USIMWABUDU SHETANI!

by Admin | 28 February 2019 08:46 am02

Mungu alipomtuma Musa, kwa Farao, tunasoma habari alimpa maagizo ya nini cha kufanya atakapofika kwa Farao, na mojawapo ya maagizo hayo alimwambia akifika aitupe chini ile fimbo aliyokuwa nayo mkononi mbele ya Farao nayo itageuka na kuwa nyoka, na kisha aitwae tena mkononi mwake nayo itageuka kuwa fimbo kama mwanzo. Na pia tunaona Bwana alimfanyisha mazoezi kabisa akiwa kule kule mlimani kabla hata ya kwenda Misri kwa Farao, maana Mungu alimwambia palepale aitupe chini ile fimbo na alipoitupa ikageuka kuwa nyoka na Musa alipoona fimbo imegeuka kuwa nyoka alitaka kukimbia..

Bwana akamwambia akamshike Yule nyoka Mkia, kwa kusitasita na kutetemeka alikwenda na kumshika, na mara saa hiyo hiyo Yule nyoka akageuka na kuwa fimbo tena..Zoezi hilo lilimsadia kupata ujasiri, pindi atakapofika kwa Farao na kuitupa chini ile fimbo itakapogeuka na kuwa nyoka, asiigope kuishika na kuitwaa tena iwe fimbo.

Sasa swali la kujiuliza ni kwanini Mungu aitumie ile fimbo kuigeuza kuwa nyoka na wala si kitu kingine, kwanini hakutaka igeuke na kuwa chuma, au igeuke na kuwa sungura, au kiumbe chochote kile tofauti na NYOKA!.

Ili tuelewe hilo vizuri, turudi kidogo kujifunza histori ya Taifa la Misri, Misri ni Taifa lililopo kwasasa katika Bara la Afrika, kaskazini mashariki mwa Afrika, na asili ya Taifa hilo ilikuwa ni wana wa HAMU, aliyekuwa mwana wa Nuhu, Yule aliyeuona uchi wa Baba yake na asiusitiri, na hivyo akalaaniwa. Kwahivyo wana wa Hamu wakasafiri pande za kusini wakajenga miji huko, na Taifa mojawapo la wana hao wa Hamu ndio Misri. Mambo mengi yaliendelea hapo katikati hatuna muda wa kutosha wa kuyazungumzia yote lakini historia inasema ndio Taifa lililokuja kuwa na nguvu kuliko mengine yote kwa wakati huo.

Utamaduni wa Taifa hilo haikuwa kumwabudu Mungu wa Israeli, kwasababu walikuwa hawamjui Mungu wa Israeli bado, hivyo walikuwa wana miungu yao mingine mingi mingi tu!, waliabudu jua, mwezi na mambo mengine mengi…lakini moja ya miungu waliyokuwa wanaiabudu na kuipa heshima ya juu zaidi, ilikuwa ni NYOKA. Na aina ya nyoka hao waliokuwa wanawaabudu anajulikana kama COBRA. Walikuwa wanaamini kuwa nyoka aina ya Cobra ni mungu mkuu ambaye ana uwezo mkubwa sana katika kulilinda taifa lote la Misri dhidi ya Maadui zao, walitumia sanamu yake kama ishara kila mahali katika nyumba zao za kawaida na katika makasri yao makubwa ya kifalme. Hata katika kofia za kifalme za wafalme kulikuwa ni kijisanamu kidogo cha cobra kwenye kipaji cha uso kinachoangalia mbele, hicho kilikuwa kinavaliwa daima waliamini kuwa kama vile nyoka aina ya Cobra anavyotema mate ya sumu dhidi ya maadui zake usoni, vivyo hivyo cobra wanayemwabudu huyo huyo atawatemea moto maadui wa Farao wote wanaokuja mbele yao.

Kwahiyo ilikuwa ni imani iliyoheshimika sana, na ilikuwa inawapa matunda, kwasababu nyuma yake alikuwa ni shetani, na kama unavyojua shetani naye anawapa anaowapenda kama anavyotaka. Kwahiyo huyo mungu wao nyoka alikuwa anawapa ushindi mara nyingi ndio maana, Taifa hilo la Misri likainuka kuwa na nguvu kila mahali.

Wengi tunafikiri kuwa miungu hiyo ya Misri haikuwa na nguvu yoyote! Usidanganyike! Ilikuwa ina nguvu kama kawaida, na wamisri walikuwa wanaona inavyowasaidia, na endapo wakiwa hawaiabudu inavyopaswa ilikuwa inawaletea madhara, kwahiyo sio kwamba wamisri walikuwa wanaabudu kitu kisicho dhahiri!.. Ukitaka kujua walikuwa wanaabudu kitu kilicho dhahiri au la! Tazama yale mapigo, Musa aligeuza fimbo kuwa nyoka nao pia wakafanya hivyo hivyo, na baadhi ya mapigo pia waliweza kuiga, sasa kama hiyo miungu yao haikuwa dhahiri kwanini iliweza kufanya ile miujiza?? Jiulize hilo, na kama hiyo miungu yao ilikuwa na nguvu ya mpaka kuweza kubadilisha fimbo kuwa nyoka unadhani ingeshindwa vipi kutemea moto kwa maadui zao wakiwa vitani??..

