Category Archive Uncategorized

JINSI YA KUSOMA BIBLIA.

Fahamu jinsi ya kusoma biblia.


Awali ya yote ninakupongeza kwa nia yako kutamani kujua jinsi ya kusoma biblia. Hapo mwanzoni kabla sijamjua vizuri Mungu, kati ya  vitabu ambavyo nilikuwa ninaona ni vigumu kuvielewa, basi kimojawapo kilikuwa ni BIBLIA.

Lakini siku, na miaka ilivyozidi kwenda niligundua kuwa sio, nataka nikuambie hakuna kitabu kilicho kirahisi kama Biblia. Kwanini ninakuambia hivyo?.. Kwasababu ni kitabu kinachoweza kusomwa na watu wa makundi yote.  Mzee anaweza kukisoma, kijana anaweza kukisoma, asiye na elimu anaweza kukisoma mwenye PH.D anaweza kukisoma..Na wote wakafaidika na kilichoandikwa mule. Vilevile hakina ngazi yoyote ya awali kukipitia ndio uelewe kama vilivyo vitabu vingine. Leo hii ukihitaji kusoma kitabu cha Fizikia, itakugharimu kwanza upitie elimu za chini uwe na msingi, vinginevyo hutaweza kukielewa..Lakini biblia haina misingi hiyo.

Tena na cha kushangaza Zaidi ni kwamba, biblia imetoa nafasi ya kueleweka na watu wasio na elimu kuliko wenye hekima na ujuzi..(Luka 10:21)

Jinsi ya kusoma biblia.

Mambo ya kuzingatia kabla hujaanza kusoma biblia.

 • Kwanza: Omba Kabla hujaanza kusoma Habari yoyote, hata kama unaifahamu, mshirikishe kwanza Roho Mtakatifu, na mwombe msaada akusaidie kuyaelewa maandiko. Siri moja ya maandiko ni kuwa Habari ile ile inaweza ikawa na mafunuo mengi sana..Hivyo usipokuwa mnyenyekevu na kujiona kwamba Habari Fulani unaijua, nakuambia utabakia kuwa hivyo hivyo. Lakini ukimwomba kwanza Roho Mtakatifu akufunulie, maandiko basi utashangaa mambo mengi sana ambayo hukuwahi hata kuyafikiria.
 • Pili: Hakikisha upo katika utulivu wa kutosha. Mahali palipo na machafuko siku zote hata akili haiwezi kukaa katika utulivu wa kuzingatia kile kinachosomwa, na hivyo Roho Mtakatifu anakosa wigo wa kukufunulia, yale anayotaka kukufunulia. Hivyo kama upo kwenye makelele basi, subiri uwe katika utulivu, tenga muda wako, hususani usiku ni muda mzuri Zaidi.
 • Tatu: Tafakari Neno, Kumbuka Neno la Mungu halisomwi kama gazeti tu, Chukua muda mrefu kuyatafari maandiko Zaidi ya kuyasoma, ikiwa na maana mtu yule anayeitafakari sura moja vizuri, ni Zaidi na mtu yule atakayesoma kitabu kizima bila kutafakari chochote kilichoandikwa. Roho Mtakatifu anazungumza kwa kasi sana, pale mtu anapojibiisha kuitafakari Habari husika.
 • Nne: Endelea kutumia muda mwingi, katika kutafakari hilo Neno, kwa jinsi unavyokaa sana katika uwepo huo ndivyo unavyompa Roho Mtakatifu wigo wa kukufunulia maandiko katika uelewa mzuri zaidi. Mpaka dakika ya mwisho unamaliza, unatoka kitu ambacho hapo kabla hukuwahi kukijua, tena moyo wako ukiwa na amani ya kutosha.
 • Tano: Kuwa na daftari na kalamu. Hiyo itakusaidia kuandika kile Mungu anachokufundisha, kwa kumbukumbu la baada usije ukasahau, Kumbuka mwanafunzi mzuri ni yule anaandika chini kile mwalimu wake anachomfundisha, kila anapomfundisha. Hivyo na wewe hakikisha unakuwa na daftari lako.

Hivyo ukizingatia hizo hatua, utakuwa umeshajua jinsi ya kusoma biblia. Pia kumbuka, kwenye suala la kitabu kipi uanzane nacho, au kipi usianzane nacho, hilo halina umuhimu sana, unaweza kuanza na kitabu chochote kile na  huko huko Roho Mtakatifu mwenyewe atakufunulia mambo ya ajabu, Na kukufikisha pale anapotaka ufike kwa siku hiyo, kwasababu hiyo ndio kazi yake aliikusudia juu yetu.

Yohana 16:13  “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake”.

Jinsi ya kusoma biblia.

Pia Kujifunza biblia ni Pamoja na kusikiliza na mafundisho mengine ya Neno la Mungu yanayohubiriwa.. Yale yanakuwa kama TUTION kwako. Hivyo hapa pia yapo mafundisho mengi ya kukusaidia kuielewa biblia, kwenye website hii yapo mafundisho Zaidi ya 1000 ya mada mbalimbali, na Maswali na Majibu mengi sana, ambayo ukiyasoma naamini utapiga hatua kubwa sana katika kuielewa biblia..Hivyo kama upo tayari bofya hapa uende moja kwa moja katika orodha hiyo….>> MAFUNDISHO

                                                                                >> MASWALI NA MAJIBU

Bwana akubariki sana.

Jinsi ya kusoma biblia.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au tutumie ujumbe kwa namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Mihimili mikuu (4) ya mkristo katika safari yake ya wokovu.

USIPOLITENDEA KAZI NENO LA MUNGU.

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOWAFUNULIA WATU MAANDIKO.

TABIA YA KIPEKEE USIYOIJUA KUHUSU NENO LA MUNGU.

