TOA HUDUMA ILIYO BORA.

by Admin | 19 August 2019 08:46 pm08

Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu ambalo ni mwanga wa njia yetu, na taa iongozayo miguu yetu..

Biblia inatuambia katikaAyubu 22:21 “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia”….Ikiwa na maana kuwa Mema hayawezi kuja wala Amani tusipomjua Mungu vizuri, hivyo moja ya tatizo kubwa linalotukabili sisi wanadamu hususani wakristo ni kutokumjua Mungu vizuri, Hatumjui Mungu anafanyaje kazi, na anawapatiaje watu mema.

Ni Dhahiri kuwa mema mengi tunayoyatafuta ni mema ya hapa duniani, kama vile kuwa na mali, kufanikiwa katika kazi, kupata mume mzuri au mke mzuri wa Maisha, kupata kibali na vingine vingi..Lakini Mema ya ufalme wa Mbinguni ni bora Zaidi na yenye faida mara dufu!

Kwa ufupi leo tujifunze ni kwa namna gani Mungu anawapatia mema watu wake (mema ya hapa duniani).

Biblia inasema Mungu ni Mungu mwenye haki (Zaburi 7:9-11, Zab.11:7, Isaya 45:21), ikiwa na maana kuwa huwapa haki wale wanaostahili haki. Mungu kamwe hawezi kumpa mtu kitu asichokistahili.

Hebu tujifunze kwa mifano kidogo. Inatokea mtu ana biashara yake ya kawaida tu!, na ni Mkristo ambaye ni mwombaji mzuri, na kila siku anaiombea kazi yake, na anatumia mpaka Mafuta, na maji kuiweka wakfu, na pia anayo mpaka picha ya Bwana Yesu nyuma ya ukuta WA jengo la biashara yake, na kila siku kabla ya kuanza kazi anaiombea hata lisaa limoja, lakini bado unakuta pamoja na jitihada zote hizo mambo bado hayaendi vizuri anapata hasara au anaishia kupata mapato kidogo…Sasa yapo mambo mengi yanaweza kusababisha hilo lakini leo tutaangalia jambo kubwa sana linalosababisha matokeo hayo!… Na hilo si lingine Zaidi ya KUTOKUTOA HUDUMA INAVYOSTAHILI.

Unaweza kuwa mkristo mwombaji kweli na mwaminifu katika kuisogeza kazi yako mbele za Mungu, lakini kama hutajifunza kutenda mapenzi ya Mungu katika kazi yako, maombi yako au ya mwingine juu yako hayatasaidia kitu, yatakuwa ni kazi bure, kama ndani ya kazi yako hutatoa huduma nzuri inayovutia, inayostahili wewe kupata faida, kama hutatoa huduma itakayomvutia yule anayetaka kununua kutoka kwako aweze kurudi tena, kama hutakuwa mnyenyekevu, na mtu wa kujishusha katika kazi hiyo, kama hutakuwa mtu wa kupokea ushauri na kuuchuja katika Neno na kuufanyia kazi, kamwe maombi hayatakusaidia chochote, kadhalika kama hutakuwa msafi katika kazi yako, kama hutakuwa ni mpole kwa wateja wako hata ukibandika picha 20 zenye sura zinazofanana na Bwana Yesu nyuma ya ukuta wa jengo hilo, na kuweka stika za Mistari ya biblia 100, hazitasaidia chochote..

Sasa kwanini Vitu hivyo havisaidii chochote katika kukuletea faida?

