by Admin | 5 December 2018 08:46 am12
Ishara kubwa Bwana Yesu aliyowapa wanafunzi wake ambayo kwa hiyo waliambiwa watakapoiona basi wajue kuwa “muda wa mavuno umekaribia” ni ishara ya MTINI. tukisoma Mathayo 24:32 inasema “Basi KWA MTINI JIFUNZENI mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu;
24.33 nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.
Na tunajua kuwa “mtini” alioumaanisha hapo si mwingine zaidi, zaidi ya TAIFA LA ISRAELI (Yeremia 24), Ikiwa na maana kuwa tutakapoona taifa la Israeli linaanza kuchipua na kuchanua tena, basi majira ya mwisho wa dunia yamekaribia sana. Kumbuka Mungu katika mpango wake wa wokovu alianza na Israeli na katika kutimiliza atatimiliza na taifa hilo hilo, kwasababu makao ya MFALME YESU atakapokuja kwa mara ya pili kuutawala huu ulimwengu mzima katika nchi ya wenye haki, hayatakuwa katika mojawapo ya nchi hizi za mataifa tulizopo sisi na zitakazokuwepo huko hapana, bali makao yake yake makuu yatakuwa pale Israeli nchi takatifu. Alishuka hapo mara ya kwanza, atashuka hapo hapo mara ya pili. Hivyo ni lazima kwanza pale patakaswe kisha mataifa mengine yafuate kabla ya yeye kuteremka ulimwenguni.
Hivyo Mungu akishamaliza kupatakasa Israeli, ndipo atakapoitumia Israeli kuitakasa dunia nzima kwa fimbo yake. Na ndio maana Mungu alisema hivi juu ya Israeli.
Yeremia 51:20 “ WEWE U RUNGU LANGU NA SILAHA ZANGU ZA VITA; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme;
21 na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;
22 na kwa wewe nitawavunja-vunja mwanamume na mwanamke; na kwa wewe nitawavunja-vunja mzee na mtoto; na kwa wewe nitawavunja-vunja kijana mwanamume na kijana mwanamke;
23 na kwa wewe nitamvunja-vunja mchungaji na kundi lake; na kwa wewe nitamvunja-vunja mkulima na jozi yake ya ng’ombe; na kwa wewe nitawavunja-vunja maliwali na maakida.”
Unaona?. Sasa kulingana na unabii wa kibiblia katika hatua tuliyopo sasa tunatazamia kushuhudia VITA KUU MBILI KUBWA zitakazopiganwa pale Israeli kabla ya mambo yote kuisha. Vita ya kwanza ni ile inayozungumziwa katika Ezekieli 38-39, ambayo ndio itakayofuata muda mfupi ujao Na vita ya pili ni ile ya HAR-MAGEDONI (Ufunuo 16:16), hiyo itakayokuja kuhitimisha utawala mbovu wa huu ulimwengu, unajulikana kama vita ya Mungu mwenyezi.
VITA YA ULIYOZUNGUMZIWA KATIKA EZEKIELI 38-39.
Siku zote Mungu kabla hajafanya jambo kubwa litakaloleta madhara huwa anatanguliza kwanza madogo madogo ili kuwakumbusha watu wachukue tahadhara kwani makubwa zaidi ya hayo yanakuja mbeleni. Na ndio maana Bwana Yesu alisema, kutakuwa na vita, na tetesi za vita, kutakuwa na njaa na matetemeko ya ardhi, hayo yote ni MWANZO WA UTUNGU, Unaona Hapo utungu wenyewe bado haujafika. Ukifika inamaanisha maafa yatakuwa makubwa zaidi kuliko haya tuyaonayo. Na ukitazama kwa ukaribu haya matetemeko ya ardhi tunayoyaona ulimwenguni na kusema ni makubwa, yanayoangamiza maelfu haya yote si kitu, Yapo matetemeko hasa yatakayokuja siku ile ya mwisho hii dunia itakapotikiswa pale visiwa na milima vitakapohama kwa nguvu ya tetemeko la ardhi ambalo Mungu atalileta mwenyewe duniani kote, na mvua ya mawe makubwa sana ambayo haijawahi kunyesha tangu ulimwengu kuumbwa, hapo ndipo wanadamu wote waliosalia wakati huo watalia na kuomba milima iwaangukie wajisitiri mbali na hasira ya Mungu. Ni mambo ya kutisha sana.
