MUNGU MWENYE HAKI.

by Devis Julius | 12 August 2019 08:46 am08


Shalom mtu wa Mungu karibu tujifunze juu ya Haki ya Mungu.

Ni wazi na inajulikana na wote kuwa Mwenyezi Mungu aliyetuumba sisi viumbe vyake vyote ni Mungu mwenye haki, hilo halina kipingamizi, lakini ni vizuri kuijua kwa mapana haki hiyo ya Mungu inatendaje kazi katikati ya viumbe vyake. 

Kazi anazofanya shetani na malaika wake walioasi ndio hizo hizo wanazozifanya Malaika wa Mbinguni ambao hawajaasi, shetani na Malaika zake wanajishungulisha sana na mambo ya wanadamu namna ya kuwavuta wanadamu wengi upande wao, kadhalika na Malaika watakatifu wanajishughulisha sana na mambo ya wanadamu namna ya kuwavuta wanadamu upande wa Mungu.

Sasa anayepambana na shetani si Mungu, Mungu hashindani na kiumbe chochote kile, yeye ni Mkuu kupita upeo wa fahamu zetu wote, hivyo hawezi kushindana na kiumbe chochote alichokitengeneza yeye…Kwahiyo anayeshindana na shetani ni Mikaeli pamoja na malaika wenzake watakatifu na si Mungu. Mikaeli ni Malaika mkuu wa vita aliyeko mbinguni aliye kiongozi wa vita kama vile shetani alivyo kiongozi wa malaika wengine walioasi….wapo malaika wa aina tofauti tofauti.

Ufunuo 12:7 “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake;

8 nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni

9 Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye”.

Sasa kama Mungu hashindani na shetani, swali linakuja yeye atakuwa anafanya kazi gani?

Jibu: Mungu anasimama kama wakili au hakimu, kuwapatia haki wale wanaostahili haki…

Hivyo kazi ya malaika watakatifu ni kusisimama kututetea sisi wanadamu kila siku mbele za uso wa Mungu, na kazi ya shetani na malaika zake ni kutushitaki…maana tafsiri yenyewe ya jina ‘shetani’ ni ‘mshitaki’…kazi yake ni kutafuta kasoro ndogo ndogo na kubwa katika Maisha yetu na kuzipeleka kwa Hakimu Mkuu (Mungu) kutafuta haki ya kututesa au kutuangamiza.

Sasa anapokuja kwako na kukuta kuwa wewe ni mwasherati, au mchawi, na unafanya hayo huku ukijua kabisa ni dhambi…..moja kwa moja anakimbiza hizo hoja mbele za Mungu, na kutaka ruksa ya kukutawala Maisha yako, atamwambia Mungu huyu kwa mapenzi yake mwenyewe anafanya hayo, na wala hajalazimishwa, ananitumikia mimi, amesikia injili yako na anajua kabisa kwa matendo yake atakwenda kuzimu, lakini bado anayafanya hayo..hivyo huyu ni wangu.. nipe ni wangu huyo.

Na wale malaika wa Mungu wanapokosa kitu cha kukutetea mbele za Mungu, kutokana na mambo unayoyafanya ya umakusudi na ukiwa na akili timamu, shetani anashinda hoja mbele za Mungu na kupewa haki yake..Mungu hana upendeleo hata kidogo ndio asili yake hiyo, anamlipa kila mtu kulingana na anachostahili, shetani anampa haki yake na Malaika vile vile anawapa haki zao… Ndio hapo mtu anajikuta ghafla ulinzi wa kiMungu umeondoka juu yake, anaanza kupitia hili na lile..na wakati mwingine hata kufa.

Lakini anapokuja na kukuta umemwamini Bwana Yesu Kristo, na umeoshwa kwa damu yake, na unaishi Maisha matakatifu, hata kama kuna viudhaifu vidogo vidogo, hivyo havitoshi kumpa shetani ushindi juu ya Maisha yako, kwasababu wale malaika ambao kazi yao ni kutembea na sisi wanautazama uso wa Baba yetu mbinguni kila siku kupeleka taarifa njema juu yetu,(Mathayo 18:10) hivyo hoja zao za kutumilikisha sisi kwa Mungu zinashinda kila siku na kujikuta tunaishi Maisha ya ulinzi na amani. Hiyo yote ni kwasababu umefunga milango yote shetani kupata vijisababu vya kukushtaki…(Kwa maelezo marefu juu ya huduma za hawa malaika watakatifu unaweza ukatutumia ujumbe inbox, tutakutumia maelezo yake kwa urefu)…

Lakini unaposikia injili na huku moyoni mwako unajua kabisa ni maneno ya Mungu ya uzima, na unaidharau kwa namna moja au nyingine, basi hiyo tayari ni point kubwa sana kwa shetani kuipeleka mbele za Mungu kupata kibali cha kuyatawala Maisha yako. Wale malaika wanaokulinda wanashindwa kukutetea na kuondoka..

