kabisa.. weka mipaka na marafiki wa jinsia tofauti, acha kutazama muvi, au picha picha mitandaoni, acha mazungumzo mabaya, ukipishana na mwanamke amevaa kizinzi macho yako yasigeuke nyuma endelea mbele. Kwa kufanya hivyo utafanikiwa kumuua huyu kahaba atokeaye mbele ya macho yako.Na hawa wa nje watakufa wenyewe. Utaishi maisha ya ushindi sikuzote.

Bwana atuponye, Bwana atusaidie.

Mathayo 23:26  “Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi”

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Mruba ni mdudu gani kwenye biblia?(Mithali 30:15)

JE UPANGA UMEINGIA MOYONI MWAKO?

JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

MOTO HUFA KWA KUKOSA KUNI.HATA UASHERATI NAO

LAKINI SISI HATUKUIPOKEA ROHO YA DUNIA.

Konzo la Ng’ombe ni nini? (Waamuzi 3:31).

KIASI NI NINI KATIKA UKRISTO?

Rudi nyumbani

Print this post

USIZISHIRIKI DHAMBI ZA WATU WENGINE.

1Timotheo 5:22 “Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine. Ujilinde nafsi yako uwe safi”.

Hapa tunaona mtume Paulo, anampa Timotheo maagizo ya namna ya kuwa kiongozi bora (Askofu bora) wa makanisa la Mungu. Utaona anampa maagizo ya utaratibu wa kuwaandika wajane, kwamba ahakikishe wanaoandikwa ni wale walio wajane kweli kweli. (soma 1Timotheo 5:9-16).

Pia utaona anampa vigezo vya uongozi kwa viongozi wapya wa makanisa mapya, kwamba wanapaswa wawe wameshuhudiwa kuwa na sifa njema…ndipo awawekee Mikono!, lakini asiwe mwepesi wa kuwawekea mikono kwa haraka.

Na pia viongozi wa makanisa (yaani wachungaji, maaskofu na wote wanaosimama kama viongozi wa kanisa) basi wanapaswa wapewe heshima maradufu, maana yake Wakumbukwe katika riziki na mahitaji yao mara dufu zaidi ya wengine, kwasababu wanakesha kwaajili ya roho za watu, kuwaombea na kuwachunga na kufundisha.

1Timotheo 5:17  “Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha.

18  Kwa maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng’ombe apurapo nafaka. Na tena, Mtenda kazi astahili ujira wake”

Na zaidi sana asikubali Mashitaka ya Wazee kwa haraka, (Juu ya wachungaji, au mashemasi)..isipokuwa kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu.. kwamaana ibilisi anapenda kuwatumia watu kuzusha jambo Fulani la uongo juu ya kiongozi wa kanisa, lengo lake likiwa ni kuliharibu kundi hilo..

Kwahiyo hapa Mtume kwa uongozo wa Roho anamwonya Timotheo asiwe mwepesi kusikiliza au kuamini maneno yazungumzwayo au mashitaka yaletwayo dhidi ya viongozi wa makanisa.. Bali alichunguze jambo kwa makini mpaka atakapopata uthibitisho kamilifu kwa vinywa vya mashahidi wengi.

Lakini la mwisho kabisa Paulo anamwambia Timotheo kuwa ASIZISHIRIKI DHAMBI ZA WENGINE!.

1Timotheo 5:22 “Usimwekee mtu mikono kwa haraka, WALA USIZISHIRIKI DHAMBI ZA WATU WENGINE. UJILINDE NAFSI YAKO UWE SAFI”.

SASA NINI MAANA YA KUZISHIRIKI DHAMBI ZA WENGINE?

Kwanza ni muhimu kufahamu hao “wengine” wanaotajwa hapo ni akina nani?.. Wengine wanaotajwa hapo sio watu wa mataifa (yaani ambao hawajaokoka), la! Bali wengine wanaotajwa hapo ni “watu walio ndani ya Kanisa”. Watenda dhambi hawapo tu Bar!, au kwenye madanguro..bali wapo wengi pia kanisani.

Sasa Mtu wa kanisani anapofanya dhambi na wewe ukaiona na kuifanya kama hiyo hiyo? Maana yake na “wewe umeishiriki ile dhambi”, Kwamfano unapomwona mtu kaingia kanisani kavaa Nusu tupu, au kavaa nguzo zinazobana au zisizo na maadili, na wewe ukaona na ukamwiga, siku inayofuata na wewe ukavaa kama yeye..basi hapo kibiblia umeshiriki dhambi za huyo mwingine, hata kama kanisa zima linafanya mambo yasiyofaa sisi tunapaswa kushiriki dhambi zao, Kwasababu kuna madhara makubwa sana ya kushiriki dhambi za wengine.

Vile vile inawezekana wewe ni Mwimbaji ndani ya kanisa, lakini kuna waimbaji wenzako matendo yao ni ya giza, maandiko yanatuonya tusishiriki dhambi zao, maana yake tusiwe kama wao..

Vile vile wewe kama ni kiongozi (Mchungaji, askofu, shemasi)..halafu ukamwona kiongozi mwingine anafanya mambo yaliyo kinyume na maandiko, aidha ni mla rushwa, au ni mwizi, au mzinzi, au mlevi na anafanya mambo mengine mabaya na wewe ukaiga ule ubaya au ukaufumbia macho..kibiblia umeshiriki dhambi zake huyo kiongozi.