NENO LA MUNGU NI DAWA ILIYO TOFAUTI NA DAWA NYINGINE.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

KABLA YA MAANGAMIZI, KRISTO HUWA ANAONYESHA KWANZA NJIA YA KUTOROKEA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

MHUBIRI.

Kitabu cha mhubiri kiliandikwa na mfalme Sulemani.

Kitabu hichi kinaeleza, jumla ya mambo yote, na mwisho kinatoa ushauri ni nini mwanadamu anapaswa achague.

Ikiwa wewe ni mmojawapo wa  wanaojiuliza nini maana ya maisha, ni nini ufanye ili upate mwisho mwema mwenye mafanikio, basi nakushauri ukipitie kitabu hichi cha mhubiri kwa utulivu, Kwasababu Mungu alikiandika mahususi kwa ajili ya watu wenye maswali kama ya kwako.

Kwa ufupi (Mhubiri)Sulemani anajaribu kueleza jinsi alivyoanza safari yake yake ya kutafuta kitu kitakachompa raha maishani, kitu kitakachotatua matatizo yake moja kwa moja, Hivyo akaanza kujaribu kufanya kwa bidii jambo moja hadi  lingine ili aone kama linaweza kumletea jawabu la maisha yake.,

 • Alijaribu kufanya biashara nyingi sana kuliko watu wote waliomtangulia duniani lakini hakupata kile alichokuwa anakitafuta..
 • Alijaribu starehe na anasa zote unaozijua wewe, lakini katika hivyo vyote bado hakupata jumla ya maisha.(Mhubiri 2:1)
 • Akajaribu kwa kujijengea makasri ya kifahari lakini bado hakuipata hiyo jumla ya maisha (Mhubiri 2:4)
 • Alijiongezea elimu kuliko watu wote ulimwenguni, alikuwa na elimu juu ya miti yote, na karibu viumbe vyote duniani lakini katika elimu yake, na hekima yake bado hakupata jumla ya mambo yote.(Mhubiri 1:13)

Mpaka mwisho wa siku akakata tamaa, akaona kila kitu ni sawa na ubatili tu, na kujilisha (kufuata) Upepo. Japokuwa alijusumbua kupata kila kitu roho yake inapenda,  lakini bado kile alichokuwa anakitazamia hakukipata.

Na ndipo mwisho wa siku  akagundua jumla ya mambo yote ambayo  mwanadamu anapaswa kuyafanya chini ya jua nayo si nyingine zaidi ya KUMCHA BWANA, NA KUZISHIKA AMRI ZAKE.

Hivyo mimi na wewe hatupaswi, kuanza tena, kufanya utafiti, wa kitu kitakachotupa jawabu la maisha duniani,..Sulemani alishatusaidia, ukisema leo hii wewe mwenyewe ngoja uanze, kwa akili zako na nguvu zako, kutafuta maana ya maisha, nakawambia utazunguka kote na utarudi pale pale Sulemani alipoishia. Na wakati huo utakuwa umeshachelewa.

Unasema, ngoja nitafute elimu sana, hiyo ndio itanipa raha, Mungu hawezi kunipa raha,..Ni kweli utaisumbukia na kuipata, na kufanikiwa lakini mwisho wa siku utakuja kugundua mbona bado kuna shimo ndani yako? Ile raha ambayo uliitazamia mbona hujaipata?

Unasema, ngoja nitafute mali, nijiwekee miradi, mingi, kwasababu hiyo itanipa raha.. Nataka nikuambie yupo aliyefanya kazi kubwa zaidi yako aliyeitwa Mhubiri Sulemani, lakini hilo mwisho wa siku halikumpa jawabu alilokuwa analitarajia.

Vivyo hivyo na wewe kama unataraji utapata raha, sehemu yoyote, aidha kwa waganga, au kwa wanadamu, na huku umemwacha Mungu nyuma, ukweli ni kwamba mwisho wa siku utakuja kugundua uliacha kitu cha thamani sana nyuma yako.

Sasa mwishoni kabisa mwa kitabu hicho cha mhubiri, maneno hayo ya Mhubiri Sulemani ndio tunayapata,

Anasema..

Mhubiri 12:13 “Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; MCHE MUNGU, NAWE UZISHIKE AMRI ZAKE, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.

14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya”.

Unaona, anasema, mche Bwana, uzishike amri zake. Hivyo ikiwa bado angali unao muda ndugu yangu, mimi na wewe tumtafute Mungu, kwasababu huyo ndio atakayetupa furaha yote ya maisha yetu..

Na ndio maana mhubiri juu kidogo  alisema..

Mhubiri 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo 2 Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;

3 Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema; Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; Na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba; Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza;

4 Na milango kufungwa katika njia kuu; Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; Na mtu kusituka kwa sauti ya ndege; Nao binti za kuimba watapunguzwa;

5 Naam, wataogopa kilichoinuka Na vitisho vitakuwapo njiani; Na mlozi utachanua maua; Na panzi atakuwa ni mzigo mzito; Na pilipili hoho itapasuka; Maana mtu aiendea nyumba yake ya milele, Nao waombolezao wazunguka njiani.

6 Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani;

7 Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.

8 Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!”.

Ubarikiwe.

Kwa ziada ya masomo kuhusu kitabu cha Mhubiri, Fungua masomo haya;

ZIKUMBUKE SIKU ZIJAZO ZA GIZA, KWA MAANA ZITAKUWA NYINGI.

FANYA MAAMUZI KABLA HAZIJAKARIBIA SIKU ZA HATARI.

HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?

UBATILI.

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

habari za ziada.

Rudi Nyumbani:

Print this post

MAPEPO NI NINI?

Mapepo ni nini?


Mapepo ni Malaika walioasi zamani ambao hawakuilinda enzi yao mbinguni. (Yuda 1:6)

Na shetani mwenyewe akiwa kama pepo mkuu.