Hivyo ni jambo la muhimu sana na kuzingatia kuyahakiki maisha yetu kila siku, kwasababu biblia inasema shetani adui yetu ni kama simba angurumaye anazunguka huko na huko kumtafuta mtu wa ammeze..

1 Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzungukazunguka, akitafuta mtu ammeze”.

Shetani hawezi kuyatawala Maisha yako ukiwa ni mtu wa unayeishi Maisha ya kumpendeza Mungu, ukiwa chini ya Damu ya mwanakondoo..Usalama wetu ni kuwa chini ya Damu ya Yesu tu , na huko sio kusema tu ‘najiweka chini ya Damu ya Yesu’..unaposema hivyo ni sawa na kusema ‘najiweka chini ya sheria za nchi’..je ukisema hivyo itakuwa na madhara yoyote?..unaona ukitaka kujiweka chini ya sheria za nchi ni kuziishi zile sheria,kuzileta kwenye Maisha yako, sio kuzitamka tu!…kadhalika kujiweka njini ya damu ya Yesu ni kuileta ile damu kwenye Maisha yako sio kuitamka tu!..kutamka kunakuja baada ya kuileta kwenye matendo hiyo damu.

Kadhalika shetani hatumnyanganyi mamlaka juu ya Maisha yetu kwa kutamka tu! (na kusema Shetani huna mamlaka juu ya Maisha yangu), hapo bado hatujamwondoa…Ili kumwondoa ni lazima tuvidhibiti vifursa vyake vyote anavyovitumia kutushitaki sisi mbele za Mungu…Na baada ya kuvifunga hivyo ndipo tunamalazia na kutamka kuwa shetani huna mamlaka yoyote juu ya Maisha yetu.

Hakuna pepo lolote linaloweza kumwingia mtu kabla halijapata kibali mbele za Mungu…Ukiona kuna roho ipo ndani yako basi jua kuna mahali mlango umeufungua maishani mwako, na hivyo shetani kapata kijisababu cha kukushitaki mbele za Mungu na kushinda.

Baadhi ya milango inayosababisha roho za mapepo kuingia ndani ya watu ni uasherati, ibada za sanamu, ushirikina, matumizi ya vipodozi na uvaaji mbaya ikiwemo mawigi, uvaaji suruali kwa wanawake, vimini, na nguo zinazobana, na upakaji wa lipstick,wanja, uvaaji hereni na uchoraji wa tattoo, utazamaji pornography, usikilizaji miziki ya kidunia ..na mambo mengine yanayofanana na hayo…

Mambo hayo ndiyo yanayoongoza kumpa shetani nafasi ya juu ya kutawala Maisha ya watu, ikiwemo kuleta magonjwa, ugomvi, shida, taabu, kukosa amani, kukosa furaha na raha pamoja na kifo.

Hivyo ukitaka kukaa mbali na shetani, suluhisho ni kutofungua mlango wowote wa kumpa shetani upenyo wa kukushtaki kwa kukaa mbali na hivyo vitu tulivyovitaja hapo juu na vingine vyote vinavyofanana na hivyo..

Kumbuka pia kukamilisha hatua zako za wokovu kama hujakamilisha, hatua hizo zipo tatu, 1)KUAMINI, 2)KUBATIZWA, na 3)KUPOKEA ROHO MTAKATIFU. Hatua hizo ni za muhimu, na pia kumbuka ubatizo sahihi ni wa kuzama mwili wote kwenye maji mengi kama neno lenyewe ubatizo linavyomaanisha, na pia ni kwa JINA LA BWANA YESU kulingana na Matendo 2:38, Na Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe anakupa kwasababu ni ahadi yake aliyowaahidi wale wote wamwombao. Na hapo sasa shetani atakapojaribu kwenda kukushitaki mbele za Mungu atashindwa, kwasababu umekamilishwa ipasavyo katika wokovu.

hivyo ukiwa hujakamilisha hatua hizo bado unayo nafasi sasa, zikamilishe kabla mwisho haujafika, kwasababu tunaishi katika siku za Mwisho, muda wowote parapanda inalia na wafu watafufuliwa na sisi tulio hai tutanyakuliwa na Bwana kwenda mawinguni, Je utakuwa mmoja wao wa watakaoenda na Bwana?

Bwana akubariki sana. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

KUNDI LA MALAIKA WALETAO MABAYA.

HUDUMA YA MALAIKA WATAKATIFU.

BIBLIA INASEMA “HAMJUI YA KUWA MTAWAHUKUMU MALAIKA? (1WAKORINTHO 6:2-3)”JE! SISI TUTAWAHUKUMUJE MALAIKA?.


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/08/12/mungu-mwenye-haki/