Na hapa Mtume Paulo anamwonya Timotheo kuwa ajihadhari asije akashiriki dhambi za wengine, ajilinde nafsi yake awe safi.

SASA MADHARA YA KUSHIRIKI DHAMBI ZA WATU WENGINE NI NINI?

Unaposhiriki dhambi za mwingine, maana yake MAPIGO nayo mnashiriki sawasawa, na LAANA pia mtashiriki sawasawa, maana yake kama Mungu amemkusudia kumwangamiza kabisa mtu huyo kutokana na tabia yake ya wizi anaoufanya kila siku ndani ya Nyumba ya Mungu, na wewe ukamwiga kwakufanya mara moja moja tu.. basi mtashiriki kiwango cha adhabu sawa.. Wewe unayeiba mara moja moja na Yule anayeiba kila siku wote kiwango chenu cha adhabu kitafanana, kwahiyo utajikuta wewe unayefanya kidogo mnapata adhabu sawa na Yule anayefanya sana.

Ndio maana Paulo anamwonya Timotheo asizishiriki dhambi za wengine, bali ajilinde nafsi yake awe safi.. Na sisi hatuna budi kuzilinda nafsi zetu ziwe safi.. Na tujiepushe na dhambi za wengine.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO

REKEBISHA YAFUATAYO ILI MAMBO YAENDE SAWA.

Bwana alimaanisha nini kusema “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake”?

Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?

Je ni kweli miaka yetu ya kuishi ni 80 tu (kulingana na Zaburi 90:10).

Rudi nyumbani

Print this post

KWA WINGI WA WASHAURI HUJA WOKOVU.

Nakusalimu katika jina kuu lenye uweza la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya Mungu ambayo ndio uzima wetu.

Mungu ana njia nyingi za kuzungumza, anaweza kutumia ufunuo wa roho, anaweza kutumia Neno, anaweza kutumia maono anaweza kutumia mambo ya asili au matukio. Lakini si wakati wote Mungu ataleta majibu kwa kupitia njia hizo. Haijalishi utakuwa ni wa kiroho kiasi gani. Ipo njia nyingine ambayo Mungu huitumia na hiyo tusipoifahamu vema, tutapata hasara ya mambo mengi kama sio kupotea kabisa. Na njia yenyewe ni kupitia mashauri yetu sisi wenyewe tunapokuwa wengi pamoja..

Kwamfano embu tafakari hivi vifungu;

Mithali 11: 14 “Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu”

Maana yake ni nini? Kwamba taifa linapokataa maoni, mapendekezo, mawazo mbalimbali, kutoka kwa wananchi wake, kamwe taifa hilo haliwezi kufanikiwa,

Maandiko bado yanasema..

Mithali 15: 22 “Pasipo mashauri makusudi hubatilika; Bali kwa wingi wa washauri huthibithika”.

Mithali 24:6 “Maana kwa mashauri ya akili utafanya vita; Na kwa wingi wa washauri huja wokovu”.

Maana yake ni nini? Kwamba palipo na vita, ni lazima yawepo maono ya askari wengi, ni jinsi gani watapambana na adui yao, huyu anasema hivi, Yule vile, na mwisho wa siku linatoka jawabu moja madhubuti ambalo litaleta mafanikio makubwa, lakini ikiwa pendekezo linatoka kwa mmoja tu yaani yule mkuu wa kikosi, ni dhahiri kuwa jeshi, litakuwa dhaifu, na matokeo yake ni kupigwa..

Amen.

Hili ni jambo la muhimu sana kwa sisi tulio wakristo. Bwana Yesu aliposema tuwe na umoja, tunie mamoja, alijua kabisa atatumia njia hiyo kuleta majibu ya mambo mengi pasipo hata kusubiria mafunuo au maono.

Utauliza jambo hili lilifanyika wapi katika kanisa kwenye agano jipya.

Utakumbuka, Paulo na Barnaba walipokwenda kuhubiri injili kwa watu wa mataifa, walitokea wayahudi kadha wa kadha, wakaanza kuwaambia mataifa kuwa msipotahiriwa ninyi hamwezi kuokoka()..Hivyo jambo hilo likaleta mkanganyiko mkubwa sana, ikawabidi hadi Paulo na Barnaba warudi Yerusalemu wakasikilize mitume na wazee wanasema nini juu ya hilo.

Hivyo walipofika Yerusalemu, akina Petro na wazee, waliitisha baraza, na kuanza kulitathimini jambo hilo. Je ni sawa watahiriwe na kuishika torati ya Musa au sio sawa.. Sasa maandiko yanatuambia walihojiana sana, huyu anasema hivi, yule vile (Lakini katika amani na upendo, na sio katika mashindano).. na matokeo yake Roho wa hekima akaingia ndani yao, likapatikana shauri moja thabiti. Na kwa kupitia hilo kanisa la mataifa likathibitika sana kwa waraka waliowaandikia, likaenenda katika furaha ya Roho Mtakatifu daima.

Embu tusome pale kidogo, litusaidie…

Matendo 15:7  “NA BAADA YA HOJA nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini.

8  Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia, akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi;

9  wala hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani…..