Sasa walipoasi ndipo wakatupwa duniani, na hiyo ilikuwa  kabla hata ya mwanadamu kuumbwa. Wote walikuwa wameshatupwa huku duniani wakisubiria hukumu yao ya mwisho.

Lakini mwanadamu alipoumbwa, na shetani akafanikiwa kumdanganya pale Edeni ndipo yeye na mapepo yake yote wakapata uhali wa mambo mengi ulimwenguni,

Haya mapepo yakaanza kuwaingia watu jambo ambalo lilikuwa haliwezekani hata kidogo, yakashikilia mambo mengi, na kufanikiwa kuharibu, kwa ufupi yalikuwa na uwezo wa kujiamulia kufanya chochote,  yakiongozwa na kiongozi wao mkuu shetani

Mpaka ilipofikia kipindi cha Yesu Kristo kuja duniani, hapo ndipo yalinyang’anywa sehemu kubwa ya mamlaka waliyokuwa nayo, waliyoyaiba kwa Adamu, Yesu ndio akayachukua yakawa ya kwake.

Ufunuo 1:17 “…………Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,

18 na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu”.

Hivyo mapepo yaliyopo duniani leo hii hayana nguvu tena juu ya mtu ikiwa tu, atakuwa ndani ya Kristo basi..Kwasababu yeye ndio aliyepewa mamlaka yote ya mbinguni na duniani kwa sasa (Mathayo 28:28)..

Zamani shetani alikuwa na uwezo hata, wa kuwaendea hata wafu na kuzungumza nao, utaona hilo katika kipindi cha Samweli jinsi Yule mwanamke mchawi alivyompandisha Samweli juu kuzungumza na Mfalme Sauli. Lakini sasahivi wafu wote wanamilikiwa na Yesu Kristo, kiasi kwamba ukifa leo, shetani hawezi kukufikia huko ulipo kwa namna yoyote ile.

Mapepo ni nini

Hivyo fahamu tu, ikiwa upo nje ya Kristo, kwa namna moja au nyingine, mapepo yatakusumbua tu, na lengo lao si lingine zaidi ya kukuua na kukupeleka kuzimu.. Ili kufahamu ubaya wa mapepo, fungua hapa usome >> Kwanini Bwana Yesu, aliruhusu yale mapepo yawaingie nguruwe?

Hivyo usijidanganye na kusema mimi siwezi kuwa na mapepo kisa tu hayajawahi kulipuka ndani yangu..Ndugu fahamu kuwa si mapepo yote ni ya kulipuka kama unavyodhani..

 • Mengine ni ya magonjwa.(Luka 13:11)
 • Mengine ni ya mateso/mkandamizo wa nafsi, mpaka kupelekea kujiua. Mf. Ndio Yule alimwingia Yuda ikampelekea kwenda kutenda dhambi na kujinyonga.
 • Mengine ni ya utambuzi: (Matendo 16:16)
 • Mengine ni mapepo bubu na kiziwi;(Marko 9:25)
 • Mengine ni ya kukudanganya.(1Wafalme 22:22) N.k.

Hivyo ikiwa wewe upo nje, kwa namna moja au nyingine ipo roho ya ibilisi imejishikamanisha  na wewe hata pasipo wewe kujijua. Njia pekee ya kuyaondoa ndani yako ni kumpa tu YESU KRISTO maisha yako. Ukishamwamini na ukatubu na ukabatizwa, basi maroho hayo yanaondoka ndani yako..Na wakati huo huo ROHO MTAKATIFU anaingia ndani yako. Hapo ndipo utakapojua tofauti yako ya wewe ni jana.

Luka 10:19 “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru”.

Naamini mpaka hapo umeshafahamu kwa ufupi mapepo ni nini.

Usisahau kuwa hizi ni siku za mwisho, Na Yesu yupo mlangoni kurudi, na shetani naye analijua hilo vizuri, hivyo utendaji wake kazi sasa sio kama ule wa zamani, mapepo/majini yanatenda kazi kwa nguvu kuliko pale mwanzo. Hivyo nawe pia unaposikia habari za wokovu usikawie kawie kwasababu, shetani naye yupo karibu yako kuindoa hii mbegu iliyopandwa ndani yako.

Ufunuo 12:12 “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu’.

Shalom.

Mada Nyinginezo:

MAJESHI YA PEPO WABAYA.

Kuna Malaika wangapi?

Kwanini Mungu anasema “Afanyaye malaika zake kuwa pepo”?

JIHADHARI NA UPOTEVU ULIOACHIWA SASA.

VIFUNGO VYA GIZA VYA MILELE.

UHARIBIFU WA MTU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

KWA KUPIGWA KWAKE SISI TUMEPONA.

Ndio kwa kupigwa kwake sisi tumepona!!

Tunao ujasiri wote wa kusema hivyo, kwasababu kuacha kwake enzi na mamlaka mbinguni, kisha kuja kuishi maisha ya taabu na mateso hapa duniani, kuanzia kuzaliwa katika zizi la ng’ombe, Kisha kuishi maisha ya umaskini tangu utoto wake hadi utu uzima,(japokuwa alikuwa ni tajiri)

1Wakorintho 8:9 “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”.

Hakuwa hata na mahali pa kulaza kichwa chake, hata mbweha na ndege walimshinda, hiyo yote ni kwa ajili yangu mimi.

alijaribiwa zaidi yetu sisi, bila kutenda dhambi yoyote, alifunga na kukesha kwa kuomba kwa ajili yangu, na kama hiyo haitoshi, ilimgharimu kuingia matesoni ateswe na ibilisi, atemewe mate, apigwe mijeledi, agongelewe misumari, adhihakiwe, achomwe mkuki, halafu mimi nisiponywe roho yangu hilo litakuwa ni jambo lisiloingia akilini.

Kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

Ni haki yako wewe na mimi kuupokea uponyaji wa roho zetu kwanza, na hiyo inakuja kwanza kwa kutubu dhambi zetu , kwa kudhamiria kutubu kwa kumaanisha kabisa kuuacha ulimwengu na tama zake, kisha ndio anakuja ndani yetu na kutuokoa na  kufanya makao na sisi. Na baada ya hapo atatuponya na miili yetu pia, kwasababu Kwa kupigwa kwake sisi tumepona, roho zetu na miili yetu pia.

Hivyo kabla sijakwenda kukuombe tatizo lako, Ni vema kwanza ukamkaribisha Bwana Yesu katika maisha yako. Ikiwa upo tayari kufanya hivyo leo basi unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Na Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu wako. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako(sawasawa na Matendo 2:38).

Sasa ikiwa wewe Ni mgonjwa, Kumbuka Bwana Yesu haponyi tu roho, anaponya pia miili yetu..mimi ninayekuandikia huu ujumbe ni shahidi alishaniponya mara nyingi, kwa kufuatisha maombi kama haya ninayokuombea vilevile atakuponya na wewe leo. Kwasababu Yesu ni yeye Yule.

Unachopaswa kufanya hapo ulipo..Weka mkono mahali unapoumwa, kisha.

Sema maneno haya kwa sauti.

EWE UGONJWA (UTAJE UGONJWA UNAO KUSUMBUA), MIMI NI MILKI HALALI YA MKUU WA UZIMA YESU KRISTO. NAKUAMURU KWA JINA LA YESU ONDOKA NDANI YANGU KUANZIA HUU WAKATI NA MILELE, KWA KUPIGA KWAKE SISI TUMEPONA. HAKUPIGWA BURE, HAKUDHARAULIWA BURE, HAKUTESWA BURE..BALI HIYO YOTE ILIKUWA NI MIMI NIUPOKEE UPONYAJI KAMILI WA ROHO YANGU NA MWILI WANGU. HIVYO ONDOKA NDANI YANGU SASA KWA JINA LA YESU KRISTO.

EE BWANA YESU, MWOKOZI WANGU, INGIA SASA NDANI YA MWILI WANGU, UNIRUDISHIE AFYA ULIYONIAHIDIA.

ASANTE KWA UPENDO WAKO.

JINA LAKO LIBARIKIWE DAIMA.

AMEN.

Sasa ikiwa  umefuatisha maombi hayo mafupi, basi kuwa na uhakika kuwa Kristo ameshakuponya tayari, ikiwa ulikuwa huwezi kufanya jambo Fulani anza kulifanya, ikiwa ni ugonjwa wa kwenye damu, nenda kapime, ikiwa ni wa viungo vyovyote vile Kristo ameshakuponya.

Hivyo usiache kwenda kushuhudia na kumpa yeye utukufu.

Bwana akubariki sana.

“Ndio Kwa kupigwa kwake sisi tumepona”.

Mada Nyinginezo:

YESU MPONYAJI.

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

FAHAMU JINSI KRISTO ANAVYOPONYA WATU ROHO.

RABI, UNAKAA WAPI?

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

 

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi Nyumbani:

Print this post

MSAMARIA MWEMA.

Msamaria mwema ni mtu wa nanma gani?


Ni kauli ambayo tunaisikia katika jamii yetu mara kwa mara. Na hiyo inatokea pale mtu mfano amekumbana na matatizo au shida Fulani halafu akakutana na mtu asiyemfahamu kisha akamsaidia kutatua tatizo hilo. Sasa mtu kama huyo baadaye akija kuulizwa ilikuwaje ukafanikiwa au ukafanikisha kitu kile katika yale mazingira? ..Ndio hapo utamsikia anasema nilikutana na msamaria mwema akanisaidia…

Lakini baadhi ya watu hawajui chanzo cha msamaria mwema ni nini?..

Habari yake tunaipata kutoka katika biblia, tusome,

Luka 10:25  “Na tazama, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?

26  Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?

27  Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.

28  Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi.

29  Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani?

30 Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa.

31  Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando.

32  Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando.

33  Lakini, MSAMARIA MMOJA katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia,

34  akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza.

35  Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.

36  Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi?

37  Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo”.

Ni yapi tunajifunza katika Habari ya msamaria mwema?

 • Ili na wewe ufanyike msamaria mema, ni sharti uwe moyo wa huruma.
 • Ni sharti, uwe mwepesi kumsaidia mtu, ambaye hata haonyeshi dalili ya kuomba msaada kwako, lakini unajua kabisa yupo katika hali ya kuhitaji msaada.
 • Upo tayari kutoa hata mali zako, au vitu vyako vya thamani kwa ajili ya kumsaidia tu mtu

Sasa ukizingatia hayo, Basi mbele za Mungu utakuwa umekidhi vigezo vya kumpenda jirani yako kama nafsi yako.. Hapo utakuwa umeshida amri ya pili iliyo kuu kuliko zote, kama yule msamaria mwema.

Kumbuka  tendo hilo lina thawabu kubwa sana mbele za Mungu.

Hivyo ni wajibu wetu sote, kulikumbuka hilo wakati wote tunapoishi humu duniani, ili na sisi Mungu atuhurumie siku ile tuurithi uzima wa milele..

Mada Nyinginezo:

JIRANI YANGU NI NANI?

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

WAKATI ULIOKUBALIKA NDIO SASA.

MKARIBIE BWANA ZAIDI ILI UFANYIKE NGUZO.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

UNYAKUO.

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

ADAM NA EVA.

Adam na eva akina nani?


Hawa ni wazazi wetu wa kwanza.

Biblia inasema

Mwanzo 1:27 “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. 

28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi”.

