IMANI YENYE MATENDO;

by Admin | 31 January 2019 08:46 pm01

Waebrania 11: 3 “Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri”.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze Neno la Mungu, leo tutajifunza somo fupi linalohusiana na Matendo ya Imani.”

Kama Biblia inavyotafsiri maana ya Imani kuwa “ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Waebrania 11:1”..

Tukitaka kujua kitu kinachoendelea upande wa pili au kinachokuja mbele yetu, au kilichokatika mazingira yetu tutatumia milango yetu ya ufahamu aidha macho, au masikio, au pua, au ngozi zetu, au ulimi..hizo zitatusaidia kujua ni nini kinaendelea upande mwingine au ni nini kinakuja mbele yetu..Kama hatuna hizo basi hatuwezi kujua chochote kinachoendelea,. Kwamfano wewe unaweza ukawa unapika pilau nyumbani kwako, lakini jirani yako aliye nyumba ya nne akajua unachofanya, japo hajakuona wala hajaingia nyumbani kwako,lakini amepata uhakika huo, na ndivyo ilivyo sasa kitu kilichomfanya ajue hayo yote si kingine zaidi ya pua yake. Vivyo hivyo na katika kuona, kuhisi, ulimi. Vyote hivi ni kuthibitisha kitu Fulani au jambo Fulani au mazingira Fulani.

Lakini Biblia haijatuambia kwamba kuona kwa macho au kusikia au kuhisi ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo, vinaweza kutupa uhakika wa mambo yaliyopo sasa yanayotuzunguka lakini sio kwa mambo yatarajiwayo, lakini Biblia inatuambia Imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo, unaweza usione, wala usisikie, wala usihisi chochote na bado ukapata uhakika kwamba kuna gari linakuja mbele yako kwa kutumia Imani na kweli ikawa hivyo..Unaweza usione, wala usihisi, wala usisikie, wala usinuse lakini ukajua mwakani kutakuwa na njaa na kweli ikawa hivyo… Hii ikiwa na maana kuwa imani ni hisia nyingine ya kipekee tofauti na hisia hizi tano tulizonazo..Kama mhubiri mmoja alivyowahi kusema kuwa “IMANI NI HISIA YA SITA TOFAUTI NA ZILE TANO”.

Kwahiyo Mungu hakuimba dunia kwa macho, wala kwa masikio wala kuhisi, wala kwa chochote kile, bali aliimba dunia kwa Imani.

Lakini leo hatutaingia huko sana, bali tutajifunza zaidi juu ya Matendo ya Imani.

Kama Biblia inavyotuambia “imani isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.”..Ni wazi kuwa Ili imani iwe hai ni lazima iwe na Matendo. Huwezi ukaona kwa macho yako gari linakuja kwa kasi mbele yako na bado ukabakia pale pale, ni ngumu sana..ni lazima utajikuta unalikwepa tu! wakati mwingine hata sio kwa kutaka..utajikuta tu mwili unajitupa upande wa pili, au mtu anapoleta kitu fulani machoni pako utajikuta tu unafumba macho, wakati mwingine sio hata kwa kutaka, unaposikia harufu ya chakula fulani ukipendacho mahali mate ni lazima yatakutoka tu! wakati mwingine sio kwa kupenda inatokea inakuwa hivyo tu…ikifunua kwamba kile unachokiona lazima ukifanyie kazi.

ndivyo inavyokuwa pia kwa Imani, siku zote lazima ifuatane na matendo fulani, kwa sababu na yenyewe ni hisi, Imani ikishahisi kama kuna kitu mbeleni kinakuja ni lazima matendo yafuate, na hayo matendo wakati mwingine sio kwa hiari ya mtu, yanajitengeneza tu yenyewe..kama vile yanavyojitengeneza pale mtu anapofumba macho ghafla kitu kinakuja machoni pake. Ndio maana biblia inasema “imani isipokuwa na matendo imekufa”.

Kadhalika tunaweza kujifunza zaidi katika uumbaji wa Mungu, Tunajua Mungu aliiumba dunia na vitu vyote kwa Imani, Bwana alisema na iwe hivi na ikawa hivyo..Lakini hakuishia kusema na iwe hivi au vile na kuishia pale. Hapana tunaona baada ya kusema na iwe hivi..akaendelea mbele “kufanya kile kitu”… na ndipo kile kitu kikatokea.. Tunasoma.

Mwanzo 1: 6 “Mungu akasema, NA LIWE anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji.

7 Mungu AKALIFANYA ANGA, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo.”

Hapo tunaona Mungu alisema…na bado Mungu akafanya…hakuishia kusema tu, bali pia akafanya. Kudhihirisha “matendo ya ile imani aliyokuwa nayo”..Kadhalika tunasoma pia katika mistari inayofuata.. ..

“14 Mungu akasema, NA IWE MIANGA katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili na majira na siku na miaka;

15 tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo.