13  Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni.

14  Simeoni ametueleza jinsi Mungu hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya jina lake.

15  Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa, 16  Baada ya mambo haya nitarejea, Nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, Nami nitaisimamisha;”

Kwa muda wako isome habari yote katika kitabu hicho cha Matendo ya mitume sura ya kumi na tano (15),

NINI BWANA ANATAKA SISI TUJUE  KAMA KANISA?

Lazima  tujifunze wakati mwingine tuwe watu wa Hoja nyingi, mapendekezo mengi, (lakini katika upendo na amani), ili kanisa lijengwe, ili injili ihubiriwe katika ufasaha wote. Kama tulivyosoma hapo juu inavyosema.. “kwa mashauri ya akili utafanya vita; Na kwa wingi wa washauri huja wokovu.” Hatutaweza kushindana na shetani kama tutakuwa hatuna mikakati, na mipango ya mara kwa mara,.

Kila kiungo katika mwili wa Kristo, kina nafasi ya kuchagia mashauri mema. Hivyo tujifunze njia hii, ili Mungu azungumze na sisi. Lakini tukikosa mapatano, “Taifa huangamia”..Sisi hatutaangamia kwa kutii agizo hili.

Bwana alibariki kanisa lake.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Kuwaogopa wanadamu huleta mtego,(Mithali 29:25)

Ni kwa namna gani, upendo husitiri wingi wa dhambi? (1Petro 4:8)

Na ulimi laini huvunja mfupa.(Mithali 25:15)

JE! NINAWEZA KUPOTEZA FURAHA YA WOKOVU?

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

Kama tunaokolewa kwa neema kwanini wokovu tuupate kwa nguvu?

MITHALI AU METHALI ZA BIBLIA

Rudi nyumbani

Print this post

EPUSHA WIVU KATIKA NDOA:

MAFUNDISHO MAALUMU KWA WANANDOA: Epusha Wivu katika ndoa:

Sehemu ya kwanza: Upande wa Mwanamke.

Huu ni mfululizo wa mafundisho maalumu yawahusuyo wanandoa: Ikiwa hukupata sehemu za nyuma, basi waweza kututumia ujumbe kwa namba zetu zilizo chini ya somo hili, tukutumie;

Leo tutaona  jinsi wivu unavyoweza kuathiri kwa sehemu kubwa mahusiano ya wanandoa.

Kibiblia wivu upo wa aina mbili:

1)  Wivu wa kipepo: Ni ule wa kumuonea mtu kijicho, yaani kutotaka, mwenzako kufanikiwa kwasababu wewe hukufanikiwa kama yeye alivyofanikiwa, kutaka kile ambacho mwenzako anacho uwe nacho wewe huku hutaki yeye awe nacho. Biblia imetuonya sana dhidi ya wivu huu, kwasababu ni zao la shetani. Ndio walikuwa nao masadukayo na makuhani kwa Bwana wetu Yesu na mitume wake, pale walipoona neema ya Mungu ipo juu yao kubwa lakini kwao haipo, (Matendo 5:17, Warumi 13:13)

2)  Wivu wa kimahusiano: Wanandoa, Huu ni wivu ambao ni wa asili, Mungu kauweka ndani ya mtu, huu upo katika mahusiano ya kindoa,au maagano Na ndio Wivu ambao Mungu amekiri pia mwenyewe anao.(Kutoka 20:5)..Huu ni wa kuulinda sana, hususani pale unapoingia kwenye ndoa, kwasababu madhara yake ni makubwa zaidi hata ya hasira, au ghadhabu. Biblia inasema hivyo katika..

Mithali 27:4 “Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; Lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu”.

Huu ndio umesababisha watu, kugombana, kuchukiana, kusalitiana  na hata wakati mwingine kuuana, na kuwasababishia matatizo na wengine ambao hata hawahusiki.

Leo  tutatazama, ni kwa namna gani, kinywa cha mwanamke, kinaweza kuwasha wivu mbaya sana, kwa upande wa pili. Na somo linalofuata tutaona tabia ambazo mwanaume anapaswa ajiepushe nazo, kuepukana na madhara ya wivu kwenye ndoa yake.

 hii itakusaida, kuishi kwa amani na utulivu na kuinusuru ndoa yako, .

Sasa embu tusome kisa hichi tunachokiona katika 1Samweli 18:7. Si kisa cha kindoa lakini ni kisa kimuhusucho Daudi na Sauli, Wengi wetu tunajua sababu iliyomfanya Sauli amchukie Daudi, ambaye hapo mwanzo alimpenda ilikuwa ni Wivu. Lakini wachache sana, wanafahamu CHANZO cha wivu huo, kilikuwa ni nini?

Biblia inatupa majibu, kilikuwa ni wanawake, waliotoka na kutoa sifa zao, mahali pasipostahili kwa wakati ule. Embu Tusome.

1Samweli 18:5 “Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; SAULI AKAMWEKA JUU YA WATU WA VITA; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia.

6 Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda.

7 NAO WALE WANAWAKE WAKAITIKIANA WAKICHEZA, WAKASEMA, SAULI AMEWAUA ELFU ZAKE, NA DAUDI MAKUMI ELFU YAKE.

8 Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme?

9 Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile”.

