EPUKA KUTOA UDHURU.

by Admin | 27 July 2019 08:46 pm07

Luka 14:16 “Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi,

17 akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari.

18 Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe.

19 Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe.

20 Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja.

21 Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete.

22 Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi.

23 Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa.

24 Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu”.

Bwana Yesu alitoa mfano huo wa karamu, kuelezea mambo yanayoendelea sasa katika roho, Kristo kama Bwana Arusi, anaalika watu sasahivi katika ufalme wake, anatuma watumishi wake huku na huko duniani kote…kuwaambia watu habari za uzima…Lakini kinachohuzunisha ni kwamba wengi ambao wangestahili kuwepo kwenye harusi ya mwanakondoo siku ile hawatakuwepo!, wengi ambao wangestahili kuwa wageni rasmi hawataingia kabisa karamuni.

Watu wengi wa dini, au wanaojiita wakristo hawataingia mbinguni, hiyo ni kulingana na maandiko! Hiyo yote ni kwanini?..Ni kutokana na kitu kimoja tu kinachoitwa UDHURU..Kutokuitikia mwaliko kutokana na visababu vidogo vidogo vya kutengenezwa.

Na maandiko yanasema pia, watoza ushuru na makahaba watawatangulia wengi kuingia katika ufalme wa mbinguni.. Ni kwanini?..Ni kwasababu hawana viudhuru katika kuitikia wito wa kumgeukia Mungu, Ni rahisi kumbadilisha kahaba amgeukie Mungu, kuliko kumrekebisha mtu ambaye ni wa kidini, ambaye tayari kashashiba na dhehebu lake, hataki tena kusikia kitu kingine, hata kama ni cha kweli vipi.

Ukiisoma tabia ya hawa watu walioalikwa Harusini na kukataa kuja, utaona kabisa walikuwa ni watu werevu, walikuwa wanatoa hoja za nguvu za kwanini wao kutokuja! Na kweli utaona kwa sehemu Fulani zinamashiko! Au ni za msingi…mwingine kwenda kujaribu ng’ombe, mwingine kaoa ni lazima akae na mke wake kidogo baada ya harusi, mwingine kanunua shamba, ni lazima akalitazame n.k.

Lakini kama ukichunguza sababu pekee za kutokuja sio hizo, lazima kutakuwa na vitu vingine ambavyo havijawapendeza kwenye hiyo karamu, labda pengine mfumo wa sherehe hawakupendezwa nao, au vinywaji wavipendavyo pengine havitakuwepo n.k…hivyo ili kuiepuka hawawezi kusema moja kwa moja hatuji, watatafuta visababu sababu vitakavyowapa kibali maalumu cha kutokufika, ili waeleweke, ndio hivyo vya kununua mashamba, kujaribu ng’ombe na kuoa na kuolewa.

Sasa umewahi kujiuliza kwanini Bwana Yesu alisema… “kama ilivyokuwa siku za Nuhu na za Lutu watu walikuwa wakiuza na kununua, wakipanda na kujenga, wakioa na kuolewa?” mpaka siku ile gharika na moto viliposhuka ghafla na kuwaangamiza wote?..Kuoa sio kubaya, wala kujenga sio kubaya, wala kuuza na kununua sio kubaya…Kibaya ni UDHURU unaoutoa wakati huu wa Neema. Unapofanya vitu vya ulimwengu kama kigezo cha kuepuka mwaliko Mungu anaokupa hicho ndicho kibaya..Na kumbuka Mungu anaujua moyo wako, haiwezekani unapata muda wa kuangalia sinema au kusikiliza umbea masaa 2 au zaidi kila siku lakini muda wa kumtafakari Mungu au kusoma Neno lake au kuhudhuria kwenye nyumba yake angalau mara moja kwa wiki huna…kwa kisingizio una majukumu Fulani? Wiki nzima ulikuwa buzy na kazi umechoka,..Biblia inasema Mungu hadhihakiwi, apandacho mtu ndicho atakachovuna.

Wagalatia 6:7 “ Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.

8 Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele”.