Lakini kama tunavyojua waliasi, na ndio hapo ikawa chanzo cha matatizo ambayo ndio mpaka leo mimi na wewe yanatuathiri.

Hawa alidanganywa na nyoka kula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, Kumbuka “alidanganywa” wala hakushawishiwa, hii ikiwa na maana kuwa hakujua kuwa kitendo anachokwenda kukifanya kingekwenda kuleta madhara yoyote kwa mtu kwa udanganyifu alioambiwa na nyoka, kwasababu alidanganywa kuwa hatakufa, bali kinyume chake atafumbuliwa macho, atakuwa kama Mungu, akijua mema na mabaya.

1Timotheo 2:13 “Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. 14 Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa”.

Lakini siku ile alipojaribu kujitetea kwa kumrushia nyoka mpira, hilo halikusaidia yeye kutoshiriki adhabu.

Vivyo hivyo na sasa, Udanganyifu mwingi umetokea leo hii duniani.. Lakini ni wajibu wako wewe kuujua ukweli na kuushika, kwasababu siku ile hautakuwa na la kujitetea na kusema, mimi mbona sikujua hili, au mimi mbona niliambiwa vinginevyo na watu wanaojiita watumishi wa Mungu.

Kumbuka si watu wote wanaojiita watumishi wa Mungu ni watumishi kweli wa Mungu,, Mtumishi wa Mungu ni lazima akufundishe kweli ya biblia, na kukuongozwa kwa Kristo na sio kwenye mambo ya ulimwengu huu.

Tusidanganywe kama Adam na Eva.

Ndio maana wakati huu wa machafuko mengi ya rohoni, ni vizuri ukawa na Kristo moyoni mwako, na kujifunza Neno la Mungu kwa bidii, ili likae ndani yako ibilisi asikushinde. Kwasababu kama Neno la Mungu halipo ndani yako kwa wingi, kamwe huwezi kuzishinda njama za mwovu,

Utakumbuka kilichomtokea Bwana Yesu kule jangwani, shetani alipomjia na maandiko na yeye alimjibu kimaandiko. Sasa huyo ni mwokozi wa ulimwengu yamemkuta. Itakuwaje mimi na wewe?

Tung’ang’anie NENO LA MUNGU. Maana hilo ndio silaha yetu nyakati hizi za mwisho dhidi ya mwovu shetani, ili tusiwe kama Adam na Eva.

Mada Nyinginezo:

UUMBAJI BORA WA MUNGU, UPO NDANI YA MWANADAMU.

MWAKA WA BWANA ULIOKUBALIWA.

JINA LA MUNGU NI LIPI?

NA UPEPO WA KUSI ULIPOANZA KUVUMA KIDOGO,

VUKA UJE MAKEDONIA UTUSAIDIE.

UZAO WA NYOKA.

KWANINI TUNAPASWA TUJIZUIE?

Rudi Nyumbani:

Print this post

WAFIRAJI KWENYE BIBLIA.

Je! biblia inasema nini juu ya wafiraji?


Ufiraji ni Neno  linalojumisha kitecho chochote cha kumwingilia mwanadamu mwanzako  kimapenzi kinyuma na maumbile.

 • Uwe unamwingilia mwanaume mwenzako (Ulawiti na ushoga),
 •  Au uwe Unamwingilia  mwanamke, hajialishi  ni mkeo, hicho tayari ni kitendo cha ufiraji.

Na ni dhambi biblia imesema hivyo na kwamba watu wote wanaofanya vitendo kama hivyo hawawezi kuurithi uzima wa milele.

1Wakoritho 6:9 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala WAFIRAJI, WALA WALAWITI,

10 wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi”.

Watu wengi wanajidanganya na kudhani kuwa wakiwaingilia wake zao, maadamu tayari wapo nao katika ndoa, sio dhambi..Ndugu usidanganyike, tendo lolote la kumwingilia mtu mwingine kinyume na maumbile haijalishi ni rafiki, au jirani, au kahaba, au mke, hiyo tayari ni ufiraji.

Na wafiraji wote watahukumiwa.

Kilichosababisha Sodoma na Gomora viangamizwe, kilikuwa ni kitendo hichi cha ufiraji,

Yuda 1:7 “Kama vile Sodoma na Gomora na miji iliyokuwa kando-kando, waliofuata uasherati kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele.
8 Kadhalika na hawa, katika kuota kwao, huutia mwili uchafu, hukataa kutawaliwa, na kuyatukana matukufu”.

Hivyo kama wewe ni mmojawapo tubu haraka sana, kwa kuacha kitendo hicho. Mgeukie Yesu Kristo ayaokoe maisha yako. Ikimbie hukumu ya Mungu. Ziwa la moto lipo kweli.

Jiepushe na utazamaji wa picha na video chafu za ngono zinazozagaa mitandaoni, watu wengi wanaingiliwa na hizi roho kwa kuzitazama tu. Utakuta hapo mwanzo, hakuwa hivyo lakini siku alipooanza kuzitazama tu, anaona kama, shinikizo fulani la nguvu linatoka ndani kumuhimiza kufanya hivyo.

Kama na wewe ni mmoja wapo basi, nakushauri, kaa mbali sana na mambo hayo, shetani anafahamu kuwa wakati wake ni mfupi aliobakiwa nao. Hivyo itazame sana mienendo yako.

Mada Nyinginezo:

JINSI SODOMA NA GOMORA ILIVYOKUWA INAVUTIA SANA..

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

SI KILA KIPENDEZACHO KINATOKA KWA BWANA.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

Baraka za Mungu.

Baraka za Mungu zinakujaje?


Ni vizuri kufahamu kuwa mafanikio sio Baraka, lakini Baraka zinaweza kupelekea mafanikio.

Unaweza ukawa ni tajiri na ukafanikiwa na mali zako zikawa ni nyingi sana, lakini ukawa bado hujabarikiwa na Mungu. Kwasababu mafanikio hata shetani naye anayatoa.