Hicho ndicho kilichokuwa chanzo, cha vita vya Daudi na anguko la Sauli,. Wanawake wale walikuwa wanasema kweli, kwa waliyoyaona, lakini hawakutumia busara kuimba mbele ya mfalme, kwa wakati ule.. Huwenda hata Daudi, alitamani wakae kimya, wasimsifie yeye zaidi ya mfalme wake, mbele ya umati.. Lakini wale wanawake hilo halikuwa akilini mwao. Hawakujua kuwa kumbe nyimbo zao, sifa zao, maneno yao, ni panga ndani ya mioyo ya wakuu wao.

Ndio ikawa sababu ya Sauli kughahiri, hata vyeo vyote alivyompa Daudi, akampokonya na kumfukuza na kutaka kumuua kabisa, kwa kosa tu la wale wanawake.  Lakini kama wale wanawake wangetumia busara, kumwimbia mfalme zaidi, basi Daudi angeendelea kustarehe na kudumishwa katika ufalme ule.

Maana yake ni nini?

Maneno yoyote ya sifa yanayotoka kinywani mwako wewe kama mwanamke, yana matokeo makubwa sana kwa upande wa pili. Sasa tukirudi katika upande wa ndoa, Wivu unatokea pale ambapo unathamini, au unasifia wanaume wengine zaidi ya mume wako. Ukiwa umeolewa tambua kuwa mume wako ndio,bora kuliko wanaume wote ulimwenguni, ndio mwenye sifa zote kuliko wanaume wote ulimwenguni.Hata kama wale wengine wamemzidi yeye kwa kiwango kikubwa kiasi gani, acha kuwazungumza zungumza mbele ya mume wako.

Hii ni kwa faida yako, na kwa wengine. Wanaume wengi wanagombana na marafiki zao vipenzi, kisa tu wake zao,wanapowasifia, wanakuwa mpaka maadui kwa sababu ndogo ndogo tu kama hizi,..Labda utasikia mmoja anasema, “mume wangu,rafiki yako huwa anapendezaga uvaaji wake, yaani navitiwa nao”..Kauli kama hizi ziepuke kinywani mwako, ili kunusuru, urafiki au ujirani wenu.

Kwa ufupi kauli zozote za sifa, zichungumze mara mbili mbili; Unaweza usione shida yoyote, au ukadhani ni jambo dogo tu, lakini upokee huu ushauri utakufaa kwa siku za mbeleni, , hilo jambo linamuathiri sana mwanaume. Usimzungumze zungumze mwanaume mwingine mbele ya mumeo, isipokuwa kwa kiasi, hata wale unaowaona kwenye tv, au unaowasiliana nao kwenye simu. Kumbuka wivu unawashwa na mambo madogo sana.

Bwana akubariki.

Je! Umeokoka? Je! Unauhakika wa maisha yako ya milele baada ya kifo? Kumbuka Kristo yupo mlangoni kurudi, dalili zote zimeshatimia, Huu si wakati wa kumbelezewa tena wokovu, ni wakati wa kujitahidi kuingia ndani ya Safina(Yesu Kristo) kwa nguvu zote, maana muda umekwisha.. Tubu dhambi zako, ukabatizwe mgeukie Bwana akupe uzima wa milele.

Maran Atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Pale mwanandoa mmoja anaposhindwa kutimiza wajibu wake ufanyaje?

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 2: Upande wa wanawake)

WANA-NDOA: Baba Mkwe, Na mama Mkwe.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

Ndoa ya serikali ni halali?

Rudi nyumbani

Print this post

NAFASI YAKO NI IPI KATIKA MWILI WA KRISTO?

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, lihimidiwe milele.

Kwanini leo hii tunaona kama vile utukufu wa Mungu umepungua makanisani?..Tunamwita Yesu aponye lakini haponyi, tunamwita atende miujiza lakini hatendi, tunamwita afungue watu lakini hawafungui kikamilifu? Ni kwanini?

Ni kwasababu yeye mwenyewe ni mgonjwa, yeye mwenyewe ni mlemavu, ana chechemea, hana masikio, yeye mwenyewe ni kipofu, yeye mwenyewe ana kisukari, amepooza, ana saratani, na homa ya ini, sasa atawezaje kuwaganga wengine? Angali yeye mwenyewe ni muathirika wa hayo mambo?

Tunashindwa kufahamu sisi tuliookoka ni viungo vya Kristo, na kila mmoja anayo nafasi ya kuujengwa mwili huo mpaka ukamilike, ili yeye kama kichwa atakaposhuka juu ya mwili wake, awe na uwezo na nguvu za kutosha kutembea na kutimiza wajibu wake, wa kuwahudumia na kuwafungua watu wake, kama alivyofanya alipokuwa hapa duniani.

Lakini changamoto tuliyonayo, ni pale tunapodhani kuwa wote, tunaweza kuwa miguu, wote tunaweza kuwa macho, wote tunaweza kuwa midomo,..Hivyo tunaelekeza bidii zetu zote, kuwa kiungo kimojapo ya hivyo.. Na hiyo yote ni kwasababu hivyo ndivyo vinavyoonekana vina utukufu kuliko vingine, kisa tu vipo kwa nje.