Unapoisikia Injili wakati huu ya kukualika kwenye ufalme wa mbinguni, inayokuambia utubu na uache dhambi na rushwa, na utapeli, na wizi, na ukahaba na wewe unaanza kusema siwezi kuacha kufanya hivyo vitu kwa wakati huu au kubadilika sasa, nina majukumu, Nipo kwenye mipango ya Harusi sina hela, Nipo nasomesha Watoto, Nina viwanja vimewekewa dhamana, nina mkopo ninatakiwa niushughulikie, hata jumapili nakuwa bize sana siwezi kuhudhuria kanisani, bado natafuta fedha za kujenga, mwezi wote huu nitakuwa bize sitapatikana, nitasafiri…

Ndugu, hicho ndio kitu kisichompendeza Mungu, kutoa UDHURU!..Nafasi yako ya wokovu atapewa mwingine! Ambaye asikiapo mara moja tu ataacha!..usidhani Mungu anafurahishwa na udhuru unaoutoa. Kaingia gharama kubwa kukuandalia Karamu yake mbinguni halafu leo, unamwangusha kwa udhuru wako, Vitu unavyovihangaikia vyote vinapita (1 Yohana 2:17)..Na mwaliko huu unaoalikwa leo ni wa muda tu! Hautadumu milele.

Kuna Neema kubwa sana sasa hivi Mungu kaiachilia katika Bara la Afrika, Roho wa Mungu sasahivi anafanya kazi sana Afrika kushawishi watu wamgeukie Mungu kwa nguvu kubwa sana ya ushawishi, ambayo hiyo haipo mabara mengine, ndio maana kwa sehemu kubwa utaona hofu kubwa ya Mungu humu Afrika, mabara mengine ni ngumu sana mtu kushawishika kuigeukia injili, ni kwasababu gani?…Ni kwasababu ile nguvu ya ushawishi (Neema) haipo kwa wingi kama huku, Injili ilianzia Asia na Ulaya na kuzunguka kwenye mabara yote na inamalizikia na Afrika…Na ikitoka huku inarudi Israeli, baada ya hapo ule mwisho unakuwa umefika..Ugumu wa kuiamini injili tunaouona sasa kwenye mataifa yaliyoendelea na utahamia huku pia hivi karibuni wakati kanisa limenyakuliwa, kutakuwa hakuna ile nguvu yakuvutwa tena kwa Mungu, Itahamia Israeli.

Sasa kwanini unaichezea hii Neema iliyopo Afrika sasa?..Neema ambayo inakupa Ushahidi wote ndani ya moyo wako kuwa Mungu yupo, utafika wakati itakuwa ni ngumu hata kuamini kuwa Mungu yupo,..ndicho kinachotokea kwa watu wa mabara mengine, kwasababu anayemfanya mtu amwamini Mungu ni Mungu mwenyewe, sasa akiondoka utamwaminije?, utamfuataje?, utatubuje? (Yohana 6: 44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka).

Wakati utafika Bwana ataingiza kwa nguvu wale ambao hawaujui ukristo kabisa, usishange moja ya hizi siku kuwaona waislamu wengi wanamgeukia Kristo, wahindu wale ambao ni waabudu ng’ombe, wanaokoka ghafla ghafla tu, watu wasioamini Mungu wapagani wanamjia Kristo kwa kasi, ukishaona hivyo ujue kuwa, tayari watu wameshakatwa. Na mambo hayo tumeshaanza kuyaona sasahivi yakiongezeka kwa kasi. Hapo ndipo wengi watatamani kuingia lakini itashindikana,

Mathayo 22:10 “Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni.

11 Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi.

12 Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa.

13 Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

14 Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.”

Kama hujatubu, usiuchezee huu muda, ambao wenzako waliokuzimu wanatamani hata dakika moja tu watengeneze mambo yao na Mungu wanakosa.. unayo nafasi sasa ya kufanya hivyo, pale ulipo tubu kwa kumaanisha kuziacha dhambi ulizokuwa unafanya kisha tafuta ubatizo sahihi wa kuzamishwa mwili wote na kwa jina la Bwana Yesu kwa ajili ya ondoleo la dhambi na Bwana mwenyewe atafanya yaliyosalia kwa kupitia Roho wake Mtakatifu. Nawe utakuwa umeanza mwendo mpya na Bwana, hata kufikia karamu yake kuu aliyowaandalia watu wake tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu.

Pia kwa Maombezi, Ushauri au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba hizi…

+225693036618 / +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Zinazoendana:

KARAMU YA MWANA-KONDOO.

NDOA NA HARUSI TAKATIFU.

UMEIZALIA MATUNDA MIAKA 4 YA NEEMA ULIYOPEWA?

JINSI YA KUITUMIA VYEMA NEEMA YA MUNGU ILIYO JUU YANGU.


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/07/27/epuka-kutoa-udhuru/