Hata Israeli wakati Fulani walipokengeuka na kuanza kuabudu mabaali, sio kwamba walikuwa wanaabudu kitu kisichokuwepo, hapana! Walikuwa wanaabudu kitu kilicho dhahiri kabisa (ambacho ni shetani mwenyewe pasipo wao kujijua)..Na hata wakati ule walipojaribu kushusha moto mbele ya Eliya juu ya ile dhabihu usidhani ni kwamba walikuwa wanafanya kitu cha kujaribisha au kubahatisha, hapana! hiyo miungu yao kushusha moto sio jambo kubwa, Na ilishawahi kushusha hapo kabla, ndio maana unaona walipata ujasiri mbele ya Eliya kulileta lile shindano, lakini kilichowashtusha ni kama tu hicho kilichomshtusha Farao kuona nyoka wake wanamezwa mbele ya macho yake, na makuhani wa mabaali vivyo hivyo walishtuka kuona mbona moto haushuki kama siku zote!..

Kwahiyo Musa wakati anamwendea Farao, Mungu alitumia ishara ya nyoka, ili kuwaonyesha wa Misri kuwa mungu wanayemwabudu sio wa kweli, ingawa anawatendea miujiza , na kwamba nguvu zake zina mipaka, yupo mwenye nguvu kuliko mungu wao cobra wanayemwabudu, ndio maana alitumia ishara ya nyoka awali kabisa ili wamisri wamwelewe vizuri, kwasababu laiti angetumia ishara ya kugeuza fimbo kuwa sungura wamisri wasingeiamini kwasababu wao wanajua miungu ni mfano wa viumbe wakali kama nyoka, na ndio maana unaona nyoka wa Musa aliwameza wale nyoka wa Farao. 

Kwa ufupi ishara ile, ilitosha kabisa kumwaminisha Farao kuwa Mungu wa Israeli ni Mungu mkuu kuliko mungu wao. Hata wamisri wote baada ya kuiona ile ishara waliamini, kulikuwa hakuna haja ya kuendelea na ishara nyingine mbele…kwasababu mbele ya macho yao wameshuhudia mungu wao cobra wanayemweshimu na anayewasaidia siku zote katika vita, amemezwa na Mungu mwingine, ni ishara madhubuti kuwa endapo wakiendelea kushindana na huyo Mungu watamezwa vile vile, kama mungu wao alivyomezwa…Lakini kwasababu Mungu alitaka kuonyesha utukufu wake wote, ndiyo akaufanya moyo wa Farao usiamini, uwe mgumu. Lakini katika hali ya kawaida, Farao tayari alishaamini.

Ndugu kama uliwahi kuomba rozari na ikakupa majibu uliyoyaomba, uliiomba fedha ikakupa, uliiomba rozari ushindi ikakupa, na ukaiamini kiasi kwamba unatembea nayo kila siku shingoni, kwasababu haikuangushi……napenda nikwambie ndugu yangu mpendwa huyo sio Mungu ni shetani nyuma ya hiyo rozari, haijalishi hiyo rozari imekufanikisha kiasi gani, nataka nikuambie yupo Mungu aliye mkuu kuliko hiyo rozari atakayeimeza hiyo rozari unayoivaa na kuiomba kila siku, Hata Farao alitumia nyoka kuamini hakuna mungu zaidi ya huyo, na nguvu za Cobra zilimfanikisha kuliko mataifa yote duniani, lakini alipokuja Mungu wa miungu na kumkataa huyo. Misri iligeuka kuwa kama jalala la dunia.

Kama umekuwa ikiisujudia sanamu kanisani kwako pasipo kujua kuwa unamwabudu shetani na imekujibu maombi na kukupa kila unachokihitaji… Mungu hakuweza kukuhukumu kwasababu ulikuwa huujui ukweli, lakini leo umeujua ukweli, umgeukie yeye mwenye nguvu kuliko hiyo sanamu, itupe leo ivunje vunje leo, acha kuiabudu kwasababu yupo Mungu juu mwenye nguvu kuliko hiyo sanamu ya BIKIRA MARIA unayoiabudu na anataka kukubariki kuliko hata hapo ulipo. Anataka kukupa mafanikio kuliko hata hayo uliyonayo. Ambayo shetani amekupiga upofu kukudanganya kwamba ni mafanikio, kumbe ni mafanikio feki,…hiyo sanamu haiwezi kukupa raha nafsini mwako, hiyo sanamu haiwezi kukusamehe dhambi, hiyo sanamu haiwezi kukufanya uwe mtakatifu, hiyo sanamu haikupi kibali cha kuingia ufalme wa mbinguni, hiyo sanamu haiwezi kuondoa ulevi ulionao! Haiondoi uasherati ndani yako!! Hiyo sanamu sio Mungu wa kweli! Kwasababu ndivyo ilivyokuwa hata kwa Farao, wale nyoka aliokuwa anawaabudu walimpa utajiri lakini walikuwa hawamhukumu kuhusu tabia yake mbaya ya kuonea watu wasiokuwa na hatia! Mungu gani huyo!