Ufunuo 6.12 “Nami nikaona, alipoifungua muhuri ya sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu,
13 na nyota zikaanguka juu ya nchi kama vile mtini upukutishavyo mapooza yake, utikiswapo na upepo mwingi.
14 Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake.
15 Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima,
16 wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo.
17 Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?”
Vivyo hivyo na kwenye suala la magonjwa na vita. Magonjwa yaliyopo leo yanatabika na homa zake ni za wastani, kadhalika na yanapatikana maeneo Fulani Fulani tu sio kila mahali haya yote ni mwanzo wa utungu,lakini yale yatakayoletwa na Mungu katika siku ile ya ghadhabu ya hasira yake, biblia inasema kutakuwa na jipu baya na bovu juu ya watu wote ulimwenguni walioipokea ile chapa ya mnyama. Jaribu kufikiri ukimwi na kansa, au ebola ni magonjwa yanayoogopeka, Lakini biblia haijayaona hayo, mpaka kulizungumzia hili jipu bovu tu lenyewe…ni baya kiasi gani mpaka wanadamu watamtukana Mungu kwa maumivu ya ugonjwa huo. Sio kutamani kuwepo huko ndugu.
Sasa tukirudi kwenye suala la vita. Leo Tunaweza kushuhudia vita ya kwanza na vya pili vya dunia vilivyoua watu zaidi ya watu milioni 80, huo ni mwanzo tu wa utungu, na lakini ipo vita itakayopiganwa siku za mwisho ambayo ndio ile ya mwisho inayojulikana kama HAR-MAGEDONI. Watu watakaouawa ni idadi kubwa mito ya damu itabubujika Israeli kwa wingi wa watu watakaouawa.
Sasa tuitazame Israeli kama jinsi ilivyofananishwa na mtini kuchipuka kwake, ambako kulikuwa ni mwaka 1948.
Tunaona kuwa tangu huo wakati Israeli ilipokuwa Taifa huru tena, mvutano mkubwa ulianza kujitokeza mashariki ya kati na duniani kote kwa ujumla. Nchi za kiharabu zikiigombania Israeli na mataifa mengine yakizisapoti.Mpaka kupeleka Israeli kuwa na maadui wengi pande zake zote. Watu wasifahamu kuwa jambo hilo linatoka kwa Bwana mwenyewe ili kuonyesha kuwa moja ya hizi siku mataifa yote yatahukumiwa na rungu la Bwana Israeli.
Hiyo Iliendelea hivyo hivyo mpaka kupelekea mwaka 1967 mataifa yote ya urabuni yakiongozwa na Syria kujikusanya kwa ajili ya kuipoteza Israeli katika ramani ya dunia. Lakini jambo hilo kama tunavyosoma katika historia, Israeli ilizipiga silaha zao za vita na vita kuisha ndani ya siku 6 tu. Kupeleka mpaka Israeli kuteka sehemu ya kubwa ya taifa lake ambalo hapo kabla lilikuwa haliyamiliki pamoja na nchi za kando kando.
Sasa hayo nayo ni mwanzo wa utungu ili kutupa sisi picha ya mambo yatakayokuja kutoka siku za hivi karibuni. Hii ilikuwa ni mataifa ya uarabuni lakini siku zinakuja mataifa yote ulimwenguni yataungana kwenda kupigana na Israeli hiyo ndiyo vita ya Har-magedoni.
Hivyo tukisoma kitabu cha Ezekieli 28-39, tunaona vita nyingine hapa ukiwa na muda wako mwenyewe unaweza kusoma sura zote mbili upate kuiona habari nzima ni vita ambayo itapiganwa tena kipindi hichi karibu na unyakuo kutokea. Embu Tusome mistari michache tu ya mwanzo.
EZEKIELI: MLANGO 38
1 Neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, kaza uso wako, umwelekee Gogu, wa nchi ya Magogu, mkuu wa Roshi, Mesheki, na Tubali, ukatabiri juu yake,
3 useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Gogu, mkuu wa Roshi, na Mesheki, na Tubali;
4 nami nitakugeuza na kutia kulabu katika mataya yako, nami nitakutoa, pamoja na jeshi lako lote, farasi na hao wapandao farasi, wote wamevaa silaha za namna zote, jeshi kubwa sana, wenye ngao na kigao, wote wakishika upanga;
5 Uajemi, na Kushi, na Putu, pamoja nao; wote wana ngao na chapeo;
6 Gomeri, na vikosi vyake vyote; nyumba ya Togarma, pande za mwisho za kaskazini, na vikosi vyake vyote; naam, watu wengi pamoja nawe.
