by Admin | 31 January 2019 08:46 pm01
Sherehe za siku hizi zinatupa picha kamili jinsi mambo yatakavyokuja kuwa huko mbeleni baada ya unyakuo kupita. Kama tunavyofahamu leo hii hakuna sherehe yoyote ya arusi utakayokwenda bila mwaliko wowote, vinginevyo ukijaribu kufanya hivyo utajikuta utaishia getini, kadhalika mwaliko peke yake hautoshi ni lazima uambatanishwe na mchango wa kiasi fulani cha fedha vinginevyo hata kama utakuwa na vigezo vyote vya kuingia harusini bado utazuiliwa tu kuingia..
Ukiwa ni msomaji wa biblia utajua kuwa ipo karamu ambayo imekwisha andaliwa huko mbinguni, hii ni karamu iliyo KUU na ya kipekee kuliko zote, iliyoandaliwa na Mungu mwenyewe kwa ajili ya Kristo na bibi-arusi wake (yaani Kanisa). Kama tunavyofahamu utaratibu wa harusi, sharti ndoa ifungishwe kwanza ndipo sherehe ifuate, vivyo hivyo katika utaratibu wa kimbinguni, ni sharti Kristo afunge ndoa kwanza na bibi-arusi wake, ndipo karamu ifuate baadaye. Na ndoa hiyo haifungiwi mahali pengine zaidi ya hapa hapa duniani. Hii inatokea pale mtu mwenyewe binafsi anapochukua uamuzi wa kumfuata Kristo, kwa kuacha maisha yake maovu ya dhambi, na kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zake, hapo ndipo anakuwa amekidhi vigezo vya kuwa mwalikwa wa karamu ile ya mwanakondoo ambayo itakuja kufanyika baadaye kidogo.
Ndugu, kosa kila kitu, kosa mali, kosa mtoto, kosa uzuri, kosa hata marafiki,potoza hata chochote unachokiona kina thamani, lakini usifikirie hata siku moja kuikosa karamu hiyo, kwasababu mahali popote biblia inapoizunguzia karamu hii inatumia neno HERI..Biblia haina maneno ya kujitosheleza kuelezea maana ya hili Neno heri, yaani tunawezeka kusema, amebahatika sana, au amebarikiwa sana, amependwa bure, yeye atakayepata neema ya kualikwa kwenye karamu hiyo, kwasababu wengi wanaojulikana kama wakristo wataikosa.
Ufunuo 19:6 “Nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, na kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi yenye nguvu, ikisema, Haleluya; kwa kuwa Bwana Mungu wetu, Mwenyezi, amemiliki.
7 Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.
8 Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni MATENDO YA HAKI YA WATAKATIFU.
9 Naye akaniambia, Andika, HERI WALIOALIKWA KARAMU YA ARUSI YA MWANA-KONDOO. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu.”
Unaona hapo? Maandiko yanamalizia na kusema “Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu”, ikiwa na maana kuwa hiyo Karamu ni lazima ije tu kwa wakati uliouamuru Mungu, na tunajua Mungu hasemi uongo. Na wana heri nyingi wale wote watakapata neema ya kualikwa humo.
Tunajua hakuna mtu yeyote asiyefurahia sherehe, au mwaliko wowote wa karamu, hiyo ni asili ambayo Mungu kamuumbia kila mwanadamu kupenda kufurahia mambo mema, lakini aliiweka hiyo kiu kwa makusudi kabisa kwa ajili ya Karamu yake mwenyewe ambayo amewaandalia watoto wake wote. Ili kusudi kwamba watu watazamapo hizi sherehe za duniani wajue kuwa ipo sherehe iliyo kuu ambayo mambo yake biblia inasema jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia inayokuja huko mbeleni, Hivyo mtu aifiripo hayo ni wajibu wake, kujitia moyo kwa kufanya juu chini kuhakikisha na yeye ni mmojawapo wa watakakuwemo kwenye karamu hiyo ambayo itafanyika mbinguni.
Lakini kama tunavyojua bibi-arusi yeyote ni lazima awe na vazi la harusi gauni jeupe zuri safi,refu, hawezi kuvaa kanga na kusema anakwenda kuolewa na ndivyo ilivyo kwa Kristo Yesu, yeyote yule atakayestahili kuwa bibi-arusi wake ni lazima awe na Vazi la harusi jeupe ling’aralo na biblia inasema vazi hilo linawakilisha MATENDO YA HAKI YA WATAKATIFU.
(Ufunuo 19: 7 “Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.
8 Naye amepewa kuvikwa KITANI nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo NI MATENDO YA HAKI YA WATAKATIFU”.
Kama vile tunavyoona sasahivi mtu hawezi kupewa kadi ya mwaliko kama hajachangia chochote, vivyo hivyo kusema umeokolewa tu halafu matendo yako hayaakisi wokovu wowote, hauna mchango wowote kwenye wokovu wako, huishi kama mtu anayemngojea Bwana wake aende naye harusini, anasa, ulevi, pornography, matusi, chuki, usengenyaji, uasherati n.k..Basi fahamu kuwa siku ile itakapofika utabaki hapa hapa duniani, hautakwenda na Bwana.
