UTENDAJI KAZI WA MPINGA-KRISTO.

by Admin | 20 March 2019 08:46 pm03

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, natumai u mzima, karibu tushiriki pamoja maneno ya uzima, leo tutazungumzia juu ya ujio wa mpinga-kristo.

Mpaka sasa dunia inatazamia ujio wa watu wawili huko mbeleni kabla ya mambo yote kuisha, wa kwanza ni KRISTO na wa pili ni MPINGA-KRISTO. Na kila mmoja amekuwa akitazamiwa na watu na bado anaendelea kutazamiwa. Lakini kuna mahali ambapo watu wengi wanakosa shabaha hususani katika namna ya kumtambua mpinga-kristo na utendaji kazi wake. Tambua kuwa njia pekee ya kumjua shetani ni kumfahamu Mungu tu, hakuna njia ya mkato, huwezi kusema unamjua vizuri shetani na huku hata mahusiano yako na Mungu ni mabovu, Neno la Mungu halipo ndani yako Roho wa Mungu yupo mbali na wewe, hapo ni sawa na unajidanganya tu hata kama utasema wewe unamjua shetani namna gani, na ndio hapo utamwona mtu anaishia kudhani shetani ni freemason aliyekaa kuzimu anawatajirisha watu na kuwaambia watoe kafara za watu ili awape utajiri, na kusababisha ajali, na mambo mabaya hilo tu,.na utakuta mtu huyo anapoteza muda wake mwingi kuchunguza ishara na alama kila mahali, na kwenye vibao, vya kichawi ili kujiepusha navyo, utakuta anafahamu alama zote wazitumiazo wachawi. Na kwa hilo anajisifu kuwa anamfahamu shetani, lakini hafahamu kuwa hivyo ndivyo shetani anavyotaka afikirie siku zote, apoteze muda mwingi kuwafahamu wachawi na vikundi vyao, lakini asidhubutu hata kidogo kumfahamu Kristo na Neno lake.

Ndugu usipoifahamu noti original utawezaje kuitambua noti feki, watu wengi wanafikiria kuwa Mpinga-kristo atakuja kuwa ni mtu wa ajabu na wa tofauti, mtu katili sana, mtu ambaye ulimwengu mzima utakwenda mbele yake na kumsujudia na mtu yeyote asipomsujudia atauawa kama kuku, mtu ambaye atawalazimisha watu kwa nguvu wapokee chapa na endapo mtu asipopokea atachinjwa hadharani bila huruma yoyote, atakuwa mtu mkali kupindukia, atakuwa anakunywa damu za watu hadharani n.k..Hivyo hiyo inawafanya watu wastarehe wadhani kuwa bado muda mrefu sana, mpaka atokee mtu wa namna hiyo, bado hajaanza kutenda kazi na siku atakapoanza tutajua…

Lakini turudi katika upande wa pili..watu vivyo hivyo wanadhani YESU yupo mbinguni ametulia , na yeye ipo siku moja atakuja, na siku atakayokuja makaburi yatafunguka na watu wote watawaona wafu wakifufuka, atasimama mawinguni, parapanda italia, malaika wataonekana kila pande, hivyo kwasasa bado unyakuo haujaanza siku utakapotekea siku ndiyo tutakapojua.

Kitu ambacho hatukifahamu mpaka sasa ni kwamba Kristo anakuja katika roho na anawanyakua watu wake mbali na watu waovu, Bwana Yesu hajakaa katika kiti fulani huko mbinguni mpaka sasa miaka elfu mbili imepita akisubiria tu siku moja ifike aje kuwachukua wateule wake, hapana badala yake tangu kuondoka kwake amekuwa na AGENDA, na bado anatenda kazi, na agenda hiyo imekuwa akifanyia kazi kizazi baada ya kizazi, amekuwa akizungumza na watu wake katika kipindi kimoja cha kanisa hadi kingine, vipindi hivyo tunaviona katika kitabu cha ufunuo 2&3. Kila nyakati amekuwa akilinyakua kanisa lake na kulihadhi mahali fulani, hata sasa bado anaendelea kuwanyakua watu wake na kuwahifadhi, na kama utakufa na ule mwisho bado haujakukuta unahifadhiwa mahali fulani ukingojea siku ya kujumuika na wengine watakao kuwa hai na kwenda nao mbinguni.

1Wathesalonike 4.13 “Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini.

14 Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye.

15 Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti.

16 Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.

17 Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele”.

Unaona hapo siku ile unyakuo haimuhusu tu yule atakayekutwa hai hapana bali inawahusu na wale wengine ambao walishakufa wakiwa wanatembea katika mstari wa Kristo kabla ya hapo.

Lakini vigezo vya kunyakuliwa vipo wazi, ni hicho si kingine zaidi ya alama utakayotiwa, au Chapa au Muhuri uliojuu yako..Na muhuri wenyewe si mwingine zaidi ya ROHO MTAKATIFU. Pasipo huo muhuri huwezi Kunyakuliwa ndugu..aidha iwe hai au uwe umekufa..