7 Ujiweke tayari, naam, jiweke tayari, wewe na majeshi yako yote waliokukusanyikia, nawe uwe jemadari wao.
8 NA BAADA YA SIKU NYINGI UTAJILIWA; KATIKA MIAKA YA MWISHO, UTAINGIA NCHI ILIYORUDISHIWA HALI YAKE YA KWANZA, BAADA YA KUPIGWA KWA UPANGA, ILIYOKUSANYWA TOKA KABILA NYINGI ZA WATU, juu ya milima ya Israeli, iliyokuwa ukiwa wa daima; lakini imetolewa katika kabila za watu, nao watakaa salama salimini wote pia.
9 Nawe utapaa juu, utakuja kama tufani, utakuwa kama wingu kuifunika nchi, wewe, na vikosi vyako vyote, na kabila nyingi za watu pamoja nawe.
10 BWANA MUNGU ASEMA HIVI; ITAKUWA KATIKA SIKU HIYO, MAWAZO YATAINGIA MOYONI MWAKO, NAWE UTAKUSUDIA KUSUDI BAYA;
11 nawe utasema, Nitapanda juu niiendee nchi yenye vijiji visivyo na maboma; nitawaendea watu wanaostarehe, wanaokaa salama, wote wakikaa pasipo kuta, ambao hawana makomeo wala malango;
12 ili kuteka mateka, na kuwinda mawindo; uugeuze mkono wako juu ya mahali palipoharibika, ambapo sasa panakaliwa na watu, na juu ya watu waliokusanyika toka mataifa, waliopata ng’ombe na mali, wakaao katikati ya dunia.
13 Sheba, na Dedani, na wafanya biashara wa Tarshishi, pamoja na wana-simba wake wote, watakuambia, Je! Umekuja kuteka mateka? Umekusanya jeshi lako, ili kuwinda mawindo? Kuchukua fedha na dhahabu, kuchukua ng’ombe na mali, kuteka mateka mengi sana?
14 Basi, mwanadamu, tabiri, umwambie Gogu, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile watu wangu, Israeli, watakapokaa salama, hutapata habari?
15 Nawe utakuja kutoka mahali pako, kutoka pande za mwisho za kaskazini, wewe, na watu wa kabila nyingi pamoja nawe, wote wamepanda farasi, kusanyiko kubwa, na jeshi kuu;
16 NAWE UTAPANDA JUU UWAJILIE WATU WANGU, ISRAELI, KAMA WINGU KUIFUNIKA NCHI; ITAKUWA KATIKA SIKU ZA MWISHO, NITAKULETA UPIGANE NA NCHI YANGU, ILI MATAIFA WANIJUE, nitakapotakaswa kwako, Ewe Gogu, mbele ya macho yao.
17 Bwana MUNGU asema hivi; Je! Wewe ndiwe niliyemnena zamani za kale, kwa vinywa vya watumishi wangu, manabii wa Israeli, waliotabiri siku zile kwa muda wa miaka mingi, ya kwamba nitakuleta upigane nao?
18 Itakuwa katika siku hiyo, Gogu atakapokuja kupigana na nchi ya Israeli, asema Bwana MUNGU, ghadhabu yangu itapanda katika mianzi ya pua yangu.
19 Kwa maana katika wivu wangu, na katika moto wa ghadhabu yangu, nimenena, Hakika katika siku ile kutakuwako tetemeko kubwa katika nchi ya Israeli;
20 hata samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama wa kondeni, na vitu vyote vitambaavyo juu ya nchi, na wanadamu wote walio juu ya uso wa nchi, watatetemeka mbele ya uso wangu; nayo milima itatupwa chini, na magenge yataanguka, na kila ukuta utaanguka chini.
21 Nami nitaita upanga, uje juu yake katika milima yangu yote, asema Bwana MUNGU; nao upanga wa kila mtu utakuwa juu ya ndugu yake.
22 Nami nitamhukumu kwa tauni, na kwa damu; nami nitanyesha mvua ifurikayo, na mvua ya mawe makubwa sana, na moto na kiberiti juu yake, na vikosi vyake, na watu wa kabila nyingi walio pamoja naye.
