MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

by Admin | 20 March 2019 08:46 pm03

Tukiachilia mbali ule waraka wa kwanza ambao Mtume Yohana aliuandika kwa watu wote, zile nyaraka mbili za mwisho zilizosalia hakuzielekezwa kwa watu wote, bali kwa watu husika, na tunaona ndio zimekuwa nyaraka fupi kuliko zote katika biblia nzima, lakini zimebeba ujumbe wa msingi sana, kwa makundi ya watu waliozungumziwa huko..Kwa mfano kama tukiutazama ule waraka wa tatu, tunasoma mtume Yohana aliuelekeza kwa ndugu mmoja anayeitwa GAYO.

Sasa wengi wanaupenda mstari mmoja maarufu sana unaotoka katika kitabu kile unaosema..”MPENZI NAOMBA UFANIKIWE KATIKA MAMBO YOTE NA KUWA NA AFYA YAKO, KAMA VILE ROHO YAKO IFANIKIWAVYO.(3YOHANA 1:2)”..Ni mstari unaopendwa na kila mmoja kwasababu ni mstari unatoa Baraka na mafanikio..Lakini tunashindwa kuelewa kuwa waraka ule haukuandikwa kwa watu wote bali kwa mtu anayeitwa GAYO peke yake ndio aliyeambiwa maneno yale ya baraka, na ni lazima ujue ni kwanini Baraka zile alizistahili yeye na si mwingine kutoka kwa Mungu, na kwa kujifunza kupitia yeye na sisi ndio tunaweza kustahili kupata Baraka kama zile, kwa ufupi kama ukisoma pale utagundua kuwa mtu huyu alikuwa na moyo wa kipekee sana, aliwakaribisha wageni waliokuwa wanasafiri kwa ajili ya kazi ya Mungu, alijitoa kwa ajili ya Bwana kweli kweli, aliwahudumia watumishi wa Mungu waliokwenda kuhubiri nchi za ugenini, kwa hali na mali kiasi cha kwamba hata watumishi hao waliosafirishwa na yeye wakawa hawana mahitaji yoyote kutoka kwa watu wasioamini, Hivyo sifa zake zikavuma katikati ya makanisa yote mpaka kuwafikia mitume..Na ndipo ukija kusoma utaona maneno hayo ya Baraka yanatamkwa mbele yake..

Sasa leo utamwona mtu ni mkristo lakini hata kutoa kitu kidogo kwa Mungu wake anaona shida, na huyo huyo bado ndio wa kwanza kumwambia Mungu, ulisema nifanikiwe katika mambo yote..Hajui kuwa ili Mungu akubariki kwa Baraka kama hizo kuu na nono sio hivi hivi tu..BALI KWA WATU WENYE TABIA KAMA ZA GAYO. Watu ambao hawapo tayari kuona kazi ya Mungu haikwamishwi na kitu chochote.

Vile vile na leo tutaona kwa ufupi juu ya ujumbe ulio katika huu Waraka wa PILI wa Yohana, je! Unamhuhusu nani?. Ni vema ukapata muda wa kuusoma wote peke yako. kwanza ni mfupi na pia itakusaidia tuende pamoja katika uchambuzi huu tunaokwenda kuuangalia..

Tunasoma…

3Yohana 1:1 “Mzee, kwa MAMA MTEULE, na watoto wake niwapendao katika kweli; wala si mimi peke yangu, bali na wote waijuao ile kweli;

Awali ya yote tunaona Hapa mtume Yohana anajitambulisha kama MZEE, na sio kama mtume, au mtumwa wa Kristo, kufikisha ujumbe kama mkomavu, mtu aliyekula chumvi nyingi, anafahamu mambo mengi yahusuyo kanisa na shamba la Mungu kwa ujumla, anayejua jinsi ya kupambanua mitego ya Yule mwovu aliyowahi kuiona katika maisha yake ya kikristo, na jinsi mitego hiyo inavyoweza kunasa makundi mbali mbali ya watu na namna yake, “kijana kwa wazee”, watoto kwa wakubwa, waume kwa wake, n.k.

Hivyo hapa waraka huu tunaona moja kwa moja anaulekeza kwa MAMA MTEULE..Na sio mama tu wa kawaida, Bali anasema mama MTEULE tena pamoja na watoto wake..Hivyo ni wazi kuwa ujumbe huu unawahusu WANAWAKE WOTE, WALE WALIO WATEULE WA KRISTO, ambao wameshaokolewa, ambao walishaoshwa dhambi zao kwa damu ya Yesu Kristo, ambao neema ya Mungu tayari ipo juu yao siku zote, ambao ni watakatifu tena wenye watoto,.