Hilo utalithibitisha katika kitabu cha Mathayo, siku ile ambayo shetani alipotaka kumtajirisha  Yesu kwa mapatano ya kumsujudia..Soma

Mathayo 4:8 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake,

9 akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia”.

Unaona, utajiri, na mali hatoi tu Mungu peke yake kama wengi wanavyodhani, bali shetani pia anatoa  tena anatoa kweli kweli, Lakini Baraka huwa Baraka huwa zinatoka kwa Mungu tu peke yake.

Tukilijua hilo sasa turudi, ili kujifunza Baraka za Mungu ni zipi.

Wagalatia 3:13 “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti;

14 ili kwamba BARAKA YA IBRAHIMU iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, TUPATE KUPOKEA AHADI YA ROHO kwa njia ya imani”.

Unaona, hapo Baraka ambayo Mungu aliiachia kwanza kwa Ibrahimu tunamjua kuwa alibarikiwa na Mungu, iliachiliwa hata na kwetu sisi kwa njia Yesu Kristo, Na Baraka yenyewe tuliyoipokea ni Roho Mtakatifu.

Leo hii hakuna Baraka kubwa kutoka kwa Mungu zaidi ya Roho Mtakatifu kuwa ndani ya mtu. Ukimkosa Roho Mtakatifu, wewe ni mlaaniwa. Lakini ukimpata Roho Mtakatifu basi umepata vitu vyote. Na mafanikio juu.

Huwezi kumpendeza Mungu kama huna Roho Mtakatifu yeye mwenyewe alisema..

Warumi 8:9 “……..Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake”.

Sasa Roho Mtakatifu tunampataje?

Tunampata kwanza kwa kutubu dhambi zetu  kwa kumaanisha, kisha tunakwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kimaandiko wa kuzamwishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, ili tupate ondoleo la dhambi zetu, na baada ya hapo sasa Mungu atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu ndani yetu. Sawasawa na Matendo 2:38

Matendo 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.

Sasa ukishakuwa na uhakika kuwa umeyafuata hayo maagizo yote kwa bidii, na umemaanisha kweli kutubu dhambi zako, na sio nusu nusu, yaani mguu mmoja nje, mwingine ndani, basi wakati huo huo Roho wa Mungu atashushwa ndani yako..(Wengi wanadhani Roho Mtakatifu ni mpaka unene kwa Lugha, hapana yeye ni zaidi ya hapo, kunena kwa lugha ni moja ya njia zake, lakini unapotubu na kubatizwa wakati huo huo Roho Mtakatifu ataingia ndani yako.) .

Na baada ya hapo sasa ndipo na mafanikio mengine yote yataambatana nawe kwa wakati wake, kwa kuwa umeyashika maagizo yake kwa bidii. Sawasawa na Kumbukumbu la Torati 28

1 Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;

2 na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako.

3 Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.

4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.

5 Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga.

6 Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo. 7 Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.

8 Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako.

9 Bwana atakuweka uwe taifa takatifu kwake, kama alivyokuapia; utakaposhika maagizo ya Bwana, Mungu wako, na kutembea katika njia zake.

10 Na mataifa yote ya duniani watakuona umeitwa kwa jina la Bwana, nao watakuwa na hofu kwako.

11 Bwana atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako kwamba atakupa.

12 Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.

13 Bwana atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakapoyasikiza maagizo ya Bwana, Mungu wako, nikuagizayo hivi leo, kuyaangalia na kufanya;”

Hivyo Baraka ya Mungu ni Roho Mtakatifu.Ukimpata huyo basi umepata kila kitu.

Lakini usidanganyike na kumwona kila mtu mwenye mafanikio na huku yupo mbali na Mungu ukadhani amebarikiwa…Huyo ni mlaaniwa tu mbele za macho ya Mungu.

Bwana akubariki.

Mada Nyinginezo:

Yuko azuiaye sasa hata atakapoondolewa! ni nani huyo?

KANUNI RAHISI YA KUFANIKIWA.

MISTARI SHETANI ANAYOITUMIA KUWAANGUSHA WATU

MISTARI SHETANI ANAYOITUMIA KUWAANGUSHA WATU

USIFIKIRI FIKIRI.

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

Rudi Nyumbani:

Print this post

Yesu ni Mungu?, Na Kama ni Mungu kwanini alikufa?

SWALI: Je! Yesu ni Mungu? Na Kama ni Mungu kwanini alikufa?


JIBU: Yesu alikuwa ni Mungu katika mwili (1Timotheo 3:16)…lakini hakuja kutafuta kuabudiwa wala kusujudiwa!…Mpaka Mungu amevaa mwili na kuja ulimwenguni, maana yake hajaja kutafuta kuabudiwa, kama angekuwa amekuja kutafuta utukufu wake basi, kulikuwa hakuna haja ya kuuvaa mwili na kushuka duniani, naamini Mbingu ilikuwa inamtosha…. hivyo ni lazima atakuwa amekuja kwa kusudi lingine na si la kutafuta utukufu. Hapo ndipo wengi wa wasio wakristo wanaposhindwa kuelewa, na baadhi ya walio wakristo.