23 Nami nitajitukuza, na kujitakasa, na kujidhihirisha, mbele ya macho ya mataifa mengi; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana”.
Sasa Nchi ya Magogu, biblia inayoitaja hapo ni eneo linalojulikana kama URUSI kwasasa. Hivyo nchi hii leo tunaoina ni nchi yenye nguvu sana kiasi kwamba inalitishia hata taifa la Marekani kwa nguvu zake na ukuu wake. Lakini biblia inasema siku moja mawazo yataliingia hili taifa ili kwenda kuishambulia Israeli. Na kibaya zaidi halitashuka peke yake, hapana bali litashuka na majeshi ya mataifa mengine mengi kama tunavyoyasoma hapo juu. Na mengi ya hayo yatakuwa na haya mataifa ya kiharabu, ambayo hayo kimsingi ni maadui wa Israeli tangu zamani, pamoja na nchi nyingi zilizokando kando ya Urusi.
Wote watapanga vita kuiendea ile nchi ndogo sana Israeli. Kama tunavyoona hata sasa Taifa linaloongoza kuwa na maadui wengi duniani ni taifa la Israeli, hivyo Urusi kwa kujipendekeza na kujionyesha kuwa yeye anayo nguvu na kwamba anaweza kuwasaidia watu waliowashindwa ISRAELI. Yeye naye siku hiyo atapanga vita na mabomu yake ya Atomiki ili kwenda kulisambaratisha taifa lile. Hawajui kuwa hapo ndipo Mungu alipokusudia uwe mwisho wa mataifa hayo yote chini ya jua. Siku hiyo Urusi itapotezwa kwenye ramani ya dunia, kwasababu Bwana atakuwa upande wa Israeli. Na wa-Rusi siku hiyo watasoma maandiko haya ya Ezekieli na kutambua kuwa unabii huo ulikuwa unawahusu wao.
Kumbuka vita hiyo japo itauwa watu wengi sana kiasi kwamba biblia inasema mizoga yao itakuwa inazikwa kwa muda wa miezi 7 ikikusanywa tu, na silaha zao zitakuwa zikitumika kama kuni kwa muda wa miaka 7, lakini huo utakuwa ni mwanzo tu wa utungu. Vita yenyewe kuu bado. Vita ya Har-magedoni ambayo itahusisha mataifa yote ulimwenguni.
Tutakuja kuizungumzia vizuri vita hii [Har-Magedoni] katika makala nyingine. Lakini tufahamu kuwa vita inayozungumziwa katika Ezekieli 38-39 ipo mbioni kutokea, kama tunavyoona sasahivi mvutano ulivyo mkubwa mashariki ya kati na ishara kuwa vita vinajiandaa kupiganwa muda wowote. Hivyo ndivyo Mungu anavyozidi kuitasa Israeli kidogo kidogo, Na ndivyo pia wanavyojiandaa kumpokea Masiya wao.
Swali tujiulize wakati sasahivi neema inarudi Israeli, mimi na wewe mpaka mambo hayo yatakapotokea tutakuwa wapi? Kumbuka ndugu tuliambiwa tukiyaona hayo yanaanza kutokea basi tunyanyue vichwa vyetu, kwa kuwa ukombozi wetu umekaribia. Ikiwa na maana UNYAKUO wetu upo karibu.
Kristo yupo mlangoni ndugu. Unasubiri nini usiufanye leo wito wako na uteule wako imara?. Walioishi kipindi chote cha nyuma kuanzia miaka ya 1900 kurudi nyuma mpaka kipindi cha kanisa la kwanza hawakukishuhudia kitu hichi sisi tunachokishuhudia leo yaani taifa huru la Israeli. Na biblia ilishasema kizazi hiki hakitapita, sasa unasubiri nini usiushindanie wokovu katika muda huu mfupi uliobaki?.
Ungependa mambo hayo yakukute kwa ghafla, Bwana amesema dunia hii itaangamizwa kwasababu ya maovu yake. Na wenye haki watapata kwa Mungu waepushwe nayo.. je! Na wewe ungependa uwe miongoni mwa watakaoharibiwa katika ile siku ya Bwana? Kama sivyo mgeukie Kristo, ambaye yeye ndio safina pekee iliyothibitishwa na Mbingu kwa wokovu wa mwanadamu.
Bwana akubariki.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/12/05/mambo-yatakayotokea-israeli-siku-za-hivi-karibuni/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.