Utasema huyo Mungu mbona watu wake ni maskini, nataka nikuambie hata Farao aliwaona wana wa Israeli ni maskini na kuwatesa kule kwenye mashimo ya matope! Lakini Misri yote ilishtuka kuona kuwa wale wanaowadharau kumbe ndio wanaomwabudu Mungu mwenye nguvu kuliko Mungu wao…..siku ile walipoona Misri yote imeteketea,…na wewe usiangalie hali ya watu wanaomwabudu Mungu wa Kweli ipoje, wapo vile kwasababu fulani tu, lakini hawatakuwa vile siku zote, ipo siku watang’aa kama jua, isikilize hii sauti ya Mungu inayozungumza nawe sasa…Mungu wa kweli sio nyoka, wala ekaristi, wala sanamu ya kiumbe chochote kile, wala sanamu ya mwanadamu yoyote Yule, wala Mungu wa kweli haabudiwi kwa kupitia sanamu ya Bikira Maria, wala chochote kile, Mungu wa kweli anaabudiwa juu mbinguni KATIKA ROHO NA KWELI.

Pengine umekwenda kwa waganga wa kienyeji na kwa kupitia wao umepata mafanikio, na wamekwambia wakristo hawamwabudu Mungu wa kweli, nataka nikuambia ndugu yangu, wamekudanganya na wamekupoteza..Wale nyoka walimpa Farao mafanikio makubwa sana kuliko uliyonayo wewe, lakini hao hao hawakuweza kumwokoa na hukumu ya Mungu iliposhuka juu ya Misri.

Na wewe siku hizi usiweke moyo wako mgumu, achana na hao waganga, kwasababu utaelekea kwenye ziwa la Moto, tupa leo hirizi zote walizokupa, choma moto, mvue mwanao hirizi zote ulizomvalisha kiunoni na shingoni na mikononi, tupa na wewe kila kitendea kazi ulichopewa na mganga wa kienyeji eti upate amani, fedha au utajiri, au vikulinde…hivyo vitendea kazi vitakulinda dhidi ya wachawi wenzako tu tena wenye nguvu kidogo kuliko mganga wako lakini wakija wachawi wengine wenye nguvu kuliko wewe na mganga wako watakuua na kukushinda tu!, na zaidi ya yote ni heri ingekuwa hivyo tu!! Ghadhabu ya Mungu bado inakungojea endapo ukikataa kutubu ndiyo itakayokuharibu kabisa kama ilivyomuharibu Farao, alipoteza fahari yake yote na kufiwa na mwanawe wa pekee.

Ukiyafahamu hayo ni wakati wa kugeuka, Bwana anakupenda na kukuhitaji, kama hujampa Bwana maisha yako, mlango wa Neema bado upo, ila hautakuwepo siku zote, biblia inasema utafika wakati mlango utafungwa, na watu watalia na kuomboleza wakiomba Bwana awafungulie, na Bwana hatawafungulia, Hivyo tubu leo kwa kumaanisha kuacha kabisa maisha ya dhambi uliyokuwa unayaishi huko nyuma, maisha ya usengenyaji, maisha ya rushwa, maisha ya uasherati, maisha ya utazamaji pornography, maisha ya usagaji, maisha ya ulawiti, maisha ya ushirikina, na uhudhuriaji wa waganga wa kienyeji,maisha ya aubuduji sanamu, maisha ya ulevi na sigara.n.k n.K

Na baada ya kufanya hivyo kama hujabatizwa nenda katafute ubatizo sahihi mahali popote pale kulingana na maandiko, na ubatizo sahihi ni wa maji mengi na kwa JINA LA YESU kulingana na Matendo 2:38, na baada ya hapo Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi, maana kwa nguvu zetu hatuwezi kamwe kushinda dhambi, na Roho huyo huyo atakusaidia kuielewa biblia na kukuongoza katika kweli yote usipotee kwa kuchukuliwa na upepo wa shetani. Na ukizingatia kufanya hivyo utakuwa umezaliwa mara ya pili, na kuwa na uhakika wa kuiona mbingu.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine, na utakuwa umeshiriki katika kuisambaza injili ya Kristo.

Maran atha!

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

NEHUSHTANI (NYOKA WA SHABA)

UZAO WA NYOKA.

WANA WA MAJOKA.

BWANA YESU ALIMAANISHA NINI ALIPOSEMA TUWE NA BUSARA KAMA NYOKA?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/02/28/usimwabudu-shetani/