Lakini tunasahau kuwa mwili, hauundwi kwa viungo vya nje tu, bali pia na vile vya ndani. Na zaidi sana vile vya ndani ndio vinaumuhimu sana, na ndio maana vimefichwa na kufunikwa na vya nje, kwasababu hivyo vikipata hitilafu tu..hata hivi vya nje haviwezi kufanya lolote.

Kwamfano moyo, ukifeli, jiulize macho yako, mikono yako, miguu yako, itakuwa na kazi gani?.. Uti wa mgongo ukifeli, mwili wote utapooza, huo mkono utawezaje kusogea?..figo zimefeli, ni nini utakachokuwa unasubiri kama sio kifo..Lakini mguu mmoja ukifeli, mwili bado unaweza kuendelea kuishi..

Biblia inasema..

1Wakorintho 12:22 “Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi.

23 Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana”.

Si kila mtu, atakuwa mchungaji katika kanisa ndio awe kiungo bora cha Kristo, si kila mtu atakuwa mwalimu, si kila mtu atakuwa nabii, au shemasi au mwimbaji..ikiwa wewe unajiona kama huwezi kusimama katika mojawapo ya nafasi hizo, haimaanishi kuwa wewe sio kiungo, suluhisho sio kujitenga na mwili wa kristo..huwenda wewe ni moyo, au figo au ini, au uti wa mgongo.. embu angalia ni nini unaweza kukifanya ukusanyikapo na wenzako..ni nini unaweza kuchangia katika mwili huo uliowekwa na Bwana..

kama ni kufuatilia na kusimamia ratiba na vipindi vyote vya kanisani, kama ni kuhamasisha na kuwaunganisha washirika, kama ni kuchangia kwa bidii kwa mali zako, kama ni kuongoza watoto, kama ni ulinzi, kama ni usafi, kama ni kuongoza maombi na mifungo..n.k. uwapo mbali au uwapo karibu. Hakikisha unafanya kwa bidii zote na sio kwa ulegevu..

Wafilipi 4:8 “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.

9 Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, YATENDENI HAYO; NA MUNGU WA AMANI ATAKUWA PAMOJA NANYI”.

Lakini usikae tu, mwenyewe, na kuwa mtu wa kwenda tu kanisani na kurudi nyumbani, kama mtembeleaji tu..miaka nenda miaka rudi, utawalaumu viongozi, utalilaumu kanisani, kumbe shida ni wewe ambaye hujasimama katika nafasi yako.  Kama ‘mapafu’ umejitenga kivyao,unaliangalia kanisa la Kristo likipumulia mirija.

Tubadilike, sote tujiwajibishe, ili Kristo ashushe utukufu wake kama kanisa la mwanzo. Hivyo ili Kristo atukuzwe, na aweze kutenda kazi yake, sote kwa pamoja tuje katika nia moja ya Kristo, kisha kila mtu asimame katika nafasi yake, Kristo akamilike, ndipo tuone matendo yake makuu, akiyatenda kama alivyofanya katika kanisa la mwanzo.

Bwana awe na nasi. Bwana awe na kanisa lake takatifu.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Matulizo ya mapenzi ni nini? (Wafilipi 2:1).

DHAMBI ILIYOMKOSESHA SHETANI:

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

Maongeo ni nini?(Wakolosai 2:19)

USHAURI KWA MWANAMKE WA KIKRISTO.

Rudi nyumbani

Print this post

Asiyetawala roho yake Ni mfano wa mji uliobomolewa,

SWALI: Nini maana ya maandiko haya?

Mithali 25:28 “Asiyetawala roho yake Ni mfano wa mji uliobomolewa, usio na kuta”.

JIBU: Mstari huu unatupa picha jinsi mtu asiyeweza kuitawala roho yake anavyoonekana rohoni.Hapo anasema, roho yake imefanana na mji uliobomolewa usio na kuta..

Zamani, miji mikubwa ilipojengwa ilikuwa ni lazima izungushiwe kuta kubwa na ndefu.. Yerusalemu ulizungushiwa kuta, Babeli ulizungushiwa kuta, Yeriko ulizungushiwa kutwa n.k.  Na lengo la kufanya vile ilikuwa ni kuulinda mji dhidi ya wavamizi, na wapepelezi, wasiingie kokote tu watakako na kuushambulia mji.

Ni vijiji na vimiji vidogo tu ndivyo vilikuwa havina kuta zinazozunguka..lakini miji yote ilikuwa ni lazima iwe na sifa hiyo.

Sasa na rohoni ndivyo ilivyo, ikiwa na maana, kama wewe si mtu wa kuitawala roho yako, ni sawa na ule mji usio na kuta..Na matokeo yake ni kuwa upo hatarini kuvamiwa na kila aina ya maadui zako wa rohoni.

Ukishindwa kuizuia roho yako na tamaa za huu ulimwengu..Kwamba kila kitu unachojisikia kukifanya, wewe unafanya, kijisikia kuzini unakwenda kuzini, ukijisikia kunywa pombe unakunywa.. ukijisikia kuvaa vimini unavaa, ukijisikia kuvaa suruali unavaa, ukijisikia kutumia mkorogo unatumia, fahamu kuwa, utakuwa ni makao ya mapepo yote mabaya duniani.