Unapoona askari wa kuongoza barabarani (Traffic man), kaondoka barabarani na kaenda nyumbani kubadilisha nguo zake hizo nyeupe…na akavaa nguo za kiraia na kuingia mtaani basi ni dhahiri kuwa huko mtaani alikokwenda hajakwenda kutafuta kuongoza magari bali kaenda kutafuta mambo yake mengine ya kawaida..labda anaenda hospitalini au sokoni au kusalimia ndugu na marafiki, au kufuatilia mambo yake mengine ambayo ni tofauti na ya kikazi….. (ni kweli bado atabaki kuwa askari, lakini yupo nje ya ofisi yake), hivyo hataweza kuyatumia yale mamlaka aliyonayo ya kuongoza magari,…na akiwa barabarani na nguo zake za kiraia, hata watu wanaweza wasimtambue kama ni askari, atakuwa kama raia wengine tu, na magari atakuwa anayakwepa tu kama raia wengine, na atazingatia sheria zote za barabarani kama raia wengine…

Na Bwana Yesu ni hivyo hivyo…alipokuwa mbinguni alikuwa ni Mungu, anayestahili kuabudiwa na kuheshimiwa…aliposhuka duniani alikivua kile cheo cha Kiungu…na kuwa kama mwanadamu (kwa lengo la kuja kumkomboa mwanadamu na si kuabudiwa kama Mungu)..na baada ya kumaliza akarudi mbinguni alikotoka katika cheo chake.

Hivyo akiwa kama mwanadamu alikuwa hana budi aishi kama wanadamu wengine, hana budi awe mtu wa ibada kama watu wengine, hana budi ale, anywe, alale, achoke, apitie yote mwanadamu wa kawaida anayopitia na hata ikiwezekana afe…ili tu kusudi lake lililomleta duniani litimie la kumkomboa mwanadamu…lakini alikuwa bado ni Mungu.

Wafilipi 2: 5 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;

6 ambaye yeye mwanzo alikuwa YUNA NAMNA YA MUNGU, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;

7 bali ALIJIFANYA kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;

8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba”.

Umeona hapo mstari wa 7?..unasema “ALIJIFANYA”..kama unakielewa Kiswahili vizuri utakuwa unajua maana ya “KUJIFANYA”..Maana yake ni kama kujigeuza/kuigiza kuwa kitu Fulani na kumbe sio…kwa lengo la kutimiza kusudi Fulani tu!…Hivyo Bwana Yesu aliyejifanya kuwa hana utukufu…ili ashuke aje kutukomboa na kutuonyesha njia jinsi mwanadamu kamili anayemcha Mungu anapaswe awe.

Hivyo kufa kwa Bwana Yesu, hakumfanyi yeye asiwe Mungu..na pia muujiza mkubwa duniani na mbinguni sio kutokufa!!… Huo ni muujiza mdogo sana…..“miujiza mkubwa ni uwezo wa mtu kuutoa uhai wake na kisha kujirudishia ule uhai”..Huo ndio muujiza mkubwa kuliko yote!..na uwezo huo alikuwa nao Yesu pekee yake.

Yohana 10:17 “Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena.

18 HAKUNA MTU ANIONDOLEAYE, BALI MIMI NAUTOA MWENYEWE. NAMI NINAO UWEZA WA KUUTOA, NINAO NA UWEZA WA KUUTWAA TENA. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu”.

Sasa utauliza ni wapi, Yesu aliutoa uhai wake mwenyewe?…kasome Luka 23:46-47. Bwana Yesu aliutoa uhai wake mwenyewe! Hakuna mtu aliyemsaidia kuutoa..hata Pilato alishangaa imekuwaje amewahi kufa kiasi kile (Marko 15:44). Na aliurudisha uhai wake mwenyewe baada ya siku tatu (kule kaburini hakuna mtu aliyeenda kumfufua au kumwombea afufuke).

Alijirudishia uhai wake mwenyewe!..Nadhani huo ni muujiza mkubwa sana.. Je wewe unaweza kufanya hivyo????

Hata mfano nikikuwekea watu wawili mbele yako mmoja hawezi kuukata mguu wake na mwingine anao uwezo wa kuukata na kuurudisha….nikakwambia kati ya hao wawili ni yupi hapo wa kuogopwa zaidi??..Bila shaka utaniambia “Yule mwenye uwezo wa kuukata mguu wake na kisha kujirudisha tena ndiye wa kuogopwa zaidi kuliko huyo mwingine”.

Kwahiyo kuupima uungu wa Bwana Yesu na kifo chake ni hoja dhaifu!!..miungu ya kipagani ndio isiyo na uwezo wa kufanya hayo..lakini Mungu wa mbingu na nchi (YESU KRISTO) anaweza kufanya mambo yote. Mpaka sasa katika historia hajatokea nabii yoyote wala mtume yeyote aliyofanya miujiza kama aliyofanya Bwana Yesu, sasa kwanini asiwe Mungu?. Na siku moja atarudi na kila jicho litamwona na kila goti litapigwa, na kila kinywa kitakiri…Wengi itakuwa ni jambo la kushtukiza sana kwao, kwasababu hawataamini kwamba kweli ndiye!..kwasababu walidanganyika wakiwa duniani kwamba hatarudi.

Lakini anatupenda na wala hataki mtu yoyote apotee bali wote tuifikie toba, ili tuokoke na tuje kutawala naye milele.

Bwana atubariki tuzidi kumjua yeye!

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Mbona Mungu anaruhusu watu wapate shida, ilhali ana uwezo wa kutuepusha?

Katika biblia Neno “Mshenzi” linatajwa.Kwanini liwekwe?

Kile kinara cha Taa ndani ya Hekalu la Sulemani kilikuwa kinawakilisha nini?

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

Agano jipya ni nini?

Agano jipya ni nini?


Tukitamka neno “agano jipya”  tunathibitisha kuwa lilishawahi kuwepo agano la zamani (La kale) hapo kabla.

Hivyo ili kufahamu agano jipya ni nini, ni vizuri kwanza ukapata msingi wa agano la Kale, lilikuwaje.

Kama tunavyojua Biblia imeundwa na maagano makuu wawili, yaani jipya na la kale.