Sasa yapo mambo 3 makuu yalipaswa yazingatiwe au yaonekane katikati wanawake watuelu wa Mungu wa namna hiyo..Na ndio hayo tutayatazama leo katika vipengele vyake. Jambo la kwanza ni..

1) KUWAONGOZA WATOTO KATIKA KWELI:

Kama ukisoma hapo utaona mzee huyu alianza kwanza kwa kuchunguza hali ya watoto wa mama Yule mkristo, katika nyumba yake, na kutamani sana kuona jinsi alivyoweza kuwajali watoto wake au watu wa nyumbani kwake kwa kuhakikisha kuwa wanamcha Mungu, wanadumu katika utakatifu, alitamani kumwona mama huyu jinsi ambavyo angejitoa katika kuangalia hali ya kiroho ya watoto wake kuliko kitu kingine chochote wakifanyacho.. na kama tunavyosoma ni kweli mwanamke huyu mteule alikuwa nacho Tunasoma.

1:1 “Mzee, kwa mama mteule na watoto wake niwapendao katika kweli; wala si mimi peke yangu, bali na wote waijuao ile kweli;

2 kwa ajili ya hiyo kweli ikaayo ndani yetu, nayo itakuwa pamoja nasi hata milele.

3 Neema, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika kweli na upendo.

4 Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba”.

Unaona hapo mstari wa 4 anasema.

“4 Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba.”

Hivyo ikiwa wewe ni mama, na unataka kuitwa MTEULE wa Kristo, Swali ni je!.unahakikisha watoto wako wanaenenda katika misingi ya kumjua Mungu?, Unawakemea wanapotenda dhambi au unawaangalia tu, je! Unafuatia hali zao za kiroho, au kila wakati upo buzy kufuatilia tu mahudhurio yao ya shuleni na huku mahusiano yao na Mungu yanadorora kila siku. Watoto wako mstari mingapi ya biblia wanaifahamu mpaka sasa, lakini nyimbo za kidunia kila siku unawasikia wakiimba lakini huwasemeshi? Na bado unajiita MAMA MTEULE wa Kristo unayempenda Mungu….Huo sio uteule mama, siku ile hautakuwepo katikati ya wanawake wateule wa Kristo kama wakina SARA na HANA, na wengineo ikiwa utawaona watoto wako wanapotea na wewe huwasemeshi kitu, ikiwa utawaona hawamjui Mungu na wewe hutaki kuwafundisha, unawanunulia kila siku vitabu vipya vya shuleni lakini biblia huwanunulii, unawalipia tution kila siku lakini fellowship na bible study huwapeleki…Huo sio uteule mama…Hali kadhalika na wewe ambaye bado hujawa na watoto, je! Hayo malengo yapo kwenye kichwa chako?

2) KUWA NA UPENDO:

Jambo la pili Mzee huyu alilotamani kuliona katikati ya mwanamke huyu mteule wa Kristo ni UPENDO.

Tunasoma.

“5 Na sasa mama, nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane.

6 Na huu ndio upendo: tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo”.

Unaona hapo? Anasema Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo. Sasa Amri hiyo aliyokuwepo tangu mwanzo ni ipi?

Marko 12:29 “Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja;

30 nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.

31 Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”

Umeona hizo mbili zote alitazamia kuziona kwa mwanamke huyu, ahakikishe kuwa kumpenda Mungu kupo ndani yake siku zote, juu ya kulea watoto katika kweli lakini pia kumcha Mungu kuwepo ndani yake, awe na amani kuwepo uweponi mwa Bwana, awe mwombaji, au msomaji wa Neno.

 

Na pia awapende ndugu, kwa furaha kabisa kama vile biblia isemavyo upendo huvumilia, upendo hauhusudu, upendo haujivuni, upendo hauhesabu mabaya,.

Lakini mwanamke anayesema ameokoka, lakini hana habari na Mungu, hataki kujifunza maneno ya Mungu, hata kusali kwake ni shida, huruma hana, ni msengenyaji wakati wote, hana uvumilivu ndani yake, akiudhiwa kidogo tu, yeye naye anaanza kusengenya. Na suala hili limekuwa hafifu kwa wanawake wengi, na hivyo kimekuwa kikwazo kikubwa sana cha UTEULE WAO pasipo wao kujijua, Hivyo kama wewe ni mwanamke na unajiita mteule fanyia kazi hilo kwa bidii, shindana na usengenyaji huo mpaka uushinde.