Kwasababu roho yako haina ulinzi. Ndugu si kila kitu unachokiona, ukifanye, au ukiangalie, au ukisikilize, unapokesha muda wote kwenye tamthilia,  kwenye simu unachati, lakini muda wa kuomba huna, muda wa kujifunza Neno huna.. Wewe ni mji usiokuwa na ukuta..

Utaombewa leo, mapepo yatatoka, lakini kesho yatarudi tena mengine mengi tu, tatizo ni hilo, umefungua malango kwa kila roho inayojisikia kukuingia ..kwasababu umeshindwa kuitawala roho yako. Leo rafiki yako anakuja kukwambia tukabeti, na wewe bila kufikiri unakimbilia huko, unatazama picha za ngono, unasikiliza miziki ya kidunia, ni lazima uvamiwe na mapepo.

Mithali 4:23 “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima”.

Hivyo ni lazima tujifunze kuzitawala roho zetu, sawasawa na maandiko yanavyotasa.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JINSI YA KUUHARIBU UJANA WAKO.

Ninawi ni nchi gani kwasasa?

Je! Ni dhambi kwa kijana aliyeokoka kuvaa suruali za kubana (model), kunyoa mitindo (mfano kiduku), ?

Kisima cha joka na lango la jaa ni nini?(Nehemia 2:13)

NJIA YA ‘UTAJIRI MKUU’ KWA KIJANA.

Nini maana ya kumpenda Bwana kwa moyo,roho, akili na nguvu zetu zote?

Ufisadi ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

Afadhali mtu akutwe na dubu aliyenyang’anywa watoto wake.

Mithali 17:12 “Afadhali mtu akutwe na dubu aliyenyang’anywa watoto wake, Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake”.

Mpumbavu kibiblia ni mtu yeyote ambaye amekataa sheria ya Mungu na Maarifa. Yaani kwa ufupi mtu asiyetaka kumjua Mungu wake ni mpumbavu. Mtu wa namna hii hatabiriki, kwasababu shetani ndiye anayekuwa bwana na kiongozi wa Maisha yake, sio Yesu..

Kwamfano Mithali 10:23 inasema..

“Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo; Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima”.

Sasa hapo biblia inaposema ni heri ukutane na dubu aliyenyang’wanya Watoto..inatupa picha jinsi gani mpumbavu alivyo hatari kuliko hata mnyama mkali dubu. Kwa kawaida dubu si mnyama mpole, na tena ukali wake unazidi pale anapokuwa na Watoto, lakini ukali huo unavuka mipaka pale anaponyang’anywa Watoto wake,Utakumbuka kile kisa cha Elisha kuwalaani wale vijana..biblia inasema arobaini na wawili kati yao waliraruliwa na dubu wawili tu jike.

Kutupa picha jinsi gani walivyohatari Wanyama hawa.. Lakini biblia inasema heri  ukutane nao kuliko mpumbavu. Mfano wa wapumbavu katika biblia ni Herode, ambaye kwa wivu wake aliwaua watoto wote, waliokuwa Yerusalemu kipindi cha kuzaliwa kwa Bwana Yesu, kama hiyo haitoshi alimuua na Yohana mbatizaji, Pamoja na Yakobo mtume wake Bwana.

Wapumbavu ndio wale wale waandishi na mafarisayo, ambao walikuwa wanazunguka huku na huko , na kuwafanya watu kuwa waongofu wapya wa dini zao, na mwisho kuwafanya  wana wa jehanamu mara mbili kuliko wao.(Mathayo 23:15).

Wapumbavu ndio manabii wa uongo walio sasa, ambao wanawatumainisha watu kuwa Mungu anawapenda wakiwa na mali au mafanikio, lakini hawakemei dhambi, na matokeo yake wengi wanakufa na kujikuta kuzimu, kwasababu walidanganywa na hila zao.

Vilevile Mpumbavu ndio mpinga-kristo atakaye kuja, ambaye ataundanganya ulimwengu mzima waipokee chapa yake, na hiyo itapelekea jopo kubwa sana la watu kufuatana naye kuzimu..Sasa biblia inasema ni heri ukutane na dubu aliyenyang’anywa Watoto wake, ambaye atakurarua tu mwili wako , baada ya hapo hawezi kukuathiri zaidi, lakini hawa, wanakurarua hadi na  roho yako, kwa kukupeleka kuzimu.

Ndio maana Bwana alisema tujiepushe naosana..

Mathayo 7:15 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.

16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?

17 Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.

18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.

19 Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.

20 Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.

21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”.

Soma NENO, dumu katika hilo, ndio salama yako nyakati hizi.. kwasababu tunaishi katika kipindi cha hatari sana. Ukiwa mvivu, utakwenda na maji yao.(Mathayo 24:24)

Bwana atusaidie..

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Mpumbavu ni nani katika biblia? (Zaburi 14:1, Mithali 10:14)

Kwanini wale dubu waliowauwa vijana wa Elisha walikuwa wa kike?

NINI MAANA YA SISI KUWA WATOTO WA MUNGU?

MAISHA ULIYOPITIA NYUMA NI USHUHUDA TOSHA WA WEWE KUMTUMIKIA MUNGU.

Nini maana ya kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua (Mithali 13:12)?.

Mruba ni mdudu gani kwenye biblia?(Mithali 30:15)

Rudi nyumbani

Print this post

Tajiri na maskini hukutana pamoja; BWANA ndiye aliyewaumba wote wawili.