 1. Agano la Kale:

Sasa msingi wa agano la kale ulitoka kwa mtu mmoja aliyeitwa Ibrahimu. Mungu alipomuita hakumuita ilimradi tu, bali aliingia agano naye akamwambia atambariki na kumfanya kuwa baba wa mataifa mengi, ikiwa tu atakuwa mkamilifu na atakwenda  katika njia zake..Tusome.

Mwanzo 17:1 “Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, Bwana akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. 

2 Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana. 

3 Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, 

4 Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, 

5 wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. 

6 Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. 

7 Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako. 

8 Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao. 

9 Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada. yako. 

10 Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa. 

11 Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi”.

Unaona, Jinsi Mungu alivyokuwa mwaminifu, baadaye Mungu akaja kumtimizia kweli agano aliliomuahidia, kwa jinsi uzao wake ulivyokuwa unaongezeka duniani kwa kasi, Lakini wakati huo wote uzao wake ulikuwa haumjui Mungu vizuri, ulikuwa bado haujajua kanuni za agano hilo ambalo Mungu aliloingia na Ibrahimu baba yao linavyopaswa liwe..

Ndio hapo wakiwa kule jangwani sasa Mungu anamtumia Musa kusema nao na kuwapa sheria na amri za kuzishika ili wafanikiwe..

Sheria hizo ndizo zilizoandikwa katika vitabu vya Torati: yaani

 • Mwanzo
 • Kutoka
 • Hesabu
 • Mambo ya Walawi
 • Kumbukumbu la Torati.

Hivyo vitabu hivyo vitano vilikamilisha Sheria yote ya Agano hilo ambalo Mungu aliingia na Ibrahimu.

Lakini hiyo peke yake haikuwa inatosha wana wa Israeli kumfahamu Mungu katika ukamilifu wote, Hivyo ilipasa  Mungu azungumze nao mara kwa mara kupitia watu mbalimbali wakamilifu na manabii wake.. Mfano tunamwona mtu kama Ayubu, Esta, Ruthu, kwa kupitia maisha ya hawa Mungu aliwafundisha wana wa Israeli jinsi ya kuishi katika njia zake. Vilevile akawa anasema nao mara kwa mara kupitia manabii wake wengi na waamuzi na mfano Samweli, Isaya, Yeremia, Danieli, Yona,Malaki N.k.

Hivyo kwa kupitia hao pia, na vitabu vyao walivyoviandika, iliwasaidia wana wa Israeli walishike na kulikumbuka agano ambalo aliingia nao zamani.

Kwahiyo tunapovisoma vitabu 39 vya Agano la Kale,.. tunafahamu kuwa ni jumuisho la sheria zote na kanuni zote za Mungu kwa wale alioingia nao agano kupitia Ibrahimu.

Sasa mpaka hapo umeshapata msingi wa Agano la kale kwa ufupi lilipoanzia..


      2.  Tukirudi kwenye agano jipya..

Hilo ni agano lingine lili bora zaidi kuliko lile la Ibrahimu.,

Hili nalo  Mungu aliingia katika agano na mtu mmoja tu, kama vile alivyoingia na Ibrahimu.. Na mtu huyo si mwingine zaidi ya YESU KRISTO.

Ibrahimu alipewa tu uzao wake wa kimwili, lakini huyu alipewa uzao wa wote wenye mwili wakimwamini tu kwa kuzaliwa mara ya pili.

Na ndio maana kuna umuhimu wa kila mmoja wetu kuzaliwa mara ya pili ili tufanyike kuwa uzao wake. yeye mwenyewe alisema..

Yohana 3:3  “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu”.

Na kubatizwa kwetu ndio ishara ya tohara yenyewe ya rohoni kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu na watoto wake wote walipotahiriwa kwa kutolewa magovi. Vivyo hivyo na sisi tunapaswa tukabatizwe kama ishara ya kutahiriwa mioyo yetu.

Lakini tukishazaliwa mara ya pili, hilo tu peke yake haitoshi, ni sharti pia tujue kanuni, na amri Mungu anazozitaka za agano hili ili tuweze kudumu ndani yake. Kama Uzao wa Ibrahimu ulivyopewa.

Hapo ndipo vitabu vya Injili ya Yesu Kristo, na vile  vya mitume, viliandikwa kwa ajili yetu ili sisi sote tutakapovisoma na kuvishika basi tuweze kudumu na kuimarika katika hilo agano jipya la Damu ya Yesu Kristo.

Ndipo hapo tunakutana na vitabu 27 vya agano jipya.

Hivyo kwa kwa hitimisho fupi.. Agano jipya ni agano Mungu aliloingia na Yesu pamoja na uzao wake wote. Ambao mimi na wewe tunahesabiwa katika uzao huo  kwa kumwamini Yesu na kubatizwa.

Tukifanikiwa kufanya hivyo basi na baraka zote, Mungu alizomuahidia Yesu Kristo, na sisi sote pia tunazishiriki na kuzirithi, ikiwemo uzima wa milele.

Bwana akubariki.

Je! Na wewe upo ndani ya agano jipya? Kama bado basi fanya hima ukaribishe Yesu leo ndani ya maisha yako akuokoe ufanyike uzao wa kifalme. Kumbuka hii ni neema ambayo sisi watu wa mataifa hatukustahili, hivyo uiichezee hata kidogo..

1Petro 2:9  “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; 10  ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema”.

Haleluya.

Mada Nyinginezo:

TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.

Je! habari ya Yusufu, inabeba ujumbe gani kwa agano jipya?

Bwana aliposema “sikuja kutangua torati bali kuitimiliza” alikuwa anamaanisha nini?

UTIMILIFU WA TORATI.

TAZAMA, MWISRAELI KWELI KWELI, HAMNA HILA NDANI YAKE!

Sanduku la Agano lilikuwa linawakilisha nini katika Agano jipya?

KUTAHIRIWA KIBIBLIA

MWAKA WA BWANA ULIOKUBALIWA.

Rudi Nyumbani:

Print this post