Ni kwasababu hujajua kuwa Mungu ni Mungu mwenye haki. Na Watumishi wa Mungu wote wanatumika katika kuwapelekea watu huduma njema sharti walifahamu hilo, Mungu hawezi kumtumia mtu kuwapikia uchafu au sumu watu wake!..hivyo kama wewe ni mchafu katika mahali ulipo kwenye kazi yako labda ya Mgahawa, hiyo ndio sababu Mungu hawezi kuinyanyua izidi kusitawi, hapo ili utumike na Mungu kuwalisha watu wake chakula bora ni sharti uwe msafi sana, kwasababu kuna watu wameamka asubuhi kutoka majumbani mwao na huku wamemwomba Mungu awaepushe na hatari zote ikiwemo sumu na uchafu kuingia katika miili yao, sasa Mungu hawezi kuwajibu hao maombi yao kwa kuwaleta kwenye mgahawa wako ambao unapika uchafu na vyakula visivyo na ubora! Kwa kujidanganya kuwa Mungu ameifunika biashara yako..hapana Mungu ni Mungu mwenye haki! Hawezi mtu kumwomba Mkate akampa jiwe!..Mungu hayupo duniani kuwapatia watu mabaya bali mema…

Hivyo ukitaka kazi yako ya mgahawa isitawi usitegemee maombi tu peke yake…Kuwa Msafi wa viwango vya juu sana,kupita wengine..pika chakula freshi na chenye viwango… ndipo Mungu atakufanya kuwa mtumishi wake kuwapatia chakula safi wanadamu wake na utaona wateja ambao hujawahi kuwaona wakimiminika kwenye hiyo kazi yako.

Na kitu kimoja kisichojulikana na wengi, ni kwamba Mungu hatendi kazi kama shetani atendavyo, shetani ndio ana kitu kinaitwa chuma ulete, au mazingaumbwe anatumia kiini macho,kwamba mtu anaweza kupata chochote katika hali hiyo hiyo aliyopo, hata akiwa mchafu, anaweza kutumia nguvu za giza, kuleta wateja..Mungu hana hicho kitu chuma ulete, wala hatumii kiini macho kuwaletea watu wake fedha!..vinginevyo sifa yake ya kuwa Mungu mwenye haki haitakuwepo!.

Kadhalika kama ni duka, Mungu hawezi kukutumia wewe kuwalisha watu vitu vilivyoisha muda wake wa matumizi (vilivyo-expire), hata kama unakesha kwa wiki mara mbili kuiombea, hata kama unaitolea sadaka nyingi kiasi gani, haiwezekani Mungu kukunyanyua.…kwanini hawezi kufanya hivyo kwasababu, yeye sio Mungu wa kuwapa watu sumu..kama tu asivyokuwa Mungu wa watumishi wa uongo (manabii wa Uongo)..Na kadhalika wafanya biashara wa uongo Mungu hawezi kuwa nao, hata wawe waombaji kiasi gani…atawaepusha watu wake na duka lako….

Pia unapokuwa katika kazi yako unapaswa uwe mnyenyekevu, hupaswi kuwa mtu wa hasira na mtukanaji, au mkorofi. Mungu hawezi kukutumia kuwahudumia watu wake uende ukawatukane na kuwazalilisha..Pia unapaswa kuhakikisha unafanya juhudi kufikisha huduma yako mpaka mlangoni mwa wateja wako au wanaohitaji!..Kwasababu hata watumishi wa Mungu wa kweli anaowatumia hutuletea Neno la Mungu mpaka ndani ya mageti yetu kwa unyenyekevu wote, na ndivyo injili ilivyofanikiwa duniani kote…Kadhalika katika kazi yako, kama unauza mkate mfikishie mteja wako mpaka mlangoni, Mungu anapendezwa na watu wanaotua huduma njema, watu wake wahudumiwe mpaka mahali walipo, na mtu anapohudumiwa kwa njia hiyo, moyoni atafurahi na hivyo atamtukuza Mungu na kumshukuru, na akishafurahi na Mungu atafurahiwa na wewe na hivyo kuibarikia hiyo kazi yako izidi kusonga mbele Zaidi..Hapo ndipo atakapomshawishi Yule mtu kuja tena, na Yule mtu kumwambia mtu mwingine, hivyo hivyo mpaka wanakuwa wengi.