Unyakuo ukishapita, mfano ikiwa ni leo, watakaokwenda kwenye hiyo karamu ambayo itakuwa ni wale biblia inayowaita wanawali werevu tu (Mathayo 25), watajikuta mbinguni, ni karamu ya miaka 7 mbinguni kabla ya kurudi tena kuja kutawala na Kristo kwa muda wa miaka 1000. Mtu asikudanganye kukwambia hiyo itakuwa ni kwa kila mtu, hapana, bali ni kwa wale Kristo aliofunga nao ndoa, wakiwa hapa hapa duniani, na waliokidhi vigezo vyote vya kuhudhuria karamu hiyo yaani wakristo watakatifu, wengine wote waliosalia pamoja na wale wakristo vuguvugu watabaki hapa duniani kwa ajili ya ile dhiki ya mpinga-kristo.
Hata vitu vya asili vinatufundisha, tukiutazama mwezi katika biblia unawakilisha kanisa la Kristo, na ile nyota ya Asubuhi inamwakilisha Yesu. Lakini unaweza ukajiuliza ni kwanini mwezi unabadilika badilika sio kama jua au nyota. Leo utauona upo kama duara, kesho kama mundu, kesho kutwa kama tufe, leo unaonekana nusu kesho robo n.k..Hii inamaanisha kuwa kanisa la Kristo, japo ni kamilifu lakini bado sio wote kwenye kanisa walio wakamilifu. Na kama ukitazama wale wanaotumia Mwezi na nyota kama nembo za taifa lao, wengine wanazitumia kama nembo za dini zao,utaona hawauchori mwezi wote, na nyota pembeni yake. Bali wanachukua kile kipande kidogo sana cha mwezi kama ukucha na kukiweka na ile nyota ya asubuhi.
Hawajui kuwa lile linamfunua Kristo na bibi-arusi wake, kwamba Kristo akija hatalinyakua kanisa zima, hapana bali ni bibi-arusi waliosafi wasio na mawaa katika ya kanisa lote. (Soma mfano wa wanawali werevu na wapumbavu utaliona hilo. Mathayo 25).
Na ndio maana upo umuhimu wa kutengeneza mambo yako sawa sasa kabla siku hizo hazijafika, Bwana anamwalika mtu yeyote aliye tayari, lakini habari mbaya ni kwamba wale wanaoalikwa kwa kuhubiriwa injili kila siku ndio wanaokuwa wakwanza kukawia na kutoa udhuru. Embu soma kisa hiki.
Luka 14: 15 “Basi aliposikia hayo mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye alimwambia, HERI YULE ATAKAYEKULA MKATE KATIKA UFALME WA MUNGU.
16 Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi,
17 akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari.
18 Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe.
19 Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe.
20 Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja.
21 Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete.
22 Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi.
23 Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa.
24 Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu”.
Unaona hapo ndugu? Kristo anapokuita leo uokoke ni kwasababu anakuwazia mawazo ya amani ili kukupa wewe tumaini katika siku zako za mwisho (Yeremia 29:11). Utajisikiaje leo hii unyakuo usikie umepita huku ukijua wenzio tayari wakati huu wameshabadilishwa miili na kupewa mingine ya utukufu, wakati kama huu wenzako wanauona uzuri wa Kristo aliokwenda kuwaandalia kwa miaka 2000, wanamwona uso kwa uso,wanapata furaha isiyoelezeka wewe upo huku chini unasubiria kukutana na dhiki ya mpinga-kristo isitoshe, ziwa la moto linakusubiria. Utajisikiaje?. Ni kilio cha kusaga meno, ni uchungu uliochanganyikana.
Piga hesabu ikiwa unapenda maisha utaona kuwa ni heri leo utubu uwe mmoja wa bibi-arusi waliotiwa muhuri na Mungu kwa Roho wake. Lakini kama dunia imekuahidia furaha kubwa zaidi ya hiyo basi uamuzi ni wako. Lakini jua kuwa hizi ni siku za mwisho na hatuna garantii ya kizazi kingine mbele yetu. Hili ni kanisa la mwisho linaloitwa Laodikia, na Mjumbe wake ameshapita, ufunuo 3:21 Pia fahamu kuwa wapo wateule wa Mungu duniani (bibi-arusi) usiku na mchana wanamlilia Bwana aje.
Ufunuo 22.17 “Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure”.
Bwana akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
UMEPATA UHAKIKA WA KUTOKUINGIA HUKUMUNI KATIKA SIKU ILE?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/31/karamu-ya-mwana-kondoo/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.