16 MUNGU AKAFANYA MIANGA MIWILI MIKUBWA, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia.

17 Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi”

Na hapa pia tunaona Mungu, alisema na Mungu akafanya.

“20 Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu.

21 Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema”.

Vivyo hivyo na hapa tunaona jambo lile lile Mungu alisema na Mungu akaumba..Kwahiyo Mungu hakuishia kusema tu, bali pia alitenda..kudhihirisha Matendo ya ile imani.

Kadhalika na mambo yote Mungu aliyoyasema kwa Neno lake aliyatendea kazi, tena kazi kubwa sana…Na ndio maana tunasoma baada ya Mungu kuumba vitu vyote kwa siku sita alipumzika siku ya saba…akaacha kufanya kazi zake zote… Sasa kama ilikuwa ni “kusema tu na kuachia pale” kwanini aseme alipumzika siku ya saba??… kwani kuzungumza tu nako kunahitaji kupumzika??..ni wazi kuwa kwa yale matendo ya Imani aliyokuwa anayafanya ndiyo yaliyomfanya apumzike. Kazi kubwa ndio ilikuwa hapo pa matendo na si pengine.

Vivyo hivyo na sisi Mungu katuumba kwa mfano wake.. Kama yeye aliiumba dunia kwa Imani yenye matendo na sisi vivyo hivyo tukitaka kupata kitu lazima tuenende kwa Imani yenye matendo. Kwanza TUNASEMA katika vinywa vyetu..huku tukiwa na uhakika kwamba kile kitu tulichokisema kitakwenda kutokea…Na moja kwa moja pasipo kulazimishwa wala kusukumwa tunaingia kwenda kuifanyia kazi ile Imani…

Kadhalika tunapohitaji riziki za ulimwengu huu, tunaweka imani yetu katika matendo..Kile tunachoamini Mungu atakwenda kutupa kwa wakati huu, hizi tunaweka katika matendo, tunakwenda kukifanyia kazi kwa bidii ili kutokee, tusipofanya hivyo hakitatokea.

Vivyo hivyo na kama tunaamini tutakwenda mbinguni siku moja, na kwamba Bwana atakuja kutunyakua kwenda naye mawinguni..Ni lazima kuanzia sasa tukifanyie kazi kile tunachokiamini, pasipo kulazimishwa wala kusukumwa, ni lazima ndani ya moyo wetu tujikute tunatendea kazi ile Imani iliyo ndani yetu. Hivyo tunapaswa tujiweke mbali na dhambi, lazima tujiweke mbali na uasherati, uchawi, rushwa, utukanaji, uvaaji mbaya, ulevi, uvutaji sigara,anasa, usengenyaji, usagaji, utoaji mimba,ulawiti,ushoga, utazamaji pornography na ufanyaji masturbation, uuaji, chuki,wivu, majigambo, ibada za sanamu na matendo yote ya giza.

Ni lazima tukeshe katika roho kama Bwana alivyotuagiza, ni lazima tuhakikishe taa zetu zimejaa mafuta mfano wa wale wanawali wenye busara, na mafuta yenyewe ni Roho Mtakatifu,

Vinginevyo mbingu tutaisahau..vinginevyo hatutaingia katika sabato yetu iliyoahidiwa katika biblia (Warumi 4:9), hatutaingia katika pumziko la milele lililoko mbele yetu, Kwasababu Bwana alipomaliza kuitendea kazi imani yake ndipo alipumzika na kuibariki ile siku.

Na sisi tukiitendea kazi vizuri Imani yetu tuliyokabidhiwa mara moja tu, tukiwa wakamilifu na kujitenga mbali na uchafu wote wa dunia hii, na kujiweka katika utakatifu tumeahidiwa kuingia katika sabato yetu ya utawala wa miaka 1000 na umilele, lakini kama hatutaitendea kazi imani hii ya Thamani iliyo katika Yesu Kristo, na kujichanganya na ulimwengu huu, na kuudharau msalaba…Neno la Mungu lisilodanganya linatuonya.

Ufunuo 21: 8 “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, SEHEMU YAO NI KATIKA LILE ZIWA LIWAKALO MOTO NA KIBERITI. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Kazi ya matendo ya Imani yako ni ipi ndugu?? Tangu umeanza kusikia Injili mpaka leo ni muda, na umezalisha nini?? matendo ya imani yako ni yapi?? UCHAFU AU UTAKATIFU?. Jibu unalo wewe, lakini kumbuka Neno moja, Bwana anasema hakawii kuja, wala kuzitimiza ahadi zake..na anakuja na ujira wake, kumlipa kila mtu kile anachostahili.. 

Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila MTU KAMA KAZI YAKE ILIVYO.

13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.

14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.

15 Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.

16 Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi”.

Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana;

USIISHIE KUTAZAMA JUU, ENDELEA MBELE.

SI SHETANI BALI NI WEWE. (CHAGUA MEMA)

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/31/imani-yenye-matendo/