Kadhalika Kama ni mjenzi Mungu hawezi kukutumia wewe kuwajengea watu nyumba ambazo zipo chini ya viwango, kwasababu kuna watu wamemwomba Mungu awapatie nyumba zilizobora na fundi aliyemwaminifu na mwenye ujuzi wa kutosha, hivyo ili Ukidhi hiyo nafasi ya kuwa Mtumishi wa Mungu katika eneo hilo, ni sharti ujitahidi kuielewa vyema hiyo kazi kwa kwenda kutafiti mbinu mpya za ujenzi, kuongeza ujuzi wako na kuongeza ustadi…ili Mungu achague kukutumia wewe na si mwingine katika nafasi hiyo, hapo ndipo utakapoona mafanikio makubwa, usikimbilie kutafuta faida ya haraka haraka, …lakini kama hutataka kutafuta kutoa huduma bora yenye viwango, Bwana Mungu atatafuta mtu mwingine hata kama asiye mkristo aliyekidhi hivyo viwango, kuifanya kazi hiyo…..kwahiyo maombi peke yake hayatoshi!. Matendo ndio yenye nguvu zaidi..Inakupasa ujitahidi uwe bora Zaidi ya wengine ili ukawafanyie watu kilicho bora wamtukuze yeye…

Kadhalika na mambo mengine yote yaliyosalia…jambo ni lile lile…. “JITAHIDI KUTOA HUDUMA ILIYO YA VIWANGO VYA KIMBINGUNI ”

Hata unapotafuta kuoa au kuolewa!! Formula ni hiyo hiyo, NI lazima uwe mtakatifu, usipofanya hivyo na kutegemea maombi peke yake, nakuhakikishia hutaolewa wala hutaoa!…au kama utaoa au kuolewa basi utaoa mtu asiyesahihi au kuolewa na mtu asiyesahihi.

Kwanini?

Kwasababu wewe ni mwenye kiburi na mwasherati halafu unamwomba Mungu akupe mume mwenye hofu ya Mungu, mpole, mnyenyekevu, atakayekujali na kukupenda na kukuheshimu, na asiyekuwa mwasherati….Hujui kwamba huyo mume unayemwomba aliye na vigezo hivyo vya hofu ya Mungu, naye pia anamwomba Mungu ampe mke aliye kama yeye alivyo, mwenye hofu ya Mungu kama yeye, msikivu kama yeye alivyo, asiye mwasherati kama yeye, asiye mwenye kiburi na aliye mnyenyekevu…. Sasa Mungu hawezi kumpa mtoto wake nyoka aliyemwomba samaki!…Kwahiyo Mungu atahakikisha anamtafutia Mke mwema yule mwanamume mwenye hofu ya Mungu kama yeye…Na huyo mke atakuwa sio wewe kwasababu wewe huna vigezo hivyo…..Wewe utaishia kupata mwenye vigezo kama vya kwako vya uasherati, kiburi, na kahaba..Lakini ukiwa mtakatifu Mungu atakupatia Mtakatifu mwenzako na wala haitachukua Muda!…Na pia utakatifu ni wajibu!..hatuwi watakatifu tu kwasababu tunatafuta wachumba!..Ni wajibu wetu kuwa watakatifu maadamu tunaitwa wakristo!

Ndio maana Kuna umuhimu wa kumjua sana Mungu, ili mema yakujie…Mungu anataka tufanye kazi ya haki, tupate haki, anataka tuwe watakatifu tuwapate watakatifu, anataka tuwe wakujitoa ndipo na wengine wajitoe kwa ajili yetu…anataka tuwe watu wa kutoa huduma njema ndipo atubariki. Anataka tumjue kwa mapana hayo….Maombi yanafaa sana endapo tutaomba na kutenda!

Zaburi 18:25 “Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili; Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu;

26 Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi.”

Bwana akubariki sana!. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

UNAWAFAHAMU MANABII WA UONGO?

MJUE SANA YESU KRISTO.

ITAFAKARI VEMA KAZI YA MUNGU


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/08/19/toa-huduma-iliyo-bora/