Waefeso 4.30 “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; AMBAYE KWA YEYE MLITIWA MUHURI HATA SIKU YA UKOMBOZI”.

Hali kadhalika na kwa mpinga-kristo, hangojewi eti mpaka kipindi fulani kitakapofika ndio adhihirishe kazi zake, ni kweli kwasasa hajatokea lakini biblia ipo wazi kabisa kuwa utendaji kazi wake upo tangu zamani na ile roho inazidi kuendelea kufanya kazi hata sasa,..na kama vile Bwana alivyokuwa na Muhuri au chapa yake, Halikadhalika ibilisi naye anayo chapa yake au Muhuri wake,.Na chapa hiyo ni KU-MPINGA-KRISTO, na mtu anampingaje Kristo? Ni kwa kumkataa Roho Mtakatifu ndani yake..Kuupinga wokovu ndani ya moyo wako..Kuzipinga-kazi za Mungu ndani ya moyo wako…Kwenda kinyume na njia za Bwana, kukaidi maagizo ya Mungu kama shetani mwenyewe alivyo. Kuutua msalaba, kulikosoa Neno la Mungu, kuipuuzia injili na kuona kama ni hadithi za kizee, kuwatukana watu wote wanaoutumainia msalaba. N.k. sasa mtu ukishajiona upo katika hali hiyo basi ujue tayari ulishapokea chapa ya mnyama..Hivyo mtu yeyote atakayekufa leo katika hali hiyo yeye naye atahifadhiwa mahali pa mateso panapoitwa, akisubiria siku ya kukamilishwa kwa wapinga-Kristo wenzake, na kwa pamoja wote wataungana na kwenda kuhukumiwa kwa kupokea chapa ya mnyama, na wote kwa pamoja watatupwa katika lile ziwa la moto.

1Yohana 2: 18 “Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo YUAJA, HATA SASA WAPINGA KRISTO WENGI WAMEKWISHA KUWAPO. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho.

2Wathesalonike 2:5 “Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo?

6 Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.

7 MAANA ILE SIRI YA KUASI HIVI SASA INATENDA KAZI; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.

8 Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake;

9 yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo;

10 na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa”.

Hivyo usidanganyike kuwa ukifa sasa bila kuufika wakati wa mpinga-kristo umeotea, kwamba umeikwepa chapa yake..fahamu kuwa chapa inapigwa hata sasa, na jua kuwa chapa ile ipo katika roho na si mwili kama vile biblia inavyosema wale watakaokutwa hai wakati wa Bwana hawatawatangulia wale waliokufa siku ile ya unyakuo..Hali kadhalika wale watakaopokea chapa ya mnyama wakati ule wa dhiki kuu, hawatawatangulia wale waliokwisha kuipokea zamani kabla ya dhiki kufika;..Watakaosalia katika ile siku ya dhiki kuu, kwa kupitia kitambulisho cha dini na udhehebu wataithibitisha chapa ya mnyama ambayo tayari imo katika roho zao.

Pia biblia inatueleza kuwa Bwana alikuja, akaondoka, na atarudi tena, halikadhalika na yule mnyama biblia inasema, alikuwako, naye hayuko naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu na kwenda kwenye uharibifu..Hii inatuweka wazi kuwa kazi zilishaanza zamani sambamba na za Bwana wetu Yesu Kristo.

Ufunuo 17:8 “Yule mnyama uliyemwona alikuwako, naye hayuko, naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu na kwenda kwenye uharibifu. Na hao wakaao juu ya nchi, wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, watastaajabu wamwonapo yule mnyama, ya kwamba alikuwako, naye hayuko, naye atakuwako”.

Unaona?, Sasa ni vizuri kufahamu pia Mpinga-Kristo mwenyewe atatokea wapi..Biblia inatueleza atatokea RUMI, katika ule utawala wa mwisho kabisa wa chuma..VATICAN ndiyo yatakayokuwa makao yake makuu, katika kiti cha KI-PAPA…Mpinga-Kristo hatashika bunduki, wala visu, anashika biblia, na anahubiri..lakini injili yake ni ya uongo.

Kwanini usifanye uamuzi sasa wa kumgeukia muumba wako?, hatari uliyonayo ni kubwa kama hutageuka sasa, mambo yote yanakaribia kuisha, ukifa leo katika dhambi huko utaenda kuwa mgeni wa nani. Tafakari hilo, usiishi tu ilimradi siku zinapita, Neema inapatikana bure, uamuzi ni wako, Ni matumaini yangu utatubu leo na kumgeukia muumba wako angali muda upo, saa zaja utakazotamani huu wakati wa sasa lakini utaukosa.

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

CHAPA YA MNYAMA

MPINGA-KRISTO NI NANI?

ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO

UFUNUO: Mlango wa 13

UFUNUO: Mlango wa 17


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/03/20/utendaji-kazi-wa-mpinga-kristo/