SWALI: Nini maana ya huu mstari? 

Mithali 22:2

[2]Tajiri na maskini hukutana pamoja;  BWANA ndiye aliyewaumba wote wawili.


JIBU: Pamoja na kwamba kutakuwa na kutokuelewana baina ya makundi haya ya watu..Maskini atamwonea wivu tajiri, na tajiri atamdharau maskini..Lakini katika hayo yote bado tu kila mmoja atamhitaji mwenzake…atakutana na mwenzake mahali fulani tu katika maisha..

Maskini atamfuata tajiri ampe kazi, vilevile tajiri atamtegemea maskini amwoshee gari lake, amfulie nguo zake, amlimie bustani yake.n.k Hivyo kila mahali uendapo makundi yote utayapata .. Na sababu tayari biblia imeshaitoa..”Kwamba Bwana ndiye aliyewaumba wote wawili”Akawaweka hapa duniani..wala mmoja hakumweka mawinguni, mwingine ardhini.

Hii ni kufunua kuwa tumewekwa kusaidiana, wala hakuna mtu anaweza kujikidhi yeye mwenyewe kwa kile alichonacho pasipo mwingine..zaidi sana yule ambaye unamwona hakufai ndiye atakayekufaa sana wakati fulani. Kwasababu ni Mungu ndiye aliyetuumba sote, mmoja hakuumbwa na shetani, na mwingine Mungu.

Hivyo hekima inatufundisha tukae kwa utulivu, tuthaminiane sisi kwa sisi

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KWA KUWA WASEMA MIMI NI TAJIRI.

Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

Azidishaye mali yake kwa riba, Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini.

JE! NINAWEZA KUPOTEZA FURAHA YA WOKOVU?

Mimi ni mweusi-mweusi, lakini ninao uzuri.

Vyombo vya uzuri ni vipi vinavyotajwa katika biblia?

Rudi nyumbani

Print this post

Mambo yale yaliyo mbali, na yale yaendayo chini sana,

SWALI: Je! maneno tunayoyasoma katika Mhubiri 7:24, yana maana gani?

[24]Mambo yale yaliyo mbali, na yale yaendayo chini sana, ni mtu yupi awezaye kuyatafuta?


JIBU:  Hapo Kuna vitu viwili.. 

1) Yale yaliyo mbali.

       2) Yale yaendayo chini sana.

Akimaanisha yaendayo mbali na upeo wa mwanadamu..na hayo si mengine zaidi ya mambo ya mbinguni, na kuzimu na ya maisha baada ya hapa..yatakuwa na mwonekano gani..picha yake halisi ipoje, miaka bilioni moja kutoka sasa watakatifu watakuwa wanafanya nini?..Hayo hakuna mtu anayeweza kuyavumbua isipokuwa Mungu tu peke yake.

Na yale yaendayo chini sana, maana yake ni yale yaliyositirika kama madini n.k. ambayo yenyewe yanapatikana chini sana. Hivyo vitu vilivyositirika/ siri za Mungu, ni mwanadamu gani anaweza kuzivumbua..

Kwamfano Siku ya unyakuo itakuwa lini, kabla ya uumbaji Mungu alikuwa anafanya nini,  maji yanajaaje kwenye mawingu, yaliyo hewa tu, halafu baadaye yanamwagika chini kama mvua, mifupa unajiumbaje ndani ya tumbo la mama mjamzito, mapigo ya moyo yanadundishwa kwa nishati gani, mpaka  hayachoki n.k Siri hizo anazo Mungu tu hakuna awezaye kuzivumbua..

Ayubu 11:7 inasema..

[7]Je! Wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu?  Waweza kuufikilia upeo wa huyo Mwenyezi?

Soma Kitabu cha Ayubu kuanzia sura ya 38-41, utaona Mungu anamuuliza mwanadamu maswali magumu ambayo mpaka sasa hakuna hata moja lililopatiwa jibu lake.

Hiyo ndio maana ya huo mstari;

Mhubiri 7:24

[24]Mambo yale yaliyo mbali, na yale yaendayo chini sana, ni mtu yupi awezaye kuyatafuta?

Yatosha sisi kumwamini yeye na kulitii Neno lake tu. Kwasababu hata tukijitahidi vipi kwa akili zetu kamwe hatutaweza kuzivumbua siri za ndani za Mungu wetu, isipokuwa yeye mwenyewe atufunulie.

Jina lake BWANA lihimidiwe. milele na milele. Amen.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Birika ni nini?, na yale Matao matano katika birika la Bethzatha ni nini?.

MUME / MKE BORA KUTOKA KWA BWANA UTAMWONA UKIWA KATIKA MAZINGIRA GANI?

nini maana ya kujikana nafsi na kujitwika msalaba?

HUJAPEWA MBAWA ZA KUKIMBIA MATATIZO

Nini maana ya ugonjwa wa kufisha? (Yeremia 17:9)

Rudi nyumbani

Print this post

HUDUMA YA MALAIKA WAWILI.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, ni wasaa mwingine tena Bwana ametupa neema ya kuutafuta uso wake. Karibu tujifunze Neno la Mungu.