3) KUJILINDA NA WADANGANYIFU. 

Hili ndio jambo la tatu na la mwisho mzee huyu mwenye hekima alimwomba mama huyu mteule alizingatie. Hapa anaendelea kusema..

“7 KWA MAANA WADANGANYIFU WENGI WAMETOKEA DUNIANI, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo.

8 Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, BALI MPOKEE THAWABU TIMILIFU.

9 Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeyeadumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia.

10 Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu.

11 Maana yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu”.

Tazama hapo anasema “KWA MAANA WADANGANYIFU WENGI WAMETOKEA DUNIANI”,…Sasa kumbuka kama wadanganyifu hawa walitokea wakati ule, watatokea na sasa, na pia zingatia jambo hili ili usichanganyikiwe roho ya mpinga-kristo ni ile ile, lakini utendaji wake kazi unabadilika kulingana na nyakati na majira. Wadanganyifu waliokuwepo wakati ule wa mitume walikuwa na kazi moja tu, yaani Kumkana Kristo kuwa hakufufuka..Kwasababu habari ya ukristo ndio kwanza zilikuwa zinaanza kuhubiriwa, Hivyo shetani ili kuuuwa ukristo usiaminiwe na wengi kwa wakati ule, alitumia udanganyifu wa kuwa Kristo hajafufuka, na pia hawezi kurudi katika mwili..Hao ndio walioitwa wapinga-kristo wa wakati ule, na ndio hao Mzee huyu alikuwa anamwonya mama huyu MTEULE ajitenge nao pamoja na mafundisho yao…Kwasababu kwa uzoefu wake wa rohoni Mungu aliompa aliona kuwa wanawake wengi wateule ndio wanaokuwa rahisi kuchuliwa na wimbi hili na wapinga-kristo zaidi ya wanaume wateule,.(sisemi kuwa wanaume hawadanganyiki), hapana bali wengi ni wanawake.

Lakini roho ile ile ya udanganyifu, inatenda kazi hata sasa isipokuwa kwa namna ya ujanja mkubwa zaidi, mpaka kufikia hatua Bwana Yesu kusema wakati huo watawadanganya yamkini hata walio WATEULE…Hivyo roho hii ya udanganyifu haiji tena kwa kusema Yesu hakufufuka, au haikuambii Yesu hatarudi, kwani mpaka sasa shetani anafahamu kuwa hakuna mkristo asiyejua kuwa Kristo alifufuka, na Yesu siku moja atarudi..kila mtu analijua hilo, lakini badala yake anakuja na udanganyifu mwingine nao ndio huu “Kushusha thamani ya wokovu na injili ya YESU KRISTO.”

Kuwafanya watu wasichukulie tena kwa uzito na umakini habari za wokovu, watu wajue kuwa ni kweli Yesu anaokoa lakini maisha yao yasiathiriwe na wokovu huo, anahakikisha kuwa mtu anakuwa vuguvugu, nusu kwa Mungu nusu kwa dunia, injili ya kisasa, injili ya I don’t care, injili ya “haijalishi!”..injili ya kutabiriwa tu mafanikio basi, lakini mambo ya toba yasigusiwe kabisa..Na hali hiyo inawalewesha hata wale ambao walikuwa wamesimama waanze kuwa vuguvugu.

Na roho hii inawakamata sana sana wakina mama, tena hata wale wateule, na ndio maana hapo Mtume Yohana anamwambia. “9 Kila apitaye cheo, wala asidumu katika MAFUNDISHO YA KRISTO, yeye hana Mungu”.

Umeona, njia pekee ya kuwatumbua hao ni kudumu katika mafundisho ya Kristo (Yaani Neno la Mungu)…

Webrania 12: 14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;

Hivyo ikiwa wewe ni mwanamke mteule unayetaka kupokea THAWABU TIMILIFU kama huyu mama, hakikisha unaufanya imara uteule wako kama maandiko yanavyosema, kwa kuzingatia hayo mambo matatu kuwa yapo ndani yako.

2 Petro 10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na UTEULE WENU; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe”.

Mungu akubariki. Tafadhali “Share” ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki zaidi.

Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

TWEKA MPAKA VILINDINI.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA TATU WA YOHANA.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU

TOA HUDUMA ILIYO BORA.


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/03/20/mambo-ya-kujifunza-katika-waraka-wa-pili-wa-yohana/