Lipo funzo kubwa sana Bwana anatufundisha nyuma ya wale malaika wake wawili aliowatuma sodoma kwa ajili ya kuuangamiza ule mji. Habari tunaifahamu, hakuna haja ya kulitazama tukio lote, lakini tutatazama huduma yao ya mwisho ambayo waliifanya kwa familia ya Lutu.. Hiyo itatufanya na sisi leo hii tuwe makini sana na hii neema ya Mungu tuliyopewa kwa kitambo.

Malaika wale walipomwambia Lutu atoke sodoma, maandiko yanasema,  Lutu akawa ‘anakawia kawia’,..Hata baada ya “kuhimizwa sana” bado akawa anakawia kawia..hapo ndipo ikabidi wale malaika wachukue jukumu wenyewe la kuwatoa kwa nguvu sodoma, kana kwamba ndio wao wenye shida. Tusome;

Mwanzo  19:15 Hata alfajiri ndipo malaika WAKAMHIMIZA LUTU, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika maovu ya mji huu. 16 AKAKAWIA-KAWIA; nao wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili, kwa jinsi Bwana ALIVYOMHURUMIA, wakamtoa wakamweka nje ya mji..

Biblia inatuambia Kwa jinsi Mungu ‘alivyomhurumia’ Lutu na familia yake, ikampelekea amtoe kwa nguvu kama katoto kanacholazimishwa kupelekwa shuleni kwa kubembelezwa.. Hivyo waliendelea kuvutwa kwa umbali mrefu kidogo.. Lutu na mke wake wakashikwa na malaika mmoja, halikadhalika mabinti zake wawili wakashikwa na malaika mwingine.. Wakati wanatembea Walikuwa wanaweza kuangalia nyuma kama watakavyo na wasiambiwe kitu. Pengine walifika mahali wakawa wanasema tumechoka, wanabembelezwa watembee tu hivyo hivyo, wanafarijiwa, wanatiwa nguvu, Kwani jukumu la wao kuokolewa halikuwa katika uwezo wa mikono yao, bali  wa wale malaika wawili.

Lakini hali hiyo haikuendelea  sana… biblia inatuambia, walipofika nje tu kidogo ya mji..Wakaachwa, na kuambiwa zamu hii, sasa kipengele kilichobakia ni juu yao wenyewe..sisi tumemaliza kazi yetu.

Mwanzo 19:17 “Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea”.

Ndipo safari ya kukimbia, ikaanza..Lakini mkewe lutu, akidhani wakati huu ni kama ule wa mwanzo akageuka nyuma akidhani watakuwepo malaika tena wa kumshika mkono,na kumvuta vuta, na kumbembeleza bembeleza kama mwanzoni.. saa ile ile akageuka kuwa jiwe la chumvi.

Maana yake ni nini?

Saa tunayoishi ni wakati ambao sio tena kubembelezewa wokovu kama ilivyokuwa miaka ya kale.. Bali tunaishi ukingoni sana mwa neema ya wokovu. Wakati ambapo tunapaswa tujiokoe nafsi zetu na huu ulimwengu mbovu unaokaribia kuisha.. Pengine utasema umejuaje tupo katika zama hizo za kujiokoa nafsi zetu wenyewe, zama za kukimbia bila kuangalia nyuma, na sio za kuvutwa na Mungu? ,..Ni kutokana na kauli ya Bwana Yesu mwenyewe aliyoisema katika vifungu hivi;

Luka 17:32 “Mkumbukeni mkewe Lutu. 33 Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya”.

Maana yake ni kuwa hakuna kusubiria tena, Mungu akuambie hivi, au akuambie vile, au akufanyie hiki kwanza au kile.. Tayari alishasema na wewe kwamba usiangalie nyuma, kuna kuna kuwa jiwe la chumvi..jiokoe nafsi yako. Hivyo unapokuwa mkristo vuguvugu, unakapokuwa mkristo-jina, ujue upo hatarini sana wakati huu.. unyakuo ukipita leo au ukifa katika hali hiyo usidhani kwamba utakuwa na nafasi ya pili.

Mlango wa neema unakaribia kufungwa kwa watu wa mataifa, na hivi karibuni Yesu anarudi, dalili zote zinaonyesha huwenda kizazi tunachoishi tutayashuhudia yote. Sasa ya nini kuendelea kuufanyia mzaha wokovu,..Yanini kuendelea kuupenda ulimwengu? Ya nini kushikamana na mambo ya sodoma kama mke wa Lutu…

Usipoupokea wokovu wa kweli leo, ujue kesho itakuwa ngumu sana kwako, kuliko siku moja nyuma. Kwasababu neema ya Mungu haidumu milele kwa mwenye dhambi..litambue hilo!

Luka 13:24 “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.

25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako;

26 ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu.

27 Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.

28 Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje.

29 Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu”.

Isikize sauti ya Mungu..ikuambiayo jiokoe nafsi yako, mkumbuke mke wa Lutu.

Nyakati zetu ni za hatari sana kuliko nyakati za kale.

Bwana atusaidie.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JINSI SODOMA NA GOMORA ILIVYOKUWA INAVUTIA SANA.

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

USITAZAME NYUMA!

Roho, Nafsi, na Mwili vina utofauti gani?

Ni SIRI gani Paulo aliyokuwa anaimaanisha katika Waefeso 5:32?

WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU

Rudi nyumbani

Print this post